073 - Al-Muzzammil

 

   الْمُزَّمِّل

 

073-Al-Muzzammil

 

 

073-Al-Muzzammil: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ﴿١﴾

1. Ee uliyejifunika.[1]

 

 

 

 

قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا﴿٢﴾

2. Simama (kuswali) usiku kucha isipokuwa kidogo tu.[2]

 

 

 

 

نِّصْفَهُ أَوِ انقُصْ مِنْهُ قَلِيلًا﴿٣﴾

3. Nusu yake, au ipunguze kidogo.

 

 

 

 

أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا﴿٤﴾

4. Au izidishe, na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali.[3]

 

 

 

إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلًا ثَقِيلًا﴿٥﴾

5. Hakika Sisi Tutakuteremshia juu yako kauli nzito.[4]

 

 

 

 

إِنَّ نَاشِئَةَ اللَّيْلِ هِيَ أَشَدُّ وَطْئًا وَأَقْوَمُ قِيلًا﴿٦﴾

6. Hakika kuamka usiku (kuswali) ni uthibiti zaidi wa kuathiri moyo na kuifahamu, na unyofu zaidi wa maneno kutua.

 

 

 

 

إِنَّ لَكَ فِي النَّهَارِ سَبْحًا طَوِيلًا﴿٧﴾

7. Hakika una mchana mrefu kwa shughuli nyingi.

 

 

 

 

وَاذْكُرِ اسْمَ رَبِّكَ وَتَبَتَّلْ إِلَيْهِ تَبْتِيلًا﴿٨﴾

8. Na dhukuru Jina la Rabb wako, na jitolee Kwake kwa kujitolea kikamilifu.

 

 

 

 

رَّبُّ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَاتَّخِذْهُ وَكِيلًا﴿٩﴾

9. Rabb wa Mashariki na Magharibi, hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi mfanye kuwa ni Mdhamini wako.

 

 

 

 

وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَاهْجُرْهُمْ هَجْرًا جَمِيلًا﴿١٠﴾

10. Na subiri juu ya yale wayasemayo, na wahame, mhamo mzuri.

 

 

 

 

وَذَرْنِي وَالْمُكَذِّبِينَ أُولِي النَّعْمَةِ وَمَهِّلْهُمْ قَلِيلًا﴿١١﴾

11. Na Niache Mimi na wanaokadhibisha walioneemeka, na uwape muhula kidogo.

 

 

 

 

إِنَّ لَدَيْنَا أَنكَالًا وَجَحِيمًا﴿١٢﴾

12. Hakika Sisi Tuna minyororo na moto uwakao vikali mno.

 

 

 

 

وَطَعَامًا ذَا غُصَّةٍ وَعَذَابًا أَلِيمًا﴿١٣﴾

13. Na chakula cha kusakama kooni, na adhabu iumizayo.

 

 

 

 

يَوْمَ تَرْجُفُ الْأَرْضُ وَالْجِبَالُ وَكَانَتِ الْجِبَالُ كَثِيبًا مَّهِيلًا﴿١٤﴾

14. Siku itakayotikisika ardhi na milima, na milima itakuwa kama rundo la mchanga tifutifu.

 

 

 

 

إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا﴿١٥﴾

15. Hakika Sisi Tumekutumieni Rasuli awe shahidi juu yenu, kama Tulivyotuma Rasuli kwa Firawni.

 

 

 

 

فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا﴿١٦﴾

16. Lakini Firawni alimuasi huyo Rasuli, Tukamshika kwa maangamizi makali mno.

 

 

 

 

فَكَيْفَ تَتَّقُونَ إِن كَفَرْتُمْ يَوْمًا يَجْعَلُ الْوِلْدَانَ شِيبًا﴿١٧﴾

17. Basi vipi mtaweza kujikinga, kama mkikufuru Siku itakayowafanya watoto kuwa wenye kutoka mvi?

 

 

 

 

السَّمَاءُ مُنفَطِرٌ بِهِ ۚ كَانَ وَعْدُهُ مَفْعُولًا﴿١٨﴾

18. Mbingu zitapasuka hapo (kwa sababu ya Siku hiyo), Ahadi Yake itatimizwa.

 

 

 

إِنَّ هَـٰذِهِ تَذْكِرَةٌ ۖ فَمَن شَاءَ اتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِ سَبِيلًا﴿١٩﴾

19. Hakika haya (yaliyotajwa kwenye Aayaat hizi) ni ukumbusho. Basi atakaye ashike njia ya kuelekea kwa Rabb wake.

 

 

 

 

إِنَّ رَبَّكَ يَعْلَمُ أَنَّكَ تَقُومُ أَدْنَىٰ مِن ثُلُثَيِ اللَّيْلِ وَنِصْفَهُ وَثُلُثَهُ وَطَائِفَةٌ مِّنَ الَّذِينَ مَعَكَ ۚ وَاللَّـهُ يُقَدِّرُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ ۚ عَلِمَ أَن لَّن تُحْصُوهُ فَتَابَ عَلَيْكُمْ ۖ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنَ الْقُرْآنِ ۚ عَلِمَ أَن سَيَكُونُ مِنكُم مَّرْضَىٰ ۙ وَآخَرُونَ يَضْرِبُونَ فِي الْأَرْضِ يَبْتَغُونَ مِن فَضْلِ اللَّـهِ ۙ وَآخَرُونَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنْهُ ۚ وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَقْرِضُوا اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا ۚ وَمَا تُقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُم مِّنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِندَ اللَّـهِ هُوَ خَيْرًا وَأَعْظَمَ أَجْرًا ۚ وَاسْتَغْفِرُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٢٠﴾

20. Hakika Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Anajua kwamba unasimama (kuswali) karibu na thuluthi mbili za usiku au nusu yake, au thuluthi yake, na kundi miongoni mwa wale walio pamoja nawe. Na Allaah Anakadiria usiku na mchana. Anajua kwamba hamuwezi kuukadiria wakati wake na kusimama kuswali, basi Amepokea tawbah yenu. Basi someni kile kilicho chepesi katika Qur-aan.[5] (Allaah) Anajua kwamba watakuweko miongoni mwenu wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wanatafuta Fadhila za Allaah, na wengineo wanapigana katika Njia ya Allaah. Basi someni kile kilicho chepesi humo. Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, na mkopesheni Allaah karadha mzuri. Na chochote kile cha kheri mnachokadimisha kwa ajili ya nafsi zenu, mtakikuta kwa Allaah kizuri zaidi na chenye ujira mkubwa zaidi[6] Na muombeni Allaah maghfirah[7], hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.[8]

 

 

 

[1] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah:

 

Bonyeza kiungo kifuatacho:  

 

073-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Muzzammil: يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ

 

Rejea pia Al-Muddath-thir (74:1), na Al-‘Alaq (96:1) ambako kuna Hadiyth inayoelezea tukio la Jibriyl (عليه السّلام) kumfikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa katika pango la Hiraa akitafakari Uumbaji wa Allaah Akateremshiwa Wahy wa kwanza kabisa.

 

[2] Qiyaamul-Layl Na Fadhila Zake:

 

Bonyeza kiungo kifuatacho:

 

Fadhila Na Faida Za Qiyaamul-Layl

 

Rejea pia Adh-Dhaariyaat (51:15) kwenye faida kadhaa na rejea nyenginezo.

 

[4] Uteremsho Wa Wahy Kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Ulikuwa Ni Mzito Mno!

 

Hadiyth ifuatayo inaelezea:

 

حَدَّثَنَا فَرْوَةُ، حَدَّثَنَا عَلِيُّ بْنُ مُسْهِرٍ، عَنْ هِشَامِ بْنِ عُرْوَةَ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ عَائِشَةَ ـ رضى الله عنها ـ أَنَّ الْحَارِثَ بْنَ هِشَامٍ، سَأَلَ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَيْفَ يَأْتِيكَ الْوَحْىُ قَالَ ‏ "‏ كُلُّ ذَاكَ يَأْتِي الْمَلَكُ أَحْيَانًا فِي مِثْلِ صَلْصَلَةِ الْجَرَسِ، فَيَفْصِمُ عَنِّي وَقَدْ وَعَيْتُ مَا قَالَ، وَهْوَ أَشَدُّهُ عَلَىَّ، وَيَتَمَثَّلُ لِي الْمَلَكُ أَحْيَانًا رَجُلاً، فَيُكَلِّمُنِي فَأَعِي مَا يَقُولُ

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها):  Al-Haarith Bin Hishaam alimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Je, Wahy unakujia vipi? Akasema: “Katika njia zote hizi: Wakati mwengine Malaika anakuja kwangu na sauti inayofanana na mlio wa kengele, na hali hiyo inaponiacha, nakumbuka kila alichosema Malaika. Na njia hii ya Wahy ndio iliyo nzito zaidi kwangu. Na wakati mwengine Malaika anakuja kwangu kwa sura za mwanaadam na kuzungumza nami, nami nakumbuka alichosema.” [Al-Bukhaariy Kitabu Cha Uanzishaji wa Uumbaji (59)]

 

[5] Kusoma Kilicho Chepesi Katika Qur-aan Ndani Ya Swalaah:

 

Katika Swalaah za fardhi, haijaamrishwa kusoma kisomo kirefu cha Qur-aan isipokuwa tu katika Swalaah ya Alfajiri kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ ۖ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا ﴿٧٨﴾

“Simamisha Swalaah jua linapopinduka hadi kiza cha usiku na (refusha) Qur-aan ya (Swalaah ya) Alfajiri. Hakika Qur-aan ya Alfajiri ni yenye kushuhudiwa.” [Al-Israa (17:78)]

 

Ama katika Swalaah nyenginezo za fardhi, Muislamu anatakiwa asome chochote kilicho chepesi kama alivyoamrishwa Swahaba ambaye aliswali kwa haraka kabisa na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwamrisha airudie Swalaah yake na asome kilicho chepesi katika Qur-aan:  

 

حَدَّثَنَا مُحَمَّدُ بْنُ بَشَّارٍ، قَالَ حَدَّثَنَا يَحْيَى، عَنْ عُبَيْدِ اللَّهِ، قَالَ حَدَّثَنِي سَعِيدُ بْنُ أَبِي سَعِيدٍ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم دَخَلَ الْمَسْجِدَ، فَدَخَلَ رَجُلٌ فَصَلَّى فَسَلَّمَ عَلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَرَدَّ وَقَالَ ‏"‏ ارْجِعْ فَصَلِّ، فَإِنَّكَ لَمْ تُصَلِّ ‏"‏‏.‏ فَرَجَعَ يُصَلِّي كَمَا صَلَّى ثُمَّ جَاءَ فَسَلَّمَ عَلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ ‏"‏ ارْجِعْ فَصَلِّ فَإِنَّكَ لَمْ تُصَلِّ ‏"‏ ثَلاَثًا‏.‏ فَقَالَ وَالَّذِي بَعَثَكَ بِالْحَقِّ مَا أُحْسِنُ غَيْرَهُ فَعَلِّمْنِي‏.‏ فَقَالَ ‏"‏ إِذَا قُمْتَ إِلَى الصَّلاَةِ فَكَبِّرْ، ثُمَّ اقْرَأْ مَا تَيَسَّرَ مَعَكَ مِنَ الْقُرْآنِ، ثُمَّ ارْكَعْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ رَاكِعًا، ثُمَّ ارْفَعْ حَتَّى تَعْتَدِلَ قَائِمًا، ثُمَّ اسْجُدْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ سَاجِدًا، ثُمَّ ارْفَعْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ جَالِسًا، وَافْعَلْ ذَلِكَ فِي صَلاَتِكَ كُلِّهَا ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliingia Msikitini na mtu akamfuata. Yule mtu aliswali akaenda kumsalimu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamuitikia Salaam kisha akamwambia: “Nenda urudie kuswali kwani hukuswali.” Yule mtu alikwenda akaswali kama mwanzo, kisha akarejea na kumsalimu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Nenda urudie kuswali kwani hukuswali.” Hilo lilijiri mara tatu. Yule mtu akasema: “Naapa kwa Aliyekutuma kwa haki! Siwezi kuswali vizuri zaidi ya hivi, basi nifundishe:  Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Unaposimama kuswali tamka Takbiyr (Allaahu Akbar) kisha soma chepesi ulichonacho katika Quraan, halafu rukuu mpaka utulie katika rukuu. Kisha inua kichwa na usimame wima (utulie), kisha sujudu mpaka utulie kabisa katika Sujuwd, kisha nyanyuka mpaka utulie katika kikao, halafu sujudu mpaka utulie katika sijdah, kisha nyanyuka mpaka utulie katika kikao, halafu fanya hivyo katika Swalaah yako yote.” [Al-Bukhaariy Kitabu Cha Adhaan Sifa Ya Swalaah (10b)]

 

Ama Swalaah ya Qiyaamul-Layl (Kisimamo Cha Usiku) ambayo imesisitizwa mno na ina fadhila nyingi adhimu kabisa [Rejea Adh-Dhaariyaat (51:15)], imependekezwa kisimamo kirefu kusoma Qur-aan, lakini haijakalifishwa kwa mtu kufanya hivyo kwani chochote anachojaaliwa mtu kusoma basi kina fadhila zake kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

 عبدالله بن عمرو عن النبي صلى الله عليه وسلم ((من قام بعشرِ آياتٍ لم يُكتبْ من الغافلينَ ، ومن قام بمئةِ آيةٍ كُتبَ من القانتينَ ومن قام بألفِ آيةٍ كُتبَ من المُقَنْطِرينَ)) صحيح أبي داود  

“Atakayesimama usiku kwa kuswali na kusoma Aayah kumi hatoandikiwa katika miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kwa Aayah mia ataandikiwa ni miongoni mwa watiifu na atakayesimama kwa Aayah elfu ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi (ya thawabu).” [Abuu Daawuwd ameisahihisha Al-Albaaniy: Swahiyh Abiy Daawuwd (1398), Swahiyh Al-Jaami’ (6439)]

 

[6] Fadhila Za Kutoa Katika Njia Ya Allaah:

 

Rejea Al-Hadiyd (57:11) kwenye faida tele na rejea mbalimbali.

 

[7] Amri Ya Kumuomba Allaah Maghfirah Na Fadhila Zake:

 

Rejea An-Nisaa (4:110), Huwd (11:3) kwenye maelezo bayan na rejea mbalimbali. Pia At-Tahriym (66:8), Nuwh (71:10), Adh-Dhaariyaat (51:18).

 

[8] Tafsiyr Ya Aayah:

 

Hakika Rabb wako ee Nabiy, Anajua kuwa wewe unasimama kwa Tahajjud (Kisimamo cha usiku kuswali) kipindi cha usiku, wakati mwingine chini ya theluthi mbili za usiku, na wakati mwingine unasimama nusu yake, na wakati mwingine theluthi yake. Na wanasimama pamoja na wewe kundi la Swahaba zako. Na Allaah Pekee Ndiye Anayekadiria usiku na mchana, na Anajua vipimo vyake na kipindi kinachopita na kusalia cha mchana na usiku. Allaah Anajua kwamba haiwezekani kwenu nyinyi kusimama usiku wote, hivyo basi Akawafanyia mambo kuwa mepesi kwenu. Na msome kwenye Swalaah ya usiku kile kilichokuwa chepesi kwenu kukisoma katika Qur-aan. Allaah Anajua kuwa miongoni mwenu kuna wanaoelemewa na ugonjwa wasiweze kusimama usiku. Na kuna watu wengine wanatembea ardhini kwa biashara na kazi wakitafuta riziki ya Allaah ya halaal. Na kuna watu wengine wanapigana Jihaad katika Njia ya Allaah ili kuliinua neno Lake na kutangaza Dini Yake. Basi someni kutoka kwenye Qur-aan kile kilicho chepesi kwenu, na endeleeni kutekeleza faradhi za Swalaah, na toeni Zakaah za lazima kwenu, na toeni swadaqa za mali yenu katika njia za wema na ihsaan kwa kutaka Radhi za Allaah. Na chochote kile mnachokifanya miongoni mwa njia za wema na kheri na matendo ya utiifu, basi mtapata malipo yake na thawabu zake kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Siku ya Qiyaamah, hali ya kuwa ni bora zaidi na chenye thawabu kubwa zaidi kuliko kile mlichokitanguliza duniani. Na ombeni maghfira kwa Allaah katika hali zenu zote. Allaah Ni Mwingi wa kuwaghufuria sana nyinyi na Mwenye Kuwarehemu. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

 

 

Share