Swalaah Ya Witr Inaswaliwa Vipi Na Vipi Kutia Niyyah?
Swalaah Ya Witr Inaswaliwa Vipi Na Vipi Kutia Niyyah?
SWALI:
nategamea muko katika hali ya afya njema na ramadhan karim mimi nina suala langu kuhusu salaa ya witri .witri inasaliwa rakaa moja ,tatu ,tano,ambazo rakaa zisizogawika kwa mbili ama sivyo na wengine wanasema utakaposali rakaa tatu haifai kusali kama sala ya magharibi yaani usalii rakaa mbili ukae atahiyat ikisha umalize rakaa ya mwisho utoe salamu na wengine wanasema usali rakaa zote tatu moja kwa moja ya mwisho ndio utoe salamu yaani usikasali rakaa mbili ikisha ukae atahiyat ikisha umalize rakaa moja kwa ufupi yaani usisali kama sala ya magharib kwa hiyo naomba jibu kutoka kwa wanalhidaaya
na utakaposali unatia nia gani ya witri? nadhani nitapata jibu kutoka kwenu inshaalah a/a
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Witr ni kuswali Rakaa moja, au tatu, au tano, au saba, au tisa au kumi na moja. Swalaah hii huswaliwa usiku baada ya Swalaah ya 'Ishaa ikiwa ni kabla ya kulala au baada ya kulala na kuamka kabla ya Alfajiri.
Mafunzo ya Sunnah yanatufundisha kuwa Rakaa zozote utakazojaaliwa kuswali, basi umalizie na Rakaa moja au tatu za Witr ambazo huswaliwa hivi:
Kuswali Rakaa mbili kwanza kisha utoe salaam. Kisha unamalizia na Rakaa moja na kutoa salaam.
Au kuswali Rakaa zote tatu kwa tashahhud (kikao) moja ya mwisho tu na kutoa salaam.
Haifai kuswali Rakaa tatu zote pamoja kwa kuleta Tashahhud mbili kama vile Swalaah ya Magharibi, bali ni kuitofautisha na Swalaah ya Magharibi kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((… ولا تشبهوا بصلاة المغرب))
((… wala msiishabihishe (hiyo witr) na Swalah ya Magharibi)) [Al-Haakim, Al-Bayhaqiy, Ibn Hibbaan, Ad-Daraaqutniy?]
Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi ya jinsi kuswali Qiyaamul-Layl
Suwrah Gani Kusoma Katika Swalaah Ya Witr
Hii ni kuhusu Swalaah ya Tahajjud ambayo ni sawa na Swalah ya taraawiyh au kwa jina lingine ni Qiyaamul-Layl.
Wakati Wa Swalaah Ya Tahajjud Na Vipi Kuiswali
Vile vile soma Faatawa zifuatazo za mas-ala mbali mbali kuhusu Swalah ya taraawiyh au Qiyaamul-Layl.
Qiyaamul-Layl, Witr, Laylatul-Qadr Na I'tikaaf
Jibu kuhusu Kutia Niyyah:
Niyyah ya ‘ibaadah yoyote haitamkwi, bali huwekwa moyoni. Na hayo ndio mafunzo sahihi ya Sunnah. Kutamka niyyah ni bid'ah. Unapojitayarisha kwenda kuswali Taraawiyh au Swalaah yoyote nyingine kwa kufanya wudhuu, na kutoka kwenda Msikitini, huwa tayari umeshatia niyyah moyoni kwa lile unaloliendea, hivyo inatosheleza kuwa nia yako imeingia moyoni.
Na Allaah Anajua zaidi