11-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaah Ya Mapambo
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Zakaah
11-Zakaah Ya Mapambo
Wanachuoni wa Salaf na Khalaf wamekhitalifiana kwa kauli mbalimbali kuhusu Zakaah ya mapambo ya dhahabu na fedha. Kuna kauli mbili mashuhuri zaidi kati ya hizo:
Ya kwanza:
Hakuna Zakaah katika mapambo ya kawaida ya mwanamke ya dhahabu na fedha (anayoyavaa). Haya ni madhehebu ya Jumhuri ya ‘Ulamaa. [Ad-Durru Al-Mukhtaar (2/41), Bidaayatul Mujtahid (1/242), Al-Majmuw’u (6/29) na Al-Mughniy (3/9-17)]
Ni kauli ya Ibn ‘Umar, Jaabir, ‘Aaishah na Asmaa bint Abiy Bakr ambao ni katika Swahaba. Dalili zao ni:
1- Hadiyth:
((ليس في الحلي زكاة))
((Hakuna Zakaah katika vipambo)). [Ibn Al-Jawziy katika At-Tahqiyq. Al-Bayhaqiy na wengineo wameihukumu kuwa haifai. Angalia Al-Irwaa (817)]
Ni Hadiyth Baatwil Marfu’u, na la sawa ni iwe mawquwf kwa Jaabir.
2- Imepokelewa toka kwa Naafi’u kuwa Ibn ‘Umar alikuwa akiwapamba mabinti zake na vijakazi wake kwa dhahabu, na haitolei Zakaah. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik (585) na Al-Bayhaqiy (4/138) kwa Sanad Swahiyh]
3- Kauli ya Ibn ‘Umar: ((Hakuna Zakaah katika vipambo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq (4/82), Ibn Shaybah (3/154) na Ad-Daaraqutwniy (2/109) kwa Sanad Swahiyh]
4- Kauli ya Jaabir bin ‘Abdillaah alipoulizwa kama kuna Zakaah katika vipambo, akasema: “Hakuna”. Akaulizwa: “Hata vikifikia dinari alfu?” Jaabir akasema: “Nyingi”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq (4/82) na Al-Bayhaqiy (4/138) kwa Sanad Swahiyh]
Na katika riwaya amesema: “Huazimwa na huvaliwa” . [Riwaya hii ni ya Ibn Abiy Shaybah (3/155)]
5- Toka kwa ‘Aaishah ya kuwa alikuwa akiwasimamia mabanati yatima wa kaka yake chini ya ulezi wake. Walikuwa na mapambo na hatoi Zakaah ya vipambo vyao. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik (584) na ‘Abdul Razzaaq (4/83), nayo ni Swahiyh]
6- Toka kwa Asmaa kuwa alikuwa hatoi Zakaah ya vipambo. [Muswannaf Ibn Abiy Shaybah (3/155) kwa Sanad Swahiyh]
7- Wanasema: “Zakaah inakuwa katika mali inayozalika na kulindwa. Na vipambo vilivyoruhusiwa havizalishi kitu, ni kama nguo tu. Lakini ikiwa atavihifadhi na kuvifanya hazina ya mali, au akavitayarisha kwa biashara, basi vitatolewa Zakaah”.
Angalizo:
Wenye kauli hii wanashurutisha kipambo kiwe katika vyenye kuruhusika kisharia. Kama haviruhusiki kama mwanamume kujiwekea dhahabu, basi ni lazima atoe Zakaah.
Ya pili:
Mapambo yote ya dhahabu na fedha ni lazima yatolewe Zakaah kama yatafikia kiwango na kupitiwa na mwaka, ni sawa yakawa ya kuvaliwa, au ya kuwekwa akiba, au ya kutayarishwa kwa biashara. [Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, riwaya toka kwa Ahmad na Ibn Hazm. Angalia Fat-hul Qadiyr (1/524), Ad-Durru Al-Mukhtaar (2/41) na Al-Muhallaa (6/78). Ni kauli ya Ibn Mas’uwd, ‘Umar, ‘Abdullaah bin ‘Amri na riwaya toka kwa ‘Aaishah]
Hoja za kauli hii ni: [Angalia Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/143) na yanayofuatia ya Sheikh wetu Mustwafaa bin Al-‘Adawiy]
1- Ujumuishi uliokuja kwenye Qur-aan Tukufu kama Neno Lake Ta’aalaa:
((وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ))
((Na wale wanaorundika dhahabu na fedha (silver) na wala hawazitoi katika Njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo)). [At-Tawbah (9:34)]
2- Hadiyth jumla zilizopokelewa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zenye kuamuru kutoa Zakaah ya dhahabu na fedha kama neno lake:
((ما من صاحب ذهب لا يؤدي ما فيها إلا جعل له يوم القيامة صفائح من نار يكوى بها))
((Hakuna yeyote mwenye dhahabu ambayo haitolei yanayostahiki ndani yake, isipokuwa itatengenezwa kwa ajili yake Siku ya Qiyaamah vipande vya bati vya moto ababuliwe navyo.…)). [Imekharijiwa nyuma kidogo]
3- Hadiyth mahsusi zilizokuja kuhusiana na utoaji wa Zakaah ya vipambo na makamio kwa asiyetoa. Kati ya Hadiyth hizo:
(a) Hadiyth ya ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake: ((Kuwa mwanamke mmoja alimwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na binti yake, na binti amevaa mkononi bangili mbili nzito za dhahabu. Akamwambia: ((Je, unatoa Zakaah ya hivi?)) Akasema: Hapana. Akasema: ((Je, utapenda Allaah Akuvalishe kwazo bangili mbili za moto Siku ya Qiyaamah?)) Akasema: Akazivua na kuzitupa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: Ni za Allaah ‘Azza wa Jalla na Rasuli Wake)). [Swahiyh Lishawaahidihi. Imekharijiwa na Abu Daawuud (1563), An-Nasaaiy (5/38), At-Tirmidhiy (637) na Ahmad (2/178)]
(b) Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Shaddaad aliyesema: ((Tuliingia kwa ‘Aaishah mke wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwangu akaona mkononi mwangu pete kubwa za fedha. Akauliza: Nini hii ee ‘Aaishah? Nikasema: “Nimezitengeneza ili nijipambie kwa ajili yako ee Rasuli wa Allaah”. Akauliza: ((Je, unazitolea Zakaah?)) Nikasema: “Hapana, au Maa Shaa Allaah”. Akasema: ((Hiyo itakutosheleza wewe na moto)). [Hasan Lishawaahidih. Imekharijiwa na Abu Daawuud (1565), Ad-Daaraqutwniy (2/105), Al-Haakim (1/389) na Al-Bayhaqiy (4/139). Katika Isnaad yake kuna maneno yanayoyaunga ya kabla yake]
(c) Hadiyth ya Asmaa binti Yaziyd aliyesema: ((Niliingia mimi na khalati yangu kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) naye [khalati] amevaa bangili za dhahabu. Akatuuliza: ((Je, mnazitolea Zakaah yake?)) Tukajibu: “Hapana”. Akasema: ((Hivi hamwogopi Allaah kuwavisheni kwazo bangili za moto? Toeni Zakaah yake)). [Hasan Lishawaahidihi. Imekharijiwa na Ahmad (6/461), na At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (24/181). Sanad yake ni Hasan kwa nyingine zenye kuitilia nguvu zilizotangulia]
4- Athar zilizopokelewa toka kwa baadhi ya Swahaba kama:
(a) Athar ya Ibn Mas’uwd: ((Kuwa mwanamke mmoja alimuuliza kuhusu Zakaah ya vipambo naye akasema: “Vikifikia dirhamu 200 basi vitolee Zakaah”. Akasema: “Mimi ninawalea na kuwasimamia mayatima wangu, je niwape wao? Akasema: “Ndio”)). [Swahiyh Lighayrihi. Imekharijiwa na Abdur-Razzaaq (4/83) na At-Twabaraaniy (9/371) kwa Sanad Swahiyh Lighayrih]
(b) Athar ya ‘Umar: ((Ya kuwa aliandika kwa Abu Muwsaa Al-Ash-‘Ariy akimwambia: Waamuru wanawake wa Kiislamu walioko kwako watolee Zakaah vipambo vyao)). [Na katika riwaya: Vipambo vitolewe Zakaah] [Ibn Abiy Shaybah (3/153), Al-Bukhaariy katika At-Taariykh Al-Kabiyr (4/217) na Al-Bayhaqiy. Sanad yake ni Mursal]
(c) Athar ya ‘Abdullaah bin ‘Amri: ((Ya kuwa yeye alikuwa akimwandikia mweka hazina wake Saalim atoe Zakaah ya vipambo vya mabanati zake kila mwaka)). [Sunan Ad-Daaraqutwniy (2/107) kwa Sanad Hasan]
(d) Athar ya ‘Aaishah kuwa amesema: ((Hakuna ubaya kuvaa vipambo vikitolewa Zakaah yake)). [Ad-Daaraqutwniy (2/107) na Al-Bayhaqiy (4/139) na Sanad yake ni Hasan]
Madhehebu haya yamesemwa kuwa sahihi kwa Sa’iyd bin Al-Musayyib, Sa’iyd bin Jubayr, Ibraahiym An-Nakh’iy, ‘Atwaa bin Abiy Rabbaah, Az-Zuhriy, ‘Abdullaah bin Shaddaad, Sufyaan Ath-Thawriy na wengineo kama alivyonukuu hilo Sheikh wetu –Allaah Amhifadhi– katika kitabu cha Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/156-157).
Kauli yenye nguvu
Baada ya kuziweka bayana dalili za makundi mawili, ninaloliona lenye nguvu –kwa upande wangu- na ‘ilmu ya yote iko kwa Allaah Ta’alaa, ni kuwa kauli isemayo ni waajib kutoa Zakaah kwa mapambo ya dhahabu na fedha katika hali zote madhali yamefikia kiwango na kupitiwa na mwaka, ndio dalili imara zaidi, yenye kinga zaidi kuitumia, na kwayo mtu hutoka kwenye mvutano.
Zakaah si waajib katika mapambo ya lulu na vito vya thamani
Ukitoa dhahabu na fedha, Zakaah si waajib kwa lulu, marijani, zubarjad (aquamarine), yaquti (sapphire) na mfano wake kwa Ijma’a, kwa kuwa hakuna dalili juu ya hilo. [Angalia Muwattwa ya Maalik (1/250), Al-Ummu cha Ash-Shaafi’iy (2/36) na Al-Majmuw’u (6/6)]
Lakini zikiwa ni mali zilizotayarishwa kwa biashara, basi zitatolewa Zakaah kama mali nyinginezo. Hii ni kauli ya Jumhuri, na uchambuzi wake unakuja katika mlango wake, In Shaa Allaah.
Ikiwa mwanamke ana pete za dhahabu zenye stoni za vito, vipi atatoa Zakaah yake?
Kama ataweza kukitoa kito bila kuiharibu pete, basi atazitolea pete peke yake –bila vito vyake– kama zitafikia kiwango na kupitiwa na mwaka. Na kama hakuweza kuvitoa ila sharti pete iharibike, hapo atakadiria na kutoa Zakaah ya dhahabu tu. Na ikiwa pete hizi ni za biashara, basi atatoa Zakaah vile vile ya thamani ya vito kama mali za biashara kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri.
Je, vyombo na tuzo za kisanii au za kikale (Antiques) za dhahabu na fedha hutolewa Zakaah?
Kutumia vyombo vya dhahabu na fedha –na hususan katika kula, kunywa na mfano wake– ni haramu kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((لا تشربوا في آنية الذهب والفضة، ولا تلبسوا الحرير والديباج، فإنها لهم في الدنيا ولكم في الآخرة))
((Msinywee katika vyombo vya dhahabu na fedha, wala msivae hariri na dibaji (hariri nzito), kwani hivyo ni vyao duniani, na vya kwenu aakhirah)). [Al-Bukhaariy (5633) na Muslim (2067)]
Na hakuna makhitalifiano kati ya ‘Ulamaa –hata wale wenye kusema kuwa si waajib kutoa Zakaah katika vipambo vya kuvaliwa na kutumiwa– ya kuwa kilichokatazwa kukitumia na kikiwa kimetengenezwa kwa dhahabu au fedha, basi ni lazima kitolewe Zakaah, ni sawa kwa mwanamume au mwanamke, kwa kuwa sababu iliyopelekea kuharamishwa inakigusa, nayo ni kuingia kwenye israfu, kibr, na kuzivunja nyoyo za masikini. Hivyo vinakuwa sawa katika uharamisho.
Na bila shaka wanawake wameruhusiwa kujipamba kwa kuwa wanalihitajia hilo kwa ajili ya waume zao, lakini si katika matumizi ya vyombo, uharamu wake unabakia palepale.
Na masanamu yameharamishwa. Na kama yametengenezwa kwa dhahabu na fedha, uharamu wake ni maradufu.
Yakithibiti haya, basi Zakaah ipo bila ya mvutano wowote kati ya ‘Ulamaa. Na hakuna Zakaah mpaka kiwango kifikie kwa uzani, au awe na kingine kilichofikia kiwango akichanganye pamoja (yaani cha aina yake). [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah]