Sumayyah Ummu 'Ammaar (رضي الله عنها)

 

Sumayyah Ummu 'Ammaar  (رضي الله عنها)

 

Muhammad Faraj Saalim (Rahimahu Allaah)

 

 

Bibi Sumayyah (Ummu 'Ammaar) (Radhwiya Allaahu 'anhaa) hakuwa mke wa Rasuli (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na nitakuelezea kisa chake In shaa Allaah.

 

 

Yafuatayo ni majina ya wake za Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam);

Khadiyjah binti Khuwaylid - 'Aaishah bint As - Swiddiyq - Hafswa binti 'Umar bin Khattwaab - Zaynab binti Jahash - (Ummu Habiybah) Ramlah binti Abu Sufyan - Sawdah binti Zam-a - Swafiyah binti Huyay - Maymuna bintil - Haarith - Zaynab Al - Hilaliyah - Juwayriyyah bintil - Haarith - Maria Al - Qubtwiyah – (Ummu Salamah) Hind binti Suhail, (Radhwiya Allaahu 'anhum).

 

 

Ama kisa cha Sumayyah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) ni kama ifuatavyo;

Jina lake ni Sumayyah binti Khubat  akijulikana kwa umaarufu wake (Ummu 'Ammaar) - yaani mama yake 'Ammaar -. Bibi huyu ni mtu wa mwanzo kufa shaahid kwa ajili ya Uislaamu na alikufa baada ya kuteswa sana na makafiri.

 

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akipita chini ya nyumba yao na kuwasikia wakiadhibiwa, alikuwa akiwaombea du'aa na akiwaambia;

“Subirini enyi watu wa nyumba ya Yaasir, kwa hakika miadi yenu ni Pepo”.

 

 

Walikuwa wakimtesa Bibi Sumayyah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) huku wakimtaka aiache dini ya kiislaamu na kurudi katika ukafiri, lakini yeye hakuwa akikubali, na kwa ajili hiyo wakaendelea kumtesa mpaka akafa Shaahid baada ya Abu Jahal kumpiga kisu kifuani pake na kumuua.

 

 

Ukoo huu ni miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika dini hii ya Kiislamu.

Jina la mumewe ni Yaasir bin 'Amiyr bin Maalik bin Kinaanah bin Qays Al Answariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) na asili yake alikuwa ni mtu wa Yemen na alikwenda Makka yeye na ndugu zake Al-Haarith na Maalik baada ya kuitwa na ndugu yao 'AbduLLaah aliyekuwa akiishi huko Makka.

 

 

Haarith na Maalik wakarudi Yemen na Yaasir akabakia Makka akiwa chini ya himaya ya mtu mmoja aitwae Abu Hudhayfah bin Al - Mughiyra bin Makhzuwm na akamuowa mmoja katika vijakazi wake aitwae Sumayyah baada ya kumuacha huru na wakapata mtoto waliyempa jina la 'Ammar (Radhwiya Allaahu 'anhu).

 

 

Ulipokuja Uislaam, Yaasir na ndugu yake 'AbduLLaah pamoja na Sumayyah na mtoto wao 'Ammaar wote wakaingia katika dini hii na kuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kusilimu.

 

 

Hapo ndipo walipoanza kupata kila aina ya mateso na adhabu lakini nuru ya Uislaamu iliyokwishajaa katika nyoyo zao iliwafanya wastahamili yote hayo.

'Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhu) siku moja walimtesa sana na kumtaka amtukane Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au watamuuwa, ikambidi awadanganye kwamba amerudi katika dini yao  akamtukana Rasuli (Swalla Allaahu 'alayh wa aalihi wa sallam) kwa kuwalaghai ili wasimtese zaidi.

 

 

Aliporudi kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuelezea juu ya yote hayo, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuuliza;

“Lakini vipi ndani ya nafsi yako unajionaje?”

'Ammaar akamwambia;

“Iymaan imetulia ndani yake”.

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhu wa aalihi wa sallam) akamwambia;

“Kama watarudia tena basi na wewe rudia”.

 

 

Ndipo ilipoteremshwa kauli Yake Subhanahu wa Ta'aalaa isemayo;

 

 

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٠٦﴾

 

106. Atakayemkufuru Allaah baada ya iymaan yake (atapata adhabu) isipokuwa yule aliyekirihishwa (kukanusha Dini ya Kiislamu) na huku moyo wake umetua juu ya iymaan. Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu. [An-Nahl: 106]

 

 

Baada ya mateso kuzidi, 'Ammaar akahajir kwenda Madiynah. Alipigana katika vita vya Badar na Uhud na vya Khandaq na alikuwepo siku ya Fungamano la ‘Aqabah.

 

 

HITIMISHO

Bibi Sumayyah (Radhwiya Allaahu 'anhu) pamoja na mumewe na mtoto wao na Waislaamu wengi wa mwanzo walipata tabu nyingi na mateso mengi sana lakini walistahamili kwa kutegemea malipo mema kutoka kwa Mola wao.

 

 

 

Kutokana na iymaan iliyothibiti ndani ya nyoyo zao na baada ya kutambua kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee itakayomletea mtu maisha matukufu hapa duniani na kesho Aakhera wakaridhika kuzipoteza roho zao kwa ajili ya kupata radhi za Mola wao Subhanahu wa Ta'aalaa.

 

Share