Uzushi Wa Du’aa Ya Mara Moja Katika Umri (Maisha)
Uzushi Wa Du’aa Ya Mara Moja Katika Umri (Maisha)
SWALI:
Tunaomba ufafanuzi kuhusu du’aa hii ambayo inaenezwa sana katika mitandao na groups mbalimbali za simu.
Dua Ya Mara Moja Kwenye Umri Wa Binadamu
Amesema Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Madhumuni Ya Hadiyth Inavyosema: Atakaye Soma Dua Hii Mda Wowote
*Ni Kama Mtu Aliyoenda Haji Mara 360
*Ni Kama Mtu Aliyokhitimu Qur-an Mara 360
*Amejikomboa Na Ibada 360
*Na Nisawa Kama Ametoa Sadaka 360 Dinari
*Na Kafariji 360 Huzuni Kubwa
* Na Kama Alivoyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
Kwenye Hadiyth Alishuka Jebreil Akasema : Ee Nabiy wa Allaah Mja Yoyote Kwenye Waja Wa Umma Yako Atakesoma Dua Hii Hata Kama Mara Moja Kwenye Umri Wa Maisha Yake Kwakukanusha Jalali Na Kuhakikisha Mambo Yake Saba
a). Atondolewa Umaskini
b). Ataondolewa Suali La Uovu Na Nakeer
c). Atamururishwa (atapitishwa)katika Njia Yake
d). Atahifadhishwa (ataondolewa)kwenye Kifo Cha Mshituko
e). Ataepushwa Na Moto
f). Ataepushwa Na Ubano Wa Kaburi
g). Ataepushwa Katika Ghadhabu Za Sultan Aljair Na Dhalimu
(na Hii Ndio Dua)
Lailah Ila Allah Aljaleel Aljabaar
Lailah Ila Allah Alwahed Alqahar
Lailah Ila Allah Alkareem Alstaar
Lailah Ila Allah Alkabeer Almuutaaal
Lailah Ila Allah Wahda La Shareekah Lahu
Ilaha Wahed
Rabaa Wa Shahed
Ahadaa Wa Swamadaa
Wa Nahnu Lahu Muslimuun
Lailah Ila Allah Wahdahu La Shareeka Lahu
Aliha Waheda
Rabaa Wa Shaheeda
Ahadaa Wa Swamadaa
Wa Nahnu Lahu Abiduun
Lailah Ila Allah Wahdahu La Shareeka Lahu
Aliha Waheda
Rabaa Wa Shaheeda
Ahadaa Wa Swamadaa
Wa Nahnu Lahu Qaaanitoon
Lailah Ila Wahdahu La Shareeka Lahu
Aleha Waheda
Rabaa Wa Shaheeda
Ahadaa Wa Swamadaa
Wa Nahnu Lahu Swabiruun
Lailah Ila Allah Muhamad Rasul Allah
Allahuma Ilayek Fawadhtu Amri
Wa Aleyka Tawakalt Ya Arhama Alrahmeen
Tusaidiane kuipitisha hata tusiwakoseshe dua hii ndugu zetu wengine
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Haya ni maradhi yaliyotoka kwa Mashia na Masufi waliyoambukizwa baadhi ya Waislamu wasiojishughulisha na elimu, na wao wakadhani ni katika dini na kuna ujira ndani yake, wakajibidiisha kueneza du'aa za kutungwa na kusingiziwa nazo Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Du'aa nyingi kama hizi za kutungwa na kunasibishwa nazo kwa uongo na dhulma kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zinapatikana katika vitabu vya du'aa za uzushi kama "Du'aa Al-Mustajaab", "Al-Jawshan Al-Kabiyr", Du'aa ya "Kanzul-'Arsh" na vinginevyo.
Kamati ya Kudumu ya Utoaji Fatwa na Tafiti za Kielimu ya Saudia chini ya Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) wamesema:
"Kitabu "Ad-Du'aa Al-Mustajaab" si cha kutegemewa kwa sababu kimekusanya idadi kubwa ya Ahaadiyth dhaifu na za kutungwa.
[Fataawa Al-Lajnah Ad-Daaimah, mj. 2, uk.449]
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:
“Ni kitabu ambacho hakiwezi kutegemewa na mtunzi wa kitabu hicho si Mwanachuoni. Hivyo, tumetoa tanbihi kwa muda mrefu na tumeeleza kuwa hicho kitabu si cha kutegemewa. Wasomaji wanapaswa kutanabahishwa kwamba hakitegemewi kwa sababu kimekusanya Hadiyth dhaifu na za kutungwa.
[Fataawa Ibn Baaz, mj. 26, uk. 354-355]
Shaykh Fawzaan (Hafidhwahu Allaah) amesema:
“Kuna kitabu ambacho kimeenezwa sana kwa watu leo hii, na kinapatikana katika maduka ya vitabu, kinaitwa “Ad-Du’aa Al-Mustajaab” cha Muhammad ‘Abdil-Jawwaad. Ni kitabu chenye hekaya kilichokusanya du’aa za kuzushwa za Kisufi na Adhkaar ambazo zimenukuliwa bila dalili zozote kutoka katika Qur-aan na Sunnah.
Jina la kitabu chenyewe lina maelezo ya elimu ya ghayb ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala). Mwandishi kakiita kitabu “Ad-Du’aa Al-Mustajaab (Du’aa Zenye Kujibiwa)”, je, ni nani kamjulisha huyo mwandishi kuwa du’aa hizo zinajibiwa? Ushahidi gani anao kwa hilo, zaidi tu ya kutaka kuwavutia watu ‘awwaam (wa kawaida wasio na elimu) na kuwahadaa kwa kitabu cha uzushi.
Nawashauri wasomaji (watafute na kuvitumia) vitabu vya du’aa na adhkaar vya kuaminika vilivyoandikwa na Wanachuoni weledi wenye kuaminika wa Ahlus-Sunnah:
1. Al-Waabil Asw-Swayyib cha Imaam Ibn Al-Qayyim
2. Al-Kalim Atw-Twayyib cha Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah
3. Al-Adhkaar cha Imaam An-Nawawiy
Vitabu hivi, havina ndani yake adhkaar za uzushi; zimekusanya adhkaar zilizopokelewa kutoka katika Qur-aan na Sunnah.
Vinatosheleza na vinakidhi haja na hakuna haja ya vitabu vya masimulizi ya ngano vilivyoandikwa na wafanya mzaha, na himidi zote ni za Allaah.
[Majmuw’ Fataawa Fadhwiylat Ash-Shaykh Swaalih bin Fawzaan, mj. 2, uk. 697]
Bonyeza viungo upate maelezo zaidi kuhusu vitabu vinginveyo vya bid'ah.
Du’aa Ya Kanzul-'Arsh (Ganjul-'Arsh) Ni Uzushi Wa Mashia Na Masufi
Du'aa Za Kanzul-Arsh Na Du'aa Za Masiku Ya Wiki Zimethibiti?
Du’aa Ya ‘Al-Jawshan Al-Kabiyr’ (Diraya Kubwa) الجوشن الكبير
Na Allaah ni Mjuzi zaidi.