081-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Damu Ya Nifasi
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
081-Damu Ya Nifasi
Ni damu inayomtoka mwanamke kwa sababu ya kujifungua.
1- Muda wake
Hakuna uchache wa muda wa kutoka kwake. Maulamaa wote wamekubaliana kuwa wakati wowote mwanamke anapoona utwahara – hata kabla ya kumalizika siku arobaini – basi ataoga, ataswali na mumewe anaweza kumwingilia. [Imenukuliwa na At-Tirmidhiy katika As-Sunan (1/429)]
Ama upeo wa juu zaidi wa muda anaosubiri mwanamke endapo damu ya nifasi itaendelea, Jamhuri ya Maulamaa wanaona kuwa ni siku arobaini, kisha ataoga na kuswali. Hili wamelitolea dalili kwa Hadiyth ya Mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anha) aliyesema:
"Wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), wanawake wenye nifasi walikuwa wakikaa siku arobaini au masiku arobaini baada ya nifasi". [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (307), At-Tirmidhiy (139) na Ibn Maajah (648). Wametofautiana katika kuifanya Hadiyth Hasan, lakini kauli yenye nguvu ni kuwa ni Hadiyth Dhwa’iyf. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi. Lakini pamoja na hivyo, inafanyiwa kazi].
2- Maulamaa wote wamekubaliana kuwa nifasi ni kama hedhi katika yote yaliyohalalishwa, yaliyoharamishwa, yaliyo makruhu na yaliyo manduwb. [Nayl Al-Awtwaar ya Ash-Shawkaaniy (1/386)]
3- Nifasi inatofautiana na hedhi kwa kuwa eda haihesabiwi, kwani eda humalizika kwa kujifungua kabla ya kutoka damu ya nifasi. [Al-Mughniy ya Ibn Qudaamah (1/350)]