041 - Fusw-Swilat
فُصِّلَت
041-Fusw-Swilat
041-Fusw-Swilat: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
حم﴿١﴾
1. Haa Miym.[1]
تَنزِيلٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ﴿٢﴾
2. Ni uteremsho kutoka kwa Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma), Mwenye Kurehemu.
كِتَابٌ فُصِّلَتْ آيَاتُهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ﴿٣﴾
3. Kitabu kilichofasiliwa waziwazi Aayaat zake, kikisomeka kwa Kiarabu kwa watu wanaojua.
بَشِيرًا وَنَذِيرًا فَأَعْرَضَ أَكْثَرُهُمْ فَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ﴿٤﴾
4. Kinachobashiria mazuri na kinachoonya. Lakini wamekengeuka wengi wao, basi wao hawasikii.
وَقَالُوا قُلُوبُنَا فِي أَكِنَّةٍ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ وَفِي آذَانِنَا وَقْرٌ وَمِن بَيْنِنَا وَبَيْنِكَ حِجَابٌ فَاعْمَلْ إِنَّنَا عَامِلُونَ﴿٥﴾
5. Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa yale unayotuitia, na masikioni mwetu mna uziwi, na baina yetu na baina yako kuna kizuizi, basi tenda nasi tunatenda.[2]
قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَاسْتَقِيمُوا إِلَيْهِ وَاسْتَغْفِرُوهُ ۗ وَوَيْلٌ لِّلْمُشْرِكِينَ﴿٦﴾
6. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; hufunuliwa Wahy kwamba: Muabudiwa wenu wa haki ni Ilaah Mmoja, basi thibitini imara Kwake, na mwombeni maghfirah. Na ole kwa washirikina.
الَّذِينَ لَا يُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ﴿٧﴾
7. Ambao hawatoi Zakaah, nao ni wenye kuikanusha Aakhirah.[3]
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ﴿٨﴾
8. Hakika wale walioamini na wakatenda mema watapata ujira usiokatika.
قُلْ أَئِنَّكُمْ لَتَكْفُرُونَ بِالَّذِي خَلَقَ الْأَرْضَ فِي يَوْمَيْنِ وَتَجْعَلُونَ لَهُ أَندَادًا ۚ ذَٰلِكَ رَبُّ الْعَالَمِينَ﴿٩﴾
9. Sema: Je, hivi nyinyi mnamkufuru Yule Aliyeumba ardhi kwa siku mbili,[4] na mnamfanyia waliolingana Naye? Huyo Ndiye Rabb wa walimwengu.
وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ مِن فَوْقِهَا وَبَارَكَ فِيهَا وَقَدَّرَ فِيهَا أَقْوَاتَهَا فِي أَرْبَعَةِ أَيَّامٍ سَوَاءً لِّلسَّائِلِينَ﴿١٠﴾
10. Na Akaweka humo milima iliyosimama thabiti juu yake, na Akabariki humo kwa kheri zisizokatika, na Akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Ni idadi madhubuti kabisa kwa wanaouliza.
ثُمَّ اسْتَوَىٰ إِلَى السَّمَاءِ وَهِيَ دُخَانٌ فَقَالَ لَهَا وَلِلْأَرْضِ ائْتِيَا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا قَالَتَا أَتَيْنَا طَائِعِينَ﴿١١﴾
11. Kisha Akazikusudia[5] mbingu (Kuziumba), nazo ni moshi, Akaziambia pamoja na ardhi: Njooni kwa khiari au kwa lazima. Zikasema: Tumekuja hali ya kuwa tumetii.
فَقَضَاهُنَّ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ فِي يَوْمَيْنِ وَأَوْحَىٰ فِي كُلِّ سَمَاءٍ أَمْرَهَا ۚ وَزَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِمَصَابِيحَ وَحِفْظًا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ﴿١٢﴾
12. Akamaliza kuziumba mbingu saba katika siku mbili, na Akaifunulia kila mbingu jambo lake. Na Tukaipamba mbingu ya dunia kwa taa na hifadhi. Hayo ni Takdiri ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.[6]
فَإِنْ أَعْرَضُوا فَقُلْ أَنذَرْتُكُمْ صَاعِقَةً مِّثْلَ صَاعِقَةِ عَادٍ وَثَمُودَ﴿١٣﴾
13. Wakikengeuka, basi sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nakuhadharisheni radi na umeme angamizi mfano wa radi na umeme angamizi wa kina ‘Aad[7] na Thamuwd[8].
إِذْ جَاءَتْهُمُ الرُّسُلُ مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّـهَ ۖ قَالُوا لَوْ شَاءَ رَبُّنَا لَأَنزَلَ مَلَائِكَةً فَإِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ﴿١٤﴾
14. Walipowajia Rusuli mbele yao na nyuma yao wakiwaambia: Msimuabudu isipokuwa Allaah, wakasema Angelitaka Rabb wetu, bila shaka Angeliteremsha Malaika. Na hakika sisi tunayakataa mliyotumwa nayo.
فَأَمَّا عَادٌ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً ۖ أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَهُمْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُمْ قُوَّةً ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ﴿١٥﴾
15. Ama kina ‘Aad, wao walitakabari katika ardhi bila ya haki, na wakasema: Nani mwenye nguvu zaidi kuliko sisi? Je, hawakuona kwamba Allaah Ambaye Amewaumba Ndiye Mwenye nguvu zaidi kuliko wao? Nao walikuwa wanazikanusha Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja) Zetu.
فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي أَيَّامٍ نَّحِسَاتٍ لِّنُذِيقَهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَخْزَىٰ ۖ وَهُمْ لَا يُنصَرُونَ﴿١٦﴾
16. Basi Tukawapelekea upepo wa dhoruba wenye mngurumo katika siku za mikosi ili Tuwaonjeshe adhabu ya hizaya katika uhai wa dunia. Na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni ya hizaya zaidi, nao hawatonusuriwa.
وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ عَلَى الْهُدَىٰ فَأَخَذَتْهُمْ صَاعِقَةُ الْعَذَابِ الْهُونِ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿١٧﴾
17. Na ama kina Thamuwd, wao Tuliwaongoza, lakini walistahabu upofu kuliko hidaaya. Basi ikawachukuwa radi na umeme angamizi wa adhabu idhalilishayo kwa sababu ya waliyokuwa wakiyachuma.
وَنَجَّيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ﴿١٨﴾
18. Na Tukawaokoa wale walioamini, na walikuwa wenye taqwa.
وَيَوْمَ يُحْشَرُ أَعْدَاءُ اللَّـهِ إِلَى النَّارِ فَهُمْ يُوزَعُونَ﴿١٩﴾
19. Na Siku watakayokusanywa maadui wa Allaah kupelekwa motoni, nao watapangwa safusafu wa mwanzo wao hadi mwisho wao.
حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٢٠﴾
20. Mpaka watakapoufikia, yatashuhudia dhidi yao masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.[9]
وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّـهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٢١﴾
21. Na wataziambia ngozi zao: Mbona mnashuhudia dhidi yetu? Zitasema: Ametutamkisha Allaah Ambaye Ametamkisha kila kitu, Naye Ndiye Aliyekuumbeni mara ya kwanza, na Kwake mtarejeshwa.
وَمَا كُنتُمْ تَسْتَتِرُونَ أَن يَشْهَدَ عَلَيْكُمْ سَمْعُكُمْ وَلَا أَبْصَارُكُمْ وَلَا جُلُودُكُمْ وَلَـٰكِن ظَنَنتُمْ أَنَّ اللَّـهَ لَا يَعْلَمُ كَثِيرًا مِّمَّا تَعْمَلُونَ﴿٢٢﴾
22. Na hamkuwa mkijisitiri hata yasishuhudie masikio yenu, wala macho yenu, wala ngozi zenu, lakini mlidhania kwamba Allaah Hajui mengi katika yale mnayoyatenda.[10]
وَذَٰلِكُمْ ظَنُّكُمُ الَّذِي ظَنَنتُم بِرَبِّكُمْ أَرْدَاكُمْ فَأَصْبَحْتُم مِّنَ الْخَاسِرِينَ﴿٢٣﴾
23. Na hiyo dhana yenu mliyokuwa mkimdhania Rabb wenu, ndiyo imekuangamizeni, na mmekuwa miongoni mwa waliokhasirika.
فَإِن يَصْبِرُوا فَالنَّارُ مَثْوًى لَّهُمْ ۖ وَإِن يَسْتَعْتِبُوا فَمَا هُم مِّنَ الْمُعْتَبِينَ﴿٢٤﴾
24. Basi wakivuta subira, lakini moto ndio makazi yao tu. Na wakiomba wapewe nafasi tena ya kufanya utiifu wa kumridhisha Allaah, basi wao si wenye kuridhishwa na kupewa.
وَقَيَّضْنَا لَهُمْ قُرَنَاءَ فَزَيَّنُوا لَهُم مَّا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَحَقَّ عَلَيْهِمُ الْقَوْلُ فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِم مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا خَاسِرِينَ﴿٢٥﴾
25. Na Tuliwawekea marafiki wa karibu, wakawapambia yaliyo mbele yao na ya nyuma yao, na ikawathibitikia kauli wawe pamoja na nyumati zilizopita miongoni mwa majini na wanaadam. Hakika wao wamekuwa ni wenye kukhasirika.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ﴿٢٦﴾
26. Na wale waliokufuru wakasema: Msiisikilize hii Qur-aan na ifanyieni rabsha huenda mkashinda.[11]
فَلَنُذِيقَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا عَذَابًا شَدِيدًا وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَسْوَأَ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٢٧﴾
27. Bila shaka Tutawaonjesha wale waliokufuru adhabu kali, na bila shaka Tutawalipa uovu zaidi wa yale waliokuwa wakiyatenda.
ذَٰلِكَ جَزَاءُ أَعْدَاءِ اللَّـهِ النَّارُ ۖ لَهُمْ فِيهَا دَارُ الْخُلْدِ ۖ جَزَاءً بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ﴿٢٨﴾
28. Hiyo ndio jazaa ya maadui wa Allaah, moto! Watapata humo makazi yenye kudumu. Ndio jazaa kwa sababu walikuwa wakizikanusha Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja) Zetu.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا رَبَّنَا أَرِنَا اللَّذَيْنِ أَضَلَّانَا مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ نَجْعَلْهُمَا تَحْتَ أَقْدَامِنَا لِيَكُونَا مِنَ الْأَسْفَلِينَ﴿٢٩﴾
29. Na watasema wale waliokufuru: Rabb wetu! Tuonyeshe wale waliotupotoa miongoni mwa majini na wanaadam tuwaweke chini ya miguu yetu ili wawe miongoni mwa wa chini kabisa.
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾
30. Hakika wale waliosema: Rabb wetu ni Allaah, kisha wakathibiti imara,[12] Malaika huwateremkia (kuwaambia): Msikhofu, wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa.[13]
نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ﴿٣١﴾
31. Sisi ni rafiki zenu walinzi katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoyahitajia.
نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ﴿٣٢﴾
32. Ni mapokezi ya takrima kutoka kwa Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu.
وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴿٣٣﴾
33. Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania kwa Allaah na akatenda mema na akasema: Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu![14]
وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ﴿٣٤﴾
34. Na wala haulingani sawa wema na uovu. Zuia (uovu) kwa ambalo ni zuri zaidi. Hapo utamkuta yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, kama ni rafiki mwandani.[15]
وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ﴿٣٥﴾
35. Na hayapati hayo isipokuwa wale waliovuta subira, na hayapati hayo isipokuwa mwenye fungu adhimu.[16]
وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴿٣٦﴾
36. Na utakapokuchochea uchochezi kutoka kwa shaytwaan, basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.
وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ﴿٣٧﴾
37. Na katika Aayaat (Ishara na Dalili) Zake, ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Msisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Allaah Aliyeviumba ikiwa Yeye Pekee mnamwabudu.[17]
فَإِنِ اسْتَكْبَرُوا فَالَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ يُسَبِّحُونَ لَهُ بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَهُمْ لَا يَسْأَمُونَ ۩﴿٣٨﴾
38. Lakini wakitakabari, basi wale (Malaika) walio kwa Rabb wako wanamsabbih usiku na mchana, nao hawachoki.
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ ۚ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۚ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٣٩﴾
39. Na katika Aayaat (Ishara na Dalili) Zake, ni kwamba unaiona ardhi imetulia kame, kisha Tunapoiteremshia maji inataharaki na kunyanyuka. Hakika Yule Aliyeihuisha, bila shaka Ndiye Mwenye Kuhuisha wafu.[18] Hakika Yeye juu ya kila kitu Ni Muweza.
إِنَّ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي آيَاتِنَا لَا يَخْفَوْنَ عَلَيْنَا ۗ أَفَمَن يُلْقَىٰ فِي النَّارِ خَيْرٌ أَم مَّن يَأْتِي آمِنًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ ۖ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٤٠﴾
40. Hakika wale wanaozipotosha Aayaat Zetu hawawezi kujificha Tusiwaone. Je, basi yule atakayetupwa katika moto ni bora au yule atakayekuja akiwa katika amani Siku ya Qiyaamah? Tendeni mpendavyo, hakika Yeye Ni Mwenye Kuona yote myatendayo.
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالذِّكْرِ لَمَّا جَاءَهُمْ ۖ وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ﴿٤١﴾
41. Hakika wale waliokanusha Ukumbusho ulipowajia (wataangamia). Na hakika Hiki ni Kitabu chenye utukufu na udhibiti.
لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ﴿٤٢﴾
42. Hakitokifikia baatwil mbele yake wala nyuma yake. Ni Uteremsho kutoka kwa Mwenye Hikmah wa yote, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.
مَّا يُقَالُ لَكَ إِلَّا مَا قَدْ قِيلَ لِلرُّسُلِ مِن قَبْلِكَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ وَذُو عِقَابٍ أَلِيمٍ﴿٤٣﴾
43. Huambiwi (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa yale yale waliyokwisha ambiwa Rusuli kabla yako. Hakika Rabb wako Ni Mwenye maghfirah na Mwenye ikabu iumizayo.
وَلَوْ جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا أَعْجَمِيًّا لَّقَالُوا لَوْلَا فُصِّلَتْ آيَاتُهُ ۖ أَأَعْجَمِيٌّ وَعَرَبِيٌّ ۗ قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ۖ وَالَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ فِي آذَانِهِمْ وَقْرٌ وَهُوَ عَلَيْهِمْ عَمًى ۚ أُولَـٰئِكَ يُنَادَوْنَ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ﴿٤٤﴾
44. Na lau Tungekifanya kisomeke kwa lugha isiyokuwa ya Kiarabu wangelisema: Mbona hazikufasiliwa waziwazi Aayaat zake? Ah! Cha lugha ya kigeni na hali (Nabiy) ni Mwarabu!?[19] Sema: Hii (Qur-aan) kwa walioamini ni mwongozo na shifaa.[20] Na wale wasioamini, wana uziwi masikioni mwao nayo ni upofu kwao. Hao wanaitwa kutoka mahali mbali.
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَاخْتُلِفَ فِيهِ ۗ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۚ وَإِنَّهُمْ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مُرِيبٍ﴿٤٥﴾
45. Na kwa yakini Tulimpa Muwsaa Kitabu kisha kikahitilafiwa. Na lau si neno lilotangulia kutoka kwa Rabb wako, ingelihukumiwa baina yao. Na hakika wao bila shaka wamo katika shaka nayo (Qur-aan) yenye kuwatia wasiwasi.
مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا ۗ وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ﴿٤٦﴾
46. Yeyote yule atakayetenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na yeyote yule atakayefanya uovu, basi ni kwa hasara yake mwenyewe, na Rabb wako Si Mwenye Kudhulumu kamwe waja.
إِلَيْهِ يُرَدُّ عِلْمُ السَّاعَةِ ۚ وَمَا تَخْرُجُ مِن ثَمَرَاتٍ مِّنْ أَكْمَامِهَا وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ ۚ وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ أَيْنَ شُرَكَائِي قَالُوا آذَنَّاكَ مَا مِنَّا مِن شَهِيدٍ﴿٤٧﴾
47. Kwake Pekee unarudishwa ujuzi wa Saa (Qiyaamah). Na hayatoki matunda yoyote kutoka mafumbani mwake, na habebi mimba mwanamke yeyote na wala hazai isipokuwa kwa Ujuzi Wake. Na Siku Atakayowaita (Aseme): Wako wapi (hao mnaodai) washirika Wangu? Watasema: Tunakiri Kwako hapana miongoni mwetu anayeshuhudia.
وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَدْعُونَ مِن قَبْلُ ۖ وَظَنُّوا مَا لَهُم مِّن مَّحِيصٍ﴿٤٨﴾
48. Na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyaomba kabla na watayakinisha kuwa hawana mahali pa kukimbilia.
لَّا يَسْأَمُ الْإِنسَانُ مِن دُعَاءِ الْخَيْرِ وَإِن مَّسَّهُ الشَّرُّ فَيَئُوسٌ قَنُوطٌ﴿٤٩﴾
49. Binaadam hachoki kuomba duaa za kheri. Na inapomgusa shari, basi huwa mwenye kukosa tumainio lolote, mwenye kukata tamaa kabisa.
وَلَئِنْ أَذَقْنَاهُ رَحْمَةً مِّنَّا مِن بَعْدِ ضَرَّاءَ مَسَّتْهُ لَيَقُولَنَّ هَـٰذَا لِي وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً وَلَئِن رُّجِعْتُ إِلَىٰ رَبِّي إِنَّ لِي عِندَهُ لَلْحُسْنَىٰ ۚ فَلَنُنَبِّئَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِمَا عَمِلُوا وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنْ عَذَابٍ غَلِيظٍ﴿٥٠﴾
50. Na Tunapomuonjesha Rehma kutoka Kwetu baada ya dhara iliyomgusa, bila shaka husema: Haya nayastahiki mimi na sidhani kama Saa itasimama. Na kama nitarejeshwa kwa Rabb wangu hakika nitapata mazuri zaidi Kwake. Basi bila shaka Tutawabainishia wale waliokufuru yale waliyoyatenda, na bila shaka Tutawaonjesha adhabu nzito.
وَإِذَا أَنْعَمْنَا عَلَى الْإِنسَانِ أَعْرَضَ وَنَأَىٰ بِجَانِبِهِ وَإِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ فَذُو دُعَاءٍ عَرِيضٍ﴿٥١﴾
51. Na Tunapomneemesha binaadam hukengeuka na kujitenga upande. Na inapomgusa shari, basi mara huwa mwenye duaa refu refu.[21]
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن كَانَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ ثُمَّ كَفَرْتُم بِهِ مَنْ أَضَلُّ مِمَّنْ هُوَ فِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ﴿٥٢﴾
52. Sema: Je, mnaonaje ikiwa (Qur-aan) ni kutoka kwa Allaah, kisha mkaikufuru, ni nani aliyepotoka zaidi kuliko yule aliye katika upinzani wa mbali?
سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٥٣﴾
53. Tutawaonyesha Aayat (Ishara na Dalili) Zetu katika peo za mbali na katika nafsi zao, mpaka iwabainikie kwamba hii (Qur-aan) ni haki! Je, haitoshelezi Rabb wako kuwa Yeye Ni Shahidi juu ya kila kitu?[22]
أَلَا إِنَّهُمْ فِي مِرْيَةٍ مِّن لِّقَاءِ رَبِّهِمْ ۗ أَلَا إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ مُّحِيطٌ﴿٥٤﴾
54. Tanabahi! Hakika wao wamo katika shaka ya kukutana na Rabb wao. Tanabahi! Hakika Yeye Amekizunguka kila kitu.
[1] الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):
Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).
[2] Nyoyo Za Makafiri Zimefunikwa Na Masikio Yana Uziwi:
Rejea Al-An’aam (6:25), Al-Kahf (18:57). Rejea pia Al-Israa (17:45-46)
[3] Maana Iliyokusudiwa Ya Washirikina Kutoa Zakaah:
‘Aliy bin Abiy Twalhah amesimulia kutoka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba inamaanisha wale ambao hawashuhudii laa ilaaha illa-Allaah (hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah). Ni rai ya ‘Ikrimah pia na ni kama ilivyo katika Suwrah Ash-Shams (91:9-10), Al-A’laa (87:14-15), An-Naazi’aat (79:18). Kinachokusudiwa kuhusu Zakaah hapa ni twahara (utakaso) wa nafsi kutokana na khulqa, maadili, tabia na sifa zote mbaya. Na iliyomuhimu kabisa kutwaharisha, ni kuepuka shirki. Na Zakaah ya mali inaitwa hivyo kwa sababu inatakasa yaliyoharamishwa, na ni sababu ya kuongezeka kwake, kuibariki na kuifanya iwe ina manufaa mengi, na iwe ni tawfiyq ya kuitumia mali katika utiifu. Qataadah amesema: “Wanazuia Zakaah ya mali.” [Tafsiyr Ibn Kathiyr]
Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amesema: Ambao wanaabudu badala ya Allaah wale ambao hawana uwezo wa kunufaisha wala kudhuru, wala kufisha wala kuhuisha, wala kufufua, na wakazitia unajisi nafsi zao (kwa shirki), na wala hawakuzitakasa kwa kumpwekesha Rabb wao na kumtakasia ibaada, wala hawaswali, wala hawatoi Zakaah, hivyo hakuna ikhlaasw kwa Muumba kwa kumpwekesha wala Swalaah, wala kuwanufaisha watu kwa Zakaah na mengineyo ya kheri. Mbali ya hayo, Aakhirah wanaikanusha. Yaani: Hawaamini kufufuliwa wala hawaamini Jannah na moto. Hivyo basi khofu ilivyowaondoka nyoyoni mwao, wamethubutu kufanya waliyoyafanya ambayo yatakuja kuwadhuru Aakhirah. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[4] Kuumbwa Ardhi Na Viliomo:
Aayah hii namba (9) na inayofuatia namba (10) Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja Alivyoumba ardhi.
Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema Ameumba kwanza ardhi kwa sababu ndio msingi, na msingi unapaswa kujengwa kwanza kisha ndio paa kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) kwengineko katika Suwrah Al-Baqarah (2:29):
هُوَ الَّذِي خَلَقَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا ثُمَّ اسْتَوَىٰ إِلَى السَّمَاءِ فَسَوَّاهُنَّ سَبْع سَمَاوَاتٍ ۚ
“Yeye Ndiye Ambaye Amekuumbieni vyote vilivyomo ardhini kisha Kisha Akazikusudia mbingu (Kuziumba) na Akazifanya timilifu mbingu saba.” [Al-Baqarah (2:29)]
Na Hadiyth inayotaja kuwa uumbaji wa ardhi na yaliyomo yalikuwa katika siku sita ni kama ifuatayo:
وعن أبي هريرة رضي الله عنه ، قال : أخَذَ رسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم بِيَدِي فَقَالَ : (( خَلَقَ اللهُ التُّرْبَةَ يَومَ السَّبْتِ ، وَخَلَقَ فيها الجِبَالَ يَومَ الأحَدِ ، وَخَلَقَ الشَّجَرَ يَومَ الإثْنَينِ ، وَخَلَقَ المَكْرُوهَ يَومَ الثُّلاَثَاءِ ، وَخَلَقَ النُّورَ يَوْمَ الأربِعَاءِ ، وَبَثَّ فِيهَا الدَّوابَّ يَومَ الخَمِيسِ ، وَخَلَقَ آدَمَ صلى الله عليه وسلم ، بَعْدَ العَصْرِ مِنْ يَومِ الجُمُعَةِ في آخِرِ الخَلْقِ فِي آخِرِ سَاعَةٍ مِنَ النَّهَارِ فِيمَا بَيْنَ العَصْرِ إِلَى اللَّيْلِ )) . رواه مسلم .
Amesimulia Abuu Huraiyrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alinishika mkono na kuniambia: "Allaah Aliumba ardhi siku ya Jumamosi, na Akaumba ndani yake majabali Jumapili, na Akaumba miti Jumatatu, na Akaumba vitu vinavyo chukiza Jumanne, na Akaumba mwangaza Jumatano, na Akawatawanya wanyama katika ardhi siku ya Alkhamisi, na Akamuumba Aadam (عليه السّلام) baada ya Alasiri katika siku ya Ijumaa, katika viumbe Vyake vya mwisho, katika saa ya mwisho ya mchana, baina ya Alasiri na usiku." [Muslim]
[5] اسْتَوَى إِلَى السَّمَاءِ" Amezikusudia (Kuziumba Mbingu):
Rejea Al-Baqarah (2:29) kwenye maelezo bayana kuhusu maana yake.
[6] Takdiri (Uwezo, Ukadiriaji) Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Katika Uumbaji Wa Kila Kitu.
Rejea Yaasiyn (36:38) kwenye maelezo na faida tele.
[7] ‘Aad:
Ni kaumu ya Nabiy Huwd (عليه السّلام). Rejea Al-‘Ankabuwt (29:40) kwenye uchambuzi wa kaumu za nyumati za awali, maasi yao na adhabu zao.
[8] Thamuwd:
Ni kaumu ya Nabiy Swaalih (عليه السّلام). Rejea Al-‘Ankabuwt (29:40) kwenye uchambuzi wa kaumu za nyumati za awali, maasi yao na adhabu zao.
[9] Viungo Vitashuhudia Matendo Ya Binaadam:
Rejea Al-Israa (17:13-14), An-Nuwr (24:24), Yaasiyn (36:65).
[11] Ujahili Wa Makafiri Kutokutaka Kusikiliza Qur-aan Ilhali Waumini Wameamrishwa Waisikilize Wapate Kurehemwa:
Rejea Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrah Al-A’raaf (7:204) kwenye maelezo bayana.
[12] Kuthibitika Imara Katika Dini:
عن أبي عمر، وقيل: أبي عَمرة سفيان بن عبد الله رضي الله عنه قَالَ: قُلْتُ: يَا رَسُول الله، قُلْ لي في الإسْلامِ قَولًا لا أسْأَلُ عَنْهُ أَحَدًا غَيْرَكَ. قَالَ: ((قُلْ: آمَنْتُ بِاللهِ، ثُمَّ استَقِمْ)). رواه مسلم
Amesimulia Abuu ‘Umar na pia imesemwa anajulikana kama Abuu ‘Amrah Sufyaan bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه): Nilimwambia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Niambie neno katika Uislamu ambalo sitamuuliza yoyote zaidi yako. Akasema: “Sema: Nimemuamini Allaah, kisha uthibitike imara.” [Muslim]
[13] Waumini Wanabashiriwa Kheri Wanapotolewa Roho Zao:
Aayah hii (31) na zifuatazo hadi namba (32), zinataja Muumini anapotolewa roho yake, kuwa Malaika humbashiria mema, na kumliwaza azihuzunike, kwa kuwa atakayoyakuta huko Jannah, ni mazuri na neema tele, na raha tupu za kudumu, na mapokezi mema kutoka kwa Rabb Mkarimu Mwenye Kurehemu. Na bishara kama hizi zimetajwa katika Suwrah kadhaa za Qur-aan. Na imethibiti katika Qur-aan na Sunnah kwamba Muumin anapotolewa roho yake, hutolewa kwa wepesi kabisa na huwa katika raha na manukato, na Malaika wanaipokea roho kwa maamkizi na bishara njema. Rejea Al-Waaqi’ah (56:88-94) kwenye maelezo bayana yanayotofautisha kati ya roho ya Muumin na roho ya kafiri, pamoja na rejea mbalimbali. Na Hadiyth ifuatayo pia inatofautisha kati ya roho ya Muumini na roho ya kafiri pindi inapotolewa:
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: الْمَيِّتُ تَحْضُرُهُ الْمَلَائِكَةُ فَإِذَا كَانَ الرَّجُلُ صَالِحًا قَالُوا: اخْرُجِي أَيَّتُهَا النَّفْسُ الطَّيِّبَةُ كَانَتْ فِي الْجَسَدِ الطَّيِّبِ اخْرُجِي حَمِيدَةً وَأَبْشِرِي بِرَوْحٍ وَرَيْحَانٍ وَرَبٍّ غَيْرِ غَضْبَانَ فَلَا تَزَالُ يُقَالُ لَهَا ذَلِكَ حَتَّى تَخْرُجَ ثُمَّ يُعْرَجُ بِهَا إِلَى السَّمَاءِ فَيُفْتَحَ لَهَا فَيُقَالُ: مَنْ هَذَا؟ فَيَقُولُونَ: فُلَانٌ فَيُقَالُ: مَرْحَبًا بِالنَّفسِ الطّيبَة كَانَت فِي الْجَسَدِ الطَّيِّبِ ادْخُلِي حَمِيدَةً وَأَبْشِرِي بِرَوْحٍ وَرَيْحَانٍ وَرَبٍّ غَيْرِ غَضْبَانَ فَلَا تَزَالُ يُقَالُ لَهَا ذَلِكَ حَتَّى تَنْتَهِيَ إِلَى السَّمَاءِ الَّتِي فِيهَا اللَّهُ فَإِذَا كَانَ الرَّجُلُ السُّوءُ قَالَ: اخْرُجِي أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْخَبِيثَةُ كَانَتْ فِي الْجَسَدِ الْخَبِيثِ اخْرُجِي ذَمِيمَةً وَأَبْشِرِي بِحَمِيمٍ وَغَسَّاقٍ وَآخَرَ مِنْ شَكْلِهِ أَزْوَاجٌ فَمَا تَزَالُ يُقَالُ لَهَا ذَلِكَ حَتَّى تَخْرُجَ ثُمَّ يُعْرَجُ بِهَا إِلَى السَّمَاءِ فَيُفْتَحُ لَهَا فَيُقَالُ: مَنْ هَذَا؟ فَيُقَالُ: فُلَانٌ فَيُقَالُ: لَا مَرْحَبًا بِالنَّفْسِ الْخَبِيثَةِ كَانَتْ فِي الْجَسَدِ الْخَبِيثِ ارْجِعِي ذَمِيمَةً فَإِنَّهَا لَا تفتح لَهُ أَبْوَابُ السَّمَاءِ فَتُرْسَلُ مِنَ السَّمَاءِ ثُمَّ تَصِيرُ إِلَى الْقَبْر ". رَوَاهُ ابْن مَاجَه
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Malaika humjia mtu anayefariki, na ikiwa mtu ni mwema husema: Toka, ee nafsi nzuri, ambayo ilikuwa katika mwili mzuri! Toka ukiwa mwenye sifa njema, na pokea bishara njema kwa mapumziko ya raha na manukato, na Rabb Asiye na ghadhabu nawe. Ataendelea kuambiwa hayo mpaka roho itoke. Kisha itapandishwa juu mbinguni na atafunguliwa mlango. Malaika watauliza: Ni nani huyu? (Malaika wengine) watajibu: Ni fulani. Itaambiwa: Karibu ee nafsi njema, ambayo ilikuwa katika mwili mwema. Ingia ukiwa mwenye sifa njema, na pokea bishara njema kwa mapumziko ya raha na manukato na Rabb Asiye na ghadhabu nawe. Ataendelea kuambiwa hayo mpaka roho ifike mbinguni ambamo Yuko Allaah. Lakini inapokuwa mtu ni mbaya kinachosemwa ni: Toka ewe nafsi mbaya ambayo ilikuwa katika mwili mwovu! Toka ukiwa mwenye kulaumiwa na pokea habari mbaya ya maji yanayotokoka na usaha na mengineyo ya mfano wake na aina yake! Ataendelea kuambiwa hivyo hadi roho itoke. Kisha itapandishwa juu mbinguni na itafunguliwa mlango. Itaulizwa: Ni nani huyu? Itajibiwa: Ni fulani. Itaambiwa: Hakuna ukaribisho kwa nafsi mbaya iliyokuwa ndani ya mwili mwovu! Rudi ukiwa mwenye kulaumiwa kwani milango ya mbinguni haitafunguliwa kwa ajili yake. Kisha itatupwa kutoka mbinguni hadi kufika kaburini.” [Ibn Maajah na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Maajah (3456)]
Rejea pia Al-A’raaf (7:40) kwenye faida.
[14] Himizo La Daawah (Kulingania) Dini Na Kudhihirisha Unyenyekevu Kwa Watu:
Hakuna yoyote aliye na kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania Tawhiyd ya Allaah (Kupwekeshwa Allaah) na kuabudiwa Yeye Peke Yake, na yule anayesema: “Mimi ni katika Waislamu.” Yaani: Wanaofuata Amri za Allaah na Sharia Zake. Katika Aayah hii, kuna usisitizo wa kumlingania Allaah (سبحانه وتعالى) na kueleza fadhila za ‘Ulamaa wenye kulingania Kwake kwa baswiyrah (nuru za ilimu na utambuzi) kulingana na yale yaliyokuja kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). [Tafsiyr Al-Muyassar]
Rejea Suwrah Yuwsuf (12:108).
Rejea Alhidaaya.com
Hadiyth: Fadhila Za 'Ilmu Na 'Ulamaa - أَحاديثُ عَنْ فَضْلِ الْعِلْم وَالْعُلَمَاء
[15] Himizo La Kulipiza Wema Baada Ya Uovu:
Wema na uovu haulingani sawa. Yaani, kutenda amali njema na matendo ya utiifu kwa ajili ya Allaah, hakuwi sawa na amali ovu na matendo ya maasi ambayo Allaah Hayaridhii, na yanasababisha ghadhabu Zake. Na wala kuwatendea watu wema hakuwi sawa na kuwafanyia ubaya, si kwa matendo yenyewe, wala namna yake, wala malipo yake.
Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaamrisha ihsaan makhsusi ambayo ina taathira kubwa. Nayo ni kumtendea wema anayekutendea mabaya kama Anavyosema:
ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ
“Zuia (uovu) kwa ambalo ni zuri zaidi.”
Yaani: Mtu akikufanyia ubaya, kwa kauli au matendo, khasa akiwa ni mtu ambaye ana haki kwako, kama vile jamaa wa karibu (mwenye uhusiano wa damu), marafiki na kadhaalika, basi wewe rejesha hilo kwa kumfanyia ihsaan. Akikukata akakhasimikiana nawe, wewe wasiliana naye. Akikudhulumu, wewe msamehe. Akikusema vibaya kwa siri au mbele yako, basi wewe usimrudishie maneno mabaya, bali msamehe na amiliana naye kwa kauli laini (ya upole). Akikususa, na akakhasimikiana nawe asikusemeshe, basi wewe msemeze kwa maneno mazuri na uwe wa kwanza kumtolea Salaam. Utakapolipiza ubaya kwa wema, utapata faida kubwa. [Tafsiyr As-Sa’diy]
Rejea pia Kauli za Allaah (سبحانه وتعالى) zinazoamrisha kuvumilia, kuzuia ghadhabu, kusamehe watu na kadhaalika. Miongoni mwazo ni: Aal-‘Imraan (3:134), Ash-Shuwraa (42:43). Pia Hadiyth ifuatayo ina mafunzo kama hayo ya kulipiza uovu kwa wema:
وعن أَبي هريرة رضي الله عنه: أنَّ رَجُلاً ، قَالَ : يَا رسول الله ، إنّ لي قَرَابةً أصِلُهم وَيَقْطَعُونِي ، وَأُحْسِنُ إلَيْهِمْ وَيُسِيئُونَ إلَيَّ ، وَأحْلُمُ عَنهم وَيَجْهَلُونَ عَلَيَّ ! فَقَالَ : (( لَئِنْ كُنْتَ كَمَا قُلْتَ ، فَكأنَّمَا تُسِفُّهُمُ الْمَلَّ ، وَلاَ يَزَالُ مَعَكَ مِنَ اللهِ تَعَالَى ظَهيرٌ عَلَيْهِمْ مَا دُمْتَ عَلَى ذَلِكَ )) رواه مسلم .
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Mtu mmoja alisema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika mimi nina jamaa wa karibu nawaunga, lakini wao wananikata. Nawafanyia wema, lakini wao wananitendea uovu, nawavumilia na kusamehe, lakini wao wanaendelea kunifanyia vitimbi Akasema: "Ukiwa kama unavyosema, basi ni kama unawalisha jivu la moto. Msaada wa Allaah hautaacha kuwa pamoja nawe maadamu utadumu juu ya hilo." [Muslim]
[16] Subira Katika Maudhi Yanampatia Mtu Hadhi Kubwa Mbele Ya Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا
“Na hayapati hayo isipokuwa wale waliovuta subira.”
Hakuna atakayeweza kupata sifa nzuri hii, isipokuwa wenye kuvuta subira na wanaovumilia katika wasiyoyaridhia, na kujilazimisha yale ambayo Anayapenda Allaah. Kwani nafsi za watu zimeumbwa na tabia ya kulipiza maovu kwa maovu na kutokusamehe. Basi itakuwaje mtu kulipa uovu kwa ihsaan?
Lakini mtu akiwa mvumilivu na akatii amri za Rabb wake, akatambua thawabu tele ambazo zinasababishwa na subira hiyo, akafahamu kuwa kulipizia maovu hakumfaidii hata kidogo, bali kutamzidishia ubaya nao, na kuzidisha uadui. Na kwamba kumtendea ihsaan hakumaanishi kuwa mtu anajidhalilisha na kushusha daraja lake, bali ni kunyenyekea kwa Allaah Ambaye Atampandisha daraja, na mambo yatakuwa mepesi kwake, atafanya kwa maridhawa na atapata furaha ndani yake. [Tafsiyr As-Sa’diy]
وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ﴿٣٥﴾
“Na hayapati hayo isipokuwa mwenye fungu adhimu.”
Yaani: Kwa sababu ni sifa ya nadra ya wanaadam, na ambayo mtu hupandishwa daraja la juu duniani na Aakhirah. Hivo basi ni katika akhlaqi (sifa) njema kabisa. [Tafsiyr As-Sa’diy]
Na subira katika Qur-aan imetajwa katika Aayah nyingi mno. Na subira zina matawi yake, na daraja zake, na thawabu zake ni tele.
Rejea kiungo kifuatacho chenye Makala ya: Swabrun Jamiyl (Subira Njema) iliyojaa faida tele, na rejea mbali mbali za Qur-aan na Hadiyth:
[17] Haramisho La Kusujudia Jua Au Mwezi Kwani Ni Vitu Vilivyoumbwa Na Allaah (سبحانه وتعالى):
Imaam Muhammad Ibn Al-Wahhaab (رحمه الله) ameinukuu Aayah hii akasema:
النَّبِيَّ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) ظَهَرَ عَلَى أُنَاسٍ مُتَفَرِّقِينَ فِي عِبَادَاتِهِمْ، مِنْهُمْ مَنْ يَعْبُدُ الْمَلائِكَةَ، وَمِنْهُمْ مَنْ يَعْبُدُ الأَنْبِيَاءَ وَالصَّالِحِينَ، وَمِنْهُمْ مَنْ يَعْبُدُ الأَشْجَارَ وَالأَحْجَارَ، وَمِنْهُمْ مَنْ يَعْبُدُ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ، وَقَاتَلَهُمْ رَسُولُ اللهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) وَلَمْ يُفَرِّقْ بَيْنَهُمْ.
“Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuta watu wakitofautiana katika ibaada zao. Kuna waliokuwa wanaabudu Malaika, wanaoabudu Manabii na Swalihina (waja wema), wanaoabudu miti na mawe, na wanaoabudu jua na mwezi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akapigana nao na wala hakutofautisha baina yao (katika walivyoviabudu).” [Al-Qawaaid Al-Arba’ – Imaam Muhammad Ibn Al-Wahhaab]
Na Imaam Ibn Kathiyr amesema:
Hapa Allaah (سبحانه وتعالى) Anakumbusha Uwezo Wake mkubwa, na kwamba Yeye Ndiye Ambaye Hana wa kulinganishwa Naye, na ni Muweza wa kila kitu. Kauli Yake hiyo inamaanisha kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ameumba usiku na giza lake, na mchana kwa nuru yake, navyo vinafuatana bila kusimama. Na Akaliumba jua kwa nuru yake inayong'aa, na mwezi kwa nuru yake. Na Akakadiria vituo vyake katika falaki (angani), Akavipa njia tofauti mbinguni, ili kwa kutofautiana kwa mienendo yao mwanaadam, apate kujua nyakati za usiku na mchana, za wiki, za miezi na za miaka, na nyakati zinazohusiana na haki za watu, ibaada na miamala mbalimbali. Zaidi ya hayo, kwa sababu jua na mwezi ni vitu vilivyoumbwa kwa uzuri kabisa vinavyoweza kuonekana katika anga za juu na za chini, Allaah (سبحانه وتعالى) Anazindusha kwamba hivyo ni vitumwa kati ya watumwa Wake na viko chini ya Ufalme Wake na Udhibiti Wake. Basi watu wasivisujudie, bali wamsujudie Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Aliyeviumba. Wala msimshirikishe, kwani kumwabudu kwenu Yeye, hakutakunufaisheni ikiwa mtaabudu vinginevyo, kwani Yeye Hasamehi kushirikishwa Naye. Ndio maana Akasema:
فَإِنِ اسْتَكْبَرُوا
“Lakini wakitakabari .”
[Tafsiyr Ibn Kathiyr]
[18] Mfano Wa Ardhi Iliyokufa (Kame), Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaihuisha Kwa Mvua, Ni Mfano Wa Kuwahuisha Watu Kutoka Makaburini Mwao Siku Ya Qiyaamah:
Rejea Ar-Ruwm (30:50) kwenye maelezo bayana na rejea mbalimbali.
[19] Hata Kama Ingeteremshwa Qur-aan Kwa Lugha Ya Kigeni Washirikina Wasingeliamini:
Rejea Ash-Shu’araa (26:198-199).
[20] Qur-aan Ni Shifaa (Poza, Tiba), Mwongozo, Mawaidha, Rehma:
Katika Aayah hii ya Suwrah Fusw-Swilat (41:44), Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema kuwa Qur-aan ni mwongozo na rehma. Ama wasioiamini, wao wana uziwi masikioni mwao, nayo ni upofu kwao.
Na katika Suwrah Yuwnus, Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema Qur-aan ni mawaidha, shifaa, mwongozo na rehma:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٥٧﴾ قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ﴿٥٨﴾
“Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rehma kwa Waumini. Sema: Kwa Fadhila za Allaah na kwa Rehma Yake basi kwa hayo wafurahi. Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya.” [Yuwnus (10:57-58)]
Rejea katika Suwrah hiyo Yuwnus (10:57-58) kwenye faida nyenginezo.
Ama kwenye Suwrah Al-Israa, Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema Qur-aan ni shifaa na rehma kwa Waumini lakini ni khasara kwa kafiri:
وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ۙ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴿٨٢﴾
“Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rehmakwa Waumini na wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa khasara.” [Al-Israa (17:82)]
Rejea katika Suwrah hiyo ya Al-Israa (17:82) kwenye faida nyenginezo:
Maudhui ya Qur-aan kuwa ni shifaa (poza, tiba), mawaidha, mwongozo na rehma kwa watu, ni maudhui pana mno, na rejea zake katika Qur-aan na Sunnah ni nyingi mno! Lakini uchambuzi wake kwa kifupi ni kama ifuatavyo:
(i) Qur-aan Ni Mawaidha:
Rejea Aayah zilizotajwa juu za Suwrah Yuwnus (10:57-58).
Kadhaalika, Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
هَـٰذَا بَيَانٌ لِّلنَّاسِ وَهُدًى وَمَوْعِظَةٌ لِّلْمُتَّقِينَ ﴿١٣٨﴾
“Hii (Qur-aan) ni ubainisho kwa watu na mwongozo na mawaidha kwa wenye taqwa.” [Aal-‘Imraan (3:138)]
Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَمَا أَنزَلَ عَلَيْكُم مِّنَ الْكِتَابِ وَالْحِكْمَةِ يَعِظُكُم بِهِ ۚ
“Na kumbukeni Neema za Allaah juu yenu na Aliyokuteremshieni katika Kitabu na Hikmah (Sunnah) Anakuwaidhini kwacho.” [Al-Baqarah (2:231)]
Rejea pia Huwd (11:120), An-Nuwr (24:34).
(ii) Qur-aan Ni Shifaa (Poza, Tiba):
Qur-aan ni shifaa ya kila aina ya maradhi iwe ya miili au ya kiroho, au maradhi ya moyo yaliyokusudiwa katika Qur-aan.
a) Qur-aan Ni Shifaa Ya Maradhi Ya Miili:
Imethibiti katika simulizi mbalimbali kwamba Swahaba walikuwa wakitumia Qur-aan kama ruqyah (kinga na tiba) ya kimiili. Na pia dalili kubwa ni kisa katika Hadiyth ifuatayo, cha kumsomea mkuu wa kijiji aliyepatwa na sumu, akasomewa Suwrah Al-Faatihah akapona:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: كُنَّا فِي مَسِيرٍ لَنَا فَنَزَلْنَا فَجَاءَتْ جَارِيَةٌ فَقَالَتْ: "إِنَّ سَيِّدَ الْحَيِّ سَلِيمٌ وَإِنَّ نَفَرَنَا غَيْبٌ فَهَلْ مِنْكُمْ رَاقٍ؟" فَقَامَ مَعَهَا رَجُلٌ مَا كُنَّا نَأْبُنُهُ بِرُقْيَةٍ، فَرَقَاهُ فَبَرَأَ فَأَمَرَ لَهُ بِثَلاَثِينَ شَاةً وَسَقَانَا لَبَنًا فَلَمَّا رَجَعَ قُلْنَا لَهُ: "أَكُنْتَ تُحْسِنُ رُقْيَةً أَوْ كُنْتَ تَرْقِي؟" قَالَ: "لاَ مَا رَقَيْتُ إلاَّ بِأُمِّ الْكِتَابِ." قُلْنَا: "لاَ تُحْدِثُوا شَيْئًا حَتَّى نَأْتِيَ أَوْ نَسْأَلَ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)." فَلَمَّا قَدِمْنَا الْمَدِينَةَ ذَكَرْنَاهُ لِلنَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فَقَالَ: ((وَمَا كَانَ يُدْرِيهِ أَنَّهَا رُقْيَةٌ؟ اقْسِمُوا وَاضْرِبُوا لِي بِسَهْمٍ)).
Amesimulia Abuu Sa'iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Tulikuwa katika safari tukateremka mahali, akaja kijakazi akasema: Bwana wetu ametafunwa na nge na wanaume wetu hawapo, je, yupo kati yenu tabibu? Akasimama pamoja naye mtu mmoja ambaye hatukudhania kuwa anajua ruqyah (utabibu). Akamtibu kwa ruqyah akapona. Akampa kondoo thelathini na akatupa maziwa tunywe (kama ni malipo). Aliporudi tukamwambia: Je, ulikuwa kweli unajua kutibu kwa ruqyah, au ulikuwa unabahatisha tu? Akasema: Hapana, bali nimemsomea Ummul-Kitaab (Suwrah Al-Faatihah). Tukasema: Tusiseme kitu hadi tumfikie au tumuulize Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Tulipofika Madiynah, tulimwelezea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Alijuaje kuwa (Al-Faatihah) ni ruqyah? Gawaneni na mnitolee sehemu (ya kondoo.” [Al-Bukhaariy]
b) Qur-aan ni Ruqyah Na Shifaa Ya Sihri (Uchawi), Uhasidi, Jicho Baya, Kukumbwa Na Mashaytwaan Na Majini Na Kila Aina Za Shari:
Suwrah Al-Baqarah:
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((لَا تَجْعَلُوا بُيُوتَكُمْ مَقَابِرَ إِنَّ الشَّيْطَانَ يَنْفِرُ مِنَ الْبَيْتِ الَّذِي تُقْرَأُ فِيهِ سُورَةُ الْبَقَرَةِ)) رواه مسلم
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Msifanye nyumba zenu makaburi. Kwa hakika shaytwaan haingii nyumba ambayo husomwa humo Suwratul-Baqarah.” [At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan Swahiyh] na katika Riwaayah ya Muslim, Hadiyth (780):
“Shaytwaan anakimbia nyumba inayosomwa ndani yake Suwratul-Baqarah.”.
Aayatul-Kursiy:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ وَكَّلَنِي رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم بِحِفْظِ زَكَاةِ رَمَضَانَ، فَأَتَانِي آتٍ، فَجَعَلَ يَحْثُو مِنَ الطَّعَامِ، فَأَخَذْتُهُ فَقُلْتُ: لأَرْفَعَنَّكَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم. فَذَكَرَ الْحَدِيثَ فَقَالَ: إِذَا أَوَيْتَ إِلَى فِرَاشِكَ فَاقْرَأْ آيَةَ الْكُرْسِيِّ لَنْ يَزَالَ عَلَيْكَ مِنَ اللَّهِ حَافِظٌ، وَلاَ يَقْرَبُكَ شَيْطَانٌ حَتَّى تُصْبِحَ. فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم: ((صَدَقَكَ وَهْوَ كَذُوبٌ، ذَاكَ شَيْطَانٌ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniwakilisha kuhifadhi Zakaah ya Ramadhwaan (Zakaatul-Fitwr). Akaja mtu akaanza kuteka chakula (cha Zakaah) kwa mikono miwili. Nikamkamata na kumwambia: Nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Kisha Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) akahadithia yote na akaongezea: Huyo (mwizi) akasema kuniambia: Utakapoingia kitandani kulala, soma Aayatul-Kursiy kwani mlinzi kutoka kwa Allaah atakulinda, na shaytwaan hatokukaribia mpaka asubuhi. Hapo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Amekwambia ukweli japokuwa yeye ni muongo, naye (huyo mwizi) ni shaytwaan.” [Al-Bukhaariy]
Aayah mbili za mwisho wa Suwrah Al-Baqarah:
عن أَبِي مَسْعُودٍ الأَنْصَارِيِّ، قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم: ((الآيَتَانِ مِنْ آخِرِ سُورَةِ الْبَقَرَةِ مَنْ قَرَأَ بِهِمَا فِي لَيْلَةٍ كَفَتَاهُ))
Amesimulia Abuu Mas‘uwd Al-Answaariyy (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesoma usiku Aayah mbili za mwisho wa Suwratul-Baqarah zitamtosheleza.” Yaani: Zinamtosheleza kumkinga na kila baya na lenye kumdhuru. [Al-Bukhaariy na Muslim]
Suwrah Al-Ikhlaasw (112) na Al-Mu’awwidhataan (kinga mbili) yaani Suwrah Al-Falaq (113) na Suwrah An-Naas (114).
Hizi ni katika Adhkaar za asubuhi na jioni kujikinga na kila shari. Na Hadiyth ifuatayo imethibiti:
عَنْ مُعَاذِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ خُبَيْبٍ، عَنْ أَبِيهِ، قَالَ: خَرَجْنَا فِي لَيْلَةٍ مَطِيرَةٍ وَظُلْمَةٍ شَدِيدَةٍ نَطْلُبُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يُصَلِّي لَنَا. قَالَ: فَأَدْرَكْتُهُ فَقَالَ: ((قُلْ)). فَلَمْ أَقُلْ شَيْئًا ثُمَّ قَالَ: ((قُلْ)) فَلَمْ أَقُلْ شَيْئًا. قَالَ: ((قُلْ)) قُلْتُ: مَا أَقُولُ؟ قَالَ: ((قُلْ هوَ اللَّهُ أَحَدٌ... وَالْمُعَوِّذَتَيْنِ حِينَ تُمْسِي وَتُصْبِحُ ثَلاَثَ مَرَّاتٍ تَكْفِيكَ مِنْ كُلِّ شَيْءٍ)). قَالَ أَبُو عِيسَى وَهَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ.
Amesimulia Mu’aadh bin ‘Abdillaah bin Khubayb (رضي الله عنه): Kutoka kwa baba yake kwamba: Tulitoka usiku mmoja wa kiza kinene na mvua tukimtafuta Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) atuswalishe Swalaah. Akasema: Nikakutana naye, kisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: قُلْ “Sema.” Lakini sikusema kitu. Kisha akasema: قُلْ “Sema.” Lakini sikusema kitu. Kisha akasema: قُلْ “Sema.” Nikasema: “Niseme nini?” Akasema:
قُلْ هوَ اللَّهُ أَحَدٌ
“Sema: Yeye Allaah Ni Mmoja Pekee.” [Suwrah Ikhlaasw namba (112)] na Al-Mu’awwidhatayni [Al-Falaq na An-Naas (113-114)] Unapoingia jioni na unapoamka asubuhi mara tatu zitakutosheleza na kila kitu.” [Hadiyth Hasan Swahiyh, Taz. Swahiyh At-Tirmidhiyy (3575), Swahiyh Abiy Daawuwd (5082).
Na pia imesimuliwa kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alirogwa akawa anaumwa, akateremshiwa Suwrah mbili hizo.
c) Qur-aan Inatibu Maradhi Ya Nyoyo: Ambayo Ni Kufru, Shirki, Unafiki, Shaka, Matamanio, Ukaidi Wa Kukubali Haqq, Maasi Na Kila Aina Ya Maovu:
Nyoyo Zenye Maradhi: Rejea Suwrah Muhammad (47:20) kwenye maelezo na rejea mbalimbali.
Moyo Uliopofuka: Rejea pia Al-Hajj (22:46) kwenye maelezo bayana.
Kinyume chake ni Moyo Uliosalimika, rejea Ash-Shu’araa (26:88-89) kwenye ufafanuzi na maelezo bayana.
Na pia rejea Ar-Ra’d (13:28) Anaposema Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa kwa Dhikru-Allaah nyoyo hutulia! Rejea pia nukta namba (iii) kwenye maelezo kuhusu Swahaba mtukufu ‘Umar Bin Al Khattwaab (رضي الله عنه) aliyeondolewa shirki, kufru, maasi kwa kusikiliza Qur-aan.
Rejea pia Alhidaaya.com kwenye makala zifuatazo:
Ruqyah: Kinga Na Tiba Katika Shariy'ah
Du’aa Za Ruqyah (Kinga) Faida Na Sharh Zake
(iii) Qur-aan Ni Mwongozo:
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ وَيُبَشِّرُ الْمُؤْمِنِينَ الَّذِينَ يَعْمَلُونَ الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ أَجْرًا كَبِيرًا ﴿٩﴾
“Hakika hii Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka kabisa, na inawabashiria Waumini wanaotenda mema kwamba watapata ujira mkubwa.” [Al-Israa (17:9)]
Imesimuliwa katika Siyrah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba Swahaba mtukufu ‘Umar Bin Al-Khattwaab alisilimu kwa kusikiza Aayah za mwanzo za Suwrah Twaahaa (20:1-8). Hivyo Qur-aan ikamuondoshea viza vya kufru, shirki na maasi na ikamuingiza katika Nuru ya Uislamu. Rejea pia Suwrah Ibraahiym (14:1) kwenye maelezo kuhusu kutolewa kutoka katika viza na kuingia katika nuru.
(iv) Qur-aan Ni Rehma:
Allaah (سبحانه وتعالى) Anatuamrisha tuwe tunaisikiliza Qur-aan inaposomwa ili Atuteremshie Rehma Yake:
وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٢٠٤﴾
“Na inaposomwa Qur-aan, basi isikilizeni kwa makini na bakieni kimya (mzingatie) ili mpate kurehemewa.” [Al-A’raaf (7:204)]
Rejea katika Aayah hiyo ya Suwrah Al-A’raaf (7:204) kwenye Tafsiyr yake.
Basi kama ilivyotangulia kutajwa juu, kuwa maudhui hii ni pana mno, lakini hayo ni machache mno miongoni mwa mengi. Na hapa si mahala pake pa kuorodheshwa yote.
[22] Aayaat Za Allaah Katika Peo Za Mbali (Angani, Ulimwenguni) Na Katika Nafsi Kudhihirisha Haqq:
Tutawaonyesha, hawa wakanushaji, Aayaat (Ishara na Dalili) Zetu za kuteka miji na kupata nguvu Uislamu katika majimbo mbalimbali, na juu ya dini nyingine, na maeneo ya mbingu na ardhi, na katika matukio makubwa Anayoyaleta Allaah (سبحانه وتعالى) humo, na ndani ya nafsi zao. Na vile vilivyomo humo miongoni mwa alama za kuvutia za utendakazi wa Allaah (سبحانه وتعالى) na maajabu ya utengenezaji Wake, (Tutawaonyesha hayo yote) mpaka iwafunukie nyinyi (makafiri), ufunuzi usiyokubali shaka yoyote, kwamba Qur-aan ndiyo haki iliyoletwa kwa njia ya Wahy kutoka kwa Rabb wa viumbe wote. Je hauwatoshi wao Ushahidi wa Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa ni dalili ya kuwa Qur-aan ni haki na kuwa aliyekuja nayo ni mkweli? Kwani Allaah (سبحانه وتعالى) Ameishuhudilia kwa kuisadikisha, na Yeye ni Shahidi wa kila kitu, na hakuna kitu chochote chenye kutolea ushahidi kuliko ushahidi wa Allaah (سبحانه وتعالى) . [Tafsiyr Al-Muyassar]
Rejea Yuwsuf (12:105), Adh-Dhaariyaat (51:20).