033-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya Kuomba Mvua (Al-Istisqaa)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

033-Swalaah Ya Kuomba Mvua (Al-Istisqaa) 

 

Alhidaaya.com

 

 

· Taarifu yake:

 

“Al-Istisqaa” ni kumwomba Allaah Aiteremshe mvua wakati wa ukame. Maulamaa wote wamekubaliana kwamba hilo ni Sunnah aliyoiweka Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini wamekhitalifiana kuhusiana na Swalaah yenyewe kama tutakavyobainisha.

 

· Hukmu Ya Swalaah Ya Kuomba Mvua

 

Ukame ukiingia, ardhi ikakauka na mvua ikapotea, imesuniwa imamu atoke pamoja na watu hadi sehemu maalumu ya kuswalia kama tutakavyoeleza, kisha aswali nao rakaa mbili. Hili ndilo lililothibiti toka kwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abbaad bin Tamiym toka kwa ami yake akisema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka kwenda sehemu ya kuswalia kwa ajili ya kuomba mvua. Alielekea Qiblah na kuswali rakaa mbili na akageuza nguo yake kwa kupindua kulia kuja kushoto.” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy].

 

Abu Haniyfah ameenda kinyume katika hili akisema: “Swalaah ya Kuomba Mvua haikusuniwa wala kutoka kwa ajili yake”. [Ibn ‘Aabidiyn (2/184) na Fat-hul Qadiyr (2/57)]

Dalili yake ni yaliyosimuliwa kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba mvua bila kuswali kama itakavyokuja.

 

Hadiyth ni hoja dhidi yake. Na kitendo chake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) cha kuomba mvua bila Swalaah hakizuii kuwa Nabiy aliyafanya yote mawili, kwani hayapingani.

 

· Yaliyosuniwa Katika Swalaah Ya Kuomba Mvua

 

1- Watu watoke pamoja na imamu kwenda sehemu ya kuswalia wakivaa nguo chakavu kidogo, kwa unyenyekevu na kwa kuomba du’aa

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka akiwa amevaa nguo chakavu, kwa unyenyekevu huku akiomba mpaka sehemu ya kuswalia. Akapanda mimbari, na wala hakukhutubu khutbah yenu hii, lakini aliendelea kufanya du’aa, kuomba kwa unyenyekevu na kupiga takbiyr. Halafu aliswali rakaa mbili kama anavyoswali katika ‘Iyd”. [Al-Albaaniy kasema ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1165), At-Tirmidhiy (555), na An-Nasaaiy. Angalia Al-Irwaa (665)].

 

2- Imamu akhutubu kabla ya Swalaah au baada ya Swalaah juu ya mimbari atakayotayarishiwa

 

Wenye kusema kwamba Swalaah ya Kuomba Mvua ni Sunnah wamekubaliana kwamba Swalaah hii ina khutbah isipokuwa riwaya katika madhehebu ya Ahmad. Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Maulamaa wengi wanasema kwamba khutbah inakuwa baada ya Swalaah.  [Ad-Dusuwqiy (1/406), Al-Ummu (1/221), Al-Majmu’u (5/77), Al-Mughniy (2/433), na Kash-Shaaful Qina’a (2/69)].

 

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Zayd asemaye: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka hadi sehemu ya kuswalia, akaomba mvua na kugeuza nguo yake wakati alipoelekea Qiblah. Akaanza na Swalaah kabla ya khutbah, kisha akaelekea Qiblah na kuomba”. [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (4/41) na asili yake ni kwenye Al-Bukhaariy (1027). Lakini humo hakuna ubainisho wa mahala pa shahidi].

 

2- Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka siku moja kwa ajili ya kuomba mvua. Akatuswalisha rakaa mbili bila ya adhana au iqaamah. Kisha akatukhutubia, akamwomba Allaah Mtukufu na akageuza nguo yake; kulia akakufanya kushoto na kushoto akakufanya kulia”. [Isnadi yake ni teketeke. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/326) na Ibn Maajah].

 

Katika riwaya nyingine iliyopokelewa toka kwa Maalik na Ahmad, wao wanasema kwamba khutbah inakuwa kabla ya Swalaah. Hoja yao ni Hadiyth ya ‘Abdullah bin Zayd asemaye: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka kwa ajili ya kuomba mvua. Akaelekea Qiblah na kuomba, halafu akaipindua nguo yake. Kisha aliswali rakaa mbili ambapo alisoma kwa sauti ya kusikika”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1024) na Muslim (894)].

 

Inavyoonekana ni kuwa suala hili lina wasaa. Khutbah inaweza kuwa kabla ya Swalaah au baada ya Swalaah. Chaguzisho hili ni riwaya ya tatu kwa mujibu wa kauli ya Ahmad na chaguo la Ash-Shawkaaniy na wengineo.

 

Imesuniwa khutbah iendane sambamba na tukio lenyewe. Imamu aonyeshe kumhitajia kidhati Allaah, kujuta na kurejea Kwake. Ni kama alivyosema Ibn ‘Abbaas wakati ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu Anhu) alipomtaka aombe mvua: “Na hii mikono yetu tumeinyoosha Kwako ikiwa imejaa dhambi, na tosi zetu tumezielekeza Kwako tukitubu, basi Tuteremshie mvua”. [Al-Haafidh ameieleza kwenye Al-Fat-h (2/497) na ameinasibisha kwa Az Zubayr bin Bakkaar katika Al-Ansaab]

 

Na mfano wa maneno kama haya ambayo tutakuja kuyagusia baadaye.

 

3- Imamu akithirishe kuomba du’aa akiwa amesimama, ameelekea Qiblah, ameinyanyua juu kabisa mikono yake na kuelekeza mgongo wa viganja vyake mbinguni. Watu nao wanyanyue mikono yao na imamu apindue nguo yake.

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Zubayr akisema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka pamoja na watu kwa ajili ya kuwaombea mvua. Akasimama na kumwomba Allaah hali ya kuwa amesimama, kisha akaelekea Qiblah, akalipindua joho lake na watu wakapata mvua”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1023), na Ad-daaramiy (1534)].

 

Imepokelewa na Anas akisema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hanyanyui mikono yake miwili kwa lolote analoliomba isipokuwa katika du’aa ya kuomba mvua. Katika du’aa hii, alikuwa akinyanyua mikono mpaka weupe wa kwapa zake huonekana”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1031) na Muslim (895)].

 

Imepokelewa na Anas akisema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba mvua akaelekeza mgongo wa viganja vyake mbinguni”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (896), Abu Daawuud (1171) na Ahmad (3/153)].

 

Na katika tamshi la Abu Daawuud: “Alikuwa akiomba mvua hivi, akanyoosha mikono yake (akaelekeza matumbo yake chini) mpaka nikaona weupe wa kwapa zake”.

 

An Nawawiy kasema: “Maulamaa wamesema: “Ni Sunnah kunyanyua mikono miwili na kuelekeza mgongo wa viganja mbinguni katika kila du’aa ya kuomba kuondoshwa janga. Na anapoomba mtu jambo lolote aelekeze viganja vyake mbinguni”.

 

Mwingine kasema: “Hikma ya kuashiria kwa mgongo wa viganja wakati wa kuomba mvua pasina du’aa nyingine, ni kuweka rajua njema ya kugeuka hali toka juu kuja chini kama ilivyosemwa kuhusiana na kupindua nguo, au ni ishara ya picha ya chenye kuombwa ambacho ni kuteremka mvua kuja ardhini”. [Fat-hul Baariy (3/601)]

 

Ama watu kunyanyua mikono yao, hayo yako kwenye Hadiyth ya Anas ikizungumzia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuomba mvua siku ya ijumaa juu ya mimbari: “..Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanyanyua mikono yake akiomba, na watu wakanyanyua mikono yao pamoja naye wakiomba”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1029)].

 

Ama imamu kupindua nguo yake kulikoelezewa kwenye Hadiyth ya ‘Abdullah bin Zayd, maana yake ni kuuleta upande wa kulia wa nguo yake upande wa kushoto na kinyume chake, na hili limependelewa na Jamhuri ya Maulamaa. Wengine wamesema kuwa ni vizuri kuipindua nguo nje kuifanya ndani, na ndani nje kutokana na Hadiyth ya Ibn Zayd asemaye: “ Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalaah ya kuomba mvua akiwa amejitanda guo la mistari. Akataka kuileta sehemu yake ya chini juu, na ilipomlemea aliipindua juu ya mabega “. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (4/41), Abu Daawuud (1164) na Al-Bayhaqiy (3/351). Angalia Al-Irwaa (3/142)].

 

Hikma ya yote hayo ni kuweka rajua njema ya kubadilika hali ya mambo, na wakati wa kupindua nguo ni baada ya kumaliza khutba.

 

4- Du’aa swahiyh za kuomba

 

(a) Imepokelewa toka kwa Jaabir akisema: “Wanawake waliokuwa wakilia walimjia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

(( Allaahumma Isqinaa ghaythan mughiythan, mariy-an naafi’an ghayra dhwaarrin ‘aajilan ghayra aajilin)), na hapo hapo mawingu yakafunga. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1169), Al-Haakim (1/327) na Al-Bayhaqiy, na kwa njia yake Al-Bayhaqiy (3/355)].

 

(b) Imepokelewa toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake akisema: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiomba mvua alikuwa akisema:

((Allaahumma Isqi ‘ibaadaka wa bahaaimaka, wanshur Rahmataka, wa Ahyi baladaka al mayyit)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1176)].

 

(c) Wakati ukame ulipoingia na Nabiy akawaahidi watu kutoka, ‘Aaishah anaelezea akisema: “Alikaa juu ya mimbari, akapiga takbiyr na akamhimidi Allaah ‘Azza wa Jalla kisha akasema: ((Hakika nyinyi mmeshtakia ukame wa nyumba zenu na kuchelewa mvua wakati wake. Na Allaah Subhaanah Amekuamuruni mumwombe, Naye Amekuahidini kuwa Atakujibuni)). Kisha akasema:

(( الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ)) Laailaaha illa Allaahu Yaf’alu maa Yuriydu. Allaahumma Anta Allaahu laa ilaaha illaa Anta. Anta Al-Ghaniyyu wanahnul fuqaraau, Anzil ‘Alaynaa alghaytha, Waj-’al maa Anzalta lanaa quwwatan wa balaaghan ilaa hiyn)). [Al-Albaaniy kasema ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1173) na Al-Haakim (1/328). Angalia Al-Irwaa (668)].

 

5- Imamu awaswalishe rakaa mbili kama Swalaah ya ‘Iyd na asome kwa sauti

 

Ni kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyotangulia isemayo: “Akaswali rakaa mbili kama anavyoswali ‘Iyd”. [Al-Albaaniy kasema ni Hasan: Tumeitaja nyuma kidogo].

Pia Hadiyth ya ‘Abdullah bin Zayd isemayo: “Kisha akaswali rakaa mbili na akasoma kwa sauti”. [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo].

 

· Kuomba Du’aa Ya Mvua Bila Kuswali

 

Imethibiti toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) njia kadhaa za kuomba mvua bila kutoka kwenda kuswali. Kati yake ni:

 

1- Kuomba du’aa ya mvua katika khutbah ya ijumaa

 

Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Mtu mmoja aliingia Msikitini siku ya ijumaa  - na Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amesimama anakhutubu – na mtu yule akamwelekea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amesimama kisha akamwambia: Ee Nabiy wa Allaah! Mali zimeangamia na mambo yameshindikana, basi tuombee Allaah Atuokoe. Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanyanyua mikono yake kisha akasema: ((Ee Mola Tuokoe, ee Mola Tuokoe!)). Anas anasema: “Wallaah, hatuoni mbinguni wingu lolote wala vijiwingu vilivyotawanyika, wala hakuna baina yetu na mlima nyumba yoyote. Kisha likachomoza nyuma yake wingu mithili ya  ngao ya vita. Lilipofika katikati ya mbingu lilitawanyika, kisha likateremsha mvua. Wallaahi, hatukuliona jua siku sita. Kisha akaingia mtu mwingine kupitia mlango ule – huku Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amesimama anakhutubu – kisha akamwelekea akiwa amesimama na kumwambia: Ee Nabiy wa Allaah! Mali zimeangamia na mambo yameshindikana, basi tuombee Allaah Aisimamishe. Nabiy wa Allaah Akanyanyua mikono yake kisha akasema: ((Ee Mola! Inyeshe pembezoni mwetu na si juu yetu. Ee Mola! Iteremshe juu ya vilima, milima tambarare, viini vya mabonde na maoteo ya miti)). Mvua ikakatika, tukatoka Msikitini tukitembea kwenye jua.” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1041) na Muslim (897)].

 

Katika Hadiyth hii kuna faida kadhaa ambazo ni: kuingiza du’aa ya kuomba mvua kwenye khutbah ya ijumaa, kuiomba du’aa hiyo juu ya mimbari bila kupindua nguo wala kuelekea Qiblah, kuifanya Swalaah ya Ijumaa ni sehemu ya Swalaah ya kuomba mvua na kujuzu kuomba du’aa ya mvua bila Swalaah mahsusi. [Fat-hul Baariy: (2/589) Chapa ya As Salafiyyah]

 

2- Kuomba du’aa ya mvua siku isiyo ijumaa na bila ya Swalaah

 

Ni kama ilivyokuja kwenye Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Wanawake wenye kulia walimjia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Nabiy akaomba:

((Allaahumma Isqinaa ghaythan mughiythan, mariy-an naafi’an ghayra dhwaarrin ‘aajilan ghayra aajilin)), mbingu zikafunga)). [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo].

 

3- Kuomba du’aa nje ya Msikiti

 

Imepokelewa toka kwa ‘Umayr mwachwa huru wa ‘Abul Lahm ya kwamba alimwona Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiomba du’aa ya mvua mbele ya Ahjar Az Zayt karibu na Az Zawraa akiwa amesimama. Anaomba akiwa amenyanyua mikono yake miwili ikiwa mkabala na uso wake na wala haikuvuka kichwa chake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1168), At-Tirmidhiy (557), An-Nasaaiy (3/159) na Ahmad (5/223)].

 

· Yanayosemwa Na Kufanywa Wakati Mvua Inaponyesha

 

1- Imesuniwa kuomba kwa du’aa Swahiyh zilizopokelewa. Kati ya du’aa hizo ni:

 

(a) Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapoiona mvua husema: ((Allaahumma swayyiban naafi’an)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1032) na Ibn Maajah (3889)].

 

(b) Pia imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema kwamba Nabiy alipokuwa akiona mvua husema: ((Rahmatun)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (899) katika sehemu ya Hadiyth].

 

2- Ni wajibu aamini kwamba wamepata mvua kwa Fadhila za Allaah na Rahma Zake na si kutokana na nyota  au sayari

 

Imepokelewa toka kwa Zayd bin Khalid Al-Juhaniy (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Nabiy wa Allaah alituswalisha Swalaah ya Alfajiri huko Al- Hudaybiyah baada ya kunyesha usiku mvua. Alipomaliza Swalaah, aliwaelekea watu akasema: Je, mnajua nini Kasema Mola wenu? Wakasema: " Allaah na Nabiy Wake Ndio wanaojua zaidi". Akasema: Amesema Mola wenu: Amepambaukiwa kati ya Waja Wangu mwenye kuniamini mimi na mwenye kunikufuru. Ama mwenye kusema: Tumepata mvua kwa Fadhila za Allaah na Rahma Zake, basi huyo ni mwenye kuniamini Mimi na mwenye kuzikataa nyota. Ama mwenye kusema: Tumepata mvua kwa mashukio kadha wa kadha ya nyota au sayari, basi huyo amenikufuru Mimi na ameziamini nyota)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (846) na Muslim (71)].

 

Ikiwa mtu ataamini kwamba mashukio ya nyota yanaleta mvua, basi huu ni ukafiri, kwani huyo anakuwa amemkufuru Allaah. Na kama hakuitakidi hivyo - lakini akasema kwa njia ya majazi nailhali anaamini kwamba mwenye kuleta mvua ni Allaah Peke Yake kwa kuwa mvua imekuwa ni ada yake kunyesha wakati nyota zinaposhuka – basi hiyo inakuwa ni shirki ndogo kwa kuwa ameinasibisha Neema ya Allaah kwa kitu kinginecho, na kwa kuwa Allaah Hakuyafanya mashukio ya nyota kuwa ni sababu ya kunyesha mvua, bali mvua ni kutokana na Fadhila za Allaah na Rahma Zake. Anaizuia Anapotaka na Huiteremsha Anapotaka. [Fat-hul Majiyd (uk. 455-459) kwa mabadilisho kidogo na ufupisho]

 

3- Imesuniwa kuomba du’aa wakati mvua inaponyesha kwani ni wakati wa uhakika wa kujibiwa du’aa (kama Hadiyth itakuwa ni Swahiyh)

 

Ni kutokana na yaliyohadithiwa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: ((Papieni kupata majibu ya du’aa zenu wakati majeshi yanapokutana, Swalaah inapoqimiwa na mvua inaponyesha)). [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh: Angalia Silsilat As-Swahiyhah (1469) na Swahiyhul Jaami’i (1026)].

 

4- Imesuniwa aiachie sehemu ya mwili wake ipigwe na mvua

 

Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Mvua ilitunyeshea tukiwa pamoja na Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nabiy akaifunua sehemu ya mwili wake ikapigwa na mvua. Tukasema: Ee Nabiy wa Allaah! Kwa nini umefanya hivyo? Akajibu: ((Kwa kuwa bado i-mbichi toka kwa Mola wake Mtukufu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (898) na Abu Daawuud (5100)].

 

5- Mvua ikikithiri na madhara yake yakahofiwa

 

Imesuniwa aombe kwa kunyanyua mikono yake miwili – kama tulivyoeleza kwenye Hadiyth ya Anas ya kuombwa du’aa juu ya mimbari Siku Ya Ijumaa -, aseme: (( Allaahumma hawaalaynaa walaa ‘alaynaa. Allaahumma ‘alal-aakaam, wadh-dhuraab, wabutuunil awdiyah wamanaabit ash-shajarah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1014) na Muslim 897)].

 

 

 

Share