003-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je Manii Ni Twahara Au Najsi?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara:

 

003-Je Manii Ni Twahara Au Najsi?

 

 Alhidaaya.com

 

 

Wanazuoni wamehitilafiana juu ya suala hili kwa kauli mbili:

 

Kauli ya kwanza:

 

Inasema kwamba manii ni najsi. Kauli hii ameisema Abu Haniyfah na Maalik, nayo ni riwaya iliyopokelewa toka kwa Ahmad. Wamelitolea dalili hilo kwa Hadiyth ya 'Aaishah alipoulizwa kuhusu manii yaliyoingia kwenye nguo akasema:  "Nilikuwa nikiyaosha kwenye nguo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kisha anatoka moja kwa moja kwenda kuswali huku athari ya doa la maji  ikiwa katika nguo yake". [Imepasishwa na Al-Bukhaariy (230) na Muslim (289)].

Na kuosha hakuwi ila kwa kitu najsi.

 

 

Kauli ya pili:

 

Wenye kauli hii wamesema kuwa manii ni twahara. Kati ya waliolisema hilo ni Ash-Shaafi'i na Daawuud. Hii ni riwaya Swahiyh zaidi kati ya riwaya mbili zilizopokelewa toka kwa Ahmad. Wamelitolea dalili hilo kwa Hadiyth ya 'Aaishah kuhusu manii, aliposema: "Nilikuwa nikiyakwangua kuyatoa kweye nguo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Muslim (288)].

 

Na kwa Hadiyth yake nyingine kwamba mgeni alishukia kwa 'Aaishah na akawa anaiosha nguo yake. 'Aaishah  akamwambia: "Ilikuwa inakutosha tu ikiwa utayaona, uoshe mahala pake, na ikiwa hukuyaona, unyunyizie maji kuzungukia hapo. Na bila shaka umeniona nikiyakwangua kwa umakini kwenye nguo ya Nabiy wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na yeye akaiswalia". [Hadiyth Swahiyh: Muslim (288)].

 

Na kutosheka kuyakwangua, kunaonyesha kuwa manii ni twahara.

 

Wenye kusema kuwa manii ni najsi, wamejibu kuwa kukwangua  hakuonyeshi kuwa manii ni twahara, bali kunaonyesha namna ya kuyatwaharisha kama vinavyotwaharishwa viatu kwa kuvipangusa katika mchanga.

 

Hili linajibiwa  kwa kusema kuwa 'Aaishah  alipoyakwangua manii mara moja na kuyaosha mara nyingine, hilo halihukumii kuwa ni najsi, kwani nguo inaoshwa kwa kuingia makamasi, mate au uchafu. Na hivi ndivyo walivyosema baadhi ya Maswahaba kama vile Sa'ad bin Abiy Waqqaasw, Ibn 'Abbaas na wengineo. Wamesema:

"Manii ni kama makamasi na mate, jisafishe uyaondoshe japokuwa kwa kijiti." [Majmuu Al-Fataawaa (21/605)].

 

Na kwa hili, inadhihiri kuwa kitendo cha 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa), kinaingia katika mlango wa kujichagulia namna ya kusafisha. [Sharhu Muslim].

 

Hukmu ya kuwa manii ni twahara inapata nguvu tunapojua kwamba Maswahaba walikuwa wakiota wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na manii hayo yalikuwa yakiingia katika miili na nguo za baadhi yao. Na lau kama yangelikuwa ni najsi, basi ingelikuwa ni lazima kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) awaamrishe wayasafishe kama alivyowaamrisha wastanji. Na kwa kuwa hakuna yeyote aliyelinukuu hili, inajulikana kwa yakini kuwa kuyaondosha hakukuwa ni jambo la lazima.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi. [Majmuu Al-Fataawaa (21/604)].

 

 

Share