077-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kuanza Na Kumalizika Hedhi
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
077-Kuanza Na Kumalizika Hedhi
[Jaami'u Ahkaamin Nisaa (1/200) na kurasa zinazofuatia]
1- Kuanza kwa hedhi kunajulikana kwa msukumo wa damu wakati wake, nayo ni damu nyeusi, nzito na yenye harufu mbaya.
2- Kumalizika kwake hujulikana kwa kukatika damu, kuwepo unjano na rangi yenye kumili weusi. Na hili linatokana na mambo mawili:
(a) Ukavu; nako ni kutoka kikiwa kikavu kilichoingizwa katika njia ya uzazi. Yaani ikiwa mwanamke ataingiza kitambaa au pamba katika utupu wake, basi hutoka kikiwa kikavu.
(b) Kuwepo maji meupe yanayotoka katika njia ya uzazi wakati wa kukatika damu ya hedhi.
Imepokelewa na mwachwa huru wa ‘Aaishah akisema:
“Wanawake walikuwa wakimwendea na kitambaa chenye pamba yenye unjano utokanao na damu ya hedhi, kisha wanamuuliza kama wanaweza kuswali, naye huwajibu akisema: “Msifanye haraka mpaka mwone maji meupe”.
Hapa anamaanisha kwamba wametwaharika na hedhi. [Ni Hadiyth Hasan kwa nyingine. Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (uk 59), Al-Bukhaariy akitoa maelezo (1/420 – Fat-h) na ‘Abdur-Raaziq (1/302) kwa Sanad Dhwa’iyf ingawa ina ushahidi kwa Ad-daaramiy (1/214), na Al-Bayhaqiy (1/337). Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi].