12-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaah Ya Mishahara Na Chumo La Kazi
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Zakaah
12-Zakaah Ya Mishahara Na Chumo La Kazi
Mtumishi mwajiriwa au mfanyakazi anayepokea mshahara kila mwezi, au kila wiki, au mfano wa hivyo, haepukiki na moja ya mawili:
Kwanza: Atakuwa na pesa (za akiba) zilizofikia kiwango, na atautumia mshahara wake wa kila mwezi bila kuigusa akiba
Na hii ndio hali ya tatu –ambayo imetajwa nyuma- kati ya hali za mali inayopatiwa manufaa katika kipindi cha mwaka. [Rejea uangalie hukmu ya mali inayopatiwa manufaa]
Hivyo basi, mtumishi huyu atajiwekea rekodi ya hesabu ya mapato yake ambapo ataandika kila pesa inayobaki katika mshahara wake, halafu ataiingiza kwenye pesa zake za akiba, kisha kila pesa ataitolea Zakaah yake baada ya kupitiwa na mwaka kuanzia tarehe ya kuzipata pesa hizo.
Kama atataka kutojisumbua na kupita njia ya usamehevu, na nafsi yake ikaonelea vyema kuwapa kipaumbele masikini na wastahiki wengineo wa Zakaah kuliko maslaha yake binafsi, basi atatolea Zakaah pesa yote aliyonayo kinapopitiwa na mwaka kiwango cha kwanza alichokimiliki katika pesa hizo. Hii inakuwa na thawabu kubwa zaidi kwake, inamnyanyulia juu zaidi daraja yake, na inampumzisha zaidi.
Na hapo, pesa alizoziongeza kwenye akiba yake baada ya kukamilika kiwango cha kwanza, zinakuwa zimelipiwa Zakaah yake mapema kabla ya kutimiza mwaka. Na kutoa Zakaah mapema kabla ya mwaka kutimia kunajuzu na hususan kama kuna dharura au maslaha. [Ni Fatwaa iliyotolewa na Tume Ya Kudumu Ya Fatwaa, Fataawaa za Al-‘Allaamah Ibn Baaz (Rahimahul Laah), Fataawaa Islaamiyyah na Jam-’u Al-Musnad (uk. 76)]
Pia anaweza kufanya jambo la tatu. Atatoa Zakaah safi ya mwezi kila mwezi -baada ya kutoa matumizi yake yote na anaowakimu kimaisha-, halafu atakuja kuitolea Zakaah pesa yake ya akiba ikishatimiza mwaka. [Fiqhu Az Zakaah cha Al-Qaradhwaawiy]
Pili: Asiwe na pesa zilizofikia kiwango na anautumia mshahara wake wote wa kila mwezi
Kama kila mwezi anaweka kiasi fulani cha akiba, basi si waajib kutoa Zakaah mpaka pesa zifikie kiwango, au zifikie kiwango kwa kuchanganywa na pesa alizoweka akiba. Na hapo ataanza kuhesabia mwaka, na inakuwa kama hali iliyotangulia.