Vipi Tuishi Na Muislamu Mwenye Ukimwi?
Vipi Tuishi Na Muislamu Mwenye Ukimwi?
SWALI:
Assalam aleikum, Swala la ukimwi limekua likiepukwa na Masheikh wetu lakini ukweli ni kwamba umetuathiri sisi pia Waislamu. Swali langu ni, Vipi tunafaa tuishi/ kutangamana na muislamu mwenye ukimwi kulingana na Uislamu?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
1. Muhimu mwanzo kuujua ugonjwa huu vizuri. Kupambanua ya ukweli yaliothibitishwa kutokana na porojo na uvumi wa watu. Yaani namna unavyoambukizwa, athari yake na kadhalika. Tukisha fahamu hayo itakuwa rahisi kujua namna ya kuamiliana na aliyeathiriwa na ugonjwa huu. (Kuna makala kadhaa Alhidaaya kuhusu mas-alah haya).
Mathalan, ukimwi hauambukizwi kwa mtu kula na muathiriwa sahani moja, lakini anaweza kuambukizwa kwa kujamiiana baina ya mume aliyeathirika na mke wake ambaye hana ugonjwa huo, au kinyume chake.
Si lazima iwe mtu amezini ndio aambukizwe ukimwi, ijapokuwa maradhi haya asili mia kubwa huambukizwa kwa kupitia kwa njia ya ngono. Mas-ala ya kunyanyapaa au kuganzaganza (stigmatization) yamesambaa kwa hali ya juu sana katika mujtamaa wa Kiislamu. Na ni jukumu la kila mmoja wetu kufanya bidii ili kuondosha ao kupunguza hali hii katika mujtamaa wetu.
Kwa hivyo ni muhimu sana kujua uhakika wa mambo.
2. Akiwa mume ameathiriwa, na mke hajaambukizwa ugonjwa huo, basi mke ana haki ya kuomba talaka kwa kupitia kwa Qaadhi, kwa sababu ya kuhatarisha maisha yake, au ikiwa ni kinyume chake basi mume ana haki ya kumpa talaka mkewe aliyeambukizwa.
3. Ikiwa mmoja kati ya wanandoa au wote wawili wameathirika, na wameishi kwa muda mrefu pamoja na hawataki kuachana, wanaweza kuishi na wanaruhusiwa kutumia mipira (condom) wakati wa kujamiiana, au njia inayokubalika kishari’ah ya kumaliza matamanio yao kama kuchezeana hadi kumaliza haja yao. Njia isiyokubalika kishari’ah ni kuingiliana nyuma ambayo ni haraam na kitendo kichafu kabisa.
Na Allaah Anajua zaidi