030-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya Tahiyyatul Masjid

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

030-Swalaah Ya Tahiyyatul Masjid 

 

Alhidaaya.com

 

 

Imesuniwa kwa anayeingia Msikitini asikae ila baada ya kuswali rakaa mbili kutokana na dalili zifuatazo:

 

1- Hadiyth ya Abu Qataadah anayesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا دخل أحدكم المسجد فلا يجلس حتى يصلي ركعتين))

((Anapoingia mmoja wenu Msikitini, asikae mpaka aswali rakaa mbili)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (444) na Muslim (714)].

 

2- Jaabir bin ‘Abdullaah anasema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru Sulayka Al-Ghatwafaaniy aswali rakaa mbili wakati alipokuja siku ya ijumaa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakhutubu, akakaa kabla ya kuswali rakaa mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (930) na Muslim (875)].

 

3- Hadiyth ya Jaabir asemaye: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru aswali rakaa mbili wakati alipoingia Msikitini kwa ajili ya fedha ya ngamia wake ambaye Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimnunua”.

 

Amri katika Hadiyth hizi zinaonyesha kwamba ni za wajibu, na makatazo yanaonyesha uharamu wa kuziacha rakaa mbili. Lakini Jamhuri ya Maulamaa akiwemo Ibn Hazm, wanaona kwamba uwajibu huu unapinduliwa kupelekwa katika uSunnah kwa dalili mbalimbali. Kati ya dalili hizo ni Hadiyth isemayo: ((Ni Swalaah tano mchana na usiku)). Muulizaji akasema tena: “Je, kuna jingine zaidi?” Akasema: ((Hapana, ila kama utaswali za Sunnah)). [Hadiyth Swahiyh: Tushaielezea mara nyingi].

 

Ash-Shawkaaniy Rahimahul Laahu ameijibu akisema kwamba neno lake Rasuli ((Ila kama utaswali za Sunnah)) linakanusha kimsingi wajibu lakini si wajibu unaotokana na sababu ambazo mkalifishwaji anachagua mwenyewe kuufanya kama kuingia Msikitini kwa mfano. Hapa mwenye kuingia, amejiwajibishia mwenyewe Swalaah kwa kuingia, kana kwamba yeye amejiwajibishia mwenyewe, na hivyo basi haisihi kuingiza cha kugeuza ujiwajibishaji huu kwa mfanowe.  [Naylul Awtwaar (3/84) chapa ya Al-Hadiyth. Faida ya maneno haya iko ndani ya Hadiyth lakini Al-Haafidh hakuitohoa humo!]

 

Ninasema:Hadiyth ya Abu Waaqid Al-Layth inaweza kutilia nguvu ya kwamba amri hizi ni Sunnah. Hadiyth inasema kwamba wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa amekaa Msikitini pamoja na watu, waliingia watu watatu. Wawili wakaelekea kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na mmoja akaondoka. Hao wawili wakasimama mkabala wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mmoja wao akaiona nafasi kwenye halaqa akakaa, na yule mwingine akakaa nyuma yao. Ama yule wa tatu, huyo aligeuza njia na kwenda zake. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomaliza darsa alisema:

((Je, niwaelezeni habari ya watu watatu? Ama mmoja wao, huyu alikimbilia kwa Allaah na Allaah Akampa hifadhi. Ama mwingine, huyu aliona haya na Allaah Akamwonea haya. Ama wa tatu, huyo aligeuza mgongo na Allaah Akamwachilia mbali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (930)].

 

Ninasema: “Walikaa na Rasuli hakuwaamuru kuswali rakaa mbili. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

· Faida

 

Tumetangulia kusema katika mlango wa “Nyakati zilizoharamishwa kuswali” kwamba Tahiyyatul Masjid ni katika Swalaah zenye sababu zinazoswaliwa wakati wowote hata katika nyakati za karaha kwa mujibu wa kauli zenye nguvu. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

· Swalaah Baada Ya Kutawadha

 

Imesuniwa kwa aliyetawadha aswali rakaa mbili au zaidi wakati wowote hata katika nyakati zilizokirihishwa kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Bilaal wakati wa Swalaah ya Alfajiri:

((Ee Bilaal! Nielezee amali yenye matarajio zaidi uliyoifanya katika Uislamu, kwani mimi nimesikia mtaharuki wa viatu vyako mbele yangu huko peponi)).

Bilaal akasema: “Sikufanya amali yoyote yenye matarajio makubwa kwangu zaidi ya kuwa sikupata kujitwaharisha wakati wowote wa usiku au mchana, ila huswali kwa twahara hiyo kile nilichoandikiwa kukiswali”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1149) na Muslim (910)].

 

 

 

Share