036-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa kuilisha Familia

 

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

 

باب النفقة عَلَى العيال

036-Mlango Wa kuilisha Familia

 

Alhidaaya.com

 

قَالَ الله تَعَالَى:

وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ﴿٢٣٣﴾

Na ni juu ya mzazi wa kiume kuwapatia chakula chao na nguo kwa mujibu wa ada. [Al-Baqarah: 233]

لِيُنفِقْ ذُو سَعَةٍ مِّن سَعَتِهِ ۖ وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ فَلْيُنفِقْ مِمَّا آتَاهُ اللَّـهُ ۚ لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا مَا آتَاهَا ﴿٧﴾

Ili mwenye wasaa agharimu kwa wasaa wake, na aliyebaniwa riziki yake, basi agharimie katika kile Alichompa Allaah. Allaah Haikalifishi nafsi yeyote ile isipokuwa kwa kile Alichoipa. [Atw-Twalaaq: 7]

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ﴿٣٩﴾

Na kitu chochote mtoacho, basi Yeye Atakilipa [Sabaa: 39]

 

 

Hadiyth – 1

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( دِينَارٌ أنْفَقْتَهُ في سَبيلِ اللهِ ، وَدِينار أنْفَقْتَهُ في رَقَبَةٍ ، وَدِينارٌ تَصَدَّقْتَ بِهِ عَلَى مِسْكِينٍ ، وَدِينَارٌ أنْفَقْتَهُ عَلَى أهْلِكَ ، أعْظَمُهَا أجْراً الَّذِي أنْفَقْتَهُ عَلَى أهْلِكَ )) رواه مسلم .

Na imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Dinari unayotumia katika Njia ya Allaah (jihaad), na Dinari unayotumia kumwacha huru mtumwa, na Dinari unayoitoa sadaka kwa maskini, na Dinari unayotumia kwa familia yako, yenye ujira mkubwa zaidi ni ile unayotumia kwa familia yako." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 2

وعن أَبي عبد الله ، ويُقالُ لَهُ : أَبو عبد الرحمان ثَوبَان بن بُجْدُد مَوْلَى رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( أفْضَلُ دِينَارٍ يُنْفقُهُ الرَّجُلُ : دِينَارٌ يُنْفِقُهُ عَلَى عِيَالِهِ ، وَدينَارٌ يُنْفقُهُ عَلَى دَابَّتِهِ في سَبيلِ الله ، وَدِينارٌ يُنْفقُهُ عَلَى أصْحَابهِ في سَبيلِ اللهِ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu 'Abdillaahi-pia anajulikana kama Abu 'Abdur-Rahman - Thawbaan bin Bujdud, mtumishi wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Dinari iliyo bora zaidi inayotumiwa na mtu ni ile anayotumia kwa familia yake, na Dinari anayoitumia kwa mnyama katika Njia ya Allaah, na kisha Dinari anayoitumia kwa sahibu zake katika Njia ya Allaah." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 3

وعن أمِّ سَلمَة رَضي الله عنها ، قَالَتْ : قُلْتُ : يَا رَسُول الله ، هَلْ لِي أجرٌ فِي بَنِي أَبي سَلَمَة أنْ أُنْفِقَ عَلَيْهِمْ ، وَلَسْتُ بِتَارِكتهمْ هكَذَا وَهكَذَا إنَّمَا هُمْ   بَنِيّ ؟ فَقَالَ : (( نَعَمْ ، لَكِ أجْرُ مَا أنْفَقْتِ عَلَيْهِمْ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Amesema Umm Salamah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kuwa alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Je, nitakuwa na ujira nitakapotumia kwa ajili ya watoto wa Abi Salamah, ilhali mimi siwezi kuwaacha wakitangatanga huku na kule ambapo wao ni watoto wangu." Akasema: "Ndio, utapata ujira kwa unachotumia kwao." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 4

وعن سعد بن أَبي وقاص رضي الله عنه في حديثه الطويل الَّذِي قدمناه في أول الكتاب في باب النِّيَةِ : أنَّ رسولَ الله صلى الله عليه وسلم، قَالَ لَهُ : (( وإنَّكَ لَنْ تُنْفِقَ نَفَقَةً تَبْتَغِي بِهَا وَجْهَ اللهِ إلاَّ أُجِرْتَ بِهَا حَتَّى مَا تَجْعَلُ في فيِّ امرأتِك )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ . 

Na imepokewa kutoka kwa Sa'ad bin Abu Waqqaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) katika hadiyth ndefu tuliyo itanguliza mwanzo wa kitabu hiki katika mlango wa Nia kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Na hakika wewe hutatumia pesa kutaka radhi za Allaah isipokuwa utapata ujira kwayo mpaka utakacho jaalia katika mdomo wa mkeo (kumlisha) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 5

وعن أَبي مسعود البدري رضي الله عنه، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( إِذَا أنْفَقَ الرَّجُلُ عَلَى أَهْلِهِ نَفَقَةً يَحْتَسِبُهَا فَهِيَ لَهُ صَدَقَةٌ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ . 

Na imepokewa kutoka kwa Abu Mas'uud Al-Badriy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mtu akiipa familia yake matumizi akiyatarajia thawabu basi hiyo ni sadaqa yake." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 6

وعن عبد الله بن عمرو بن العاص رضي الله عنهما ، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( كَفَى بِالمَرْءِ إثْمَاً أنْ يُضَيِّعَ مَنْ يَقُوتُ )) حديث صحيح رواه أَبُو داود وغيره .

ورواه مسلم في صحيحه بمعناه ، قَالَ : (( كَفَى بِالمَرْءِ إثْمَاً أنْ يحْبِسَ عَمَّنْ يَمْلِكُ قُوتَهُ )) .

Na imepokewa kutoka kwa 'Abdillaahi bin 'Amr bin al-'Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhummaa) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Inatosha mtu kuwa na dhambi kwa kumtupa anyemlisha." Hadiyth Swahiyh [ Abu Daawuud na wengineo]

Muslim ameinukuu katika Sahihi yake kwa maana yake: "Yatosha kwa mtu kuwa na dhambi kwa kumzuilia rizki anayemtegemea."

 

 

Hadiyth – 7

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه: أن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( مَا مِنْ يَوْمٍ يُصْبِحُ العِبَادُ فِيهِ إلاَّ مَلَكانِ يَنْزلاَنِ ، فَيقُولُ أحَدُهُمَا : اللَّهُمَّ أعْطِ مُنْفقاً خَلَفاً ، وَيَقُولُ الآخَرُ : اللَّهُمَّ أعْطِ مُمْسِكاً تلَفاً ))  مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakuna siku yoyote waja wanapambazuka ndani yake, ila Malaika wawili wanateremka, mmoja wao anasema: 'Ee Allaah, mpe badali mwenye kutoa.' Na mwengine anasema: 'Ee Allaah, mpe hasara mwenye kuzuia' " [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 8

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( اليَدُ العُلْيَا خَيْرٌ مِنَ اليَدِ السُّفْلَى ، وَابْدَأ بِمَنْ تَعُولُ ، وَخَيْرُ الصَّدَقَةِ مَا كَانَ عَنْ ظَهْرِ غِنىً ، وَمَنْ يَسْتَعْفِفْ يُعِفَّهُ اللهُ ، وَمَنْ يَسْتَغْنِ يُغْنِهِ اللهُ )) رواه البخاري .

Na imepokewa kutoka kwake Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mkono wa juu ni bora kuliko mkono wa chini. Anza kwa unayemlisha. Sadaka bora inakuwa kwa mwenye kujitosha. Anayejizuia Allaah Humtosheleza, na mwenye kukinai, Allaah Humkinaisha." [Al-Bukhaariy]

 

 

Share