Fataawaa: Mukhtasari Wa Fataawaa Za Zakaatul-Fitwr
01-Nini Hukmu Ya Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:
Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa kila Muislamu mdogo au mkubwa, mwanamue au mwanamke aliye huru au mtumwa.
[Fataawaa (14/197)]
02-Kitu Gani Kinatolewa Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:
Itolewe swaa’ (pishi) ya chakula au swaa’ ya tende au swa’aa ya shayiri au swaa’ zabibu, au swaa’ ya jibini na kwa aina hizo ya vyakula, ni kama ilivyo kauli sahihi ya ‘Ulamaa kwamba ni chakula ambacho kinatumika na watu katika nchi zao kama vile mchele, au nafaka (kama ngano, mahindi) na punje (kama mtama, uwele) na aina kama hizo.
03-Wakati Gani Inapaswa Kutolewa Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:
Kutolewa kwake (Zakaatul-Fitwr) ni siku ya tarehe 28 na 29 na 30 ya usiku wa ‘Iyd, na asubuhi ya ‘Iyd kabla ya Swalaah.
[Fataawaa (14/32-33)]
04-Sababu Ya Kutoa Zakaatul-Fitwr
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aemesema:
Kutoa (Zakaatul-Fitwr) ni kudhihirisha shukurani za neema za Allaah (Ta’aalaa) kwa mja kwa Fitwr (kufungulia) Ramadhwaan na kuikamilisha kwake.
[Fataawaa (18/257)]
05-Nani Anayepasa Kupewa Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
Hakuna anayepasa kupewa isipokuwa aina moja ya watu; nao ni mafakiri.
[Fataawaa 18/259)]
06-Hukmu Ya Kuwawakilisha Watoto Au Wengineo Katika Kutoa Zakaatul-Fitwr
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
Inajuzu mtu kuwakilisha wanawe wamtolee Zakaatul-Fitwr katika wakati wake (wa kuitoa hiyo Zakaatul-Fitwr), japokuwa kwa wakati wake (ni wakati wa) katika nchi nyingine.
[Fataawaa (18/262)]
07-Je, Inajuzu Fakiri Kumwakilisha Mtu Mwengine Kumpokelea Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
Inajuzu hivyo (Fakiri kumwakilisha mtu ampokelee Zakaatul-Fitwr).
[Fataawaa (18/268)]
08-Je, Kuna Kauli Maalumu Ya Kusemwa Inapotolewa Zakaatul-Fitwr?
Al-Lajnah Ad-Daaimah
Hatujui du’aa yoyote ile maalumu inayosemwa inapotolewa Zakaatul-Fitwr.
[Fataawaa Al-Lajnah Ad-Daaimah (9/387)]
09-Je, Inajuzu Kutoa Thamani Ya Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) Na Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:
Kwa kauli ya ‘Ulamaa wengi, haijuzu kutoka thamani yake kwa kuwa inakhalifu yaliyonukuwa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum).
[Fataawaa (14/32)]
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
Kuitolea (Zakaatul-Fitwr) thamani yake, haijuzu kwa sababu kilichofaridhiwa ni chakula.
[Fataawaa (18/265)]
10-Je, Inalazimika Niswaab (Kiwango Cha Mali) Katika Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:
(Zakaatul-Fitwr) haina niswaab bali inamwajibikia kila Muislamu kujitolea kwa ajili yake na watu wa nyumbani kwake, na wanawae, na wake zake na wafanya kazi wake wa nyumbani ikiwa atakuwa na chakula cha ziada cha kumtosheleza yeye na wao usiku na mchana.
[Faataawaa (14/197)]
Niswaab: Ni kiwango cha mali ambacho mtu akiwa nacho kwa muda wa mwaka analazimika kuitolea Zakaah.
11-Ni Kwango Gani Kinachotolewa Cha Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:
Lilo waajib katika (kiwango cha) Zakaatul-Fitwr ni swaa’ (pishi) moja ya chakula cha mji, na kiasi chake ni kupima kwa kilo, na ni takriban kilo mbili na nusu.
[Fataawaa (14/203)]
12-Je, Inajuzu Kutoa Zakaatul-Fitwr Nchi Asiyokuweko Mwenye Kutoa?
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:
Sunnah, ni kuigawa baina ya Mafakiri katika nchi ya yule anayetolewa na si kuitoa nchi nyingine ili kuwanufaisha Mafakiri wa nchi yake na kuwakidhia haja zao.
[Fataawaa (14/213)]
13-Wapi Inatolewa Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
Zakaatul-Fitwr inatolewa katika sehemu ambayo inakufikia wewe Al-Fitwr (kumalilza Ramadhwaan na kuingia katika ‘Iydul-Fitwr) hali ya kuwa uko hapo japokuwa ni mbali na nchi yako.
[Fataawaa Ibn 'Uthaymiyn]
14-Je, Mtumishi Wa Nyumbani Anawajibika Kutoa Zakaatul-Fitwr?
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
a. Mtumishi huyo wa nyumbani anawajibika kutoa Zakaatul-Fitwr kwa sababu yeye ni katika Waislamu.
b. Na asli ni kwamba Zakaatul-Fitwr ni juu yake kuitoa, lakini ikiwa watu wa nyumba yake (Waajiri) wakimtolea basi hakuna ubaya katika hilo.
[Fataawaa Ibn 'Uthaymiyn]
15-Je, Inajuzu Kuwatolea Zakaatul-Fitwr Watoto Walio Matumboni (Kwa Waja Wazito)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
Zakaatul-Fitwr haitolewi kama ni waajib kwa watoto walio matumboni mwa mja mzito, bali inatolewa kama ni mustahab (inapendekezwa)
[Fataawaa (18/263)]
16-Je, Inajuzu Kuwapa Zakaatul-Fitwr Watumishi Wasiokuwa Waislamu?
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
Haijuzu kuwapa (Zakaatul-Fitwr) Mafakiri (wasio Waislamu) isipokuwa ni kuwapa Mafakiri wa Kiislamu tu.
[Fataawaa (18/285)]
17-Zakaatul-Fitwr Inatolewa Kwa Mtu Mmoja Au Zaidi Ya Mmoja?
Al-Lajnah Ad-Daaimah
Inajuzu kuitoa Zakaatul-Fitwr ya mtu mmoja kumpa mtu mmoja, na vile vile inajuzu kuigawa kwa watu kadhaa.
[Fataawaa Al-Lajnah Ad-Daaimah (9/377)]
18-Nini Hukmu Ya Kuipokea Zakaatul-Fitwr Kisha Kuiuza?
Al-Lajnah Ad-Daaimah
Ikiwa anayeipokea ni mwenye kustahiki, inajuzu (kwake) kuiuza baada ya kuipokea.
[Fataawaa Al-Lajnah Ad-Daaimah (9/380)]
19-Hukmu Ya Kuichelewesha Zakaatul-Fitwr Mpaka Baada Ya Swalaah Ya ‘Iyd Bila Ya Dharura.
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
Kuichelewesha (Zakaatul-Fitwr) mpaka baada ya Swalaah ni haramu, wala haina malipo.
[Fataawaa (18/266)]