059-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je, Inajuzu Kwa Mwenye Hedhi Na Mwenye Janaba Kuingia Msikitini Na Kukaa Humo?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

059-Je, Inajuzu Kwa Mwenye Hedhi Na Mwenye Janaba Kuingia Msikitini Na Kukaa Humo?

 

Alhidaaya.com

 

 

Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Maimamu wanne na wengineo (kinyume na Adh-Dhwaahiriyyah) wanasema kuwa ni haramu kwa mwenye hedhi, mwenye nifasi na mwenye janaba kukaa Msikitini. Hayo yamepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Ibn Mas-’oud . [Al-Majmu’u (2/184) na baada yake, Al-Mughniy (1/145) na Al-Lubaab Sharh Al-Kitaab (1/43). Ash-Shaafi’iy na Ahmad wamejuzisha kupita Msikitini bila kukaa, na Al-Muhalla (2/184) na baada yake].

 

Wenye kupinga hili wametoa dalili zifuatazo:

 

1- Ni Neno Lake Allaah (Subhaanahuu wa Ta’alaa):

((يا أيها الذين آمنوا لا تقربوا الصلاة وأنتم سكارى حتى تعلموا ما تقولون ولا جنبا إلا عابري سبيل حتى تغتسلوا))

((Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah hali mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema, wala hali mna janaba – isipokuwa mmo safarini – mpaka mkoge)). [An-Nisaai (4:43)]

 

Wanasema kuwa makusudio ya Swalaah hapa ni sehemu za kuswalia, nazo ni Misikiti. Na katika Aayah, mwenye janaba anazuiliwa kuingia humo isipokuwa tu kama ni msafiri. Kisha wakawaweka mwenye hedhi na mwenye nifasi katika kipimo kimoja na mwenye janaba!!

 

Wenye kujuzisha hili wamewajibu wakisema:

 

Hii ni moja kati ya taawili mbili za masalaf katika Aayah hii. Na taawili nyingine ni kuwa makusudio ni Swalaah yenyewe, na si Msikiti. Kwa hivyo basi, maana inakuwa: Na wala msikaribie Swalaah mkiwa na janaba ila baada ya kuoga, isipokuwa kama mko safarini, basi hapo, swalini kwa kutayamamu. Na kwa ajili hiyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Anasema baada ya hapo:

((وإن كنتم مرضى أو على سفر....فلم تجدوا ماء فتيمموا))

((Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini………na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi)).

 

Kisha kuna mlahadha katika kipimo cha mwenye hedhi kwa mwenye janaba, kwani mwenye hedhi ana udhuru na hawezi kuoga kabla ya kutwaharika damu, na wala hawezi kuiondosha hedhi yake kinyume na mwenye janaba ambaye anaweza kuoga.

 

2- Ni Hadiyth ya Jisrah binti Dujaajah toka kwa ‘Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((إنى لا أحل المسجد لحائض ولا جنب))

((Hakika mimi sihalalishi Msikiti kwa mwenye hedhi wala kwa mwenye janaba)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (232), Al-Bayhaqiy (2/442) na Ibn Khuzaymah (2/284). Tazama Al-Irwaa (193)].

 

Wenye kujuzisha wamejibu wakisema:

Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, haifai kutolea hoja, kwani Hadiyth imezungukia kwa Jisrah, naye hawezi kuwa amepokea Hadiyth peke yake.

 

3- Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) aliamuru kuwatoa vijizee vikongwe, waliotawishwa na wenye hedhi kwenda Swalaah ya ‘Iyd ili washuhudie kheri na du’aa ya Waislamu, na wenye hedhi hukaa kando na sehemu ya kuswalia. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (324) na Muslim (890)].   

Wamesema: Na ikiwa hali ni hii kwa upande wa sehemu za kuswalia, basi Misikiti ni awla zaidi kuzuiwa.

 

Wenye kujuzisha wamejibu wakisema:

Makusudio ya “Al-Muswalla” katika Hadiyth ni Swalaah, kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) na Maswahaba wake walikuwa wakiswali ‘Iyd uwanjani na si Msikitini, na ardhi yote ni twahara, na haijuzu kuzuiliwa huko kuihusu baadhi ya Misikiti tu bila ya mingine. Kisha imepokelewa Hadiyth hiyo hiyo kwa tamko:

((فأما الحيض فيعتزلن الصلاة))

((Ama wenye hedhi, hao hukaa mbali na Swalaah)).

Na Hadiyth hii iko katika Swahiyh Muslim na kwingineko.

 

4- Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akielemeza kichwa chake kwangu nailhali yuko jirani na Msikiti, nami namweka sawa nikiwa hedhini.”

 

Wamesema: Akajizuilia kumweka sawa Msikitini kwa vile yeye ana hedhi.

 

Wenye kujuzisha wamejibu wakisema:

Hili walilolitolea dalili haliko wazi. Inawezekana kuwa hakuingia kutokana na sababu nyingine isiyokuwa hedhi kama kuwepo wanaume Msikitini na mfano wa hilo.

 

Kisha wenye kujuzisha mwenye hedhi na janaba kuingia Msikitini wametoa dalili hizi zifuatazo:

 

1- Ni utakasifu wa kiasili. Kwa vile hakuna makatazo yoyote sahihi, asili itakuwa ni uhalali. Muislamu ameruhusiwa kuswali mahala popote Swalaah inapomkuta.

 

2- Imethibiti kwamba washirikina waliingia Msikitini kwa kufungiwa humo na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam). Na Allaah Amesema:

(( إنما المشركون نجس فلا يقربوا المسجد الحرام بعد عامهم هذا))

((Hakika washirikina ni najsi, basi wasiukaribie Al Masjidul Haraam baada ya mwaka wao huu)).[At-Tawbah (9:28)]  

 

Ama Muislamu, yeye ni twahara kwa hali zote kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam):

((إن المسلم لا ينجس))

((Hakika Muislamu hanajsiki)). [Hadiyth Swahiyh: Imetangulia karibuni].

 

Hivyo basi, vipi azuiwe Muislamu kuingia, na kafiri aruhusiwe?!

 

Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Sharia imefarakisha kati ya Muislamu na kafiri, na kwa kufarakisha huku, dalili imepatikana juu ya uharamu wa kukaa mwenye janaba na hedhi Msikitini, na imethibiti makafiri kuwekwa mahabusu humo!!. Na sharia inapofarakisha, haijuzu kusawazisha. Na hii ni qiyaas pamoja na matni, nayo imeharibika!!

 

Ninasema:

“Hii ikiwa imethibiti matni, nalo li wazi!”

 

3- Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo: “Kijakazi mweusi alikuwa katika kitongoji cha Waarabu, wakamwacha huru. Kisha alikwenda kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akasilimu. Akawa na kijihema ndani ya Msikiti.”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (439)].

 

Wamesema: Mwanamke huyu anakaa ndani ya Msikiti wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam), na wanawake kawaida yao ni kupata hedhi, lakini Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) hakumzuia kutokana na hilo, wala hakumwamuru atoke nje ya Msikiti anapopatwa na hedhi.

 

Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Ni dhahiri kwamba mwanamke huyu hakuwa na jamaa zake wala hifadhi isipokuwa Msikiti, akalazimika kuishi humo. Hivyo, hawezi kupimiwa na mwanamke mwingine. Na hili ni tukio la hali maalumu ambalo dalili ya wazi ya kuzuia haipingwi na tukio hili!!

 

4- Hadiyth ya Abuu Hurayrah kuhusiana na mwanamke aliyekuwa anasafisha Msikiti akafariki, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akamuulizia. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (458) na Muslim (956). Kwa wawili hawa kuna shaka kama alikuwa ni mwanamke au mwanamume. Lakini kwa tamko la Hadiyth iliyopo kwa Abuu Khuzaymah na Al-Bayhaqiy (4/48) kwa Sanad Swahiyh, inatilika nguvu kwamba ni mwanamke].

 

Mwanamke huyu hakulazimika kusafisha Msikiti nyakati zote, na wala Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) hakumkataza akae mbali na Msikiti wakati wa hedhi.

 

5- Hadiyth ya Abuu Hurayrah kuhusiana na Ahlus Swafah kulala ndani ya Msikiti wakati wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6452) na At-Tirmidhiy (479).

 

Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Ahlus Swafah hawakuwa na ndugu wala jamaa wala chochote kama inavyoonekana wazi katika matni ya Hadiyth.

 

6- Imethibiti katika Swahiyh kwamba Ibn ‘Umar alikuwa akilala Msikitini wakati ni kijana kapera. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3530) na Muslim (2479)].

Na kijana mara nyingi anapolala huota, lakini hakukatazwa kukaa Msikitini wakati anapokuwa na janaba.

 

Wenye kupinga wamejibu wakisema: Haikuelezwa kwamba Rasuli alilijua hilo akamkubalia!!

Wenye kujuzisha wamejibu wakisema: Lau kama hilo lingefichika kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam), basi kwa Allaah Mtukufu halifichiki, na kwa hivyo, ilitakikana ajulishwe hilo kwa njia ya wahyi ili amkataze.

 

Imejibiwa: Si lazima wahyi uteremke ili kumjulisha kila kosa linalofanywa na Maswahaba. Ni mara ngapi Maswahaba wamefanya makosa kwa kutojua kwa dalili ya kuuliza kwao maswali wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam).

 

7- ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) alipopata hedhi wakati wa Hajji, Rasuli alimruhusu kufanya amali zote za Hajji isipokuwa kuzunguka Al-Ka’abah. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1650). Itakuja kwenye mlango wa Hijjah].

 

Hii inaonyesha kwamba inajuzu kwake kuingia Msikitini, kwa kuwa mwenye kuhiji lazima aingie humo.

 

Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alitaka kumfundisha kwamba inajuzu kwa mwenye hedhi kufanya amali zote za Hijjah isipokuwa twawaaf. Ama hukmu ya kuingia Msikitini, yeye anajua kwamba hilo ni marufuku kwani yeye ndiye msimulizi wa Hadiyth. Kisha Rasuli hakumkataza kuswali akiwa hedhini – na mahujaji wanaswali -. Je, inawezekana tukasema aswali na yeye yuko hedhini?!!

 

Ninasema: "Jibu hili lina mwelekeo ikiwa patathibiti Hadiyth inayokataza, nayo ni Dhwa’iyf".

 

8- Hadiyth ya 'Aaishah aliyesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) aliniambia: "Nipe kijijamvi toka Msikitini". Nikamwambia: "Nina hedhi". Akasema: Hedhi yako haiko mkononi mwako". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (298), Abuu Daawuud (261), At-Tirmidhiy (134) na An-Nasaaiy (1/192)].

 

Hili linatuhisisha kwamba kijijamvi kilikuweko Msikitini, naye Rasuli akashikilia Bi 'Aaishah aingie Msikitini ili ampatie.

 

Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Hadiyth imekuja kwa tamko jingine lisemalo: " Wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akiwa Msikitini alisema: ((Ee 'Aaishah! Nipatie nguo)) Akasema: Nina hedhi. Akasema: Hedhi yako haiko mkononi mwako."[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (299) na An-Nasaaiy (1/192)].

 

Hadiyth hii iko wazi kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa Msikitini wakati 'Aaishah na kijijamvi alikuwa nje. Akamwamuru aingize mkono wake tu na si mwenyewe.

 

Ninasema: "Hadiyth hii inabeba hili na lile. Hivyo yatakikana kuipomosha isiwepo kwenye dalili za makundi mawili".

 

9- Athar ya 'Atwaa bin Yasaar aliyesema: "Niliwaona watu katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) wakikaa Msikitini na wao wana janaba, wanapotawadha wudhuu wa Swalaah."[Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa ”ikhraaj” na Sa’iyd bin Mansour katika Sunanih (4/1275)].

 

Ninasema: "Baada ya mapitio haya ya hoja za wenye kupinga na wenye kujuzisha kuhusiana na kukaa Msikitini kwa wenye janaba, hedhi na nifasi, linaloonekana ni kuwa dalili za wapingaji hazipandi kufikia uharamu wa kukata ingawa mimi ninapiga breki katika suala hili. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi".

 

 

Share