054 - Al-Qamar
الْقَمَر
054-Al-Qamar
054-Al-Qamar: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَرُ ﴿١﴾
1. Saa imekaribia na mwezi umepasuka.[1]
وَإِن يَرَوْا آيَةً يُعْرِضُوا وَيَقُولُوا سِحْرٌ مُّسْتَمِرٌّ ﴿٢﴾
2. Na wanapoona Aayah (Ishara, Dalili) hukengeuka na husema: Sihiri ya siku zote, tumeizoea.[2]
وَكَذَّبُوا وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَكُلُّ أَمْرٍ مُّسْتَقِرٌّ ﴿٣﴾
3. Na wakakadhibisha (haki), na wakafuata hawaa zao, na kila jambo litafikia ukomo.
وَلَقَدْ جَاءَهُم مِّنَ الْأَنبَاءِ مَا فِيهِ مُزْدَجَرٌ ﴿٤﴾
4. Na kwa yakini imekwishawajia kati ya habari muhimu ambayo ndani yake kuna makemeo makali.
حِكْمَةٌ بَالِغَةٌ ۖ فَمَا تُغْنِ النُّذُرُ ﴿٥﴾
5. Ni hikmah iliyofikia upeo timilifu kabisa lakini hayafai kitu maonyo.[3]
فَتَوَلَّ عَنْهُمْ ۘ يَوْمَ يَدْعُ الدَّاعِ إِلَىٰ شَيْءٍ نُّكُرٍ ﴿٦﴾
6. Basi jitenge nao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Siku atakayoita muitaji kuliendea jambo baya mno la kuogofya.
خُشَّعًا أَبْصَارُهُمْ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ كَأَنَّهُمْ جَرَادٌ مُّنتَشِرٌ ﴿٧﴾
7. Macho yao yakiwa dhalili, watatoka katika makaburi kama kwamba wao ni nzige waliosambaa.
مُّهْطِعِينَ إِلَى الدَّاعِ ۖ يَقُولُ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا يَوْمٌ عَسِرٌ ﴿٨﴾
8. Wakikimbia mbio kwenda kwa muitaji huku wamebenua shingo zao. Makafiri watasema: Hii ni siku ngumu mno!
كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ فَكَذَّبُوا عَبْدَنَا وَقَالُوا مَجْنُونٌ وَازْدُجِرَ ﴿٩﴾
9. Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuwh, wakamkadhibisha Mja Wetu, wakasema: Majnuni. Na akakaripiwa.[4]
فَدَعَا رَبَّهُ أَنِّي مَغْلُوبٌ فَانتَصِرْ ﴿١٠﴾
10. Basi akamwita Rabb wake: Hakika mimi nimeshindwa nguvu basi Nusuru.
فَفَتَحْنَا أَبْوَابَ السَّمَاءِ بِمَاءٍ مُّنْهَمِرٍ ﴿١١﴾
11. Tukafungua milango ya mbingu kwa maji yanayofoka na kumiminika kwa nguvu.
وَفَجَّرْنَا الْأَرْضَ عُيُونًا فَالْتَقَى الْمَاءُ عَلَىٰ أَمْرٍ قَدْ قُدِرَ ﴿١٢﴾
12. Na Tukazibubujua ardhi chemchemu, basi yakakutana maji kwa amri iliyokwisha kadiriwa.
وَحَمَلْنَاهُ عَلَىٰ ذَاتِ أَلْوَاحٍ وَدُسُرٍ ﴿١٣﴾
13. Na Tukambeba kwenye ile (jahazi) yenye mbao na misumari.
تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا جَزَاءً لِّمَن كَانَ كُفِرَ ﴿١٤﴾
14. Inatembea chini ya Macho Yetu, ni jazaa kwa yule aliyekuwa amekanushwa.
وَلَقَد تَّرَكْنَاهَا آيَةً فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٥﴾
15. Na kwa yakini Tumeiacha iwe ni Aayah (Ishara, Mazingatio). Je basi yuko yeyote mwenye kuwaidhika?
فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿١٦﴾
16. Basi vipi ilikuwa Adhabu Yangu na Maonyo Yangu?
وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٧﴾
17. Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan ili ipate kusomwa, kuhifadhiwa na kufahamika.[5] Basi je, yuko yeyote mwenye kuwaidhika?
كَذَّبَتْ عَادٌ فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿١٨﴾
18. Kina ‘Aad walikadhibisha. Basi vipi ilikuwa Adhabu Yangu na Maonyo Yangu?
إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي يَوْمِ نَحْسٍ مُّسْتَمِرٍّ ﴿١٩﴾
19. Hakika Sisi Tuliwapelekea upepo wa adhabu; wa sauti kali na baridi kali katika siku ya nuhsi yenye kuendelea mfululizo.
تَنزِعُ النَّاسَ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ مُّنقَعِرٍ ﴿٢٠﴾
20. Unawang’oa watu kama kwamba ni vigogo vya mtende vilong’olewa.
فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٢١﴾
21. Basi vipi ilikuwa Adhabu Yangu na Maonyo Yangu?
وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٢٢﴾
22. Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan ili ipate kusomwa, kuhifadhiwa na kufahamika. Basi je, yuko yeyote mwenye kuwaidhika?
كَذَّبَتْ ثَمُودُ بِالنُّذُرِ ﴿٢٣﴾
23. Kina Thamuwd walikadhibisha maonyo.
فَقَالُوا أَبَشَرًا مِّنَّا وَاحِدًا نَّتَّبِعُهُ إِنَّا إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ ﴿٢٤﴾
24. Wakasema: Ah! Tumfuate binaadam mmoja miongoni mwetu? Hakika hapo sisi tutakuwa katika upotofu na wazimu.
أَأُلْقِيَ الذِّكْرُ عَلَيْهِ مِن بَيْنِنَا بَلْ هُوَ كَذَّابٌ أَشِرٌ ﴿٢٥﴾
25. Ah! Ameteremshiwa yeye tu ukumbusho baina yetu? Bali yeye ni muongo mkubwa, mfidhuli mwenye kutakabari mno.
سَيَعْلَمُونَ غَدًا مَّنِ الْكَذَّابُ الْأَشِرُ ﴿٢٦﴾
26. Watakuja kujua kesho nani muongo mkubwa mfidhuli mwenye kutakabari mno.
إِنَّا مُرْسِلُو النَّاقَةِ فِتْنَةً لَّهُمْ فَارْتَقِبْهُمْ وَاصْطَبِرْ ﴿٢٧﴾
27. Hakika Sisi Tutawapelekea ngamia jike awe jaribio kwao. Basi (ee Nabiy Swaalih عليه السلام) watazame na vuta subira.
وَنَبِّئْهُمْ أَنَّ الْمَاءَ قِسْمَةٌ بَيْنَهُمْ ۖ كُلُّ شِرْبٍ مُّحْتَضَرٌ ﴿٢٨﴾
28. Na wajulishe kwamba maji ni mgawanyo baina yao (ngamia na wao), kila sehemu ya maji itahudhuriwa (kwa zamu).
فَنَادَوْا صَاحِبَهُمْ فَتَعَاطَىٰ فَعَقَرَ ﴿٢٩﴾
29. Wakamwita swahibu wao, akakamata (upanga) akaua (ngamia).
فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٣٠﴾
30. Basi vipi ilikuwa Adhabu Yangu na Maonyo Yangu?
إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ صَيْحَةً وَاحِدَةً فَكَانُوا كَهَشِيمِ الْمُحْتَظِرِ ﴿٣١﴾
31. Hakika Sisi Tuliwapelekea ukelele angamizi mmoja tu, basi wakawa kama mabuwa makavu ya mtengenezaji zizi.
وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٣٢﴾
32. Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan ili ipate kusomwa, kuhifadhiwa na kufahamika. Basi je, yuko yeyote mwenye kuwaidhika?
كَذَّبَتْ قَوْمُ لُوطٍ بِالنُّذُرِ ﴿٣٣﴾
33. Kaumu ya Luutw walikadhibisha maonyo.
إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ حَاصِبًا إِلَّا آلَ لُوطٍ ۖ نَّجَّيْنَاهُم بِسَحَرٍ ﴿٣٤﴾
34. Hakika Sisi Tuliwapelekea tufani ya mawe isipokuwa familia ya Luutw. Tuliwaokoa nyakati kabla ya Alfajiri.
نِّعْمَةً مِّنْ عِندِنَا ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي مَن شَكَرَ ﴿٣٥﴾
35. Neema kutoka Kwetu. Hivyo ndivyo Tunavyomlipa ambaye ameshukuru.
وَلَقَدْ أَنذَرَهُم بَطْشَتَنَا فَتَمَارَوْا بِالنُّذُرِ ﴿٣٦﴾
36. Na kwa yakini aliwatahadharisha Nguvu Zetu za kuadhibu lakini wakatilia shaka maonyo.
وَلَقَدْ رَاوَدُوهُ عَن ضَيْفِهِ فَطَمَسْنَا أَعْيُنَهُمْ فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٣٧﴾
37. Na kwa yakini walimshawishi awape wageni wake, Nasi Tukawapofoa macho yao. Basi onjeni Adhabu Yangu na Maonyo Yangu.
وَلَقَدْ صَبَّحَهُم بُكْرَةً عَذَابٌ مُّسْتَقِرٌّ ﴿٣٨﴾
38. Na kwa yakini iliwafikia asubuhi mapema adhabu ya kuendelea.
فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٣٩﴾
39. Basi onjeni Adhabu Yangu na Maonyo Yangu.
وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٤٠﴾
40. Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan ili ipate kusomwa, kuhifadhiwa na kufahamika. Basi je, yuko yeyote mwenye kuwaidhika?
وَلَقَدْ جَاءَ آلَ فِرْعَوْنَ النُّذُرُ ﴿٤١﴾
41. Na kwa yakini watu wa Firawni walifikiwa na maonyo mengi.
كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كُلِّهَا فَأَخَذْنَاهُمْ أَخْذَ عَزِيزٍ مُّقْتَدِرٍ ﴿٤٢﴾
42. Walikadhibisha Aayaat (Ishara, Miujiza, Dalili) Zetu zote, Tukawakamata mkamato wa Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Uwezo wa juu kabisa.
أَكُفَّارُكُمْ خَيْرٌ مِّنْ أُولَـٰئِكُمْ أَمْ لَكُم بَرَاءَةٌ فِي الزُّبُرِ ﴿٤٣﴾
43. Je, makafiri wenu (enyi Maquraysh) ni bora kuliko hao (ummah) wa awali? Au mna msamaha katika Maandiko Matukufu?
أَمْ يَقُولُونَ نَحْنُ جَمِيعٌ مُّنتَصِرٌ ﴿٤٤﴾
44. Au wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu.
سَيُهْزَمُ الْجَمْعُ وَيُوَلُّونَ الدُّبُرَ ﴿٤٥﴾
45. Utashindwa mjumuiko wao na watageuka nyuma (watimue mbio).
بَلِ السَّاعَةُ مَوْعِدُهُمْ وَالسَّاعَةُ أَدْهَىٰ وَأَمَرُّ ﴿٤٦﴾
46. Bali Saa ndio miadi yao, na Saa ni janga kubwa na chungu zaidi.
إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ ﴿٤٧﴾
47. Hakika wahalifu wamo katika upotofu na wazimu.[6]
يَوْمَ يُسْحَبُونَ فِي النَّارِ عَلَىٰ وُجُوهِهِمْ ذُوقُوا مَسَّ سَقَرَ ﴿٤٨﴾
48. Siku watakayoburutwa motoni kifudifudi: Onjeni mguso wa moto mkali mno.
إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ ﴿٤٩﴾
49. Hakika Sisi Tumekiumba kila kitu kwa Qadar[7] (makadirio, majaaliwa).
وَمَا أَمْرُنَا إِلَّا وَاحِدَةٌ كَلَمْحٍ بِالْبَصَرِ ﴿٥٠﴾
50. Na Amri Yetu haiwi ila ni moja tu, kama upepeso wa jicho.
وَلَقَدْ أَهْلَكْنَا أَشْيَاعَكُمْ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٥١﴾
51. Na kwa yakini Tumewaangamiza wenzenu. Je, basi yuko yeyote mwenye kuwaidhika?
وَكُلُّ شَيْءٍ فَعَلُوهُ فِي الزُّبُرِ ﴿٥٢﴾
52. Na kila kitu wakifanyacho kimo katika madaftari ya rekodi.
وَكُلُّ صَغِيرٍ وَكَبِيرٍ مُّسْتَطَرٌ ﴿٥٣﴾
53. Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa[8]
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَهَرٍ ﴿٥٤﴾
54. Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na mito.
فِي مَقْعَدِ صِدْقٍ عِندَ مَلِيكٍ مُّقْتَدِرٍ ﴿٥٥﴾
55. Katika makao ya haki kwa Mfalme Mwenye Nguvu zote, Mwenye Uwezo wa juu kabisa.
[1] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah:
Bonyeza kiungo kifuatacho:
054-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Qamar Aayah 1-2: اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَرُ
[2] Makafiri Kutokuamini Aayaat (Na Ishara, Dalili) Za Allaah Na Kuzipachika Sifa Ovu, Na Kutokumuamini Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
Rejea Al-Furqaan (25:4) kwenye uchambuzi bayana na rejea mbalimbali za maudhui hii ya washirikina kumpachika Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) sifa kadhaa ovu na kuipachika Qur-aan pia sifa ovu.
Na washirikina wakiiona dalili na ushahidi juu ya ukweli wa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), wanakataa kuziamini na kuzisadiki, bali kukanusha na kupinga, na wanasema baada ya dalili kujitokeza: “Huu ni uchawi wenye ubatilifu na wenye kuondoka na kupotea na hauna sifa ya kudumu.” [Tafsiyr Al-Muyassar]
[3] Maonyo Hayakuwafaa Washirikina Wa Makkah Na Makafiri Wengineo:
Maonyo ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Aayaat za Qur-aan, na Ishara, Dalili, Hoja, Miujiza, na Mazingatio, yako wazi kabisa katika Qur-aan yanayothibitisha Tawhiyd Yake. Anathibitisha Allaah (سبحانه وتعالى) katika Kauli Yake:
قُلْ فَلِلَّـهِ الْحُجَّةُ الْبَالِغَةُ ۖ فَلَوْ شَاءَ لَهَدَاكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿١٤٩﴾
“Sema: Basi Ni Allaah Pekee Mwenye hoja timilifu. Na Angelitaka Angelikuhidini nyote.” [Al-An’aam (6:149)]
Na baadhi ya Kauli Zake (سبحانه وتعالى) nyenginezo zinataja kuwa ubalighisho wa Risala, au Aayaat (na Ishara, Dalili, Hoja) za Allaah hazikuwafaa lolote kwa kuwa hawakuamini hivyo basi wakabakia katika ushirikina na ukafiri wao:
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ جَاءَتْهُمْ كُلُّ آيَةٍ حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ﴿٩٧﴾
“Japokuwa itawajia kila Aayah (Ishara, Dalili, Mawaidha) mpaka waone adhabu iumizayo.” [Yuwnus (10:97)]
قُلِ انظُرُوا مَاذَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَمَا تُغْنِي الْآيَاتُ وَالنُّذُرُ عَن قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ﴿١٠١﴾
“Sema: Tazameni yaliyoko mbinguni na ardhini. Lakini Aayaat (Ishara, Dalili) zote na maonyo (ya Rusuli) hayawafai kitu watu wasioamini.” [Yuwnus (10:110)]
وَلَوْ أَنَّنَا نَزَّلْنَا إِلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةَ وَكَلَّمَهُمُ الْمَوْتَىٰ وَحَشَرْنَا عَلَيْهِمْ كُلَّ شَيْءٍ قُبُلًا مَّا كَانُوا لِيُؤْمِنُوا إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ يَجْهَلُونَ ﴿١١١﴾
“Na lau kama Sisi Tungeliwateremshia Malaika, na wao wakasemeshwa na wafu, na Tukawakusanyia kila kitu mbele yao, basi bado wasingeliamini ila Allaah Atake, lakini wengi wamo katika ujahili.” [Al-An’aam (6:111)]
وَكَأَيِّن مِّنْ آيَةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ ﴿١٠٥﴾
“Ni Aayah (Ishara, Dalili) nyingi sana katika mbingu na ardhi wanazipitia na huku wao wanazipuuza.” [Yuwsuf (12:105)]
[4] Ukadhibishaji Wa Nyumati Za Awali Na Aina Za Maangamizi Yao:
Kuanzia Aayah hii namba (9) hadi Aayah namba (42), wanatajwa kaumu wa nyumati za nyuma na jinsi walivyokadhibisha Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja, Miujiza) za Allaah na adhabu mbalimbali zilizowasibu. Rejea Al-‘Ankabuwt (29:40) kwenye uchambuzi wa maudhui hii na rejea mbalimbali:
[5] Qur-aan Imefanywa Sahali Kuisoma Na Kuihifadhi Kwa Mwenye Kuitafakari, Kuizingatia Na Kuitendea Kazi:
Aayah hii tukufu imekariri mara nne katika Suwrah hii. Na hii ni uthibitisho wa Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى) ya Ahadi ya kuifanya Qur-aan kuwa ni nyepesi kuisoma na kuihifadhi pindi mtu ataitafakari na kuizingatia na kuyafanyia kazi maamrisho yake.
Na Ameijaalia kuwa nyepesi kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), rejea Suwrah Maryam (19:97), Ad-Dukhaan (44:58).
Tafsiyr:
Yaani: Tumefanya hii Qur-aan Tukufu kuwa nyepesi kwa maneno yake kwa ajili ya kuhifadhi na kuisoma. Na Tumefanya maana zake kuwa nyepesi kuzifahamu na kuzijua kwa sababu ina kauli bora kabisa, na ina ukweli zaidi katika maana zake, na ina tafsiri iliyo bayana kabisa. Basi kwa yeyote anayeitafuta (kujifunza), Allaah (سبحانه وتعالى) Humfanyia wepesi matilabu yake kwa wepesi wa hali juu kabisa, na Humsahilishia. Na Adh-Dhikr (Ukumbusho), inajumuisha kila kitu ambacho wanakifanyia watu kazi katika (hukmu za) halaal na za haraam, hukumu za amri na makatazo, hukmu za malipo na mawaidha, mafunzo, na itikadi sahihi za manufaa na khabari za kweli. Ndio maana ikawa ilimu ya kuihifadhi Quraan na Tafsiyr yake ni ilimu iliyo nyepesi kabisa na tukufu zaidi, kwani ni ilimu ya manufaa ambayo pindi mja akiitafuta, basi atasaidiwa (na Allaah). Baadhi ya Salaf wamesema kuhusu Aayah hii wakiuliza: Je kuna yeyote anayetafuta ilimu asaidiwe? Na ndio maana Allaah (سبحانه وتعالى) Anawagutusha Waja Wake Akiwaambia:
فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٧﴾
“Basi je, yuko yeyote mwenye kuwaidhika?”
[Tafsiyr As-Sa’diy]
[6] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah:
Bonyeza kiungo kifuatacho:
054-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Qamar Aayah 47-49: إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ
[7] Qadar: Takdiri, Makadirio, Majaaliwa, Hukmu.
Sisi Tumekiumba kila kitu kwa mujibu wa Tulichokikadiria, Tukakihukumu, na Tumekijua vyema, na pia Tumekiandika katika Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa). [Tafsiyr As-Sa’diy]
[8] Kila Kubwa Na Dogo Limeandikwa Katika Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa).
Amali za mwanaadam ziwe kubwa au ndogo vipi zimerekodiwa katika Ubao Uliohifadhiwa mbinguni. Hata iwe ni kauli au neno dogo vipi. Rejea Kauli za Allaah (سبحانه وتعالى) zifuatazo zenye kuthibitisha haya: Al-An’aam (6:38), Al-Kahf (18:49), Az-Zalzalah (99:7-8).