02-Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Mwenye Hedhi Akitoharika Kabla Ya Alfajiri Lakini Akaoga Baada Ya Swalaah Swawm Yake Sahihi?
Fataawaa Mas-ala 60 Kuhusu Hedhi Na Nifaas
02-Mwenye Hedhi Akitoharika Kabla Ya Alfajiri
Lakini Akaoga Baada Ya Swalaah Swawm Yake Sahihi?
Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah)
SWALI:
Muulizaji huyu anasema: Pindi aliyekuwa na hedhi akitoharika na kukoga (ghuslu) baada ya Swalaah ya Alfajiri akaswali na kukamilisha Swawm ya siku ile, je yampasa kuilipa?
JIBU:
Pindi aliyekuwa na hedhi akitoharika kabla ya kuchomoza Alfajiri, hata kama ni kwa dakika moja lakini akathibitika kutoharika kwake ikiwa ni Ramadhwaan, itamlazimu afunge na Swawm yake siku hiyo itakuwa sahihi wala haimpasi kulipa; kwani alifunga akiwa ametoharika na kama hajakoga ila baada ya kuchomoza Alfajiri basi si neno kwake, kama vile ambavyo mtu atakuwa na janaba baada ya jimai au kuota na akakesha na hakukoga ila baada ya kuchomoza Alfajiri basi Swawm yake itakuwa sahihi.
Kwa mnasaba huu ningependa kuwatanabahisha katika jambo lingine kwa mwanamke inapomjia hedhi hali ya kuwa yuko kwenye Swawm siku ile kwani baadhi ya wanawake wanadhani kuwa hedhi inapowajia baada ya kufuturu kwake (Magharibi) na kabla ya Swalaah ya ‘Ishaa, hudhani kuwa Swawm yake imeharibika siku ile. Hii si kweli na haina asili yoyote ile bali ni kuwa hedhi inapomjia baada ya kuzama kwa jua (Magharibi) walau kwa muda mdogo, basi Swawm yake huwa ni sahihi.