10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Mambo Yenye Kubatilisha Swiyaam

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swiyaam

 

10-Mambo Yenye Kubatilisha Swiyaam

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Swawm kiujumla inabatilika kwa kukosekana sharti moja kati ya shuruti zake, au kuharibika nguzo kati ya nguzo zake. Na mizizi ya mambo haya yenye kufunguza ni mitatu ambayo Allaah ameitaja katika Kitabu Chake:

 

((فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ))

((Basi sasa waingilieni na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe (mapambazuko) wa Alfajiri kutokana na uzi mweusi (wa kiza cha usiku). Kisha timizeni Swiyaam mpaka usiku)). [Al-Baqarah (2:187)]

 

‘Ulamaa wote bila makhitalifiano wanasema kuwa ni lazima mfungaji ajizuie wakati wa Swawm na vyakula, vinywaji na kujimai. Kisha wakakhitalifiana katika hilo katika masaail, baadhi yake yamenyamaziwa na mengine yamezungumziwa.

 

Yenye Kubatilisha Yanagawanyika Vigawanyo Viwili

 

(a) Yenye kubatilisha Swiyaam na kuwajibisha kulipa

 

Ni kula na kunywa kwa makusudi huku mfungaji akikumbuka kuwa amefunga. Ikiwa atakula au kunywa kwa kusahau, basi atatimiza Swawm yake na wala hatoilipa siku. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((من نسي -هو صائم- فأكل أو شرب، فليتم صومه، فإنما أطعمه الله وسقاه))

((Aliyesahau –naye amefunga- akala au akanywa, basi aitimize Swawm yake, kwani hakika Allaah Amemlisha na Amemnywesha)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1423) na Muslim (1155)]

 

Hukmu ni moja katika hili kwa Swawm ya Faradhi au ya Sunnah kutokana na ujumuishi wa dalili kwa Jumhuri kinyume na Maalik. Yeye ameihusisha hukmu hii kwa Swawm ya Ramadhwaan tu. Anasema ikiwa mtu amesahau katika Swawm isiyo ya Ramadhwaan, akala au akanywa, basi ni lazima ailipe. Lakini lililo sahihi ni kuwa hakuna tofauti.

 

Na kula ni kuingiza kitu hadi tumboni kwa njia ya mdomo, na kiujumla huhusisha vyenye manufaa na vyenye madhara, na visivyo na manufaa wala madhara.

 

Ikiwa mtu amekula au amekunywa au ameingilia akidhani jua limekuchwa au alfajiri bado haijachomoza, kisha ikamdhihirikia kinyume chake

 

‘Ulamaa katika hili wana madhehebu mawili:

 

La kwanza: Ni lazima alipe. Ni dhehebu la Jumhuri ya ‘Ulamaa wakiwemo Maimamu wanne. [Al-Bahru Ar-Raaiq (2/292), Al-Muntaqaa cha Al-Baajiy (2/292), Mughnil Muhjaat (1/432), Ash-Sharhul Kabiyr (2/31) na Al-Mughniy (3/354)]

 

La pili: Hana cha kulipa. Ni dhehebu la Is-Haaq, na riwaya toka kwa Ahmad, Daawuwd, na Ibn Hazm. Limenasibishwa kwa Jumhuri ya Salaf. Ni chaguo la Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah. [Al-Muhalla (6/220,229), Al-Majmuw’u (6/311) na Majmuw’ul Fataawaa (25/231)]

 

Dhehebu hili ndilo lenye nguvu kutokana na yafuatayo:

 

1- Kauli Yake Ta’aalaa:

((وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ ۚوَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا))

((Na wala hakuna dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini isipokuwa katika yale yaliyoyakusudia nyoyo zenu; na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu)). [Al-Ahzaab (33:5)]

 

2- Kauli Yake Ta’aalaa:

((رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا))

((Rabb wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea)). [Al-Baqarah (2:286)]

Na Allaah –kama ilivyo kwenye Hadiyth Akasema- : “Na’am”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (135)]

 

3- Hadiyth ya Asmaa bint Abiy Bakr aliyesema: ((Tulikula enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) siku ambayo mawingu yalitanda, kisha jua likachomoza. Hishaam (msimulizi toka kwa mama yake Faatwimah toka kwa Asmaa) akaulizwa: Wakaamuriwa kulipa? Akasema: Ni lazima kulipa. Na Mu’ammar akasema: “Nimemsikia Hishaam akisema: Sijui kama walilipa au la)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1959)]

 

 

Hadiyth hii ya Asmaa haionyeshi uthibitisho wala ukanushi wa kulipa. Ama maneno ya Hishaam, hayo kayasema kwa rai yake. Hilo linadokezwa na swali aliloulizwa na Mu’ammar.

 

Kwa picha hii, tunapata kufahamu kuwa hawakuamuriwa kulipa, na kama wangewajibikiwa kulipa, basi hilo lingehifadhiwa. Na kwa kuwa halikuhifadhiwa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), jukumu la dhima linakuwa halipo, na kulipa hakuna.

 

4- Kauli Yake Ta’aalaa:

((وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ))

((Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe (mapambazuko) wa Alfajiri kutokana na uzi mweusi (wa kiza cha usiku)). [Al-Baqarah (2:187)]

 

Kuanza Swawm hapa kumefungamanishwa na kudhihiri wazi Alfajiri na si tu kuchomoza.

 

5- Asiyejua jambo husamehewa. Katika Hadiyth ya ‘Uday toka kwa Haatim amesema: ((Ilipoteremka (حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ) nilichukua kamba nyeusi na kamba [iqaal] nyeupe, nikaziweka chini ya mto. Nikaanza kulitaamuli giza, na sikuweza kuona chochote. Nikarauka mapema kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na nikamweleza hilo [akacheka], akasema:

((إنما ذلك سواد الليل والنهار))

((Hakika hilo ni weusi wa usiku na [weupe wa] mchana)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4509) na Muslim (1090)]

 

 

Rasuli hakumwamuru kulipa kwa kuwa hajui, na hakukusudia kukaidi Amri ya Allaah na Rasuli Wake, bali yeye aliona kuwa hiyo ndiyo Hukmu ya Allaah na Rasuli Wake, na hivyo akasamehewa. [Sharhu Al-Mumti’i (6/403)]

 

Kauli hii ndiyo yenye nguvu kwa kuwa inawafikiana sambamba na dalili. Lakini yafuatayo ni lazima yachungwe:

 

1- Mwenye kufungua kabla jua halijazama, kisha ikambainikia kuwa bado halijazama, basi ni lazima aendelee kujizuia, kwa kuwa amefungua kwa msingi wa kuwepo sababu, kisha akagundua kuwa haipo.

 

2- Akila huku ana shaka ya kuchomoza Alfajiri, basi Swawm yake ni sahihi, kwa kuwa asili ni kuendelea usiku mpaka Alfajiri idhihiri kihakika au dhana yake itopee. Na akila huku ana shaka ya kuchwa jua, basi Swawm yake ni baatwil, kwa kuwa asili ni kubakia mchana. Hivyo haijuzu kula pamoja na shaka, na ni lazima alipe madhali hakujua kuwa amekula baada ya kuchwa jua. Akijua amekula baada ya kuchwa jua, basi hakuna kulipa hapo. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Kula na kunywa kwa makusudi kunawajibisha kulipa tu

 

[Sharhu Fat-hil Qadiyr (2/70), Al-Mudawwanah (1/219), Al-Majmuw’u (6/329), Al-Mughniy (3/130) na vAl-Muhallaa (1/185)]

 

Yamesemwa haya na Ash-Shaafi’iy, Ahmad –kwa iliyo mashuhuri kwake-, Ahlu Adh-Dhwaahir na ‘Ulamaa wengi. Na hii ni kutokana na kutokuwepo Aayah au Hadiyth yenye kuwajibisha kafara isipokuwa katika jimai tu kama itakavyokuja mbeleni. Kafara ni kwa jimai tu na haivuki zaidi ya hapo kwenda kwenye mengineyo, kwa kuwa jimai ni ukiukaji mbaya wa utukufu wa Mwezi, na mtu anaweza kujikaza asiikaribie hadi usiku kinyume na alivyozoea katika kula na kunywa, na kwa kuwa pia haja ya kuikataza ni kubwa zaidi na hukmu ya kuikiuka ni ya usisitizo zaidi.

 

Lakini Maalik, Abu Haniyfah, Is-Haaq na baadhi wengineo, wanasema kuwa kula na kunywa kwa makusudi kunawajibisha kulipa na kutoa kafara, kwa kuwa kipimo chao ni kimoja na jimai, na vyote vinashirikiana katika kukiuka utukufu wa Swawm.

 

Kauli ya kwanza ndio sahihi zaidi kwa kuwa hakuna dalili thabiti, na asli ni kuwa kafara hazifanyiwi kipimo. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

3- Kujitapisha kwa makusudi

 

Ikiwa matapishi yatamshinda yakatoka yenyewe, basi halipi wala hatoi kafara bila makhitalifiano yoyote. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((من ذرعه القيء فليس عليه قضاء، ومن استقاء عمدا فليقض))

((Aliyelemewa na matapishi basi halipi, na aliyejitapisha kwa makusudi basi alipe)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd 2380), At-Tirmidhiy (716), Ibn Maajah (1676), Ahmad (2/468) na wengineo. Al-Bukhaariy na Ahmad wameitia kasoro kama ilivyo katika Naswbur Raayah (2/448). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Al-Irwaa (923) na Swahiyh Al-Jaami’i (6243)]

 

4, 5- Hedhi na nifasi

 

Mwanamke akipata hedhi au nifasi ijapokuwa katika dakika za mwisho za mchana, basi Swawm yake itatenguka, na ni lazima ailipe siku hii kwa ‘Ijma’a ya ‘Ulamaa.

 

6- Kujichua (kupiga punyeto) kwa kukusudia

 

 

Ni kufanya kusudi kuyatoa manii kwa njia isiyo ya jimai kama kuyatoa kwa kuichezea dhakari kimahaba kwa mkono au kujigusisha gusisha au mfano wa hayo kwa lengo la kuyatoa kwa ashiki. Na ikiwa manii yatamtoka kwa kufanya hayo kimakusudi huku anakumbuka kuwa amefunga, basi Swawm yake itabatilika na ni lazima ailipe kwa mujibu wa Jumhuri ya ‘Ulamaa. [Ad-Durar Al Mukhtaar (2/104), Al-Qawaaniynu Al-Fiqhiyyah (81), Rawdhwat At-Twaalibiyna (2/361), Al-Ummu (2/86), Al-Mughniy (3/48) na Kash-Shaaful Qinaa (2/352)]

 

Lakini Ibn Hazm anaona kuwa ikiwa atajitoa manii –bila kujamii-, basi Swawm yake haiharibiki hata kama amefanya makusudi. Amesema: “Haikuja kwa hilo matini yoyote wala Ijma’a wala kauli ya Swahaba wala Qiyaas”. [Al-Muhallaa (6/203-205]

 

Ninasema: “Madhehebu ya Jumhuri ndiyo yenye uzito zaidi. Yanatolewa dalili kwa Kauli Yake Ta’aalaa katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy kuhusiana na mfungaji:

 

((يدع طعامه وشرابه وشهوته من أجلي))

((Anaacha chakula chake, kinywaji chake na matamanio yake kwa ajili Yangu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1984) na Muslim (1151) toka kwa Abu Hurayrah)]

 

Na kujitoa manii ni matamanio, na pia kutoka manii yenyewe. Na linalothibitisha kuwa manii huitwa matamanio ni kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((وفي بضع أحدكم صدقة))

((Na katika kumwingilia mmoja wenu mke wake ni swadaqah)). Wakasema: Ee Rasuli wa Allaah! Mmoja wetu anafanya matamanio yake na anapata ajri? Akasema:

 

((أرأيتم لو وضعها في الحرام))

((Nielezeni, lau angeyaweka katika haramu [si angepata dhambi?])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1006) toka kwa Abu Hurayrah]

 

Kile kinachowekwa ni manii, na yeye ameyaita matamanio (shahwah).

Ama kama atafikiria, au akaangalia akamwaga, na wala hakukusudia kwa kufikiria huko au kumwangalia mwanamke na mfano wa hivyo kumwaga manii, basi Swawm yake haiharibiki.

 

 

7- Niya ya kuvunja Swawm

 

[Al-Muhallaa 6/175), Al-Majmuw’u (6/314), Al-Mughniy (3/35) na Al-Mabsuwtw 3/87)]

 

Ikiwa atanuwiya kuvunja Swawm yake (na yeye amefunga), na akaazimia kwa kukata shauri kufungua kwa makusudi na huku anakumbuka kuwa yuko katika Swawm, basi Swawm yake itaharibika hata kama hakula au hajanywa kwa kuwa kila mtu ni kwa lile alilolinuwiya ((لكل امرئ ما نوى)) . Na kwa kuwa kuingia katika Swawm hakuhitajii kitendo isipokuwa niya ya Swawm, na hivyo hivyo kutoka hakuhitajii kitendo isipokuwa niya. Na kwa vile niya ni sharti ya kutekeleza Swawm, na yeye ameibadili kwa kinyume chake, na bila sharti, ‘ibaadah haitekelezeki.

 

Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Dhwaahir, Ahmad, Abu Thawr, Adh-Dhwaahiriyyah na Asw-haab Ar-Raay, isipokuwa Asw-haab Ar-Raay wamesema ikiwa atarudi akanuwia kabla ya kufika nusu ya mchana, basi kutamtosheleza kwa mujibu wa asili yao ya kufaa kutia niya mchana.

 

8- Kuritadi

 

[Al-Mughniy (3/25) na Kash-Shaaful Qinaa (2/309)]

 

Hatujui baina ya ‘Ulamaa mvutano wowote kuwa mwenye kuritadi wakati wa Swawm, basi Swawm yake inabatilika, na atalazimika kuilipa kama atarudi tena katika Uislamu, ni sawasawa alirudi siku hiyo hiyo au baada ya kumalizika. Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

((لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ))

((Ukifanya shirki bila shaka zitaporomoka ‘amali zako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika)). [Az-Zumar (39:65)]

 

Na kwa kuwa Swawm ni ‘ibaadah ambayo sharti yake ni niya, hivyo kuritadi kunaiharibu.

 

(b) Yenye Kubatilisha Swiyaam Na Kuwajibisha Kulipa Na Kafara

 

Ni jimai peke yake na si jingine zaidi. Toka kwa Abu Hurayrah amesema: ((Tulipokuwa tumekaa mbele ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), mara ghafla alimjia mtu na kumwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Nimeangamia. Akamwambia: Una nini? Akasema: Nimemwingilia mke wangu na mimi nimefunga. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamuuliza: Je, una mtumwa umwache huru? Akasema hapana. Akamuuliza: Basi je unaweza kufunga miezi miwili mfululizo? Akasema hapana. Akamuuliza: Je unaweza kuwalisha masikini sitini? Akasema hapana. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa salaam) akanyamaza. Na wakati sisi tuko katika hali hiyo, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliletewa tenga lenye tende kavu. Akauliza: Yuko wapi muulizaji? Akasema: Mimi hapa. Akamwambia: Chukua hizi uzitoe swadaqah. Mtu yule akasema: Kwa walio mafukara zaidi kuliko mimi ee Rasuli wa Allaah? Naapa wal Laah! Kati ya pande mbili za Madiynah, hakuna watu wenye nyumba iliyo masikini zaidi kuliko watu wa nyumba yangu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akacheka mpaka chonge zake zikaonekana, kisha akamwambia: Basi walishe watu wako)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1936) na Muslim (1111)]

 

Jumhuri ya ‘Ulamaa wanaona kuwa kujamii mfungaji katika mchana wa Ramadhwaan kwa makusudi na kwa khiyari kwa kukutana tupu mbili na kukizamisha kichwa cha dhakari katika moja ya njia mbili (mbele au nyuma kuliko haramishwa), kunafunguza, na ni lazima kuilipa siku na kutoa kafara, ni sawa amemwaga manii au hakumwaga.

 

Ninasema (Abu Maalik): “Kigezo cha Jumhuri katika kuwajibisha kulipa kwa mwenye kujimai katika Mwezi wa Ramadhwaan, ni ziada iliyokuja katika baadhi ya Asaaniyd za Hadiyth hii, nayo ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam alisema mwishoni:

((وصم يوما مكانه))

((Na funga siku moja mahala pake)), nayo ni ziada dhwa’iyf haithibiti. [Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyotangulia imesimuliwa kupitia Az-Zuhriy toka kwa Humayd bin ‘Abdul Rahmaan toka kwa Abu Hurayrah bila kutaja kulipa]

 

Na kwa ajili hiyo, Ibn Hazm –Rahimahul Laah- anaona kuwa ni waajib kwake kutoa kafara tu bila kulipa. Na hili lina nguvu na mwelekeo sahihi zaidi, na linaendana na yaliyozungumziwa nyuma kuhusiana na kulipa Swalaah, na yatakayokuja kuzungumziwa kuhusiana na kulipa Swiyaam- ya kuwa hakuna usharia wa kulipa kwa mtu aliyeacha ‘ibaadah –bila ya udhuru- isipokuwa kwa dalili mpya. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Je, ni waajib kafara kwa mwanamke kama ilivyo kwa mwanaume?

 

Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyotangulia ni kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwamuru mwanaume kafara, na akanyamaza kuhusu mwanamke. Na kwa hili, ‘Ulamaa wamekhitalifiana kwa kauli kadhaa kuhusu mwanamke aliyeingiliwa na mumewe; je atoe kafara au asitoe?

 

Ya kwanza: Si waajib kwa mwanamke kutoa kafara yoyote. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, na kauli ya Ahmad isemayo kuwa kafara moja inawatosheleza wote wawili, na ni waajib kwa mwanamume tu pasina mwanamke. Na hii ni kwa yafuatayo:

 

1- Ni kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakumwamuru mwanamke kutoa kafara pamoja na kuwa mumewe amemjimai, na tendo limefanyika kutokana na wote wawili pamoja, yeye na mumewe. Hii inadulisha kuwa lau Rasuli angeliona kuwa ni lazima kafara juu yake, basi angemlazimisha, na wala asingelinyamazia hilo.

 

2- Hiyo ni haki ya mali iliyohusishwa na jimai, hivyo imehusishwa na mwanamume tu kama mahari.

 

Ya pili: Ni waajib kafara kwa mwanamke kama ilivyo kwa mwanamume. Ni kauli ya Jumhuri; Abu Haniyfah, Maalik, na kauli ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad katika moja ya riwaya mbili swahiyh toka kwake. Kuna makhitalifiano na changanuzi kati yao kuhusu mwanamke muungwana, kijakazi, mwanamke aliyeridhia tendo  na aliyelazimishwa. Wamesema:

 

1- Kwa sababu mwanamke amevunja hadhi ya Swawm ya Ramadhwaan kwa jimai, hivyo ni lazima naye atoe kafara kama mwanamume. Na sharia haikubagua usawa kati ya watu katika ahkaam isipokuwa katika maeneo maalum yaliyoainishwa na dalili. Na kama itamlazimu kulipa kwa kuwa amevunja Swawm kwa jimai ya kukusudia kama ilivyo wajibu kwa mwanamume, basi ni wajibu kwake vile vile kafara sawa na mwanamume kutokana na sababu hii.

 

2- Ama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kutomwamuru mwanamke kutoa kafara, hapa tukio linazingatiwa kuwa ni hali maalum na si hali ya wote. Inawezekana mwanamke (wa Swahaba yule) alikuwa hajafunga kwa udhuru wa maradhi au safari, au alikuwa amelazimishwa, au amesahau kuwa kafunga, au mfano wa hivyo.

 

3- Mwanamke hakumuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hukmu ya hilo kama alivyouliza mumewe, na mume kukiri alilolifanya mkewe hakumwajibishii hukmu madhali hakukiri.

 

4- Inawezekana kuwa sababu ya Rasuli kunyamazia hukmu ya mwanamke ni maneno aliyoyafahamu ya mumewe kuwa mkewe hana uwezo wa chochote.

 

Ya tatu: Inawatosha wote wawili kafara moja isipokuwa kama kafara itakuwa ni kwa kufunga, hapo itawabidi wote wawili wafunge. Haya ni madhehebu ya Al-Awzaa’iy.

 

Ninasema: “Madhehebu ya Jumhuri ndiyo yenye nguvu zaidi, na kauli ya Ash-Shaafi’iy haiko mbali pia. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

Angalizo

 

Mwanamke akilazimishwa, au akisahau, au akiwa hajui, basi halipi wala hatoi kafara kwa mujibu wa kauli swahiyh. Pia mwanamume akisahau au akiwa hajui. Haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Mughniy (3/27) chapa ya Ihyaau At-Turaath Al-‘Arabiy]

 

Je, ni lazima kafara iwe kwa mpangilio?

 

Jumhuri wanasema kuwa ni lazima kafara iwe kwa mpangilio. Asihamie kufunga miezi miwili isipokuwa baada ya kushindwa kumwacha huru mtumwa, na asihamie kuwalisha masikini sitini ila baada ya kushindwa kufunga kwa mujibu wa inavyoonyesha Hadiyth iliyotangulia ya Abu Hurayrah. [Al-Mughniy (3/344), Bidaayatul Mujtahid (1/451) na Fat-hul Baariy (4/198)]

 

Lakini Maalik anasema kuwa mtu hukhiyarishwa kutokana na riwaya ya Muslim kuhusiana na Hadiyth toka kwa Abu Hurayrah: ((Kwamba mtu mmoja alifungua katika Ramadhwaan, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwamuru atoe kafara kwa kumwacha huru mtumwa, au afunge miezi miwili mfululizo, au alishe masikini sitini)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1111)]

 

Wamesema: “Hailazimu mpangilio kutokana na riwaya ya Al-Bukhaariy kwa Hadiyth, kwani mfano wa swali kama hili linaweza kutumika kwa jambo la kukhiyarishwa. Hivyo inachukulika Rasuli kumwelekeza Swahaba huyo kumwacha huru mtumwa kuwa hilo anaweza kulitekeleza kulipia kafara yake [pengine alikuwa anamiliki watumwa wengi]. Wengine wameuchukulia mpangilio kama ni wa kupewa kipaumbele, na kuchaguzwa mtu  lipi la kutoa fidia kama suala linalojuzu”.

 

Ama Jumhuri, wao wamepita mkondo wa kughilibisha (tarjiyh),  wakatilia nguvu riwaya ya mpangilio kuliko riwaya ya kuchaguzwa wakisisitiza kuwa waliosimulia Hadiyth ya mpangilio ni wengi zaidi na Asaaniyd zao zinakutana zote kwa Imamu (msimulizi) mmoja, na pia msimulizi wa Hadiyth ya kuchaguzwa amecheza na maneno ya Hadiyth. Hivyo mpangilio ni salama na akiba zaidi na unatosheleza. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Je, kafara hutolewa kwa idadi ya jimai?

 

[Bidaayatul Mujtahid (1/453), Al-Mughniy (3/341) na Al-Majmuw’u (6/370)]

 

1- Mwenye kujimai mchana wa Ramadhwaan kisha akatoa kafara, halafu akajimai siku nyingine,  basi ni lazima atoe kafara nyingine kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa.

 

2- Mwenye kujimai katika siku moja mara kadhaa, basi hawajibikiwi isipokuwa na kafara moja tu kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa.

 

 

3- Mwenye kujimai katika mchana wa Ramadhwaan na hakutoa kafara, kisha akajimai siku nyingine, hapa kuna kauli mbili:

 

Ya kwanza: Ataitolea kafara kila siku, kwa kuwa kila siku ni ‘ibaadah kando, na kafara ikilazimu kwa kuiharibu Swawm moja, basi kafara haziingiliani. Ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na Al-Jamaa’ah.

 

Ya pili: Atatoa kafara moja tu madhali bado hajaitolea kafara jimai ya kwanza. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Maswahibu zake, Al-Awzaa’iy na Az-Zuhriy kwa kulinganishia na adhabu ya kisharia (hadd).

 

Kauli ya kwanza ina nguvu zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

Share