Habbat Sawdaa: Manufaa Yake - 2

 

Habbat-Sawdaa: Manufaa Yake - 2

 

Imekusanywa Na: Iliyaasah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 

  عن أبي هريرة رضي الله عنه أنه سمع رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: «في الحَبَّةِ السوْدَاءِ شِفَاءٌ من كل دَاءٍ إلاَّ السَّام

Amesimulia Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba kamsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Katika Habbat-Sawdaa kuna Shifaa (Poza) ya kila maradhi isipokuwa sumu.” [Al-Bukhaariy]

 

Kunyonyoka Nywele

 

Saga unga wa Habbat-Sawdaa katika juisi ya chirichiri   pamoja na kijiko cha siki nyepesi na kikombe cha mafuta ya zeituni, halafu sugua kichwani kwa mafuta hayo kila siku jioni pamoja na kukiosha kichwa kwa maji na sabuni kabla ya kupaka.

 

Maumivu ya Kichwa

 

Chukua unga wa Habbat-Sawdaa, karafuu iliosagwa nusu ya kiwango cha Habbat-Sawdaa na anisuni (anise), halafu changanya pamoja. Chukua kiasi cha kijiko kimoja (cha chai), wakati wa kuumwa na kichwa, na ule na maziwa lala (mala), pamoja na kupasugua mahala paumapo kwa mafuta ya Habbat-Sawdaa.

 

Ukosefu Wa Usingizi

 

Chukua kijiko cha Habbat-Sawdaa, uchanganye na gilasi ya maziwa moto yaliochanganywa na asali, baada ya kupoa kiasi unywe.

 

Chawa Na Mayai Yake

 

Chukua unga wa Habbat-Sawdaa uliosagwa vizuri usage kwenye siki mpaka uwe kama marhamu au losheni (lotion), halafu jipake kichwani. Baada ya kunyoa nywele au kuisugua marhamu kwenye vizizi vya nywele, halafu kaa kitako katika mwanga wa jua kitambo cha robo-saa. Na usioshe kichwa ila baada ya masaa matano. Utafanya hivyo kila siku kwa muda wa wiki moja.

 

Kisunzi Na Maumivu Ya Sikio

 

Tone moja la mafuta ya Habbat-Sawdaa ndani ya sikio husafisha sikio, pamoja na kuyanywa na kusugua sehemu za panda na nyuma ya kichwa, humaliza kisunzi.

 

Upaa Na Mabaka

 

Utachukua kijiko cha unga wa Habbat-Sawdaa, siki kiasi cha kikombe kimoja na juisi ya kitunguu saumu kiasi cha kijiko kidogo, vyote hivyo utavichanganya na vitakua namna ya   marhamu, utajipaka baada ya kunyoa sehemu ya nywele na kuchanja kidogo – kisha utafunga bendeji, utaiacha mpaka asubuhi, baadae utajipaka mafuta ya Habbat-Sawdaa,utaendelea hivyo kwa muda wa wiki moja.

 

Malengelenge ya Neva katika Ngozi

 

Jipake mafuta ya Habbat-Sawdaa au marhamu yake sehemu ya malengelenge. Fanya hivyo mara tatu kila siku mpaka iondoke kwa Uwezo wa Allaah.  

 

Maradhi Ya Wanawake Na Uzazi

 

Dawa kubwa inayosahilisha kuzaa ni Habbat-Sawdaa iliochemshwa ikachanganywa na asali na kiziduo cha babunaji (chamomile). Habbat Sawdaa ni kama burashi katika uke wa mwanamke yenye faida kubwa kwao pamoja na kutumua mafuta ya Habbat-Sawdaa katika kila kinywaji cha moto kwa maradhi yote ya wanawake.

 

Meno Na Maumivu Ya Mafido na Koo

 

Kiziduo cha Habbat-Sawdaa na kutumia kwa kusukutua kwa kugogomoa, husaidia mno maradhi yote ya mdomo na koo, vivyo hivyo pamoja na kubugia kijiko cha Habbat-Sawdaa na kumeza kwa maji yenye vuguvugu kila siku na kujipaka mafuta yake sehemu ya koo kwa nje na kuusugua ufizi kwa ndani. 

 

Maradhi Ya Tezi

 

Chukua unga wa Habbat-Sawdaa na uchanganye  na asali na mkate wa nyuki kila siku, kwa kipindi cha mwezi mmoja. 

 

Chunusi (Acne)

 

Chukua unga wa Habbat-Sawdaa changanya katika mafuta ya ufuta (simsimu) pamoja na kijiko cha unga wa ngano. Vyote hivyo ujipake usoni kuanzia jioni hadi asubuhi, halafu utaosha kwa maji yenye vuguvugu kwa sabuni. Utaendelea kufanya hivyo kwa muda wa wiki moja. Na uwe ukinywa mafuta ya Habbat-Sawdaa katika kinywaji chochote cha vuguvugu.

 

Maradhi Yote ya Ngozi

 

Chukua mafuta ya Habbat-Sawdaa, mafuta ya waridi (marashi jabali) na unga wa ngano asili, vyote hivyo kwa viwango sawa, ule unga wa ngano uwe zaidi kuliko mafuta, halafu uchanganye vizuri. Kabla ya kujipaka, upanguse sehemu yenye ungonjwa kwa kitambaa kilichoroweshwa siki nyepesi, halafu kaa kwenye jua, baadae ujipake dawa hio kila siku. Lakini ujizuie na kila chenye kuchochea hisia kama vile, samaki, mayai, maembe na mfano wake.                                                  

 

Chunjua (Wart)

 

Chukua unga wa Habbat-Sawdaa uchanganye katika siki nzito na usugue kwa kitambaa cha sufi au katani mahala pa sugu asubuhi na jioni kwa muda wa wiki moja.

 

Kuung`arisha Uso Na Kuurembesha

 

Changanya unga wa Habbat-Sawdaa katika mafuta ya zeituni, na jipake usoni halafu upigwe na mwanga wa jua kidogo. Tiba hiyo utaifanya wakati wowote katika mchana na siku yeyote.

 

Kuunganisha Mvunjiko Haraka

 

Supu ya adesi (dengu), kitunguu maji pamoja na yai la kuchemsha na kijiko kikubwa cha unga wa Habbat-Sawdaa, utachanganya na supu hiyo japo siku baada ya siku; halafu unywe. Na utasugua sehemu zilizo karibu na mvunjiko kwa mafuta ya Habbat-Sawdaa, na baada ya kufungua bendeji utajisugua kwa mafuta ya Habbat-Sawdaa yenye vuguvugu; kila siku.

 

Mvilio Wa Damu (Contusion)

 

Chemsha vizuri konde moja la Habbat-Sawdaa katika chombo cha maji, kisha utakiingiza kiungo kilichovilia damu ndani ya maji hayo ya vuguvugu kwa muda wa robo saa au zaidi pamoja na kukitaharakisha kiungo hicho. Baada ya hapo utajipaka mafuta ya Habbat-Sawdaa bila ya kufunga kitu. Lakini hutakiwi kukipa uzito kiungo hicho au kukitaabisha. Tiba hiyo utaifanya kila siku kabla ya kulala.

 

Baridi Yabisi (Rheumatism)

 

Chemsha mafuta ya Habbat-Sawdaa na sugua kwayo ile sehemu yenye ugonjwa, usugue kwa nguvu kama kwamba unasugua mfupa wala sio ngozi! Na utayanywa baada ya kuyachemsha vyema na kuyachanganya na asali kidogo. Utaendelea na tiba hiyo kwa muda hadi upone.

 

 (Ki) Sukari (Diabetes)

 

Utachukua unga wa Habbat-Sawdaa kiasi cha kikombe kimoja, manemane (myrrh) iliosagwa kiasi cha kijiko kikubwa. Pia Habbat-Rashaad au Habbat-Hamraa (Cress seeds), nusu kikombe, komamanga iliosagwa kiasi cha kikombe kimoja, mzizi wa kabichi uliosagwa baada ya kukaushwa kiasi cha kikombe kimoja na kijiko kidogo cha mvuje. Vyote hivyo utavichanganya na utakula kabla ya kula chakula kiasi cha kijiko kimoja, utakula na maziwa lala ili iwe rahisi kumeza.

 

Shinikizo la Damu (High Blood)

 

Kila unywapo kinywaji cha vuguvugu, tia matone machache ya mafuta ya Habbat-Sawdaa. Pia ujipake mafuta hayo mwili wote, japo wiki mara moja.  

 

Uvimbe Wa Figo (Nephritis)

 

Tengeneza kibandiko (cha kitambaa) kutokana na unga wa Habbat-Sawdaa uliochanganywa katika mafuta ya zeituni, kisha utabandika sehemu yenye maumivu ya figo pamoja na kubugia funda la kijiko cha Habbat-Sawdaa kila siku kabla ya kula chakula kwa muda wa wiki moja tu; uvimbe utakwisha In Shaa Allaah.

 

Kuvunjavunja Vijiwe Vya Tumboni

 

Chukua unga wa Habbat-Sawdaa kiasi cha kikombe kimoja kisha uchanganye katika kikombe cha asali, na utasaga kitunguu saumu punje tatu; utakua ukichukua nusu yake ule kabla ya kula chakula kila siku. Pia itakua bora lau utakula limau kila baada ya kula dawa; kwani husafisha kabisa.

 

Kukojoa Kwa Maumivu (Dysuria)

 

Paka mafuta ya Habbat-Sawdaa juu ya kinena kabla ya kulala pamoja na kunywa kikombe cha mafuta hayo yaliochemshwa na kutiwa asali; kila siku kabla ya kulala.  

 

Jongo (Edema)

 

Weka kibandiko (cha kitambaa) cha unga wa Habbat-Sawdaa uliochanganywa katika siki juu ya kitovu, kwanza ataweka kitambaa. Pia utakula Habbat-Sawdaa kijiko kimoja asubuhi na jioni kwa muda wa wiki moja.

 

Kifuko Cha Nyongo Na Vijiwe Vyake

 

Chukua Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kimoja, manemane iliosagwa robo kijiko na asali kiasi cha kikombe kimoja; vyote hivyo atavichanganya viwe mraba (kama jamu); halafu awe akila kila asubuhi na jioni.

 

Wengu

 

Weka kibandiko (kilichopashwa moto) cha Habbat-Sawdaa iliochanganywa katika mafuta ya zeti katika ubavu wa kushoto, jioni. Na wakati huo huo kunywa kikombe cha kiziduo cha uwatu kilichochanganywa na asali na mafuta ya Habbat-Sawdaa kidogo, utaendalea na dawa hiyo kwa muda wa wiki mbili mfululizo.

 

Maradhi Yote ya Kifua na Baridi

 

Chukua mafuta ya Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kikubwa utie kwenye maji halafu uyaweke juu ya moto mpaka ianze kufuka moshi, hapo uanze kuuvuta ule moshi puani huku ukiwa umejifunika kichwa ili ule moshi usiende upande mwingine. Utafanya hivyo kila siku kabla ya kulala, pamoja na kunywa kiziduo cha zaatari kilichochanganywa na unga wa Habbat-Sawdaa; asubuhi na jioni.

 

Mchango (Msokoto Wa Tumbo) (Colic)

 

Chemsha vyema anisuni (anise)kamuwn (cumin) na nanaa kwa vipimo sawa kisha tia asali kidogo, halafu tia matone saba ya Habbat-Sawdaa; kunywa kinywaji hicho kikiwa na vuguvugu pamoja na kupaka mafuta ya Habbat-Sawdaa mahala panaposokota. Baada ya muda mchache maumivu yataondoka.

 

Kuharisha

 

Chukua juisi ya chirichiri iliochanganywa na unga wa Habbat-Sawdaa kijiko kikubwa, kisha kunywa kiasi cha kikombe kimoja mara tatu kwa siku.

 

Uziwi

 

Chemsha Habbat-Sawdaa pamoja na karafuu, na kunywa bila ya kuongeza kitu; mara tatu kwa siku.

 

Gesi Na Maumivu

 

Bugia unga laini wa Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kimoja kabla ya kula chakula ukifuatisha gilasi ya maji yenye vuguvugu iliotiwa asali kiasi cha vijiko vitatu. Utakariri kila siku kwa muda wa wiki moja.

 

 

.../3

Share