56-Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Swafaa Na Marwah Na Hukmu Ya Mwenye Hedhi Na Hukmu Ya Tahiyyatul-Masjid
Fataawaa Mas-ala 60 Kuhusu Hedhi Na Nifaas
56-Swafaa Na Marwah Na Hukmu Ya Mwenye Hedhi Na Hukmu Ya Tahiyyatul-Masjid
Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah)
SWALI:
Je, Al-Mas’aa (sehemu ya Swafaa na Marwah) ni katika Msikiti (Al-Haram)? Je, mwenye hedhi anaruhisiwa kuikurubia? Na je anayeingia Msikitini kupitia eneo la Mas’aa aswali Tahiyyatul-Masjid? (Rakaa za kuamkia Msikiti)
JIBU:
Kinachodhihiri ni kuwa Al-Mas’aa sio katika Msikiti na ndio maana ikawekwa ukuta unaotenganisha lakini ni ukuta mfupi na hapana shaka kuwa hili ni jambo la kheri kwa watu, na lau ingeingia au kuingizwa Msikitini na kufanywa sehemu ya Msikiti basi ingekuwa mwanamke akipatwa na hedhi katikati ya Twawaaf na Sa’yi basi atazuiwa kufanya Sa’yi na lile ambalo nalifutu hapa ni kuwa mwanamke akipata hedhi baada ya Twawaaf na kabla ya kufanya Sa’yi huyo atafanya Sa’yi kwa sababu Al-Mas’aa haizingatiwi kuwa ni Msikiti.
Ama Tahiyyatul-Masjid inaweza kusemwa: Kuwa mtu akifanya Sa’yi kati ya Swafaa na Marwah baada ya Twawaaf kisha akarejea Msikitini basi ataiswali lau hata akiacha Tahiyyatul-Masjid si neno juu yake na bora zaidi atumie fursa hiyo kuswali rakaa mbili kwani kuswali sehemu hii ni bora zaidi.