57-Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Baada Ya Kuhiji Amepata Hedhi Akaona Hayaa Akaswali Na Kutufu Al-Ka’bah Na Kutekeleza Sa’yi
Fataawaa Mas-ala 60 Kuhusu Hedhi Na Nifaas
57-Baada Ya Kuhiji Amepata Hedhi Akaona Hayaa
Akaswali Na Kutufu Al-Ka’bah Na Kutekeleza Sa’yi
Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah)
SWALI:
Anauliza muulizaji: Nilikuwa nimeshahiji ikanijia ada yangu ya mwezi nikaona haya kumwambia mtu nikaingia Al-Haram (Msikitii wa Makkah) nikaswali na kutufu na kufanya Sa’yi. Nifanye nini baada ya hapo na suala hili limenijia baada ya nifaas?
JIBU:
Haiwi halaal kwa mwanamke akiwa ni mwenye hedhi au mwenye nifaas kuswali iwe ni Makkah au katika mji wake au sehemu yoyote ile kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mwanamke:
أليس إذا حاضت لم تصل ولم تصم
“Si unajua kuwa mwanamke akiwa na hedhi haswali wala hafungi.”
Na Waislamu wamekubaliana katika ‘Ijmaa kuwa si halaal kwa mwenye hedhi kufunga, wala haiwi halaal kwake kuswali. Na kwa ajili hii mwanamke ambaye amefanya hivyo juu yake ni kutubia kwa Allaah na kuomba maghfirah kwa yaliyotokea.
Ama kuhusu Twawaaf yake akiwa katika hali ya hedhi sio sahihi. Ama Sa’yi yake ni sahihi. Kwa sababu kauli inayokubalika ni kuruhusiwa kutanguliza Sa’yi kuliko Twawaaf katika Hajj, na kwa hili inampasa kwake arejee kufanya Twawaaf; kwa kuwa Twawaaf Al-Ifaadhwah ni nguzo katika nguzo za Hajj. Wala haitimii kutahallal (kujivua katika ihraam) ya pili isipokuwa kwayo na kwa ajili ya hilo, mwanamke huyu hawezi kuingiliwa na mumuwe akiwa ameolewa hadi afanye Twawaaf, wala haolewi akiwa bado hajaolewa hadi afanye Twawaaf. Na Allaah Mjuzi zaidi