059 - Al-Hashr

 

   الْحَشْر

 

059- Al-Hashr

 

 

059-Al-Hashr: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

سَبَّحَ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿١﴾

1. Vimemsabihi Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi[1], Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.[2]

 

 

 

 

هُوَ الَّذِي أَخْرَجَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ مِن دِيَارِهِمْ لِأَوَّلِ الْحَشْرِ ۚ مَا ظَنَنتُمْ أَن يَخْرُجُوا ۖ وَظَنُّوا أَنَّهُم مَّانِعَتُهُمْ حُصُونُهُم مِّنَ اللَّـهِ فَأَتَاهُمُ اللَّـهُ مِنْ حَيْثُ لَمْ يَحْتَسِبُوا ۖ وَقَذَفَ فِي قُلُوبِهِمُ الرُّعْبَ ۚ يُخْرِبُونَ بُيُوتَهُم بِأَيْدِيهِمْ وَأَيْدِي الْمُؤْمِنِينَ فَاعْتَبِرُوا يَا أُولِي الْأَبْصَارِ﴿٢﴾

2. Yeye Ndiye Aliyewatoa wale waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu kutoka majumbani mwao katika mkusanyiko wa kwanza. Hamkudhania kwamba watatoka, nao wakadhani kwamba husuni zao zitawakinga dhidi ya Allaah. Lakini Hukmu ya Allaah ikawafikia kutoka ambako wasipotazamia, na Akavurumisha kiwewe katika nyoyo zao. Wanaziharibu nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini. Basi pateni funzo enyi wenye uoni wa kutia akilini.

 

 

 

 

وَلَوْلَا أَن كَتَبَ اللَّـهُ عَلَيْهِمُ الْجَلَاءَ لَعَذَّبَهُمْ فِي الدُّنْيَا ۖ وَلَهُمْ فِي الْآخِرَةِ عَذَابُ النَّارِ﴿٣﴾

3. Na lau kama Allaah Asingeliwaandikia kufukuzwa na uhamisho, Angeliwaadhibu duniani, na Aakhirah watapata adhabu ya moto.

 

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ شَاقُّوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۖ وَمَن يُشَاقِّ اللَّـهَ فَإِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٤﴾

4. Hayo ni kwa kuwa wao wamempinga Allaah na Rasuli Wake. Na yeyote anayempinga Allaah, basi hakika Allaah Ni Mkali wa Kuakibu.[3]

 

 

 

 

مَا قَطَعْتُم مِّن لِّينَةٍ أَوْ تَرَكْتُمُوهَا قَائِمَةً عَلَىٰ أُصُولِهَا فَبِإِذْنِ اللَّـهِ وَلِيُخْزِيَ الْفَاسِقِينَ﴿٥﴾

5. Hamkukata aina yoyote ya mtende au mliouacha umesimama juu ya mashina yake, basi ni kwa Idhini ya Allaah, na ili Awahizi mafasiki.[4]

 

 

 

 

وَمَا أَفَاءَ اللَّـهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ مِنْهُمْ فَمَا أَوْجَفْتُمْ عَلَيْهِ مِنْ خَيْلٍ وَلَا رِكَابٍ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يُسَلِّطُ رُسُلَهُ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ ۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٦﴾

6. Na ngawira ya bila jasho[5] Aliyoitoa Allaah kwa Rasuli Wake kutoka kwao, basi hamkuiendea mbio kwa farasi wala kwa ngamia, lakini Allaah Huwapa mamlaka na nguvu Rusuli Wake dhidi ya Amtakaye. Na Allaah juu ya kila kitu Ni Muweza.

 

 

 

 

مَّا أَفَاءَ اللَّـهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ مِنْ أَهْلِ الْقُرَىٰ فَلِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاءِ مِنكُمْ ۚ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

7.  Ngawira ya bila jasho Aliyoitoa Allaah kwa Rasuli Wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Allaah na Rasuli, na kwa ajili ya jamaa wa karibu, na mayatima, na masikini na msafiri aliyeharibikiwa, ili isiwe mzunguko wa zamu baina ya matajiri tu miongoni mwenu. Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi jiepusheni.[6] Na mcheni Allaah. Hakika Allaah Ni Mkali wa Kuakibu.

 

 

 

 

 

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ﴿٨﴾

8. Wapatiwe (pia) mafuqara Muhaajiruna[7] ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na mali zao, wanatafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah, na wananusuru (Dini ya) Allaah na Rasuli Wake. Hao ndio wakweli.

 

 

 

 

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿٩﴾

9. Na wale waliokuwa na masikani (Madiynah) na wakawa na iymaan kabla yao, wanawapenda wale waliohajiri kwao, na wala hawahisi choyo yoyote vifuani mwao kwa yale waliyopewa (Muhaajiruna), na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe wanahitaji. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.[8]

 

 

 

 

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٠﴾

10. Na wale waliokuja baada yao wanasema: Rabb wetu! Tughufurie pamoja na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imaan[9], na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Rabb wetu! Hakika Wewe Ni Mwenye Huruma mno, Mwenye   Kurehemu.

 

 

 

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ نَافَقُوا يَقُولُونَ لِإِخْوَانِهِمُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَئِنْ أُخْرِجْتُمْ لَنَخْرُجَنَّ مَعَكُمْ وَلَا نُطِيعُ فِيكُمْ أَحَدًا أَبَدًا وَإِن قُوتِلْتُمْ لَنَنصُرَنَّكُمْ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ﴿١١﴾

11. Je, huoni wale waliouvaa unafiki, wanawaambia ndugu zao waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu: Mkitolewa bila shaka nasi tutatoka pamoja nanyi, na wala hatutomtii yeyote abadani dhidi yenu. Na mkipigwa vita, bila shaka tutakunusuruni. Na Allaah Anashuhudia kwamba wao kwa hakika ni waongo.

 

 

 

 

لَئِنْ أُخْرِجُوا لَا يَخْرُجُونَ مَعَهُمْ وَلَئِن قُوتِلُوا لَا يَنصُرُونَهُمْ وَلَئِن نَّصَرُوهُمْ لَيُوَلُّنَّ الْأَدْبَارَ ثُمَّ لَا يُنصَرُونَ﴿١٢﴾

12. Wakitolewa, hawatotoka pamoja nao, na wakipigwa vita, hawatowasaidia, na hata wakiwasaidia, bila shaka watageuzia mbali migongo (wakimbie), kisha hawatonusuriwa.

 

 

 

 

لَأَنتُمْ أَشَدُّ رَهْبَةً فِي صُدُورِهِم مِّنَ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ﴿١٣﴾

13. Hakika nyinyi (Waumini) ni tisho zaidi katika vifua vyao kuliko Allaah. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasiofahamu.

 

 

 

 

لَا يُقَاتِلُونَكُمْ جَمِيعًا إِلَّا فِي قُرًى مُّحَصَّنَةٍ أَوْ مِن وَرَاءِ جُدُرٍ ۚ بَأْسُهُم بَيْنَهُمْ شَدِيدٌ ۚ تَحْسَبُهُمْ جَمِيعًا وَقُلُوبُهُمْ شَتَّىٰ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْقِلُونَ﴿١٤﴾

14. Hawatopigana nanyi wote pamoja isipokuwa katika miji iliyozatitiwa kwa husuni au kutoka nyuma ya kuta. Uadui wao baina yao ni mkali. Utawadhania wameungana pamoja, kumbe nyoyo zao zimetengana. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiotia akilini.

 

 

 

كَمَثَلِ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ قَرِيبًا ۖ ذَاقُوا وَبَالَ أَمْرِهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿١٥﴾

15. Ni kama mfano wa wale walio kabla yao hivi karibuni tu. Walionja matokeo ya uovu wa mambo yao, na watapata adhabu iumizayo.

 

 

 

 

كَمَثَلِ الشَّيْطَانِ إِذْ قَالَ لِلْإِنسَانِ اكْفُرْ فَلَمَّا كَفَرَ قَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِّنكَ إِنِّي أَخَافُ اللَّـهَ رَبَّ الْعَالَمِينَ﴿١٦﴾

16. (Wanafiki ni) kama mfano wa shaytwaan alipomwambia binaadamu: Kufuru! Alipokufuru, (shaytwaan) alisema: Hakika mimi sihusiki nawe! Mimi namkhofu Allaah Rabb wa walimwengu.[10]

 

 

 

 

فَكَانَ عَاقِبَتَهُمَا أَنَّهُمَا فِي النَّارِ خَالِدَيْنِ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الظَّالِمِينَ﴿١٧﴾

17. Basi hatima yao wote wawili ikawa kwamba wao wawili watakuwa motoni wadumu wote humo. Na hiyo ndio jazaa ya madhalimu.

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١٨﴾

18. Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myatendayo.

 

 

 

 

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ نَسُوا اللَّـهَ فَأَنسَاهُمْ أَنفُسَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ﴿١٩﴾

19. Na wala msiwe kama wale waliomsahau Allaah, Naye (Allaah) Akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio mafasiki.

 

 

 

 

لَا يَسْتَوِي أَصْحَابُ النَّارِ وَأَصْحَابُ الْجَنَّةِ ۚ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمُ الْفَائِزُونَ﴿٢٠﴾

20. Hawalingani sawa watu wa motoni na watu wa Jannah, watu wa Jannah ndio wenye kufuzu.[11]

 

 

 

 

لَوْ أَنزَلْنَا هَـٰذَا الْقُرْآنَ عَلَىٰ جَبَلٍ لَّرَأَيْتَهُ خَاشِعًا مُّتَصَدِّعًا مِّنْ خَشْيَةِ اللَّـهِ ۚ وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ﴿٢١﴾

21. Lau Tungeliiteremsha hii Qur-aan juu ya mlima, ungeliuona unanyenyekea ukipasukapasuka kutokana na khofu ya Allaah.[12] Na hiyo ni mifano Tunawapigia watu ili wapate kutafakari.

 

 

 

 

هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ ۖ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ﴿٢٢﴾

22. Yeye Ni Allaah, Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye. Mjuzi wa ya ghaibu na ya dhahiri, Yeye Ndiye Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu.[13]

 

 

 

 

هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾

23. Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye Kusadikisha ahadi na Kuaminisha, Mwenye Kudhibiti Kushuhudia Kuchunga na Kuhifadhi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Jabari Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye Ukubwa na Uadhama, Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha.

 

 

 

 

هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٢٤﴾

24. Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji, Mwanzishi wa viumbe bila kasoro, Muundaji sura na umbile, Ana Majina Mazuri kabisa.[14] Kinamsabihi Pekee kila kilichoko katika mbingu na ardhi, Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

[1] Kila Kitu Kinamsabbih Allaah (عزّ وجلّ):

 

Rejea Al-Hashr (57:1) kwenye rejea zinazotaja viumbe na vitu Alivyoviumba Allaah kuwa vinamsabbih Yeye Allaah (عزّ وجلّ).

 

[2] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah:

 

Kuanzia Aayah hii hadi namba (4) kuna sababu ya kuteremshwa. Bonyeza kiungo kifuatacho:  

 

059-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Hashr Aayah 01-04 سَبَّحَ لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ

 

[3] Tofauti Ya Adhabu Na Ikabu:  

 

Maneno mawili hayo yametumika sana katika Qur-aan, lakini yanatofautiana kwa kiasi fulani. 

 

Ikabu ni malipo ya adhabu anayostahiki mtenda dhambi kwa kitendo chake cha kuasi.

 

Ama adhabu ni maumivu yenye kuendelea au yasiyoendelea ambayo yanamhusu mtu anapotenda dhambi hivyo akawa amestahiki adhabu.  Au ni adhabu kwa asiyetenda dhambi kwa maana asiyestahiki. Mfano wa asiyestahiki ni mtu kuwa katika mateso au mitihani bila ya kuwa ametenda dhambi, mathalan mitihani ya maradhi akawa mtu anapata maumivu ya kuendelea, hivyo inasemwa anaadhibika. Na adhabu ni ya jumla zaidi. Ama ikabu ni makhsusi kwa mtenda dhambi.

 

Rejea Al-Mujaadalah (58:5) kwenye aina za adhabu. 

 

 

[5] Al-Fay-u: Ngawira Inayopatikana Bila Ya Kupigana Vita:

 

Al-Fay-u ni ngawira ambayo ni mali wanayoipata Waislamu kutoka kwa makafiri bila ya kupigana vita. Na imetajwa katika Suwrah hii, Al-Hashr (59:6-7). Ama ngawira ambayo inapatikana baada ya kupigana vita inaitwa “ghanima.” Rejea Al-Anfaal (8:41). 

 

[6] Kutii Amri Ya Allaah Na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) Na Kujiepusha Na Makatazo Yao, Na Laana Ya Allaah Kwa Wenye Kuchanja, Wenye Kutoa Nyusi, Wenye Kuchonga Meno, Wenye Kubadilisha Umbile La Allaah:  

 

Hadiyth zifuatazo zinataja hayo:

 

عَنْ عَلْقَمَةَ، عَنْ عَبْدِ اللَّهِ، لَعَنَ اللَّهُ الْوَاشِمَاتِ، وَالْمُسْتَوْشِمَاتِ، وَالْمُتَنَمِّصَاتِ وَالْمُتَفَلِّجَاتِ لِلْحُسْنِ، الْمُغَيِّرَاتِ خَلْقَ اللَّهِ تَعَالَى، مَالِي لاَ أَلْعَنُ مَنْ لَعَنَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم وَهْوَ فِي كِتَابِ اللَّهِ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ‏ ‏‏.‏

Amesimulia ‘Alqamah (رضي الله عنه): Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) amesema: Allaah Amewalaani wenye kuchanja, na wenye kuchanjwa, na wenye kunyoa nyusi, na wenye kuchonga meno kwa urembo, na wenye kubadilisha umbile la Allaah (سبحانه وتعالى). Kwa nini nisimlaani yule aliyelaaniwa na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na aliyelaaniwa katika Kitabu cha Allaah?:

 

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

“Na lolote analokupeni Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi jiepusheni.” [Al-Hashr (59:7) Hadiyth amepokea Imaam Al-Bukhaariy Kitabu Cha Mavazi (77)]

 

Na pia:

 

عن أسماءَ رضي الله عنها : أنَّ امْرَأَةً سَأَلَتِ النَّبيَّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَتْ : يا رسولَ اللهِ إنَّ ابْنَتِي أصَابَتْهَا الحَصْبَةُ ، فَتَمَرَّقَ شَعْرُهَا ، وإنّي زَوَّجْتُهَا ، أفَأَصِلُ فِيهِ ؟ فقالَ : ()لَعَنَ اللهُ الوَاصِلَةَ وَالمَوْصُولَةَ)) . متفق عليه .

وفي روايةٍ : ((الوَاصِلَةَ، والمُسْتوْصِلَةَ)) .

Amesimulia Asmaa (رضي الله عنها) kwamba mwanamke fulani alimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ee Rasuli wa Allaah! Binti yangu amepatwa na surua zikapuputika nywele zake, nami nimemuozesha; Je, niziunganishe? Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamjibu: "Allaah Amemlaani mwenye kuunganisha nywele zake (au nywele za mwengine kwa nywele nyengine) na mwenye kuungwa (au kuvaa nywele hizo)." [Al-Bukhaariy, Muslim na An-Nasaaiy] 

 

Na katika riwaayah nyengine: "Mwenye kuunganisha nywele na mwenye kumtaka mwengine amfanyie kazi hiyo (mwenye kutamani kuzivaa nywele hizo za bandia)." 

 

[7] Muhaajiruna:

 

Muhaajiruna ni wale waliohamia kutoka Makkah kwenda Madiynah. Ama Answaar, hawa ni watu wa Madiynah.

 

[8] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah:

 

Kuna kisa cha kusisimua ngozi kuhusu familia ya Answaar waliojinyima chakula na badala yake kuwapendelea wageni wale, ilhali wao wenyewe walikihitajia chakula hicho. Bonyeza kiungo kifuatacho:

 

059-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Hashr Aayah 09: ‏وَيُؤْثِرُونَ عَلَى أَنْفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ

 

[9] Waliotangulia Kwa Imaan:

 

Ni sawa na Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٠٠﴾

Na wale waliotangulia awali (katika Uislamu) miongoni mwa Muhaajiruwn na Answaar na wale waliowafuata kwa ihsaan, Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia Jannaat zipitazo chini yake mito, wadumu humo abadi. Huko ndiko kufuzu kukubwa kabisa. [At-Tawbah (9:100)]

 

[10] Shaytwaan Huwapotosha Watu Kisha Huwakanusha Na Kuwageuka!:

 

Rejea Suwrah Ibraahiym (14:22) kwenye maelezo, faida na rejea mbalimbali.

 

[11] Hawalingani Sawa Watu Wa Motoni Na Wa Peponi:

 

Rejea Al-Jaathiyah (45:21) kwenye faida na rejea mbalimbali.

 

[12] Vitu Alivyoviumba Allaah Vinashtuka Kwa Kumkhofu Allaah (عزّ وجلّ):

 

Rejea Suwrah Maryam (19:90), Ash-Shuwraa (42:5) kwenye faida.

 

[13] Tofauti Ya Ar-Rahmaan Na Ar-Rahiym:

 

Rejea Al-Faatihah (1:1)

 

[14] Majina Mazuri Kabisa Ya Allaah (سبحانه وتعالى)

 

Rejea Faharasa ya Majina Mazuri Kabisa Ya Allaah Na Sifa Zake.

 

 

Share