082 - Al-Infitwaar
الإِنْفِطَار
082-Al-Infitwaar
082-Al-Infitwaar: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
إِذَا السَّمَاءُ انفَطَرَتْ ﴿١﴾
1. Mbingu itakapopasuka.[1]
وَإِذَا الْكَوَاكِبُ انتَثَرَتْ ﴿٢﴾
2. Na sayari zitakapoanguka na kutawanyika.
وَإِذَا الْبِحَارُ فُجِّرَتْ ﴿٣﴾
3. Na bahari zitakapopasuliwa.
وَإِذَا الْقُبُورُ بُعْثِرَتْ ﴿٤﴾
4. Na makaburi yatakapopinduliwa chini juu na kufichuliwa.
عَلِمَتْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ وَأَخَّرَتْ ﴿٥﴾
5. Nafsi hapo itajua yale iliyoyakadimisha na iliyoyaakhirisha.[2]
يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ ﴿٦﴾
6. Ee binaadamu! Nini kilichokughuri hata umkufuru Rabb wako Mkarimu?
الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ ﴿٧﴾
7. Ambaye Amekuumba, Akakusawazisha (umbo sura, viungo), na Akakulinganisha sawa.[3]
فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ ﴿٨﴾
8. Katika sura Aliyotaka Akakutengeneza.
كَلَّا بَلْ تُكَذِّبُونَ بِالدِّينِ ﴿٩﴾
9. Laa hasha! Bali mnakadhibisha malipo.
وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ ﴿١٠﴾
10. Na hakika juu yenu bila shaka kuna wenye kuhifadhi (na kuchunga).
كِرَامًا كَاتِبِينَ ﴿١١﴾
11. Watukufu wanaoandika (amali).[4]
يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ ﴿١٢﴾
12. Wanajua yale myafanyayo.
إِنَّ الْأَبْرَارَ لَفِي نَعِيمٍ ﴿١٣﴾
13. Hakika Al-Abraar[5] (watendao khayraat kwa wingi) bila shaka watakuwa katika neema (taanasa, furaha n.k).
وَإِنَّ الْفُجَّارَ لَفِي جَحِيمٍ ﴿١٤﴾
14. Na hakika watendao dhambi bila shaka watakuwa katika moto uwakao vikali mno.
يَصْلَوْنَهَا يَوْمَ الدِّينِ ﴿١٥﴾
15. Watauingia waungue Siku ya malipo.
وَمَا هُمْ عَنْهَا بِغَائِبِينَ ﴿١٦﴾
16. Nao hawatokosa kuweko humo.
وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ﴿١٧﴾
17. Na nini kitakachokujulisha ni ipi Siku ya malipo?
ثُمَّ مَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ﴿١٨﴾
18. Kisha nini kitakachokujulisha ni ipi Siku ya malipo?
يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ ﴿١٩﴾
19. Siku ambayo nafsi haitokuwa na uwezo wowote juu ya nafsi nyingine,[6] na amri Siku hiyo ni ya Allaah Pekee.
[1] Miongoni Mwa Matukio Ya Siku Ya Qiyaamah:
Kuanzia mwanzo wa Aayah hadi namba (4) ni miongoni mwa matukio ya Siku ya Qiyaamah. Rejea At-Takwiyr (81:1) kwenye faida inayohusiana.
[2] Kila Mtu Atatambua Matendo Yake Aliyoyatenda Duniani:
Rejea At-Takwiyr (81:14) kwenye faida zinazohusiana na maudhui hii.
[3] Binaadam Ameumbwa Katika Umbo Bora Kabisa:
Aayah hii na ifuatayo namba (8) inataja jinsi binaadam alivyoumbwa katika umbo bora kabisa na sura nzuri. Rejea Kauli Zake Allaah (سبحانه وتعالى) nyenginezo katika Aayah zifuatazo: Aal-‘Imraan (3:6), Al-Muuminuwn (23:12-14), Al-Infitwaar (82:7-8), At-Tiyn (95:4).
[4] Amali Za Wanaadam Zinaandikwa Na Malaika:
Amali au tendo lolote analolitenda binaadam linaandikwa na kurekodiwa katika daftari lake ambalo litakunjuliwa Siku ya Qiyaamah ajionee matendo yake, hata tendo liwe dogo vipi au neno dogo vipi liwe jema au ovu. Rejea Al-Israa (17:13-14) kwenye faida na rejea mbalimbali na maudhui zinazohusiana. Rejea pia At-Takwiyr (81:10), Az-Zalzalah (99:4-8). Rejea pia Qaaf (50:18) kwenye faida kuhusu kuchunga ulimi kwa kuwa hata neno dogo vipi linarekodiwa.
[5] Maana Ya Al-Abraar:
Neno الأَبْرَارُ ni wingi wa neno البَرُّ, na maana yake ni watu waliokithirisha kufanya mambo mema ya kumridhisha Allaah. Na البَرُّ ni Jina katika Majina ya Allaah lenye maana ya Mwingi wa Ihsaan na Fadhila kama Anavyosema Mwenye Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ ﴿٢٨﴾
Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa Ihsaan na Fadhila, Mwenye Kurehemu. [Atw-Twuur (52:28)]
Na kwa mwanaadam lina maana ya mtu mwenye kukithirisha matendo ya kheri.
Pia neno hili البَرُّ lina maana ya bara (nchi kavu) kinyume na bahari. Na nchi kavu kama tuonavyo kheri na baraka zake ni nyingi zisizo na hesabu.
Kiistihali inamaanisha upana na wingi mno wa amali njema (khayraat). Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja wingi wa khayraat katika Aayah namba (177) ya Suwrah Al-Baqarah kama ifuatavyo:
لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا ۖ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ ﴿١٧٧﴾
Wema uliotimilika si kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na Magharibi, lakini wema uliotimilika ni mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na akawapa mali juu ya kuipenda kwake jamaa wa karibu na mayatima na masikini na msafiri na waombao na katika kukomboa watumwa, na akasimamisha Swalaah na akatoa Zakaah, na watimizao ahadi zao wanapoahidi, na wenye subira katika dhiki za ufukara na maafa ya magonjwa na njaa na katika vita. Hao ndio waliosadikisha na hao ndio wenye taqwa. [Al-Baqarah 2:177)]
Na birr pia ni katika katika kuwafanyia wema wazazi, kwa kuwa kuwafanyia wema wazazi ni kwingi mno. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu Nabiy Yahyaa (عليه السّلام):
وَبَرًّا بِوَالِدَيْهِ وَلَمْ يَكُن جَبَّارًا عَصِيًّا ﴿١٤﴾
Na mtiifu mno kwa wazazi wake wawili, na wala hakuwa jabari wala muasi. [Maryam (19:14)]
Na pia kumhusu Nabiy Iysaa (عليه السّلام) Suwrah hiyo ya Maryam (19:32).
Na katika kutoa mali anayoipenda zaidi mtu ni katika al-birr. Bonyeza kiungo kifuatacho:
037-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Kutoa Ukipendacho Katika Vizuri
Hamtoweza Kuufikia Wema Uliokunjuka Mpaka Mtoe Katika Vile Mnavyovipenda!
Bonyeza pia kiungo kifuatacho kwenye faida nyenginezo:
Kubainisha Wingi Wa Njia Za Kheri (Riyaadhwus-Swaalihiyn)
Na Al-Abraar (waja wema) wametajwa mara kadhaa katika Qur-aan, na miongoni mwa Aayah zilizowataja ni: Al-Insaan (76:5), Al-Mutwaffifiyn (83:18) (83:22).
[6] Hakuna Atakayemfaa Mwenzake Siku Ya Qiyaamah Hata Wenye Uhusiano Wa Ndugu:
Rejea ‘Abasa (80:34-37) kwenye rejea mbalimbali. Rejea pia Al-Hujuraat (49:13) kwenye faida nyenginezo kuhusu maudhui hii.