Swalaah Katika Kanisa Inafaa?

Swalah Katika Kanisa Inafaa?

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assallam Aleikum

Mimi ni mkazi wa hapa England jina  …..swali langu ni kuhusu tatizo la msikititi hapa tunapoishi. Sisi tunasali kwenye kanisa ambayo tumeikodi hapa tunapoishi. Ni swala ya ijumaa na ramadhani taraawiyh. Je inaturuhusu sisi kuswali mahala hapo, ndani hapana sanamu lakini nje kuna Msalaba. Mahali penyewe hapauzwi haramu na kila ijumaa ya mwisho wa mwezi watu huja ku donate damu na pia masherehe mengine tofouti hufanyika. Naomba unijibu kwa mifano ya maswahaba na muhimu zaidi kwenye quraan na hadith, ili niweze kuwaeleza  wenzangu

 

 

JIBU: 

 

 AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Nimepatiwa vitu vitano ambavyo hakupatiwa mwengine kabla yangu: ((Ardhi yote imefanywa kwangu (na Ummah wangu) kuwa ni Msikiti na twahaarah, hivyo yeyote katika Ummah wangu anaweza kuswali popote Swalah inapomuingilia...”)) [Al-Bukhariy na Muslim kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ]

 

Hii Hadiyth ni ya kijumla kabisa katika utendaji kazi wake na hii ni kuwa Swalah kama nguzo muhimu sana ya Kiislamu haina udhuru isipokuwa zile ambazo zinajulikana na kila mmoja na hasa zinapatikana kwa kina dada kama kuwa katika ada ya mwezi, au kutokwa na damu ya uzazi baada ya kuzaa, n.k. Sasa hapa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)      anatuelekeza kuwa ardhi yote ni tohara na Msikiti hivyo unaweza kuswali popote isipokuwa unapoona najisi iliyo ya dhahiri kabisa.

 

Hivyo, kanisa liko katika ardhi na ndio pia tunapata athari ya Swahaba mtukufu kama ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye ana kauli mashuhuri pale alipokwenda Baytil Maqdis ili kuchukua funguo za mji huo kutoka kwa kasisi Sophronius. Wakati wa moja wapo wa Swalah ulifika akiwa ndani ya kanisa, na yule kasisi mwenyeji wake akamwambia waweza kuswali hapa ndani lakini akakataa kufanya hivyo kwa kumwambia: “Sio kuwa nimekataa kwa sababu ni haramu lakini sitaki Waislamu watakaokuja baadae kutaka kulifanya hili kanisa kuwa Msikiti kwa sababu mimi nimeswali ndani yake”.

 

Kwa hali yenu ilivyo ikiwa mutaweza kupata sehemu nyengine ya kukodisha itakuwa bora zaidi na tunaamini kuwa zipo nyingi kwa jinsi tunavyofahamu hali ya Uingereza na kupatikana kwa nyumba nyingi za council za kukodisha kama wanavyofanya wenzenu wa miji mingine wanapofanya Mihadhara yao na shughuli za ndoa na pia Swalah za 'Iyd n.k.

 

Hamjafikia udhuru wa kuswali kanisani kwa hali yoyote, na bora zaidi muepukane na jambo hilo ingawa kuna baadhi ya Maulamaa wanaonelea kuwa hakuna tatizo iwapo patakuwa humo ndani hakuna masanamu na mapicha au kumezikwa watukufu wao.

 

Tunaona kwenye hadiyth maarufu ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  iliyopokewa na bi 'Aishah (Radhwiya Allaahu 'anha)  kuwa:  Aliporudi mmoja wa wake zake (Ummu Salamah) kutoka Habashah (Ethiopia) na kumsifia uzuri wa makanisa waliyokuta kule, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alimjibu: (('Hao ni watu ambao, anapokufa mmoja wa watu wema wao, basi hujenga nyumba za kuabudia juu ya kaburi lake na kuweka picha na masanamu ndani yake. Hao ni viumbe viovu kabisa mbele ya Allaah [Al Bukhaariy na Muslim]

 

Kwa hiyo tunaona kwenye hadiyth hiyo kuwa wana tabia ya kuzika watukufu wao ndani ya majumba yao ya ibada na kama ilivyo sheria, ni haramu kuswali penye kaburi au kulielekea kama hadiyth zinavyoonyesha. Huenda kwa wakati huu si wote wanaozika watukufu wao ndani ya makanisa/mahekalu yao, lakini ni vizuri kuwa na tahadhari.

Na kama hamtopata sehemu kabisa ya kuswalia ikasababisha msipate kuswali Swalah ya Ijumaa na ni hapo tu mlipopata, basi munaweza kuswali humo ingawa ni Makuruhu. Na misalaba ilioko nje kama mnaweza kuondosha ni vizuri pia na kama haiwezekani basi si kikwazo, ila muhakikishe ndani hakuna masanamu wala mapicha. 

 

Jaribuni kule ndani mutoe misalaba na mapicha yalioko ndani kisha muendelee na ‘Ibadah zenu, na kama itashindikana kutoa basi baadhi ya 'Ulamaa wanasema mnaweza kuyafunika kwa nguo au chochote, na haswa yale ambayo mkiswali mnayaelekea. Kwani Malaika haingii sehemu yenye masanamu/picha

Inasemwa katika vitabu vya historia kuwa:

 

  • Abuu Muwsaa al-Ash'ariy na 'Umar  bin 'Abdil-'Aziyz waliswali kanisani. 
  • Ash-Sh'abiy, 'Ata, na Ibn Siriyn hawakuona tatizo lolote kwamtu kuswali  kanisani, hasa ikiwa yuko hapo ndani na wakati wa Swalah umefika.
  • Al-Bukhariy amesema: "Ibn 'Abbaas alikuwa akiswali makanisani isipokuwa yale ambayo yana masanamu".
  • Waislamu wa Najran walimuandikia 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) ) kumwambia ya kwamba hawana sehemu iliyo safi na nzuri zaidi kuliko kanisa. 'Umar  aliwajibu: Linyunyizieni maji na majani na kisha muswali ndani yake".
  • Kwa mujibu wa Hanafi na Shafi'i, haipendezi kiujumla kuswali katika sehemu hizo.
  • Imaam Ahmad kuwa haitofaa kuswaliwa humo kama kuna masanamu/mapicha.
  • Na Imaam Maalik kakataza kabisa hata kwa udhuru. 
  • Pia inajulikana kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hakuzunguka Al Ka'abah hadi yalipovunjwa masanamu yote. 
  • Imaam Muhammad bin 'Abdil-Wahhaab anasema katika kitabu cha  Tawhiyd "aifai kuswali katika maeneo yenye kufanyiwa ibada za kishirikina".

 

Na kama tunavyojua, hawa wakristo wanamshirikisha Allaah kwa utatu wao; kuwa na mungu baba, mungu mwana, na roho mtakatifu.

 

Mwisho, kwa hoja hizo hapo juu, tunawanasihi ndugu zetu mjitahidi kadiri muwezavyo kutafuta maeneo mengine na mjiepusha na shub-ha hiyo, na kama tulivyosema na tujuavyo kuwa Uingereza maeneo ni mengi na yanakodishwa kwa gharama nafuu zinazomudiwa kwa hali ya kipato cha huko, kwa hiyo msuitafute njia za rahisi rahisi na mkato kwa sababu labda mmepata rai ya mwanachuoni mmoja au baadhi ya watu. Daima mfuate Hadiyth isemayo:

((Acha chenye kukutia mashaka na fuata kisichokutia mashaka)) [Imenukuliwa na  An-Nasaaiy na at-Tirmidhiy ambaye amesema ni Hadith Hasan Sahiyh kutoka kwa Abuu Muhammad al-Hasan bin 'Aliy  (Radhiya Allaahu 'anhu)]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share