Al-Lajnah Ad-Daaimah: Usiseme ‘Swadaqa Allaahu Al-‘Adhwiym’ Baada Ya Kusoma Qur-aan
Usiseme ‘Swadaqa Allaahu Al-‘Adhwiym’ Baada Ya Kusoma Qur-aan
Al-Lajnah Ad-Daaimah
(Watu wengi katika jamii wana mazoea baada ya kumaliza kusoma Qur-aan, kusema ‘Swadaqa Allaahu Al-‘Adhwiym’. Wengi wakiwa wameathirika kwa mazoea ima ya kusikia kwenye radio au ya kuona video mbalimbali au Misikitini kutoka kwa wasomaji Qur-aan mbalimbali walio mashuhuri.
Ada hiyo, haina dalili yoyote katika shariy’ah. Bali ni kinyume na ilivyothibiti kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na waja wema waliotangulia).
Baada ya kumaliza kusoma Qur-aan usiseme ‘Swadaqa Allaahu Al-‘Adhwiym’, lakini sema:
سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ، أشهد أن لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ، أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتُوبُ إِلَيْك
“Subhaanaka Allaahumma wa Bihamdika, Ash-hadu Allaa ilaaha illa Anta, Astaghfiruka wa Atuwbu ilayka.”
Ni jambo la ki-Sunnah ambalo wanaghafilika nalo watu wengi baada ya kumaliza kusoma Qur-aan.
Ushahidi juu ya hilo ni Hadiyth kutoka kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliposema:
“Hajapatapo kukaa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kikao chochote na wala hajawahi kusoma chochote kwenye Qur-aan , na wala hajaswali Swalaah yoyote ila alikhitimisha (alimalizia kikao hicho) kwa maneno (fulani).
Nikasema:
“Ee Rasuli wa Allaah, ninakuona hukai kikao chochote, wala humalizi kusoma Qur-aan, wala humalizi kuswali Swalaah yoyote ila unakhitimisha (unamalizia) kwa kusema maneno hayo?
Akasema (Rasuli Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Ndio, yeyote ambaye atasema khayr atakhitimishiwa khayr hiyo. Na ambaye atazungumza maovu basi maneno (haya) yatakuwa ni kafara kwake (kwa yale maovu aliyoyasema katika kikao chake hicho).
سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ، أشهد أن لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ، أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتُوبُ إِلَيْك
“Subhaanaka Allaahumma wa Bihamdika, Ash-hadu Allaa ilaaha illa Anta, Astaghfiruka wa Atuwbu ilayka.”
[Umetakasika Ee Rabb wangu, na Himidi ni Zako, Nashuhudia kwa hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Nakuomba maghfirah na natubia Kwako.]
[Hadiyth hii Isnaad yake ni sahihi kaitoa Imaam An-Nasaaiy kwenye ‘Sunan Al-Kubraa.’
Na amesema Al-Haafidhw Ibn Hajr katika ‘An-Nukat’, mj. 2, uk. 733, kuwa Isnaad yake ni sahihi.
Na amesema Imaam Al-Albaaniy katika ‘Silsilat Al-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah, mj. 7, uk. 495, kuwa Isnaad hii ni sahihi vilevile kwa sharti ya Imaam Muslim.
Imaam An-Nasaaiy kaikusanya Hadiyth hii kwenye Sunan yake na akaiwekea mlango aliouita, “Chenye (Maneno) Kukhitimishiwa Kisomo Cha Qur-aan.”
Hivyo basi, baada ya ushahidi huo juu, na kukosekana ushahidi wa yale yaliyozooleka na watu wengi, kusema ‘Swadaqa Allaahu Al-‘Adhwiym’ baada ya kumaliza kusoma Qur-aan ni bid’ah; jambo lililozushwa katika Dini, na hivyo, watu wajiepushe na matumizi ya neno hilo katika mahali hapo.
Na kulijaalia neno 'Swadaqa Allaahu Al-‘Adhwiym' na mfano wake kuwa ndio la kukhitimishia kisomo cha Qur-aan ni bid’ah (uzushi).
Kwa sababu haijathibiti kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliyasema hayo maneno baada ya kumaliza kisomo cha Qur-aan. Na lau yangekuwa maneno hayo yapo kishariy'ah basi angeyasema mwisho wake ( wakati anapomaliza kusoma Qur-aan).
Na kwa hakika imethibiti kutoka kwake kwamba amesema:
"Yeyote atakayezua katika jambo (Dini) letu, lile ambalo halimo humo, basi atarudishiwa.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Wa bi-LLaahit-Tawfiyq wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyinaa Muhammad wa aalihi wa Swahbihi wa sallam.
[Al-Lajnatu Ad-Daaimah Lil-Buhuwth Al-‘Ilmiyyah Wal-Iftaa [Fatwa Namba 7306]