Imaam Ibn Baaz: Hukmu Ya Kusema Wazi Au Wasiwasi Kwa Kutokubaliwa Du'aa

Hukmu Ya Kusema Wazi (Au Kudhihirisha Wasiwasi) Kwa Kutokubaliwa Du'aa

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

Alhidaaya.com

SWALI:

Je inapokuwa haijahakiki kwangu jambo niloliomba huwa naghadhibika na husema maneno katika nafsi yangu na kuhusu Allaah mfano husema: “Kwanini Yaa Rabb Huitikii du'aa yangu?” Na husema mengineyo pia. Naomba tafadhali uniongoze kuhusu haya. Na je, binaadamu anapohisi kuwa du'aa yake haikutakabaliwa afanyeje??

JIBU:

Ni juu yako ee muulizaji na kila Muislamu mwanamme na mwanamke inapochelewa kutakabaliwa (du'aa yako) basi jirudie nafsi yako na ujipime kwani Allaah ni Hakiymun-‘Aliym (Mwenye hikma na Mjuzi) Huenda Anaichelewesha kutakabaliwa (hiyo du'aa) kwa hikma kubwa ili mja akithirishe du’aa kwa Muumba wake, na kujilazimisha Kwake, na  kujidhalilisha kwa Utukufu Wake na kungʼangʼania katika kuomba haja yake na kuzidisha kurudi Kwake na kunyenyekea Kwake. Ili kwa kufanya hivyo, (mja mwenye kuomba) apate kheri na manufaa mengi na aweze kuutengeneza moyo na kumridhia Mola wake. Yote haya ni adhimu zaidi na yenye manufaa zaidi kuliko haja yake. 

Pia huenda Allaah (سبحانه وتعالى) Akachelewesha (kujibu du'aa) kwa sababu nyinginezo kama vile (muombaji) kujichanganya katika maasi kama kula chumo la haraam au kuwaasi wazazi wawili na maasi mengineyo. Basi inawajibika kwa muombaji du’aa ajihesabu nafsi yake na akimbilie kuomba tawbah huku awe na matumaini kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anamtakabalia tawbah yake na Atamuitikia du’aa yake.

Na huenda Akaichelewesha kwa hikma nyingine Anayoijua Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى) kama vile ilivyo katika Hadiyth Swahiyh:

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ (رضي الله عنه)  أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ وَلاَ قَطِيعَةُ رَحِمٍ إِلاَّ أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثلاَثٍ:  إِمَّا أَنْ تُعَجَّلَ لَهُ دَعْوَتُهُ وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الأَخِرَةِ وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنْ السُّوءِ مِثْلَهَا))  قَالُوا إِذًا نُكْثِرُ قَالَ:  ((اللَّهُ أَكْثَرُ))

Kutoka kwa Abu Sa’iyd(رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وسلم) amesema: ((Hakuna Muislamu atakayeomba du’aa ambayo haina dhambi wala kukata undugu wa uhusiano wa damu isipokuwa Allaah Atampa mojawapo ya matatu; ima Amharakishie du’aa yake, au Amuwekee akiba Aakhirah au ima Amuepushe nayo ovu kama hilo)) Wakasema: Basi tutazidisha (kuomba du’aa). Akasema: ((Allaah Mwingi zaidi [wa kuongeza])) [Ahmad]

 Basi itakapochelewa haja yako kutakabaliwa, usimlaumu Mola wako wala usiseme: “kwanini, kwanini Yaa Rabb” bali ni juu yako kujirudi nafsi yako kwani Mola wako ni Hakiymun-‘Aliym. Rudia nafsi yako na tazama kwani huenda una dhambi au maasi fulani ikawa ndio sababu ya kuchelewa kuitikiwa. Au huenda kuna jambo jengine lililosababisha kuchelewa kuitikiwa. Yote hayo huwa ni kheri kwako. Basi haijuzu kumlaumu Mola wake yasiyomstahiki (سبحانه وتعالى), lakini ni juu yako kujilaumu nafsi yako na utazame ‘amali zako na nyendo zako mpaka ujitengeneze nafsi yako ili uthibitike katika amri ya Mola wako na uache kufanya Anayoyakataza na usimame (usivuke) katika mipaka Yake.

Pia inapasa kutambua kwamba (سبحانه وتعالى) huenda Akachelewesha jibu kwa muda mrefu kama vile Alivyomcheleweshea kumtakabalia Nabiy Ya’quwb kuhusu kumrudisha kwake mwanawe Yuwsuf. Naye ni ni Nabiy mtukufu (عليه السلام) . Pia kama alivyochelewesha kumpa shifaa Nabiy Wake Ayyuwb (عليه السلام) .

Na huenda Allaah Akampa muombaji yaliyo kheri zaidi kuliko aliyoyaomba na huenda Akamuepusha na shari (ikawa kheri kwake) kuliko aliyoyaomba kama tulivyoitaja katika Hadiyth iliyotangulia:

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ (رضي الله عنه)  أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ وَلاَ قَطِيعَةُ رَحِمٍ إِلاَّ أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثلاَثٍ:  إِمَّا أَنْ تُعَجَّلَ لَهُ دَعْوَتُهُ وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الأَخِرَةِ وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنْ السُّوءِ مِثْلَهَا))  قَالُوا إِذًا نُكْثِرُ قَالَ:  ((اللَّهُ أَكْثَرُ))

Kutoka kwa Abu Sa’iyd(رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وسلم) amesema: ((Hakuna Muislamu atakayeomba du’aa ambayo haina dhambi wala kukata undugu wa uhusiano wa damu isipokuwa Allaah Atampa mojawapo ya matatu; ima Amharakishie du’aa yake, au Amuwekee akiba Aakhirah au ima Amuepushe nayo ovu kama hilo)) Wakasema: Basi tutazidisha (kuomba du’aa). Akasema: ((Allaah Mwingi zaidi [wa kuongeza])) [Ahmad]

Akabainisha (عليه الصلاة والسلام) kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) huakhirisha jibu mpaka Aakhirah, au Huitakabali duniani, kutokana na hikma kubwa kwa sababu hivyo ina maslahi na manufaa zaidi kwa mja Wake, na Humuepusha na shari kubwa kabisa ikawa ni kheri kwake kuliko kutakabaliwa du’aa yake.

Basi kuwa na husnu-dhwann (dhana nzuri) kwa Allaah na endelea kuomba du’aa....

[Fataawa Ibn Baaz: Hukmu Al-Muswaarahah Bi ’Adami Qabuwl Ad-Du’aa, Juz. 5: 303].

Share