Iyd - Yaliyo Ya Sunnah Na Yaliyo Bid'ah Katika Sherehe Za 'Iyd
'Iyd - Yaliyo Ya Sunnah Na Yaliyo Bid'ah Katika Sherehe Za 'Iyd
www.alhidaaya.com
BismiLLaahi wa AlhamduliLLaah wa swalaatu wa salaam 'alaa RasuliLLaah Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa aswahaabihi wa salam.
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) kumwambia Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
“Kwa kila jamii ya watu kuna sikukuu, na hii ‘Iyd ndiyo sikukuu yetu.” [Al-Bukhaariy na Muslim].
“Sikukuu yetu” ina maana kubwa kwa Waislamu, kwa sababu inatujulisha kwamba hii ni yetu na asili yake imetokea kwenye shariy’ah zetu tu peke yake. Kwa kuwa sherehe hizi zimeegemea kwenye taratibu za kidini, ni muhimu sana kuzifafanua ili ziwe na furaha kubwa na mikusanyiko yenye kuleta hisia ya kuwa hizi sikukuu ni zetu (sisi Waislamu), na ni tofauti na zile sikukuu za Mushrikiyn. Haturuhusiwi kusherehekea Krismasi, Hanuka, au sikukuu za Kipagani, na shukrani zetu zote tuzielekeze kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) peke yake.
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) ametuamrisha katika hutuba zake nyingi kuwa tujitofautishe na Mushrikiyn (Wapagani), na hizi ‘Iyd mbili ni miongoni mwa sikukuu zile ambazo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) ametutaka tuchukue tahadhari kubwa ya kujitofautisha sana nao (Mushrikiyn). Ndiyo sababu akasema, baada ya kuona watu wa Madiynah walipokuwa na sherehe mbili wakizisherehekea kabla ya kuja Uislamu, “Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)) ameshakupeni nyinyi kilicho bora kuliko vyote (sikukuu): ‘Iydul-Adhw-haa (ya kuchinja) na ‘Iydul-Fitwr”. [Ahmad, Abuu Dawuwd na An Nasaaiy].
‘Iydul-Adhw-haa huja baada ya kumalizika ‘ibaadah ya Hajj na ‘Iydul-Fitwr huja baada ya kumalizika Swawm ya mwezi wa Ramadhwaan. Kwa hivyo haishangazi hiyo, ni lazima tuzionyeshe na tuzifafanue ‘Iyd zetu. Kutokana na bayana hizi zilizo wazi, Wanachuoni wa Kiislamu ni lazima watilie mkazo sana juu ya kuzitofautisha sherehe zetu kutokana na zile za Mushrikiyn.
Hii ni kwa sababu sherehe zina taathira kubwa katika akili na tabia ya mwana Aadam. Kuwa tofauti katika Sherehe vile vile ina maana kwamba ni lazima tusijishirikishe (tusihudhurie) kabisa katika sherehe za Mushrikiyn. ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Msijifundishe lugha ya Mushrikiyn – bila ya kuwa kuna umuhimu ndani yake – wala Msiingie makanisani wakati wa sherehe zao kwa sababu Hasira za Allaah huteremka juu yao.” [Al-Bayhaqiy].
Sisi, Waislamu, huenda hata tufunge (Swawm) katika siku za sikukuu za Mushrikiyn. Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anha) amesema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) alikuwa na kawaida ya kufunga siku za Jumamosi na Jumapili, na alipoulizwa Alisema: Kuna siku mbili katika siku za sherehe za Mushrikiyn kwa hivyo napenda kwenda kinyume na wao katika sherehe zao.” [Ahmad na An-Nasaaiy].
Kulikadiria wazo hili la kuwa tofauti na Mushrikiyn, ni muhimu sana kusema kwamba: Ili tuwe tofauti kwenye sherehe zetu na katika mwenendo ambao Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) ametutaka tuwe nao, ni lazima tufuate mwenendo wake (Sunnah) kikamilifu. Kwa kufanya hivyo kutatupatia malipo mema (thawabu) ya kuwa wafuasi wa kweli wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam).
Kwa hivyo, tukitaka kuwa wafuasi wake ni lazima tuelewe ni yepi Bid’ah (uzushi) katika sherehe zetu. Bid’ah inakuja pale Sunnah hutumika mahali pasipo pake! Ibn Taymiyyah amesema:
“Hakuna nafasi katika moyo wa bin Aadam kwa yote mawili; Sunnah na Bid’ah.” [Al-Iqtidhwaa].
Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) Amesema:
“Sema – Ee Muhammad – Ikiwa kweli mnampenda Allaah basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni.” [Aali-‘Imraan, 3:31]
Ndugu wapenzi, tunawasilisha kwenu baadhi ya matendo ya Sunnah katika sikukuu ili muweze kujaribu kuyatekeleza. Vile vile yanawasilishwa baadhi ya yaliyokuwa Bid’ah ili katika sikukuu muweze kuyaepuka. Kuna umuhimu mkubwa sana katika kufuata mwenendo wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) wa ‘Iyd ili kikweli kweli tuweze kusema kwamba sikukuu zetu ni tofauti na zile sikukuu za Mushrikiyn.
Yaliyo Sunnah Katika 'Iyd
Kuvaa Mavazi Mazuri
Siku ya ‘Iyd ni Sunnah kuvaa mavazi mazuri kabisa tuliyo nayo. Imehadithiwa kwamba Ibn ‘Umar alikuwa akifanya hivyo pamoja na Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam). [Fat-hul-Baariy]
Kuswali Swalaah Ya 'Iyd
Ni Waajib kuswali Swalaah ya ‘Iydul-Fitwr kwa kauli yenye nguvu kutokana na Hadiyth ifuatayo:
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) na Maswahaba zake hawakuacha kabisa kufanya hivyo, na vile vile walikuwa wakiwakusanya watu kuitekeleza Swalaah hiyo wakiwemo wanawake wenye hedhi (hawaingii kwenye kuswali lakini wanashuhudia khayr na du’aa kwa Waislamu), watoto na vikongwe. [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kula Tende Kabla Ya Kwenda Kuswali (Katika 'Iydul-Fitwr)
Ni Sunnah kula tende kabla ya kuondoka kuelekea kuswali Swalaah ya ‘Iyd ili kuonyesha kwamba hatujafunga.
“Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) alikuwa hatoki kwenda kuswali Swalaah ya ‘Iyd ila baada ya kula tende.” [Al-Bukhaariy na Ahmad].
Ama katika 'Iydul-Adhwhaa ni Sunnah kutokula kabla ya kwenda Msikitini, na anaposhuka baada ya Swalaah ni bora kitu cha kwanza kula ni ile nyama ya Udhw-hiyah ikiwa itapatikana.
Kuleta Takbira Kwa Sauti
Ni Sunnah kuleta Takbira kwa sauti tunapotoka majumbani mwetu kuelekeya kwenye Swalaah ya ‘Iyd. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) alikuwa akileta Takbira mpaka anamaliza Swalaah. [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy]
Hakuna Hadiyth inayohusiana na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) kwamba nini kisemwe wakati wa kuleta Takbira tunapoelekeya kuswali, lakini Ibn Mas’uud alikuwa akisema yafuatayo:
Allaahu Akbar (Allaah ni Mkubwa zaidi) (mara mbili)
Laa Ilaha Illa Allaah (Hapana muabudiwa wa haki ila Allaah)
Allaahu Akbar (Allaah ni Mkubwa zaidi) (mara mbili)
Wa Lillaahil Hamdu (Na Shukrani Zote ni za Allaah) [Imesimuliwa na Ibn Abiy Shaybah].
Kubadilisha Njia Wakati Wa Kwenda Kuswali Na Wakati Wa Kurudi
Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia:
“Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) alikuwa akirudi kutoka kwenye Swalaah ya ‘Iydul-Fitwr kupitia njia tofauti na ile aliyoendea.” [Al-Bukhaariy]
Kuswali Kwenye Muswallaa
Ni Sunnah kwa wenye kuswali Swalaah ya ‘Iyd kuswali kwenye muswallaa (katika eneo au uwanja ulio wazi) na si Misikitini. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) hakuwahi kuswali Swalaah ya ‘Iyd Msikitini. Abu Sa’iyd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) alikuwa akienda kuswali ‘Iydul-Fitwr na ‘Iydul-Adhw-haa kwenye Muswallaa, na kitu cha awali alichokuwa akikifanya ni kuswali.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Swalaah Ya 'Iyd Haina Adhaana Wala Iqaamah
Jaabir bin Samurah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kasema:
"Niliswali zaidi ya mara moja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salam) na haikuweko Adhana wala Iqaamah." [Muslim]
Hakuna Swalaah Ya Sunnah Kabla Au Baada Ya Swalaah Ya 'Iyd
Ibn ‘Abbaas amesimulia:
“Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) Aliswali rakaa mbili kwa ajili ya ‘Iyd na hakuswali tena baada yake au kabla yake.” [Al-Bukhaariy]
Ruhusa Kwa Wanawake Kupiga Dufu Na Kuimba Kimaadili
Siku ya Sikukuu inaruhusiwa wanawake kupiga dufu na kuimba nyimbo zenye maadili wao peke yao bila kuchanganyikana na wanaume.
Yaliyokuwa Bid'ah (Uzushi Katika Dini) Katika 'Iyd
Ni Bid’ah (Uzushi Katika Dini)
Kunyoa Ndevu
Kunyoa ndevu hasa kwa makusudi ya kukusudia ‘Iyd.
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) ametukataza kunyoa ndevu zetu; ni aibu kufanya hivyo katika siku kubwa ambayo ni ya kufafanua na kudhihirisha tofauti ya sherehe zetu na zile za Mushrikiyn, Muislamu hunyoa ndevu akajisafisha kabisa na kuonekana kuwa hana tofauti (hufanana) na Mushrikiyn.
Kuwaiga Makafiri Katika Mienendo Yao Na Pongezi Zao
Kuwaiga Mushrikiyn katika mienendo yao, maamkizi yao na mavazi yao, na kupeana mikono na Wanawake.
'Ulamaa wanasema kunachukiza kupongezana kwa kusema: "Kullu 'Aamin Wa Antum Bikhayr" au "Kullu Sannatin Wa Anta Twayyib" na mfano wa pongezi kama hizo ambazo zimeigwa kutoka kwa Makafiri na zikabadilishwa lugha.
Kadhalika, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) amekataza vikali kuingiliana na wanawake wasio Mahram na kupeana nao mikono. Amesema:
“Ni bora kwa mwanamme kudungwa sindano katika kichwa chake kuliko kuushika mkono wa mwanamke ambaye si halali yake.” [Silsilat Al-Ahaadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy]
Baadhi ya Waislamu wamefika mbali kuwaiga Makafiri hadi imefikia wakikutana wanaume na wanawake wasio halali kishariy'ah wanakumbatiana na hata kupigana mabusu mashavuni wakiona ndio maendeleo kumbe ni kumuasi vikali Allaah na kufanya maovu yenye kupelekea kwenye zinaa. Na yote hii misiba ni atahari za Matelevisheni na utandawazi na kupenda kuiga kudhani kila kinachofanywa na Wamagharibi ni maendeleo na kizuri kumbe ni ulimbukeni na uovu na kujiwekea maandalizi ya Motoni!
Kusherehekea Kwa Tafrija (Party) Za Maasi
Kukusanyika na kuchanganyika wanawake na wanaume kwa karamu, kusikiliza muziki, ngoma, kuvaaa mavazi yasiyo katika shariy’ah na kuweko vinywaji vya haramu.
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) amesema:
"Kutakuja watu katika ummah wangu watakaozini, wanaume watakaovaa hariri, wengine watakunywa ulevi, na muziki utahalalishwa.” [Al-Bukhaariy, Abuu Dawuwd na Al Bayhaqiy].
Wanawake Kutotimiza Hijaab
Wanawake kutokuvaa vazi la stara (hijaab), kujipamba, kunyoa nyusi, na kuonyesha mapambo yao wazi kama kutokufunika nywele, kujiremba na kujitokeza mbele ya wasio Mahram wao.
Kufanya hivyo kunadhaniwa kwamba ni kusherehekea ‘Iyd na ilhali kunatendwa dhambi kubwa.
Kuzuru Makaburi
Kuna watu wamejenga itikadi kuwa ni lazima kuzuru makaburini siku ya ‘Iyd! Itikadi hizi za kizushi zimeigwa kutoka kwa Mashia!
Inaruhusiwa kuzuru makaburini siku yoyote katika mwaka na si kutengwa siku maalum kama siku ya ‘Iyd ni kufanya hivyo.
Kutembelea Wagonjwa
Kadhaalika, baadhi ya watu hudhani kuwa siku ya ‘Iyd ni lazima au kuna fadhila kubwa kuwazuru wagonjwa Mahospitalini n.k.
Huu pia ni ufahamu mbaya. Hakuna Sunnah wala fadhila maalum za kuzuru wagonjwa siku ya ‘Iyd. Bali kuzuru wagonjwa huwa ni wakati wowote ule.
Kufanya Israfu
Kuharibu pesa na kufanya israfu ya chakula badala ya kuwapa maskini (na mafakiri).
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)) Atusaidie tuepukane na Bid’ah, na Atuelekeze kwenye kuzifuata Sunnah za Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam).