Kuvaa Nywele Za Bandia Kufunika Nywele Turkey Kwa Sababu Ya Kukatazwa Hijaab
SWALI:
Asalaam aleykum, ALLAH akuridhieni kwa kutufundisha uislam. suala la kuweka nywele za bandia, mfano sisi tupo TURKEY na tunasoma katika mazingira magumu sana ya kiuslam, kwa mfano wasichana haturuhusiwi kuingia na hijabu shuleni na hata darasani. kwa hiyo huwa wanavaa mawigi na wachache wao huwa wanavaa makofia fulani ambayo huwa yanaficha nywele zao but walimu wengine huwa wanjua kwamba kwamba lengo la kuvaa lile kofia ni kuficha nywele kwa hiyo huwa wanawavua au wnawatoa darasani.kutokana na shida hii huwa wanaamua kuvaa nywele za bandia, naomba fatwa kuhusu hili....!
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.Mtume (swala llahu alayhi wasalam) amekataza kwa Muislamu kuvaa nywele za bandia na anayefanya hivyo atapata laana ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama ilivyokuja dalili katika Hadiyth ifuatayo:
Mwanamke wa Ki-Answaariy aliyemuozesha binti yake ambaye nywele zake zilianza kung'ooka. Mwanamke huyo wa Ki-Answaariy alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtajia kwamba "Mumewe (mume wa mwanangu) ameona kwamba nimwachie avae nywele za bandia" Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Usifanye hivyo kwani Allaah Huteremsha laana Yake kwa wanawake kama hao wanaoongeza nywele za bandia) [Al-Bukhaariy 7:133 kutoka kwa Mama Wa Waumini 'Aaishah Radhiya Allaahu 'anha]
Ikiwa kama kuna dharura yoyote ile na ambayo itapelekea kukosekana kwa maslahi Fulani ya mtu kujisaidia katika maisha yake basi ataruhusiwa kwa dharura. Ama kwa ambaye chuo chake kimemkataza kutekeleza sheria ya Allaah atalazimika kumtii Mwenyezi Mungu na atafute Chuo ambacho anaweza kutekeleza Sheria ya Mwenyezi Mungu na huku akiendelea na masomo yake, kwa sababu haifai kumridhisha kiumbe yeyote katika maasi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((على المرء المسلم السمع والطاعة فيما أحب وكره إلا أن يؤمر بمعصية، فإن أمر بمعصية فلا سمع ولا طاعة) رواه مسلم .
((Muislamu inampasa asikie na atii katika anayoyapenda na anayoyachukia isipokuwa anapoamrishwa katika maasiya. Anapoamrishwa kufanya maasiya basi asisikie wa kutii)) [Muslim]
Na Allaah Anajua zaidi
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
