Al-Husayn Bin 'Aliy (رضي الله عنه)

 

  Al-Husayn Bin 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhumaa)

 

Muhammad Faraj Saalim As-a'ay (Rahimahu Allaah)

 

 

Manukato mazuri ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Ukoo wake

 

Jina lake ni Al-Husayn bin 'Aliy bin Abi Twaalib bin 'Abdil-Muttwalib bin Haashim bin Manaaf bin Qusay kutoka katika kabila la Ki-Quraysh tumbo la Bani Haashim, na umaarufu wake ni; 'Abu 'Abdullaah' na maana yake ni Baba yake 'Abdullaah.

 

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) ni mjukuu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kipenzi chake, mtoto wa pili wa 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu) na mama yake ni Bibi Fatimah binti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ndugu zake ni wengi, lakini mashuhuri katika hao ni kaka yake Al-Hasan bin 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhuma) Khalifa wa tano wa Waislamu.

 

Amesema Ja'afar Asw-Swaadiq (Radhwiya Allaahu 'anhu):

"Baina ya Al-Husayn na Al-Hasan kaka yake ni twahara moja."

 

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikufa Shahiyd katika mji wa Karbalaa - Iraq mwaka wa 61 Hijri tarehe kumi mwezi wa Muharram akiwa na umri wa miaka 57.

 

 

Kuzaliwa kwake

 

Alizaliwa Madina tarehe 5 Shaaban mwaka wa 4 wa Hijri na mara baada ya kuzaliwa alipelekwa kwa babu yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyemlisha tende baada ya kuilainisha kwa mdomo wake mtukufu.

 

Alipotimia siku saba, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa jina la Al-Husayn akamchinjia mbuzi wa 'Aqiyqah na kumuamrisha mama yake amkate nywele zote kisha azitolee sadaka kiasi cha uzito wake.

 

 

Anasema Imam Ahmad katika Musnad yake katika hadithi iliyopokelewa na 'Aliy bin Abi Talilb (Radhwiya Allaahu 'anhu):

 

"Alipozaliwa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimpa jina la ami yake Hamza na alipozaliwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimpa jina la Ja'afar. Anasema Aliy: "Akaniita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: 'Nimeamrishwa nibadilishe majina ya hawa wawili.' Nikamuambia: "Allaah na Mtume wake ndio wenye kujua zaidi." Akawapa majina ya Al-Hasan na Al-Husayn." [1]

 

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki dunia, Al-Husayn alikuwa na umri wa miaka mitano. Abubakar (Radhwiya Allaahu 'anhu) Khalifa wa mwanzo wa Waislamu alikuwa akiwapenda sana Al-Husayn pamoja na kaka yake Al-Hasan na alikuwa akiwakirimu na kuwatukuza, na hali ilikuwa hivyo pia alipotawala ‘Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu).

 

 

Wake zake

 

  1. Shaharbano binti Yizd Jard bin Shahriyar Kisra (mama yake Ali Zayn Al Abdidiyn)
  2. Laylah binti Murrah Al Thaqafiyah (mama yake Ali Al Akbar)
  3. Ummu Ja'afar Al Qadhaiyah (alifariki wakati wa uhai wa 'Aliy bin Abi Talib
  4. Ar-Rabaab bint Mru'ul Qays Al Kilaabiyah (mama yake 'Abdullaah Al Radhiy'a na Sakina bintil Hussayn)
  5. Ummu Is'haq bin Talha bin Abdullah

 

 

Wanawe

 

  1. Ali Al Akbar (mkubwa)
  2. Ali Al Asghar ( 'mdogo' au As-Sajjaad)
  3. 'Abdullaah Al Radhiy'a (au Ash-Shahiyd aliyeuliwa pamoja na baba yake Karbalaa akiwa mtoto mchanga)
  4. Ja’afar
  5.  Sakinah
  6. Faatimah
  7. Ruqayyah
  8. Zaynab

 

Inasemekana pia kuwa alikuwa na Ali Al Awsat (Ali wa kati) na Muhammad

 

 

 

Baadhi ya sifa zake

 

Imepokelewa kutoka kwa Hani bin Hani kutoka kwa 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa amesema:

"Al-Husayn amefanana sana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kifuani mpaka nyayoni."

Imepokelewa kutoka kwa Hammaad bin Zayd kutoka kwa Hishaam kutoka kwa Muhammad kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa alisema:

"Nilikuwepo siku ile Ibn Ziyad alipokuja na kichwa cha Al-Husayn akiwa anakichocha kwa kijiti. Nikasema: "Hakika amefanana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)."

Kutoka kwa 'Abdullaah bin Abi Yazid alisema:

"Nilimuona Al-Husayn bin 'Aliy. Nywele na ndevu zake zilikuwa nyeusi sana isipokuwa baadhi ya ndevu zake sehemu ya mbele."

Kutoka kwa Abi Nuumin alisema:

"Nilikuwa kwa 'Abdullaah bin ‘Umar bin Khattwaab, akaja mtu kuuliza juu ya damu ya mbu. 'Abdullaah bin ‘Umar akamuuliza:

"Ni mtu wa wapi wewe?"

Akamuambia:

"Mtu wa Iraq."

'Abdullaah bin ‘Umar akamuambia:

"Muangalieni mtu huyu, ananiuliza juu ya damu ya mbu wakati wao ndio waliomuua mjukuu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na mimi nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema :"Al-Hasan na Al-Husayn ni manukato yangu mazuri ya hapa duniani."

Kutoka kwa Abu Ayub Al Ansariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema:

"Niliingia nyumbani kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nikawakuta Al-Hasan na Al-Husayn wakicheza juu ya kifua chake. Nikamuuliza: "Unawapenda?"

Akaniambia: "Vipi nisiwapende wakati hawa ndio manukato yangu mazuri ya hapa duniani."

[Attabarani katika Muujam yake]

 

Anasema Imam Adh-Dhahabiy katika 'Siyar aalam an-Nubalaa' kuwa; hadithi kama hii zimepokelewa pia kutoka kwa Ibni ‘Umar na Ibni ‘Abbaas na ‘Umar na Ibni Mas’uud na Malik bin Al Huwayrith na Abi Sa’iyd na Hudhayfa na Anas na Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhum) kupitia njia mbali mbali zenye kuipa nguvu.

 

Imepokelewa pia kuwa siku moja Al-Hasan na Al-Husayn walipoingia msikitini, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

"Mwenye kupenda kuwaangalia mabwana wa vijana wa Peponi awaangalie hawa."

Na kutoka kwa Imam Ahmad na Attabarani na Attirmidhiy kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

"Husayn ni mjukuu katika wajukuu. Mwenye kunipenda basi ampende na Al-Husayn pia."

Imepokelewa pia katika hadithi sahihi kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Al-Hasan na Al-Husayn ni mabwana wa vijana wa Peponi."

Na akasema:

"Mola wangu mimi ninawapenda na Wewe wapende pia."

 

 

 

Maisha yake

 

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa akimpenda na kumheshimu sana na mtiifu kwa baba yake 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu), na alikuwa akimpenda na kumtii pia kaka yake Al-Hasan (Radhwiya Allaahu 'anhu).

Juu ya kutoridhika kwake siku ile kaka yake alipojiuzulu ukhalifa kwa ajili ya kumuachia Mu’awiyah bin Abi Sufyan (Radhwiya Allaahu 'anhu), Al-Husayn alinyamaza na hakushindana naye.

Al-Hasan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipofariki dunia wakati wa ukhalifa wa Mu’awiyah, Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa katika nchi ya Constantinople akipigana jihadi, na wakati huo Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ndiye aliyekuwa Khalifa wa Waislamu.

Mu’awiyah akiwa bado yuhai aliamua kumrithisha mwanawe Yazid ukhalifa. Jambo hilo halikumridhisha Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliyekataa kufungamana naye kwa sababu aliona kuwa yeye ndiye anayestahiki zaidi kuliko Yazid. [2]

 

 

Darja yake

 

Watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 'Ahlul Bayt' wana daraja kubwa sana ndani ya nyoyo za kila Muislamu. Tunawapenda, tunawaheshimu na tunawasalia na kuwasalimia na kuwaombea dua na rehma kila tunapomsalia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Isipokuwa hatuzidishi kama wanavyofanya wenye kuvuka mipaka katika mapenzi yao katika kusujudu mbele ya makaburi yao na kuomba msaada kutoka kwao badala ya kuelekeza dua zao kwa Allaah Subhanahu wa Taala. Sisi tunawaheshimu na kuwaombea dua kama alivyotufundisha Allaah katika kitabu Chake kitukufu Aliposema:

"Na walio kuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu walio tutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walio amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu."

Al Hashr- 10

 

Al-Husayn na kaka yake Al-Hasan (Radhwiya Allaahu 'anhum) wao pia wana daraja kubwa sana kwetu Waislamu, kama tulivyoona katika hadithi nyingi zilizotangulia.

 

Tunaamini pia kuwa kuuliwa kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) ni msiba mkubwa sana kwa Waislamu na kwamba amekufa shahiyd tena kishujaa. Na tunaamini kuwa kuuliwa kwake ni dhulma kubwa sana iliyofanywa na kikundi kilichopewa amri hiyo na 'Abdullaah bin Ziyad, lakini sisi hatuigeuzi siku aliyouliwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) kila mwaka kuwa ni siku ya makumbusho na maombolezo na vilio na kujipiga vifua na kumwaga damu na kuwalaani watu, bali sisi daima tunasema kama alivyotufundisha Allaah katika kitabu Chake kitukufu:

"Sema: Ewe Allaah! Muumba mbingu na ardhi! Mjuzi wa yasiyo onekana na yanayo onekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika waliyo kuwa wakikhitalifiana."

Az-Z’Umar – 46

 

Allaah Amependa kumnyanyua zaidi Al-Husayn na kumpa daraja hiyo ya ushahiyd, na ametaka kuwadhalilisha waliyemuua na kuwalipa wanachostahiki.

Anasema Shaykh Al-Islam Ibn Taymiyah:

"Allaah Amemkirimu kwa kumruzuku kifo cha shahiyd, na Amemdhalilisha aliyemuua na kila aliyeshirikiana naye au kuridhika na kitendo hicho. Na yeye Al-Husayn anayo mifano mema kwa waliomtangulia katika njia hiyo, na Allaah Anasema:

"Na uwape habari njema wanaosubiri. Ambao uwapatapo msiba husema:"Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake Yeye tutarejea."

Al Baqarah – 155-156

 

 

Daraja yake mbele ya Masahaba (Radhwiya Allaahu 'anhum)

 

Katika kitabu cha 'Tariykh' cha Ibni Asakir, imeandikwa; Kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Kalbiy amesema: "Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisema kumuambia mtu mmoja wa kabila la Kikureshi: 'Utakapoingia ndani ya msikiti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ukaona vifungu vya watu wanasoma darsi, utakapoliona fungu ambalo watu wanaosikiliza wametulia kimya kama kwamba ndege wametua juu ya vichwa vyao wanaogopa wasiruke, basi ujuwe kuwa hapo ndipo penye darsi ya Abu 'Abdullaah (Al-Husayn) (Radhwiya Allaahu 'anhu), mahali hapo hapana mchezo hata kidogo. [3]"

 

Na katika Tariykh pia; Kutoka kwa Hammad bin Salamah kutoka kwa Abil Muhzim amesema: "Tulikwenda kusalia jeneza la mwanamke, na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa pamoja nasi. Likaletwa na jeneza la mwanamume na kuweka ubavuni mwake na kusaliwa. Tulipokuwa tukipeleka majeneza, Al-Husayn alichoka akakaa katikati ya njia. Abu Hurayrah akakaa karibu yake huku akipangusa mchanga ulio miguuni mwa Al-Husayn. Al-Husayn akamuambia: "Ewe Abu Hurayrah, kwa nini unafanya hivi?" Abu Hurayrah akamuambia: "Niache. Kwani wallahi lau kama wangekujua vizuri watu, basi wangekunyanyua juu ya mabega yao."

 

Imepokelewa katika kitabu cha Tariykh pia kuwa; Wakati wa ukhalifa wa ‘Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) zililetwa nguo kutoka Yemen, na ‘Umar alikuwa amekaa baina ya mimbari ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kaburi lake akigawa nguo. Wakatokea Al-Hasan na Al-Husayn kutoka katika nyumba ya mama yao Faatimah (Radhwiya Allaahu anha). ‘Umar alijaribu kuwachagulia nguo awape lakini hakupata za kiasi chao, akasema: "Wallahi sioni furaha yoyote ndani ya nafsi yangu mpaka nikupatieni na nyinyi." Wakasema: "Ewe amiri wa waumini, si haba, umeweza kuwavisha watu wengi." Akaagizia nguo nyingine kiasi chao kutoka Yemen, na zillipowasili alifurahi sana akasema: "Sasa hivi imeingia furaha ndani ya nafsi yangu. [4]"

 

 

 

Ukhalifa wa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu 'anhu) (kaka yake Al-Husayn)

 

Ili kuifahamu vizuri sira ya Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu), hatuna budi kurudi nyuma kidogo angalau kwa muhtasari kuidurusu historia kuanzia siku ile aliyouliwa Khalifa wa nne wa Waislamu, 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu) baba yake Al-Husayn.

Baada ya 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuuliwa, watu wa mji wa Al-Kuufah - Iraq - walifungamana na mwanawe Al-Hasan bin Ali (Radhwiya Allaahu 'anhuma) awe Khalifa wa tano.

Baada ya fungamano kumalizika, jeshi kubwa liliondoka kuelekea Sham 'Syria', kwa sababu watu wa Sham walikuwa mpaka wakati ule hawataki kuutambua ukhalifa wa Amiril Muuminin 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu).

Aliondoka na jeshi kwa nia ya kufanya sulhu na watu wa huko kwa sababu Al-Hasan (Radhwiya Allaahu anhu) anajulikana kuwa yeye ni mtu asiyependa vita. Inajulikana pia kuwa tokea hapo mwanzo wakati watu wa Sham walipokataa kuutambua ukhalifa wa baba yake, na baba yake alipoamua kupeleka majeshi kwa ajili ya kupambana na watu wa Sham, Al-Hasan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimnasihi sana baba yake kutofanya hivyo.

Dalili nyingine ni kule kumuondoa Qais bin Saad katika uongozi wa jeshi na kuliweka chini ya uongozi wa 'Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhuma).

Kutoka kwa Al-Hasan Al Basriy (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisema:

"Nilimsikia Abubakar akisema: "Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akihutubia, akaja Al-Hasan. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Mwanangu huyu ni bwana. Na huenda Allaah kupitia kwake akasuluhisha baina ya makundi mawili ya Waislamu."

Al-Bukhaariy

Mu’awiyah na Al-Hasan hatimaye walikutana, na Al-Hasan alikubali kumuachia ukhalifa Mu’awiyah, na mwaka ule ukaitwa 'Mwaka wa umoja'.

 

 

 

Ukhalifa wa Mu’awiyah bin Abi Sufyan (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Abubakar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alihukumu muda wa miaka miwili na miezi mitatu kisha akafariki dunia.

Na ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alihukumu muda wa miaka kumi, na ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu anhu) alihukumu miaka kumi na mbili na Ali (Radhwiya Allaahu 'anhu) miaka mine na miezi tisa, na Al-Hasan (Radhwiya Allaahu anhu) alihukumu muda wa miezi sita.

 

Utawala wa Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu 'anhu) uliendelea kwa muda wa karibu miaka ishirini mpaka mwaka wa 60 Hijri, na wakati wote huo hapakuwa na matatizo ya aina yoyote katika dola ya Kiislamu, bali kulikuwepo na ufunguzi na kutekwa kwa nchi nyingi za kikafiri, na utulivu ulienea katika maeneo yote ya dola kubwa ya Kiislamu.

Katika muda huo alifariki dunia Al-Hasan bin 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu), ikasemekana kuwa alitiliwa sumu ndani ya chakula chake, na ukweli anaujuwa Allaah peke yake, kwani hapana dalili yoyote yenye isnadi sahihi yenye kutuhakikishia juu ya jambo hilo, lakini inajulikana kuwa alifariki dunia katika mwaka wa 49 Hijri. [5]

 

 

 

Kuteuliwa kwa Yazid bin Mu’awiyah

 

Katika mwaka wa 50 Hijri, Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimteuwa mwanawe Yazid kuwa khalifa wa Waislamu baada yake, akawataka watu wafungamane naye.

Maulamaa wengi wanasema kuwa hapa Mu’awiyah alikwenda kinyume na mwenendo wa Makhalifa waongofu waliotangulia.

Wanasema kuwa fungamano hilo ni sahihi kisheria isipokuwa lina baadhi ya makosa yakiwemo:

 

1- Kuanzisha uzushi mpya kwa kumrithisha mwanawe ukhalifa wakati hapo mwanzo ukhalifa ulipatikana kwa mashauriano baina ya Waislamu kwa kumchagua mtu asiyekuwa na uhusiano wa kiaila na Khalifa.

2- Walikuwepo wenye kuustahiki zaidi ukhalifa kuliko Yazid kama vile 'Abdullaah bin ‘Umar na 'Abdullaah bin Az-Zubayr na Al-Husayn bin 'Aliy na wengi wengine (Radhwiya Allaahu 'anhum).

Amesema Ibn Al-‘Arabiy:

"Mu’awiyah ameacha lililo bora zaidi, nalo ni kujaalia Ukhalifa upatikane kwa mashauriano bila ya kumuingiza yeyote katika watu wa aila yake, wachilia mbali mwanawe. Hata hivyo watu walikubali kufungamana naye, na kwa ajili hiyo fungamanao lilikuwa sahihi kisheria [6].

 

 

 

Yazid alistahiki kuwa Khalifa?

 

Ibni Kathiyr alitaja kisa cha 'Abdullaah bin Mutiy'a na sahibu zake waliomuendea Muhammad bin Al-Hanafiyah mtoto wa 'Aliy bin Abi Twaalib, ndugu kwa baba wa Al-Hasan na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhum), wakamuambia:

"Yazid hastahiki kuwa Khalifa kwa sababu anakunywa pombe na hasali swala zake sawa sawa."

 

Muhammad bin Al Hanafiyah akasema:

"Mimi sikuyaona hayo mnayoyasema. Nilionana naye na nilikaa kwake. Ni mtu anayesali swala zake sawa sawa na ni mwenye kupenda kheri. Anapenda kujifunza elimu ya fiqhi na kufuata mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)."

Wakasema:

"Huenda alikuwa akifanya hayo mbele yako tu."

Muhammad akasema:

"Anaogopa nini hata afanye hivyo? Mlimsikia yeye mwenyewe akisema hivyo?"

Wakasema:

"Sisi tunaona hivyo tu, hata kama hatukumsikia wala kumuona."

Muhammad akawaambia:

"Allaah amewakataza Waislamu kusema bila dalili." Kisha akawasomea kauli ya Allaah isemayo:

"Isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua."

Al Zukhruf-86

 

Kwa hivyo zile habari kuwa Yazid alikuwa akinywa ulevi ni uvumi tu, na hapana isnadi yoyote sahihi yenye kuthibitisha hayo. Kisheria ni haramu kwa Muislamu kumtuhumu mwenzake bila ya dalili.

Na kutokana na kauli ya Muhammad bin Al-Hanafiya (Radhwiya Allaahu 'anhu), ambaye ni ndugu wa Al-Hasan na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) tunapata dalili kuwa Yazid hakuwa hivyo.

 

 

 

Ukhalifa wa Yazid bin Mu’awiyah

 

Yazid alitawala mwaka wa 60 Hijri na wakati huo alikuwa na umri wa miaka 36, na katika watu waliokataa kumtambua ni Al-Husayn na 'Abdullaah bin Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu 'anhum) ambao wakati huo walikuwepo Madina, na walipotakiwa kwa lazima kumtambua Yazid waliondoka na kukimbilia Makkah.

 

 

Watu wa Iraq wanamuandikia Al-Husayn

 

Habari ziliwafikia watu wa Iraq kuwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) amekataa kufungamana na Yazid bin Mu’awiyah, na kwa vile hawakuwa wakimtaka Yazid, bali hawakuwa wakimtaka hata Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu 'anhu) baba yake Yazid. Wao hawamtaki mwengine isipokuwa 'Aliy bin Abi Twaalib na wanawe (Radhwiya Allaahu 'anhum).

Wakaanza kumuandikia Al-Husayn bin 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) wote kwa pamoja wakimuambia: "Sisi tunafungamana na wewe tu na hatumtaki mwengine isipokuwa wewe."

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipoona kuwa barua nyingi sana (kwa maelfu) zinamfikia, alimtuma mtoto wa ami yake Muslim bin ‘Aqiyl akachunguze hali ilivyo huko Al-Kuufah ili apate kujuwa ukweli wa mambo.

Alipowasili huko na baada ya kuulizia na kufanya upelelezi, Muslim alielewa ukweli kuwa watu wa huko hawamtaki Yazid, bali wanamtaka Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu).

 

Alifikia nyumba ya mtu mmoja anayeitwa Hani bin Uruwah, na makundi makubwa mkubwa ya watu yalikuwa yakimuendea kufungamana naye kuwa wanamtaka Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) awe Khalifa wao.

Habari juu ya makundi hayo ya watu zilimfikia Nu’umaan bin Bashir gavana wa Yazid wa Al-Kuufah, ambaye hakuonyesha kukasirishwa wala hakujaribu kuwazuwia watu wala hata kumuarifu Khalifa Yazid.

Hata hivyo watu walizifikisha habari hizo kwa Yazid na kumuarifu juu ya kutojali kwa Nu’umaan juu ya yanayotendeka huko, na Yazid akaamua kumuondoa Nu’umaan katika ugavana na kumuweka badala yake ‘Ubaydullah bin Ziyad aliyekuwa pia gavana wa mji wa Basra.

‘Ubaydullah aliwasili Al-Kuufah nyakati za usiku akiwa amejifunika uso. Ikawa kila anapowasalimia makundi ya watu walikuwa wakimjibu: "Wa alaykumussalaam ewe mwana wa binti yake Mtume wa Allaah." Wakimdhania kuwa ni Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu). Kwa sababu aliingia usiku akiwa ameufunika uso wake.

‘Ubaydullah akaelewa kuwa ni kweli watu wanasubiri kuwasili kwa Al-Husayn. (Radhwiya Allaahu 'anhu).

 

‘Ubaydullah alipowasili katika kasri yake alimtuma mtu mmoja aitwae ‘Aqiyl akapeleleze na kuwaletea jina la mkubwa wa mpango huo. ‘Aqiyl akawadanganya watu kuwa yeye ni mtu kutoka mji wa Hims aliyekuja na Dinari elfu tatu kwa ajili ya kuchangia kuja kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu). Akawa anauliza na kuuliza mpaka akaifikia nyumba ya Hani bin Uruwah akaingia na kumkuta Muslim bin ‘Aqiyl humo. Akafungamana naye na kumpa zile Dinari elfu tatu.

Akawa pamoja nao mpaka alipopata habari zao kwa ukamilifu, ndipo aliporudi kwa ‘Ubaydullah bin Ziyad na kumpa habari zote.

 

 

Kuuliwa kwa Muslim bin ‘Aqiyl

 

Baada ya watu wengi kufungamana naye, na kuhakikisha kuwa mipango yote inakwenda kama ilivyopangwa, Muslim bin ‘Aqiyl alimuandikia Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) kumtaka aje Iraq.

Ubaydullah bin Ziyad baada ya kutambua juu ya matayarisho ya kuja kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu), alituma askari kwenda kumkamata Hani bin Uruwah, na walipomuendea na kumuuliza: "Yuwapi Muslim?" Hani akawajibu: "Sijuwi yuko wapi. Wallahi lau kama amejificha chini ya miguu yangu basi sitoinyanyua."

 

‘Ubaydullah akampiga Hani kisha akaamrishwa atiwe jela.

Habari zikamfikia Muslim bin ‘Aqiyl aliyeondoka na jeshi la watu wapatao elfu nne na kuizunguka kasri ya ‘Ubaydullah bin Ziyad, na watu wa Al-Kuufah wote wakatoka na kumuunga mkono.

Wakati huo viongozi wa makabila makubwa ya Al-Kuufah walikuwa ndani ya kasri ya ‘Ubaydullah aliyewataka wawatishe watu wao ili waache kumuunga mkono Muslim.

 

Wakatoka na kuwatisha kuwa jeshi kubwa linakuja kutoka Sham, jambo lililoingiza hofu ndani ya nyoyo zao, na kidogo kidogo, mmoja baada ya mwengine wakaanza kuondoka na kumuacha mkono Muslim bin ‘Aqiyl. Alitoka na jeshi la watu elfu nne akajikuta amebakiwa na watu wapatao thelathini tu, na kulipopambazuka Muslim alijikuta amebaki peke yake. Wote wamekwishamkimbia.

Walipotambua kuwa Muslim amebaki peke yake, likatumwa jeshi la watu wapatao sabini na kulizunguka hema lake. Walijaribu mara tatu kuingia ndani ya hema lakini Muslim alipambana nao kwa upanga wake na kuwatoa nje kila wanapojaribu.

Wakaamua kumrushia mawe, na yeye akaamua kuwatokea nje na kupambana nao, akawaua wengi na mwisho wakakubaliana nae kuwa aondoke hapo na kurudi alikotoka, na Muslim akakubali

 

Muslim akaondoka na kuanza kuzunguka katika barabara za mji wa Al-Kuufah. Kiu kilimshika akagonga mlango wa nyumba ya mwanamke mmoja wa kabila la Bani Kinda na kuomba maji.

Bibi alimuuliza: "Nani wewe?"

Akamuambia: "Mimi ni Muslim bin ‘Aqiyl." Kisha akamuhadithia habari zake na namna watu walivyomuacha mkono na kwamba Al-Husayn atakuja kwa sababu keshaarifiwa. Yule bibi akamkaribisha nyumbani kwake, akamletea maji na chakula, lakini mwanawe akampelekea habari ‘Ubaydullah bin Ziyad aliyetuma askari wengine wapatao sabini. Wakaizunguka nyumba na Muslim akatoka na kupambana nao lakini hatimaye wingi uliushinda ushujaa, akaishiwa nguvu ikambidi asalimu amri.

Wakamchukua na kumpeleka katika kasri ya ‘Ubaydullah bin Ziyad huku akikabbir na kumtaja Allaah.

‘Ubaydullah akamuuliza:

"Kipi kilichokuleta huku?"

Muslim akasema: "Fungamano na Al-Husayn bin 'Aliy liko juu ya shingo yetu."

‘Ubaydullah akamuambia: "Nitakuua."

Akasema: "Kabla ya kuniua niruhusu niusie."

Akamuambia: "Usia."

Akageuka huku na kule akamuona ‘Umar mtoto wa Sa’ad bin Abi Waqaas. Akamuambia: "Wewe ndiye uliye karibu zaidi na mimi. Kwa Rehma ya Allaah nakuusia." Akamshika mkono, akaenda naye pembeni kidogo na kumtaka amtume mtu kwenda kwa Al-Husayn na kumuambia kuwa arudi alikotoka. ‘Umar akamtuma mtu kumjulisha Al-Husayn kuwa mpango wao umekwishajulikana na kwamba watu wa Al-Kuufah wamekwenda kinyume na ahadi zao.

Katika maagizo ya Muslim ni kauli mashuhuri sana aliyotaka aambiwe Al-Husayn nayo ni:

"Rudi wewe na watu wa nyumba yako, na wasikubabaishe watu wa Al-Kuufah. Watu wa Al-Kuufah wamekudanganya na wamenidanganya mimi pia. Na mtu muongo hana rai."

Muslim bin ‘Aqiyl akauliwa siku ya Arafat na wakati huo Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliondoka Makkah Sikukuu mosi kuelekea Iraq kabla ya kuuliwa Muslim kwa siku moja.

 

 

 

Masahaba wanamnasihi Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Masahaba wengi walijaribu kumzuia Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) asiondoke, wakiwemo 'Abdullaah bin ‘Umar na 'Abdullaah bin ‘Abbaas na 'Abdullaah bin Amru bin Al Aas na Abu Sa’iyd Al-Khudry na 'Abdullaahi bin Az-Zubayr na Muhammad bin Al-Hanafiyah – ndugu yake kwa baba (Radhwiya Allaahu 'anhum).

Wote hawa waliposikia kuwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) anataka kwenda Al-Kuufah walimkataza.

 

1. 'Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimuambia: "Ingelikuwa sioni  vibaya kufanya hivyo mbele ya watu, basi ningelikuzuia kwa nguvu zangu zote usiende huko. Bora ubaki hapa usiende Iraq kwani watu wa Iraq ni wenye njama na wanapenda kwenda kinyume. Bora nenda Yemen kwani huko kuna ngome na watu wema." Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) akamuambia: "Ewe mwana wa ami yangu. Wallahi naelewa vizuri kuwa unaninasihi na ni mwenye huruma, lakini mimi nishatia azma ya kwenda kwa hivyo sitorudi nyuma." Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) akamuambia: "Basi kama huna budi nenda peke yako usiwachukuwe watoto wako na wanawake, kwani nahofia usije ukauliwa kama alivyouliwa ‘Uthmaan huku wanawe na wanawake wakishuhudia."

 

2. "Imepokelewa kuwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa Makkah alipopata habari kuwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) keshaondoka kuelekea Iraq. Alifunga safari ya mwendo wa siku tatu mpaka alipomfikia. Akamuuliza: "Unakwenda wapi?" Akamuambia: "Iraq." Kisha akamuonyesha barua alizopokea kutoka kwa watu wa Iraq akimtaka aende huko na kwamba watu wote huko wako pamoja naye. Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akamuambia: "Usiende." Lakini Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikataa. Akamuambia: "Nitakuhadithia hadithi. Jibril alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamhiarisha achague baina ya dunia na akhera, akachagua akhera na hakuitaka dunia. Na wewe ni sehemu yake (asili yako inatokana na yeye) Wallahi Allaah hajauweka mbali nanyi (ufalme) isipokuwa kwa hekima yake ya kukutakieni yaliyo bora zaidi." Hata hivyo Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikataa kurudi. 'Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akamkumbatia huku akilia sana. Kisha akamuaga kwa kumuambia: "Buriani." Nina hakika kuwa unakwenda kuuliwa."

 

 

3. 'Abdullaah bin Zubayr (Radhwiya Allaahu anhu) naye alimuambia Al-Husayn: "Unakwenda wapi? Unakwenda kwa watu waliomuua baba yako na ndugu yako? Usiende." Lakini Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikataa katakata.

 

4. Abu Sa’iyd Al-Khudry (Radhwiya Allaahu 'anhu) naye alimuambia: "Ewe Aba 'Abdullaah! Mimi nakunasihi, na mimi nakuhurumieni. Nimesikia kuwa wamekuandikieni baadhi ya wafuasi wenu huko Al-Kuufah wakikutakeni muende kwao. Msiende. Nilimsikia baba yako akiwa Al-Kuufah akisema: "Wallahi nimewachoka na kuwachukia, na wao wamenichoka na kunichukia, na mimi nimechoka nao na kuwachukia. Hawana utiifu hata kidogo. Aliyekuwa pamoja nao amepata hasara kubwa. Wallahi hawana nia nzuri wala azimio jema katika jambo, wala hawana subira mbele ya upanga."

 

 

5. Alipokuwa njiani kuelekea Iraq alikutana na mshairi maarufu Al Farazdaq, akamuuliza: "Unatokea wapi". Akamuambia: "Iraq." Al-Husayn akamuuliza: "Nini habari zao?" akamuambia: "Nyoyo zao ziko pamoja nawe na panga zao ziko pamoja na Bani Umayyah." Akasema: "AAllaahul Mustaaan. [7]"

 

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa njiani akielekea Iraq wakati zilipomfikia habari za kuuliwa kwa ‘Aqiyl kwa njia ya mjumbe aliyetumwa na ‘Umar bin Sa’ad. Ikampitikia arudi, lakini baada ya kuwashauri watoto wa Muslim bin ‘Aqiyl wakamuambia: "Hapana. Tusirudi mpaka tulipe kisasi cha baba yetu". Al-Husayn akaikubali rai yao.

 

Alipopata habari za kuwasili kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu), ‘Ubaydullah bin Ziyad alituma jeshi la watu wapatao elfu moja chini ya uongozi wa Al Hurr bin Yazid At-Tamimiy kwenda kumzuia asiweze kuingia Al-Kuufah. Na alipokutana naye karibu na mji wa Al Qadisiyah akamuuliza:

"Unakwenda wapi ewe mwana wa binti yake Mtume wa Allaah?"

Akamuambia: "Nakwenda Iraq."

Akamuambia: "Basi mimi nakuamrisha urudi ili Allaah asinipe mtihani wa kupambana na wewe. Bora urudi ulikotoka, au uende Sham alipo Yazid, lakini usiende Al-Kuufah."

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikataa na akaendelea na safari yake kuelekea Al-Kuufah, na Al Hurr akawa anajaribu kumzuia Al-Husayn.

Al-Husayn akamuambia: "Kaa mbali na mimi, akukose mama yako."

Al Hurr akamuambia: "Wallahi neno hilo angeliniambia mwengine yeyote nisingemuacha, lakini nifanye nini na hali mama yako ni bibi wa mabibi wa ulimwengu. [8]"

Al Hurr akamuuliza: "Kitu gani kilichokuleta?"

Akamuambia: "Barua zenu na wajumbe wenu."

Al Hurr akasema: "Barua gani na wajumbe gani?

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) akasema: "Ewe ‘Uqbah zilete zile barua."

Akazitoa barua nyingi sana.

Al Hurr akasema: "Sisi si katika waliokuletea barua hizi. Sisi tumeamrishwa kukukamata na kukupeleka kwa ‘Ubaydullah bin Ziyad.

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) akasema: "Mauti ni bora kuliko hayo." Akapanda farasi wake, na sahibu zake nao wakapanda farasi wao na kuondoka kuelekea Karbalaa huku jeshi la Al Hurr likimfuata na kujaribu kumzuia.

 

 

 

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) anawasili Karbalaa

 

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) akaendelea na safari mpaka alipowasili Karbalaa. Akauliza: "Panaitwaje mahali hapa?" Wakamuambia: "Karbalaa". Akasema: "Kurab na balaa." Na maana yake ni (misiba na balaa), na hii ilikuwa siku ya pili ya Muharram mwaka 61 [9].

Kikosi kingine cha jeshi la ‘Ubaydullah chini ya uongozi wa ‘Umar bin Sa’ad kikawasili, na kumtaka Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) afuatane nao kwa ‘Ubaydullah bin Ziyad. Al-Husayn alikataa na kumtaka ‘Umar amruhusu ende Sham kwa Yazid. ‘Umar akataka muda ende kumshauri ‘Ubaydullah, na ‘Ubaydullah akakubali, lakini katika majlis yake palikuwepo na mtu aitwae Shumar bin Dhil Jawshan aliyesema: "Hapana Wallahi! Tusimruhusu. Sisi ndiye tutakayempeleka Sham." ‘Ubaydullah akapendezewa na fikra hiyo, akasema: "Kweli, lazima tumpeleke chini ya ulinzi wetu."

‘Ubaydullah akamuambia Shumar: "Nenda wewe ukamlazimishe akubali kusalimu amri na kupelekwa kwa Yazid chini ya ulinzi wangu, na ikiwa ‘Umar ataregarega basi chukua wewe uongozi."

Shumar akaondoka na kuelekea mahali alipo Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) akiwa amezungukwa na jeshi la ‘Umar bin Sa’ad na Al Hurr bin Yazid At-Tamimiy, na alipojulishwa kuwa lazima apelekwe Sham chini ya ulinzi wa askari wa ‘Ubaydullah bin Ziyad alikataa akawaambia: "La Wallahi! Sikubali kusalimu amri kwa ‘Ubaydullah bin Ziyad."

 

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa na watu sabini na mbili wakati jeshi la Iraq lilikuwa na watu wapatao elfu tano. Na pande mbili hizo zilipokabiliana Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alilihutubia jeshi la ‘Ubaydullah na kuwaambia: "Jiulizeni vizuri; Je! Inajuzu kupigana vita na mtu kama mimi? Mimi ni mwana wa binti yake Mtume wenu, na hapana ulimwenguni mwana wa binti wa Mtume isipokuwa mimi. Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema juu yangu pamoja na kaka yangu: "Hawa ni mabwana wa vijana wa Peponi."

Akawanasihi waliache jeshi la ‘Ubaydullah na kuungana naye, na watu thelathini wakakubali kujiunga naye akiwemo kiongozi wao Al Hurr bin Yazid At-Tamimiy.

Wakamuuliza Al Hurr: "Wewe umekuja ukiwa kiongozi wetu na sasa hivi unatuacha mkono?"

Akawaambia: "Ole wenu! Mimi niliishauri nafsi yangu niingie Peponi au Motoni nikachagua Peponi. Wallahi sitochagua kuingia Motoni hata kama nitakatwakatwa na kuunguzwa."

Ulipoingia wakati wa Swalah, Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliwaswalisha makundi yote mawili Swalah ya adhuhuri baada ya kuwauliza kama watapenda kuswali pamoja au kila kundi liswali na imamu wake, na wote kwa pamoja walimtaka yeye awe imamu wao. Na wakati wa alasiri ulipoingia aliwaswalisha tena.

Kabla ya magharibi kuingia walijaribu kuingia ndani ya hema lake, na wakati huo Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa amejinyosha kidogo juu ya tandiko huku akiwa ameushika upanga wake tayari kwa hatari yoyote itakayomkabili. Dada yake alimsikia akisema: "Nimemuota Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyeniambia: "Leo utakuwa pamoja nami."

Kisha Al-Husayn akawauliza: "Wanataka nini?" Watu wake wakamuambia: "Hatujui." Akawaambia: "Kawaulizeni."  Wakatoka watu ishirini juu ya farasi wao akiwemo Al-‘Abbaas bin 'Aliy bin Abi Twaalib ndugu yake Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) wakawauliza: "Mnataka nini?" Wakasema: "Lazima akubali kusalimu amri kwa ‘Ubaydullah bin Ziyad au apigane." Wakawaambia: "Mpaka tumuulize kwanza."

Wakarudi kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) na kumjulisha, akawaambia: "Tupeni muda wa usiku huu mmoja na kesho tutakujulisheni. Niacheni nisali kwa ajili ya Mola wangu kwani mimi napenda kusali kwa ajili ya Mola wangu Mtukufu."

Usiku kucha wakawa wanasali huku wakimuomba Allaah yeye pamoja na waliokuwa naye – Allaah awe radhi nao wote.

 

 

Mapambano yanaanza

 

Asubuhi yake kabla mapambano kuanza, Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliwahutubia wanawe na watoto wa ndugu zake aliokuwa nao, akawaambia: "Nyinyi bora muondoke, nimekwishakupeni ruhusa."

Wakamuambia: "Na watu watasema nini? Kuwa tumemuacha Shaykh wetu na kiongozi wetu na bwana wetu na bin ami yetu bila ya kumhami? Hapana Wallahi hatutofanya hivyo, bali tupo tayari kuzitoa nafsi zetu na za watu wetu na mali zetu muhanga kwa ajili yako. Na tuko tayari kupigana mpaka tufe kwa ajili yako. Yana faida gani maisha baada yako?"

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) akawakabili adui zake, akauchukua msahafu na kuuweka mbele yake kisha akainyanyua mikono yake juu kumuomba Allaah na hapo ndipo mapambano yalipoanza.

Mishale na mkuki ikaanza kuvurumishwa huku na kule, na jeshi kubwa la adui likaanza kushambulia kwa nguvu upande wa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambao juu ya uchache wao walipigana kufa na kupona na wakaweza kuwashinda na kuwarudisha nyuma.

Watu wa jeshi la Ibni Ziyad wakaomba msaada kutoka kwa wenzao. Kikawasili kikosi cha watu wapatao mia tano. Ukaingia wakati wa Swala ya adhuhuri, na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) akamuambia kiongozi wa upande wa pili: "Waamrisheni wasimamishe vita ili tuswali Swala ya adhuhuri." Wakakataa, na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) pamoja na wenzake wakaswali Swala ya hofu huku wakiendelea na mapambano.

 

Jeshi la upande wa pili likaongezeka, wakapata nguvu na kuweza kumkaribia Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu), na watu wa upande wa Al-Husayn walioelewa kuwa hawana uwezo wa kulishinda jeshi hilo kubwa, wakawa wanamzunguka Al-Husayn kumkinga huku wakipambana kwa nguvu zao zote tena bila ya hofu kila mmoja akitamani auliwe mbele yake (Radhwiya Allaahu 'anhum).

Wakaanza kuuliwa mmoja baada ya mwingine mpaka akabaki Al-Husayn (Radhwiya Allaahu anhu) peke yake. Alibaki muda mrefu akiwa amesimama mbele yao kama simba, hapana aliyethubutu kumsogelea, kila mmoja akiogopa kupata mtihani wa kumuua mjukuu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hali ikaendelea hivyo mpaka alipowasili Shumar bin Dhil Jawshan aliyeanza kupiga kelele kuwaambia watu wake: "Ole wenu nyinyi! Mnaogopa nini? Mzungukeni, mfuateni, muueni."

Wakamzunguka Radhwiya Allaahu anhu aliyewakabili kwa upanga wake akipambana nao kwa ushujaa mkubwa akimuua kila aliyejaribu kumsogelea. Akaendelea hivyo mpaka alipochoka na nguvu kuanza kumuishia. Lakini juu ya kuchoka kwake waliogopa kumkaribia.

Shumar akaanza kupiga kelele tena: "Muuweni, mkamateni." Na hapo ndipo mtu mmoja aitwae Zara'a bin Shariyk alipompiga kwa ghafla tena kwa nguvu juu ya bega lake la kushoto, na mwingine aitwae Sinan alimpiga kwa mkuki, na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) akaanguka, na hapo ndipo walipoweza kumuendea na kumkata kichwa chake – Allaah atawashinda Inshaallah. Inasemekana aliyemkata kichwa chake ni Shumar. Na hii ilikuwa siku ya Ijumaa siku ya ‘Ashuraa mwaka wa 61Hijri.

 

Kichwa chake kikachukuliwa na kupelekwa Al-Kuufah kwa ‘Ubaydullah bin Ziyad, na kilipowasili akawa anakichokoa kwa kijiti huku akikiingiza mdomoni mwake. Na Anas bin Malik (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliyekuwepo katika majlis hiyo wakati huo akainuka na kuondoka huku akisema kwa ukali: "Wallahi wewe ni mtu mbaya. Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akipabusu mahali hao unapokipitisha kijiti."

Anasema Abdul Malik bin ‘Umayr: "Niliingia kwa Ibni Ziyad nikakiona kichwa cha Al-Husayn kimewekwa ndani ya chombo. Na Wallahi hazikupita siku nyingi nikaingia kwa Al Mukhtar bin Abi Ubayd nikakiona kichwa cha Ibni Ziyad ndani ya chombo mbele ya Al Mukhtar."

Tutasoma juu ya Al Mukhtar kila tukiendelea mbele na kisa chetu.

 

Imepokelewa kutoka kwa Al Amash kutoka kwa ‘Umara bin Umayr amesema: "Kilipoletwa kichwa cha Ibni Ziyad pamoja na vichwa vya sahibu zake vikawekwa ndani ya msikiti wa Al Rahbah, niliwasikia watu wakiseama: "Kesha kuja kesha kuja tena." Nikaliona joka kubwa lililokuja na kuvipitia vichwa vyote vilivyokuwepo kisha lilipowasili penye kichwa cha Ibni Ziyad likaingia ndani ya pua yake na kubaki humo muda, kisha likatoka na kuondoka taratibu mpaka likatoweka. Nyoka huyo huyo alirudia kufanya hivyo mara mbili au tatu."

Attimidhy 3939

 

Amesema Ibrahim Al-Nukhaiy (Radhwiya Allaahu 'anhu): "Ningelikuwa mimi miongoni mwa waliomuua Al-Husayn kisha nikaingia Peponi, ningeliona haya kuuangalia uso wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)."

Attabarani.

 

 

 

Waliouliwa pamoja na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Waliuliwa pamoja na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) wengi kati ya watu wa nyumba yake.

Katika ndugu zake aliuliwa:

Ja'afar na ‘Abbaas na Abubakar na Muhammad na Uthman.

Katika watoto wake:

Ali Al Akbar (huyu si Ali Zayn al Abidiyn) na 'Abdullaah.

Katika watoto wa Al-Hasan:

'Abdullaah na Al-Qaasim na Abubakar

Katika watoto wa ‘Aqiyl:

Ja’afar na 'Abdullaah na Abdur-Rahman na 'Abdullaah bin Muslim na Muslim bin ‘Aqiyl aliyeuliwa Al-Kuufah tokea mwanzo.

Katika watoto wa 'Abdullaahi bin Ja’afar:

Aun na Muhammad

Watu kumi na nane katika watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wote waliuliwa kwa dhulma na uadui katika vita hivi ambavyo idadi ya pande mbili hazikuwa sawa.

Lakini ajabu ni kuwa miongoni mwa waliouliwa waliokuwa pamoja na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) walibeba majina ya Abubakar bin 'Aliy na ‘Uthmaan bin 'Aliy na Abubakar bin Hasan, lakini huwasikii kutajwa unaposikiliza kanda za kaseti za Kishia au unaposoma vitabu vyao vilivyoandikwa juu ya kuuliwa kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu), ili pasisemwe kuwa 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu) na watu wa nyumba yake waliwapa watoto wao majina ya Abubakar na ‘Umar na ‘Uthmaan, na kwamba Al-Hasan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimpa mwanawe jina la Abubakar.

 

Kutoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu anha) amesema: "Jibril alikuwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Al-Husayn alikuwa pamoja nami. Akalia Al-Husayn. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaingia na kumuinamia. Jibril akamuuliza: "Unampenda ewe Muhammad?" Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Ndiyo nampenda."

Akasema: "Hakika umati wako watamuua na ukitaka nitakuonyesha udongo wa ardhi atakaouliwa juu yake." Akamuonyesha, na ardhi hiyo inaitwa Karbalaa."

Imam Ahmad katika 'Fadhail'

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa amesema: "Nilimuota Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika nusu ya mchana nywele zake zikiwa zimetimka na mwili wake umejaa vumbi huku akiwa amebeba chupa ndani yake mna damu. Nikamuuliza: "Ewe Mtume wa Allaah, kitu gani hiki?"

Akasema: "Damu ya Al-Husayn na sahibu zake, sijaacha kuifuatilia mpaka leo."

Anasema ‘Umarah: "Msimulizi wa hadithi hii; tukayahifadhi hayo tukagundua kuwa ile ndiyo siku aliyouliwa."

Imam Ahmad mlango wa 'Musnad 'Abdullaah bin ‘Abbaas'

 

Na hivi ndivyo alivyokufa Shahiyd Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) na aliyeamrisha kuuliwa ni ‘Ubaydullah bin Ziyad ambaye hajaishi muda mrefu naye pia akauliwa, na aliyemuwa ni Al Mukhtar bin Abi Ubayd kwa kulipa kisasi cha Al-Husayn.

Al Mukhtar alikuwa miongoni mwa waliomuacha mkono Muslim bin ‘Aqiyl kama walivyofanya watu wa mji wa Al-Kuufah waliomtaka Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) aje kwao wakamuahidi kuwa watapigana kwa ajili yake.

Wote walimuacha mkono ‘Aqiyl akauliwa, hapana hata mmoja aliyekwenda kumsaidia. Na alipokuja Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) hali ikawa ni ile ile wote walimuacha mkono akauliwa, hapana hata mmoja aliyekwenda kumsaidia isipokuwa Al Hurr bin Yazid At-Tamimiy na wachache aliokuwa nao, hawa ndio waliomsaidia, na wote hawa walitoka katika jeshi la Ubaydullah bin Ziyad. Ama watu wa Al-Kuufah wote walimuendea kinyume wakamuacha mkono, hapana hata mmoja aliyeunyanyua mkono wake kumsaidia. Na hii ndiyo sababu kila mwaka wanaendelea kupiga vifua vyao na kufanya wanayofanya kwa majuto ya makosa yao na ya baba zao, kama wanavyosema katika vitabu vyao.

 

 

Msimamo wa Ahlul Sunnah juu ya kifo cha Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

1-  Kuuliwa kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) ni msiba mkubwa kwa Waislamu wote, hasa kwa vile yeye ni mjukuu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kipenzi chake na manukato yake mazuri. Hata hivyo Waislamu walikwishapitiwa kabla yake na misiba mingi sana ikiwemo kuuliwa kwa Sayiduna 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu) baba yake Al-Husayn, ambaye bila shaka daraja yake ni kubwa zaidi kupita ya Al-Husayn.

 

Kabla ya hapo misiba mikubwa zaidi ilipatikana ya kuuliwa kwa Khalifa wa pili wa Waislamu ‘Umar bin Khattwaab na Khalifa wa tatu ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhum).

Kabla ya wote hao, Mitume ya Allaah kama vile Yahya na Zakariya 'alayhimu swalaatu wa ssalaam nao pia waliuliwa, na hao wote bila ya shaka daraja zao ni kubwa zaidi mbele ya Allaah kuliko Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu).

 

2-  Haijuzu kwa Muislamu anapopatwa na msiba au kwa ajili ya kumbukumbu ya msiba wowote kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama vile kujikatakata, kulia, kupiga vifua nk. Kwani imepokelewa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Hayupo pamoja nasi atakayejipiga makofi ya mashavu akachana nguo zake na kutamka maneno ya kijahilia (yaliyokuwa yakitamkwa na washirikina kabla ya Uislamu)."

Al-Bukhaariy

Na akasema:

"Mimi najitenga mbali na (kila) mwenye kupiga kelele na mwenye kukata nywele na mwenye kuchana nguo." (anapokutwa na msiba).

Muslim – Kitab al Iman

Na akasema:

"Kwa hakika mwenye kuomboleza kwa kupiga kelele asipotubu atavalishwa siku ya Kiama ngao ya shaba na nguo ya moto."

Muslim – Kitab al Iman

Kwa hivyo ni wajibu kwa kila Muislamu anapopatwa na msiba aseme kama alivyotufundisha Allaah Subhanahu wa Taala katika kitabu chake kitakatifu:

"Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake Yeye tutarejea."

Al Baqarah-156

 

3- Zipo riwaya zinazosema kuwa kichwa cha Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) kilipelekwa Sham kwa Yazid na kilipowekwa mbele yake, Yazid alilia sana akasema: "Ningeliridhika na kunitii kwenu tu, bila ya kumuua Al-Husayn. Wallahi ningelikuwa mimi nisingelikuua."

Na ziko riwaya nyingine zinazosema kuwa; kichwa chake hakikupelekwa Sham, bali alizikwa huko Karbalaa mahali alipofariki – Allaah Ndiye Ajuae.

 

 

Msimamo wa Yazid katika kuuliwa kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Anasema Shaykh ‘Uthmaan Al-Khamiys katika kitabu chake 'Hiqbah mina ttariykh':

"Yazid hakushiriki kabisa katika kuuliwa kwa Al-Husayn, wala hakutoa amri hiyo. Na huku si katika kumtetea Yazid, bali Yazid alimtuma ‘Ubaydullah bin Ziyad kumzuia tu Al-Husayn asiweze kuingia mji wa Al-Kuufah, na wala hakumuamrisha kumuua, bali Al-Husayn mwenyewe alielewa hayo akataka aruhusiwe kwenda Sham kwa Yazid ili akauingize mkono wake ndani ya mkono wa Yazid, lakini ‘Ubaydullah alikataa akashikilia kuwa lazima asalimu amri kwake.

 

 

Funga ya ‘Ashuraa

 

Funga ya siku ya ‘Ashuraa haina uhusiano wowote na kuuliwa kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) kama inavyodaiwa, bali inatokana na mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyosimuliwa katika Sahih Al-Bukhaariy kuwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhuma) alisema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoingia Madina aliwakuta Mayahudi wakifunga siku ya ‘Ashuraa akawauliza: "Kwa nini mnafunga siku hii?" wakamuambia: "Hii ni siku tukufu ambayo Allaah alimuokoa Musa na kaumu yake akamzamisha Firauni na kaumu yake. Musa akafunga siku hii kumshukuru Allaah, na sisi tunafunga." Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Na sisi tunamsitahiki zaidi Musa kupita nyinyi." Akafunga Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akaamrisha watu wafunge.

 

 

 

 

Marejeo:

 

Siyar aalaam an Nubalaa -           Imam Adh-dhahaby

Hiqbah minat Tariykh      -           Shaykh Uthmaam Khamiys

Al Bidaayah wan Nihaayah -       Imam Ibni Kathiyr

Maqtal Al_Husayn            -           Naasir bn Muhammad Al Ahmad

 


[1] Imam Ahmad na Abu Yaala na Al Bazaar na Attabarani

[2] Siyar aalam al Nubalaa (Imam Adh-Dhahabiy)

[3] Ibni Asakir katika 'Tariykh'

[4] Ibni Asakir katika 'Tariykh'184/183/14

[5] Hiqbah mina Tariykh (Shaykh ‘Uthman Al-Khamiys)

[6] Hiqbah mina Tariykh (Shaykh ‘Uthman Al-Khamiys)

[7] Al Bidaya wal Nihaya (Ibni Kathiyr)

[8] Maqtal Al-Husayn (Naasir bin Muhammad Al Ahmad)

[9] Abdur-Razzaq Al Musawiy al Muqrum (Man qatal l Hussayn)

 

 

 

Share