Kumwita Mtoto Jina La Maulaana

 

SWALI:

Je naweza kumwita mtoto wangu jina lake "Mulana" bin Fulani.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kama tunavyokariri kusema kila wakati kuwa Uislam ni Dini kamili inayokidhi mahitaji yote ya mwanadamu. Uislam ni mfumo kamili wa maisha katika kila nyanja katika masaa 24 ya kila siku yetu. Uislam umetupatia muongozo katika mas-ala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiafya na mengineo mengi. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: "Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote" ().

Katika mfumo huu kamili Uislam umetupatia muongozo kuhusu kupeana majina. Hii ni ada ya kijamii ya mtoto kupatiwa jina azaliwapo. Uislam umetilia maanani sana jambo hili na kuliwekea hukumu zake. Kwa hilo, Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: "Enyi mlioamini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu" (49: 11).

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuwekea mfumo ambao tunaupata katika dondoo zifuatazo:

1.  Inafaa mzazi amchagulie jina zuri mtoto wake kama alivyosisitiza hilo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Kwa yakini siku ya Qiyaama mtaitwa kwa majina yenu na kwa majina ya baba zenu. Basi yaboresheni majina yenu" (Abu Daawuud).

 

2.    Majina yaliyo bora kuitwa mtoto ni 'Abdullaah na Abdur-Rahmaan (Muslim).

 

3.  Haifai kwa mzazi kumpatia mtoto wake jina baya. Hilo limekatazwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka akawa anayabadilisha majina hayo. 'Aa'ishah (Radhiya Allaahu 'anha) amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akilibadilisha jina baya" (at-Tirmidhiy).

 

Binti fulani wa Ibn 'Umar alikuwa akiitwa  Aasiya (muasi), Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akambadilisha na kumuita Jamiylah (mzuri) (at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

 

4.  Asimuite jina linaloashiria ukorofi na kisirani. Babu yake Sa'iyd bin Musayyib amesema: "Nilimwendea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza: 'Nani jina lako?' Nikamwambia: 'Naitwa Hazn (gumu)'. Akasema: 'Wewe ni Sahl (wepesi)'" (al-Bukhaariy).

 

5.  Haifai kumuita mtoto jina ambalo ni maalum kwa ALLAAH (Subhaanahu wa Ta'ala) kama vile al-Ahad (mmoja pekee), Asw-Swamad (Mwenye kukusudiwa kwa haja zote), Allah, al-Khaaliq (Muumbaji), ar-Razzaaq (Mwenye kuruzuku), na kadhalika. Yupo mtu ambaye alipewa lakabu na kaumu yake ya Abal Hakam (baba wa hukumu) na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akambadilisha na kumuita Abu Shurayh (baba wa mtoto wake mkubwa Shurayh). Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema aliye khabithi mno siku ya Qiyaama ni yule aliyejiita Malikul Muluk (mfalme wa wafalme) kwani hakuna mfalme ila ALLAAH.

 

6.   Mzazi anafaa ajiepushe na majina yenye baraka au fali njema ili isije ikaleta karaha kujibu hayupo wakati aitwapo. Majina hayo ni kama Aflah (aliyefaulu), Naafi (mwenye manufaa), Yasaar (usahali). Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Maneno yapendezayo zaidi kwa Allaah ni manne: Subhaanallah, Alhamdullillah, Laa ilaaha illa Llah na Allaahu Akbar. Usimuite mwanao Yasaar, wala Rabaah wala Najiih wala Aflah. Kwani utauliza: 'Yuko huko?' Halafu mtu aseme: 'Laa (hayuko)'. Hayo ni manne, msinizidishie" (Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).

 

7. Mzazi anafaa asimuite mtoto majina yanayoabudishwa asiyekuwa Allaah kama vile 'Abdul-'Uzza (mja wa 'uzza   (mungu sanamu), 'Abdul-Ka'bah (mtumwa wa Ka'bah), 'Abdun-Nabiy (mtumwa wa Nabii) na kadhalika.

Hizi ni baadhi ya kanuni ambazo zipo katika Uislam lau tutazifuata basi hatutapata shida katika kuwachagulia watoto wetu majina yaliyo mazuri.

Ama kuhusu swali lako ikiwa tutakuwa tumekuelewa vyema unaposema Mulana labda unamaanisha Mawlaana (lenye maana ya Mola au bwana, mtukufu). Kwa kuchukua maana ya pili ambayo inatumika sana jina hilo halina neno kuitwa mtoto lakini ikiwa makusudio na maana ni kuwa jina hili ni tofauti itabidi muulizaji atupatie maana yake ili tuweze kumnasihi.

Neno Mawlaana kwa lugha nyengine kama Ki-Urdu lina maana tofauti. Maana yake ni Shaykh kwa huku kwetu, yaani mtu mwenye ilimu ndio utapata katika vitabu vilivyoandikwa na wanachuoni wa Pakistan au India kwa mfano Mawlana Abul Hasan 'Aliy Nadwi, na kadhalika.

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share