07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Shuruti Za Kuswihi Swiyaam
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swiyaam
07-Shuruti Za Kuswihi Swiyaam
Ili Swiyaam iswihi, lazima yawepo mambo mawili:
1- Kutwaharika na hedhi na nifasi
Hili ni sharti la wajibu wa kutenda na kuswihi kwa pamoja. [Fat-hul Qadiyr (2/234) na Haashiyatu Ad-Dusuwqiy (1/509)]. Tutakuja kulizungumzia hili muda si mrefu.
2- Niya
Swawm ya Ramadhwaan ni ‘ibaadah, hivyo haiswihi isipokuwa kwa niya kama ‘ibaadah nyinginezo. Allaah Ta’aalaa Anasema:
((وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ))
((Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki)). [Al-Bayyinah (98:5)]
Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((إنما الأعمال بالنيات))
((Hakika si jinginelo, matendo ni kwa niya)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa sehemu nyingi nyuma]
Na kwa vile kujizuia kunaweza kuwa kwa sababu ya mazoea, au kukosa hamu ya kula, au ugonjwa, au mazoezi au mengineyo, hivyo hakuwajibiki ila kwa niya. An-Nawawiy amesema: “Swawm haiswihi ila kwa niya, na mahala pake ni moyoni”. [Rawdhwat At Twaalibiyn (2/350)]
Ili Niya Itosheleze Ni Lazima Iwe Na Masharti Manne
(a) Kukata shauri na kudhamiria kikweli: Kunashurutishwa ili kuondosha kabisa mbabaiko, hata lau akinuwia usiku wa shaka kufunga kesho, na kesho ikawa Ramadhwaan, basi haitomtosheleza. [Kwa kuwa ni niya ya nusu nusu]
(b) Kuainisha: Ni lazima kuainisha niya katika Swawm ya Ramadhwaan, au Swawm ya Faradhi au Swawm ya Wajibu. Haitoshi uainisho wa Swawm bila jina, wala uainisho wa Swawm fulani isiyo Ramadhwaan kwa mujibu wa Jumhuri kinyume na Abu Haniyfah. [Al-Hidaayat (2/248), Ar-Rawdhwah (2/353) na Kash-Shaaful Qinaa (2/315)]
(c) Kuilaza niya: Nako ni kuitia niya usiku, na wakati wake ni kati ya jua kuchwa hadi kuchomoza Alfajiri. Sharti hili ni la madhehebu ya Maalik, Shaafi’iy na Hanbal. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar toka kwa Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((من لم يجمع الصيام قبل الفجر، فلا صيام له))
((Ambaye hakunuwia na kuazimia Swiyaam kabla ya Alfajiri, basi hana Swiyaam)). [Imetiwa kasoro kwa Waqf. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2454), At-Tirmidhiy (730), An-Nasaaiy (4/196) na Ibn Maajah (1700) kwa Sanad Swahiyh, lakini imetiwa doa kwa Waqf. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyhul Jaami’i (6538)]
Je, ni lazima kutia niya usiku kwa Swiyaam ya Sunnah?
Tumeshaitaja Hadiyth isemayo:
((من لم يجمع الصيام قبل الفجر، فلا صيام له))
((Ambaye hakunuwia na kuazimia Swiyaam kabla ya Alfajiri, basi hana Swiyaam)).
Na imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: ((Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliingia kwangu siku moja akauliza: ((Je, mna chochote?)) Tukasema: Hapana. Akasema: ((Basi kwa hivyo mimi nafunga)). Kisha akatujia siku nyingine tukamwambia: Ëe Rasuli wa Allaah! Tumeletewa zawadi ya “hays” [Chakula cha mchanganyo wa samli na tende]. Akasema: Nionyeshe. Hakika niliamka nikiwa nimefunga)) Akaila. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1451)]
‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu kutia niya usiku katika Swiyaam ya Sunnah kutokana na Hadiyth hizi mbili. Jumhuri wamepita njia ya kukusanya, wakaichukulia Hadiyth ya Hafswa kuwa inahusiana na Swiyaam ya Faradhi, na Hadiyth ya ‘Aaishah kuwa inahusiana na Swiyaam ya Sunnah. Na niyah ya Swawm ya Sunnah ni kuanzia mchana kabla jua halijapinduka, na wengine wamesema hata baada ya jua kupinduka. Sheikh wa Uislamu amesema baada ya Hadiyth ya ‘Aaishah: “Na hii inadulisha kwamba yeye (Rasuli) aliizindua Swawm mchana, kwa kuwa alisema: فإني صائم ((Basi kwa hivyo mimi nafunga)), na الفاء hii inadulisha sababu, na maana inakuwa: Mimi nafunga kwa sababu hakuna chochote kwenu. Na inajulikana kuwa lau angenuwia na kuazimia Swawm tokea usiku, basi Swawm yake isingelikuwa kwa sababu hii. Vile vile, neno lake: فإني إذن لصائم ((Basi kwa ajili hiyo nafunga)), na إذن ni bayana zaidi kuelezea sababu kuliko الفاء “ [Sharhu Al-‘Umdah (1/86)]
Wametilia vigezo utoaji dalili wao kwa kusema kuwa hili ndilo walilolifahamu Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kutokana na kitendo cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Kwani imethibiti uzindushi wa niya ya Swawm ya Sunnah kuanzia mchana toka kwa Ibn Mas’uwd, Ibn ‘Abbaas, Abu Ayyuwb, Abu Ad-Dardaai, Hudhayfah na Abu Twalha (Radhwiya Allaahu ‘anhum).
Kadhalika, wametolea dalili agizo la Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa watu la kufunga Siku ya ‘Aashuwraa. Ilikuwa imefaradhishwa kabla ya Fardhi ya Ramadhwaan.
((من أكل فليصم بقية يومه، ومن لم يكن أكل فليصم))
((Aliyekula, basi na afunge siku yake iliyobakia, na ambaye hakuwa amekula, basi na afunge)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]
Maalik, Al-Layth, na Ibn Hazm ambaye Ash-Shawkaaniy ameungana naye, hawa wameshika msimamo wa kulalia penye uzito zaidi (At-Tarjiyh), wakaichukua Hadiyth ya Hafswah. Hawakufarikisha kati ya Swawm ya Sunnah wala Faradhi katika kushurutisha kutia niya usiku. Wakasema: “Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) – katika Hadiyth ya Hafswah- ((لا صيام)) siainishi, na ni kanushi, hivyo linazihusu Swiyaam zote, na haitoki humo isipokuwa ile ambayo imethibiti kwa dalili kuwa haishurutishwi kutiliwa niya usiku. [Naylul Awtwaar 4/233]
Wamejibu kuhusu Hadiyth ya ‘Aaishah kuwa hakuna ndani yake linalogusia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakuwa amenuwiya kufunga kuanzia usiku, wala kuwa aliamka asubuhi akiwa hakufunga, kisha akanuwia kufunga baada ya hapo. Lakini linaloelezwa ni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akiamka na Swiyaam ya Sunnah, kisha anafungua, na hili linaruhusika. Hivyo yamkinika alinuwiya tokea usiku na akataka kufungua. Na hilo linadulishwa na neno lake katika Hadiyth ya ‘Aaishah: ((فلقد أصبحت صائما)). Na haijuzu kuacha la yakini katika Hadiyth ya Hafswah kwa la dhana imkinikayo katika Hadiyth ya ‘Aaishah. [Al-Muhallaa (6/72)]
Na wamejibu kuhusu Hadiyth ya ‘Aashuwraa ya kuwa niya bila shaka imeswihi katika mchana wa ‘Aashuwraa kwa kuwa kurejea usiku hakuwezekaniki tena, na mvutano ni kwa linalowezekanika likakhusu kujuzu katika picha kama hii.
Ninasema: “Kila dhehebu katika mawili linabebwa na dalili, na kushurutisha kutia niya usiku katika Swiyaam ya Sunnah ni jambo la akiba zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.
(d) Kujadidisha niya kila usiku wa Ramadhwaan
Ni lazima kutia niya ya kufunga kila usiku katika nyusiku za Ramadhwaan –kwa mujibu wa Jumhuri ya ‘Ulamaa- kutokana na ujumuishi wa Hadiyth ya Hafswah iliyotangulia, na kwa kuwa kila siku ni ‘ibaadah kando, na siku hizi hazifungamani zenyewe kwa zenyewe na haziharibiki kwa kuharibika baadhi yake, nazo zinaingiliwa na yanayokwenda kinyume nayo, nazo ni nyusiku ambazo yanaruhusika ndani yake yaliyoharamishwa mchana.
[Raddu Al-Muhtaar (2/87), Al-Majmuw’u (6/302) na Kash-Shaaful Qinaa (2/315)]
Ama Zafr na Maalik –nayo ni riwaya toka kwa Ahmad- wao wanaona kwamba niya moja inatosheleza kwa mwezi wote mwanzoni mwake kama Swalaah, na pia katika kila Swawm ya kufunga siku mfululizo kama kafara ya Swawm na Dhwihaar. [Al-Qawaaniynu Al-Fiqhiyyah (uk. 80) na Ash-Sharhul Kabiyr (1/521)]
Ninasema: “Kauli ya kwanza (ya kutia niya kila usiku) ndio yenye nguvu zaidi kutokana na ujumuishi wa Hadiyth. Ibn ‘Abdul Hakam –ambaye ni katika ‘Ulamaa wa Maalik-amepondokea kwenye usawa na kukubaliana na madhehebu ya Jumhuri ya ‘Ulamaa”.
Faida
Niya inafanyika kwa picha iliyotangulia kwa kuamka saa za mwisho wa usiku na kula na kunywa katika wakati huo na hususan kwa yule ambaye si ada yake kufanya hivyo katika masiku yasiyo ya Ramadhwaan. Kwa kuwa niya ni kukikusudia kitu au kukitaka, na hili lishapatiwa makusudio yatakiwayo. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.