Hadiyth Inayosema "Uislamu Ni Nadhifu Basi Fanyeni Unadhifu..." Je, Ni Sahihi?

 

Hadiyth Inayosema "Uislamu Ni Nadhifu Basi Fanyeni Unadhifu..." Je, Ni Sahihi?

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam alykum naulizia swali kuhusu usahihi wa hadithi ya al islamu nadhifu....

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hadiyth hiyo ni dhaifu ameeleza udhaifu wake Imaam Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika Dhwa’iyf Al-Jaami’ (2281, 1414), As-Silsilah Adhw-Dhwa’iyfah (2470). Hadiyth imetolewa na Ibn Hibbaan katika Al-Majruwhiyn (2/314) na Atw-Twabaraaniy katika Mu’jam Al-Awsatw (4893).

 

Hadiyth yenyewe hiyo ambayo ni dhaifu iko hivi:

 

الْإِسْلَامُ نَظِيفٌ فَتَنَظَّفُوا، فَإِنَّهُ لَا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ إِلَّا نَظِيفٌ

 

Uislamu ni nadhifu basi fanyeni unadhifu kwani haingii Jannah (Pepo) isipokuwa aliye nadhifu.   

 

Tanabahi kwamba Uislamu umefundisha unadhifu katika nususi mbali mbali zilizothibiti katika Qur-aan na Sunnah. Mfano kwenda na nguo nzuri na safi Msikitini Allaah ('Azza wa Jalla) Ameamrisha:

 

يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ

Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu (ya mavazi ya sitara na twahara) katika kila mahala pa ‘Ibaadah. [Al-A’raaf: 31]

 

Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):

 

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ﴿٤﴾

Na nguo zako twaharisha. [Al-Muddaththir: 4]

 

 

Na Hadiyth nyingi zenye kutaja kuhusu unadhifu katika Uislamu na ambazo zimethibiti usahihi wake miongoni mwazo ni:

 

الطَّهُورُ شَطْرُ الْإِيمَانِ

((Twahaarah ni nusu ya iymaan) [Muslim (223) na wengineo]

 

 

Na pia:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((الإيمَانُ بِضْعٌ وَسَبْعُونَ)) أَوْ ((بِضْعٌ وَسِتُّونَ شُعْبَةً، فَأَفْضَلُهَا قَوْلُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ،  وَأَدْنَاهَا إِمَاطَةُ الأَذَى عَنْ الطَّرِيقِ، وَالْحَيَاءُ شُعْبَةٌ مِنْ الإِيمَانِ)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Iymaan ni sabini na kitu)) au alisema ((Tanzu sitiini na kitu. Ilio bora kabisa ni kauli ya ‘Laa ilaaha illa-Allaah’, na ya chini kabisa ni kuondosha taka njiani. Na kuona hayaa ni utanzu katika tanzu za Iymaan)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Pia:

إِنَّ اللَّهَ جَمِيلٌ يُحِبُّ الْجَمَالَ

((Hakika Allaah ni Mzuri Anapenda Uzuri)). [Muslim]

 

Na pia:

 

Kutoka kwa Mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mambo kumi ni katika fitwrah (maumbile ya asli ya Kiislam): “Kupunguza masharubu, kufuga ndevu, kupiga mswaki, kupitisha maji puani (kusafisha), kukata kucha, kusafisha penyo za vidole, kung’ofoa (kunyoa) nywele za kwapa, kunyoa nywele za sehemu za siri, na kujisafisha kwa maji baada ya kujisaidia na msimuliaji akasema kasahau la kumi, lakini inaweza kuwa ni kusafisha mdomo (kusukutua)” [Muslim na Abuu Daawuwd].

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share