11-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Mambo Ambayo Hayabatilishi Swiyaam
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swiyaam
11-Mambo Ambayo Hayabatilishi Swiyaam
1- Kuamka na janaba siku ya Swiyaam
Aliyelala –naye amefunga- kisha akaota, Swawm yake haiharibiki, bali ataendelea nayo kwa Ijma’a. [Raddu Al-Muhtaar (2/98) na Al-Qawaaniyn Al-Fiqhiyyah (81)]
Vile vile, aliyepata janaba usiku kisha akaamka na janaba yake asubuhi, Swawm yake ni sahihi na wala hatolipa kwa mujibu wa Jumhuri. Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah na Ummu Salamah: ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anaingiliwa na Alfajiri na yeye ana janaba kutokana na wakeze, kisha anaoga na kufunga)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1926) na Muslim (1109)]
2- Kumbusu mke na kugusana naye ngozi kwa ngozi kama atadhamini kuwa hawezi kumwaga manii
Toka kwa ‘Aaishah amesema: ((Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akibusu na kukumbatia naye amefunga, na alikuwa mwenye kudhibiti zaidi matamanio yake kuliko yeyote kati yenu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1927) na Muslim (1106)]
Pia amesema ‘Aaishah: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa ananibusu, yeye amefunga, na mimi nimefunga)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2384) na ‘Abdul Razzaaq)]
Ibn Hazm amesema (6/208): “Wakati alipokufa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), ‘Aaaishah alikuwa binti wa miaka 18. Kwa hilo, imebatilika kauli ya aliyetofautisha katika hilo kati ya mzee na kijana (kuwa mzee inafaa na kijana haifai), na kauli ya aliyesema kuwa busu ni makruhu wakati ambapo kisahihi, busu ni jambo zuri, lililo stahabiwa, ni Sunnah katika Sunan na kurubisho la mtu kwa Allaah Ta’aalaa kwa kumfuata Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)”.
Ninasema: “Na wala haisemwi kuwa kujuzu kubusu kwa mfungaji ni mahususi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kutokana na haya yafuatayo:
1- Toka kwa ‘Umar bin Abiy Salamah kuwa alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam): Je, mfungaji anapiga busu? Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwambia: Muulize huyu (akimnyooshea) Ummu Salamah. Akamweleza kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anafanya hilo. Akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Umeshasamehewa dhambi zako zilizopita na zijazo. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwambia:
((أما والله إتي لأتقاكم لله وأخشاكم له))
((Ama wal Laah. Hakika mimi ndio mchaji zaidi wenu kwa Allaah na mwenye kumwogopa zaidi wenu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1108). Angalia Sharhu An-Nawawiy]
2- Toka kwa Jaabir kuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: ((Nilijawa na furaha na hamu siku moja, nikakisi na mimi nimefunga. Nikamjia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) nikamwambia: Hakika nimefanya jambo kubwa sana leo. Akauliza: Ni lipi? Nikasema: Nimebusu na mimi nimefunga. Akasema: Unasemaje lau umesukutua kwa maji? Nikasema: Hivyo haina ubaya. Akasema: Kwa lipi?)). [Hadiyth Swahiyh Lighayrih. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2382), Ahmad (1/53), ‘Iyd bin Humayd katika Al-Muntakhab (21), nayo ni Swahiyh Lighayrihii kama alivyosema Sheikh wetu Allaah Amhifadhi]
المباشرة ni kugusana ngozi ya mwanamume na mwanamke bila kufikia maeneo ya kujimai kama kubusu. Toka kwa Masruwk amesema: ((Nilimuuliza ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa: Ni lipi linaruhusiwa kwa mwanamume aliyefunga kwa mkewe? Akasema: Kila kitu isipokuwa jimai)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq (8439)]
Na toka kwa ‘Amri bin Sharhabiyl: ((Kwamba Ibn Mas’uwd alikuwa akimchezea mkewe katikati ya mchana naye amefunga)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq (8442) na Ibn Abiy Shaybah (3/63)]
Na toka kwa ‘Ikrimah amesema: ((Sa’ad bin Maalik aliisugua tupu yake (mkewe) kwa mkono wake na yeye amefunga)). [Swahiyh Lighayrihii. Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq (8444), na ina Hadiyth mwenza kwa Ibn Abiy Shaybah (3/63)]
Ninasema: “Lililo sahihi ni kuwa si makruhu kupiga busu au kugusa. Ikiwa atapiga busu au akagusa madhii yakamtoka yeye au mkewe, basi hakuna kitu juu yao. Lakini ikiwa yeye anajijua kuwa atamwaga manii kwa kufanya hivyo, basi haitojuzu kufanya. Na kama atafanya akamwaga manii yeye au mkewe, basi aliyemwaga kati yao ndiye ambaye Swawm yake itabatilika, na ni lazima ailipe. [Al-Majmuw’u (6/323). Angalia Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/361)]
3- Kuoga na kujimwagia maji kichwani ili kujipooza na joto
Ni kwa yaliyotangulia nyuma kidogo ((kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa Alfajiri inamwingilia na yeye ana janaba kutokana na wakeze, kisha huoga na kufunga)).
Baadhi ya Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘al;ayhi wa aalihii wa sallam) wamesema: ((Hakika nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) huko Al-‘Arj anamimina maji juu ya kichwa chake naye amefunga kutokana na kiu au kutokana na joto)). [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2348)]
4- Kusukutua na kupaliza bila kupandisha sana maji
Toka kwa Laqiytw bin Swabrah amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((وبالغ في الاستنشاق إلا أن تكون صائما))
((Na yavute sana maji juu katika kupaliza isipokuwa kama umefunga)). [Hadiyht Swahiyh. Tumeitaja katika mlango wa twahara]
Hakuna ubaya kwa mfungaji kusukutua hata kama si katika wudhuu au ghusl, na wala unyevu wa maji unaobakia kinywani baada ya kusukutua hauharibu Swawm akiumeza pamoja na mate, kwa kuwa haiwezekani kujikinga nao. [Raddu Al-Muhtaar (2/98)]
Na ikiwa atasukutua au akapaliza maji puani na maji yakamponyoka yakafika kooni bila kukusudia wala kuzembea, basi haina neno kwake kwa mujibu wa kauli mbili swahiyh za ‘Ulamaa. Hili limesemwa na Al-Awzaa’iy, Is-Haaq na Ash-Shaafi’iy katika moja ya kauli zake mbili kinyume na kauli ya Abu Haniyfah na Maalik kuwa hilo linafunguza.
5- Kuonja chakula kwa haja mradi tu kisifike ndani
Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: ((Hakuna ubaya kuonja siki au kitu maadamu hakikuingia kwenye koo yake na yeye amefunga)). [Hasan Lighayrihi. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (3/47). Ina Hadiyth mwenza kwa Al-Bukhaariy (4/153) ikiwa Mu’allaq na Al-Bayhaqiy (4/261)]
Sheikh wa Uislamu amesema: “..na kuonja chakula ni makruhu bila haja lakini hakufunguzi. Ama kwa haja, basi ni kama kusukutua”. [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/266). Angalia Al-Mabsuwtw (3/93)]
Na inaingia kwenye maana ya kuonja, kutafuna chakula kwa haja. Toka kwa Yuwnus toka kwa Al-Hasan amesema: “Nilimwona akimtafunia mtoto chakula –na yeye amefunga- anakitafuna kisha anakitoa toka kinywani mwake na kukiweka mdomoni mwa mtoto”. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdur Razzaaq (7512). Ina mwenza kwa Ibn Abiy Shaybah (3/47)]
Faida
Ni makruhu kwa mfungaji kutafuna ubani mkali kama hautotoa utomvu wowote wa kuingia ndani na haukuwa na ladha inayosikika kooni, kwa kuwa ubani hukausha koo na kuleta kiu. Na kama unatoa utomvu unaoingia hadi kooni, basi unafunguza kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri. [Al-Mughniy (3/109), Al-Majmuw’u (6/353) na Fat-hul Baariy (4/160)]
6- Kuumika (الحجامة) na kuchangia damu kwa asiyechelea kudhoofu mwili
"الحجامة" kuumika, ni kufyonza damu kwa kikombe kidogo baada ya kuchanja ngozi. Ufyonzaji huu unaweza kuwa mkavu bila damu. [Kamusi ya Al-Wajiyz]
Imepokelewa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa Asaaniyd tofauti kuwa amesema:
((أفطر الحاجم والمحجوم))
((Amefungua muumikaji na muumikwa)). [Swahiyh kwa Asaaniyd zake. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (774), Abu Daawuwd (2367) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (931)]
Na imethibiti toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) ya kuwa:
((أن النبي صلى الله عليه وسلم احتجم وهو صائم))
((Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliumika na yeye amefunga)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1939), Abu Daawuuwd (2372) na At-Tirmidhiy (776)]
Lakini madhehebu ya Ahmad, Ibn Siyriyn, ‘Atwaa, Al-Awzaa’iy, Is-Haaq, Ibn Al-Mundhir na Ibn Khuzaymah na ambayo yamekhitariwa na Ibn Taymiyah, yanasema mwenye kuumikwa hufungua kwa kufanyiwa hijaamah. Ni kauli pia ya ‘Aliy, Abu Hurayrah na ‘Aaishah. Hoja ya madhehebu haya ni:
[Al-Inswaaf (3/302), Al-Furuw’u (3/48), na Majmuw’u Al-Fataawaa (25/255)]
1- Hadiyth:
((أفطر الحاجم والمحجوم))
((Amefungua muumikaji na mwenye kuumikwa)).
2- Imaam Ahmad amesema kuwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyotangulia ni Dhwa’iyf, nayo ipo kwa Al-Bukhaariy?!
3- Wamesema: Hata tukisema kuwa ni Swahiyh, lakini hata hivyo ni Mansuwkh.
Ibn Taymiyah ameongeza –toka kwa ‘Ulamaa wa Hanbal- kuwa muumikaji hufungua vile vile kama ataifyonza chupa.
Ama Jumhuri; Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy na wengineo, wao wanasema kuwa kuumika hakumfunguzi muumikaji wala mwenye kuumikwa. Haya yamesemwa pia na Ibn Mas’uwd, Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas, Anas, Abu Sa’iyd Al-Khudriyy na kundi la Masalaf. Hoja zao ni: [Al-Mabsuwtw (3/56), Al-Qawaaniyn Al-Fiqhiyyah (105), Al-Majmuw’u (6/349) na Fat-hul Baariy (4/209)
1- Kuwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas imethibiti na ni Swahiyh. Wamejibu madai ya Imaam Ahmad anayesema kuwa ni Dhwa’iyf kwa kutumia kauli ya Muhannaa aliyesema: “Nilimuuliza Ahmad kuhusu Hadiyth hii akasema kuwa hakuna ndani yake neno ((صائم)) mfungaji, bali lililopo ni ((محرم)) aliyehirimia, kisha akaziweka bayana Asaaniyd zake toka kwa Ibn ‘Abbaas lakini hakuna ndani yake Sanad ya Ayuuwb iliyoko kwa Al-Bukhaariy”.
Al-Haafidh amesema: “Hadiyth ni Swahiyh, haina shaka kabisa”.
2- Wamesema: Hadiyth ya ((أفطر الحاجم والمحجوم)) ((Amefungua muumikaji na mwenye kuumikwa)), ni Mansuwkh, na An-Nawawiy amezungumza sana kuhusu hilo. Kauli hii wameisema akina Ash-Shaafi’iy, Al-Bayhaqiy, Ibn ‘Abdul Barri na wengineo.
3- Wamesema Hadiyth ((أفطر الحاجم والمحجوم)) ni Dhwa’iyf.
Ninasema: “Uhakika ni kuwa hakuna uthibitisho wa madai ya kuwepo naskh toka kwa makundi mawili na hususan hilo likiambatana na kutojua historia. Kisha Hadiyth mbili ni Swahiyh, na hakuna yoyote iliyokosolewa kati yao. Na hizi hapa njia mbili ambazo ni lazima kuishilia kwenye moja kati yao:
(a) Ima isemwe kuwa kufungua muumikaji na mwenye kuumikwa kumenasikhiwa na Hadiyth nyingine, nayo ni Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: ((Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam ameruhusu kuumika kwa mfungaji)). [Swahiyh Lighayrih. Imekharijiwa na An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (3241), Ad-Daaraqutwniy (2/182) na Al-Bayhaqiy (4/264). Angalia Al-Irwaa (4/74)]
Ibn Hazm (6/204) amesema: “Isnaad yake ni Swahiyh, hivyo ni wajibu kuitumia, kwa kuwa ruksa inakuwa baada ya kuazimia. Hivyo imedulisha kuwa kubatwilika Swiyaam kwa kuumika kumenasikhiwa sawasawa kwa muumikaji au mwenye kuumikwa.
(b) Au isemwe kuwa katazo la kuumika kwa mfungaji si la kuharamisha, hivyo Hadiyth ya ((Amefunga muumikaji na mwenye kuumikwa)) itachukuliwa kimajazi, kwa maana kuwa kitendo chao kitapelekea kufungua. Hili linatiliwa nguvu na Hadiyth iliyosimuliwa na ‘Abdul Rahmaan bin Abiy Laylaa toka kwa mtu mmoja katika Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuwa Rasuli wa Allaah: ((Amekataza kuumika na kuendelea na Swiyaam bila kufungua- lakini hakuyaharamisha mawili haya- kwa ajili ya kulinda afya za Swahaba Wake..))”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2374) na ‘Abdur Razzaaq (7535). Swahaba kutojua jambo hakudhuru].
Hivyo inaduilisha kuwa yeye alilichukia hilo kwa yule ambaye alikuwa anadhoofika kwa kufanya hayo. Linatiliwa nguvu na Hadiyth iliyothibiti ya kuwa yeye alimwambia Anas bin Maalik: ((Je mlikuwa mnaifanya hijaamah makruhu kwa mfungaji enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam? Akasema hapana, isipokuwa kutokana na kudhoofu mwili)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1940)]
Ninasema: “Na hili ndilo bora zaidi kukubalika, na hivyo madhehebu ya Jumhuri yanakuwa na nguvu zaidi ya kuwa hijaamah haitengui Swawm, lakini inakuwa makruhu kuifanya kwa mtu ambaye inamdhoofisha, na inakuwa ni haramu ikiwa udhoofu huo utakuwa sababu ya mtu kufungua. Na kutoa damu ni sawa na kufanya hijaamah, na yaliyosemwa kuhusu hijaamah ndiyo hayo hayo kuhusu kutoa damu. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.
7-10 – Kutia wanja, kupigwa bomba mapitio ya haja kubwa (mkunduni), kutia matone ya dawa puani na kunusa manukato
[Madhehebu ya Hanafiy, Shaafi’iy na baadhi ya Maalik, yanasema kuwa wanja haufunguzi sawasawa mtu akihisi ladha yake kooni au la. Na hili limesimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar, Anas na Ibn Ubayya Awfaa. Lakini madhehebu ya Maalik na Ahmad yanasema kuwa wanja unabatwilisha Swawm ukifika kooni. Angalia Al-Bidaayah (1/126), Al-Majmuw’u (6/348), Al-Qawaaniyn Al-Fiqhiyyah (104) na Al-Inswaaf (3/299)]
[Jumhuri wanasema kupigwa bomba mkunduni kunafunguza. Lakini Daawuwd, Al-Hasan bin Swaaleh na Maalik, wanasema hakufunguzi. Angalia Al-Hidaayah (1/115), Al-Majmuw’u (6/320), Al-Qawaaniyn (104) na Al-Inswaaf (3/299)]
Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah amesema: “Ama wanja na sindano , na matone ya dawa yananayotiwa kwenye mrija wa mkojo (urethra), na kutibu jeraha kwenye ubongo au jeraha la ndani ya mwili, haya ni katika mambo ambayo ‘Ulamaa wamevutana. Baadhi yao wamesema hakuna chochote katika hayo kinachofunguza, wengine wamesema yote yanafunguza isipokuwa wanja, wengine wamesema yote isipokuwa matone, na wengine wamesema wanja na matone havifunguzi lakini vinginevyo vyote vinafunguza.
Na lililo dhahiri zaidi ni kuwa hakuna chochote katika hayo kinachofunguza Swawm, kwani Swawm ni jambo ambalo anahitaji kulijua kila mtu katika Diyn ya Uislamu. Na lau kama Allaah na Rasuli Wake wameyaharamisha katika Swawm na yanaiharibu, basi ingelikuwa ni waajib kwa Rasuli kuyabainisha. Na kama angelieleza hilo, basi Swahaba wangelijua na wangelifikisha kwa umma kama walivyofikisha sharia nyinginezo. Na kwa vile hakuna yeyote katika ‘Ulamaa aliyenukulu hilo toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) si kwa Hadiyth Swahiyh, wala Dhwa’iyf wala Mursal, inajulikana kuwa hakueleza chochote katika hilo, na Hadiyth iliyozungumzia wanja ni Dhwa’iyf”. [Ni Hadiyth isemayo: ((Ya kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliamuru aletewe ithmud ya miski wakati wa kulala. Akasema: ((Aiepuke mfungaji)), nayo ni Munkar. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2377)]. [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/233-234)]
Na akasema: [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/242)] “Inavyojulikana ni kuwa wanja na mfano wake ni katika vitu ambavyo ni vigumu kuepukana navyo kwa watu wote kama ilivyo kwa mafuta, kuoga, bukhuri na mafuta mazuri. Na kama haya yangekuwa yanafunguza, basi Rasuli angebainisha kama alivyobainisha mengine yanayofunguza kwa kuyafanya. Na kwa kuwa hakubainisha hilo, itajulikana kuwa wanja ni katika aina za manukato, bukhuri na mafuta. Na bukhuri inaweza kupanda hadi puani ikafika kwenye ubongo, na mwili ukazimuka. Na mafuta hufyonzwa na mwili na kuingia ndani yake, na mtu hupata msisimko. Pia mafuta mazuri humfanya ajihisi yuko imara. Na kwa kuwa mfungaji hakukatazwa hayo, inadulisha kuwa anaruhusiwa kujitia manukato, kujifukiza udi, kujipaka mafuta mazuri na kujitia wanja. Baadhi ya Waislamu katika enzi yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) waliwahi kujeruhiwa majeraha ya kwenye ubongo au ya kufika ndani ya mwili katika Jihaad au katika harakati nyingine. Na kama hali hiyo ingekuwa inafunguza, basi Rasuli angebainisha”.
Na akasema (Rahimahu-Allaah) - [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/235). Angalia Al-Muhalla (6/215)] : “Na waliosema kuwa mambo haya yanafunguza, hawana dalili yoyote toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), bali wamelisema hilo kwa kutegemea Qiyaas. La nguvu zaidi walilolitolea hoja ni kauli yake Rasuli:
((وبالغ في الاستنشاق إلا أن تكون صائما))
((Na yavute sana maji juu katika kupaliza isipokuwa kama umefunga))”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa nyuma]
Akaendelea kusema [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/244)]: “Nacho ni Qiyaas dhwa’iyf kwa kuwa anayepaliza maji kwa tundu za pua yake, maji hayo huteremka hadi kwenye koo yake na kisha tumboni. Na kwa hilo, linatokea lile linalotokea kwa mwenye kunywa kwa mdomo wake ambapo kwa kufanya hivyo, maji huupa lishe mwili wake, huondosha kiu na chakula tumboni mwake husagwa kama inavyofanyika kwa kunywa maji. Na lau isingelikuja Hadiyth kuhusu hilo, ingejulikana kuwa hii ni katika namna ya unywaji, kwani hakuna tofauti kati yao isipokuwa katika kuingia maji kupitia mdomoni, na hilo si la kuzingatiwa, bali kuingia maji kwenye kinywa tu hakufunguzi, hili si lenye kufunguza wala si sehemu ya lenye kufunguza kwa kuwa halina athari, bali ni njia kuelekea kwenye lenye kufunguza. Mambo hayako hivyo kwa wanja, bomba la kwenye haja kubwa na kutibiwa ugonjwa wa kwenye ubongo na majeraha ndani ya mwili, kwani wanja hautoi lishe kabisa, na hakuna yeyote anayeingiza wanja ndani ya mwili wake si kwa mdomo wala kwa pua. Pia bomba la mapitio ya haja kubwa halitoi lishe, bali hupakua na kuvitoa vilivyoko mwilini mfano wa kama lau amenusa kitu katika viharishi au akashtuka mshtuko mkubwa uliosababisha mkorogeko mkali wa tumbo, na bomba hili halifiki tumboni. Na dawa inayofika tumboni katika kutibu jeraha la ndani ya mwili au kwenye ubongo haifanani na chakula kinachoingia humo”.
Ibn Taymiyah – (Rahimahu-Allaah) - amezungumza kwa urefu sana katika kutengua Qiyaas hiki, na tunachoweza kufaidika nacho kwa ufupi ni:
- Ni kuwa Hadiyth imethibitisha kuharibika Swawm kwa kula na kunywa lakini mambo haya hayaitwi kula au kunywa wala hayakusudiwi kwayo kula au kunywa. Na kwa msingi huo, sindano ya bomba na sindano kwa aina zake zote hazifunguzi ila tu kama itakuwa ni ya kulishia, hili ni la kutafitiwa.
- Linalopatikana kwa linalopatikana kwa kula na kunywa hujumuishwa nalo.
- Sababu ya kutenguza Swawm kutokana na kula au kunywa inaweza isiwe tu kula, bali inaweza kuwa mchanganyo wa kupata lishe na kuburudika kwa chakula na kinywaji. Linalothibitisha hili ni kuwa mgonjwa ambaye analishwa kwa mpira kwa masiku kadhaa, anakuwa anatamani sana chakula. [Kayaeleza haya Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah)- katika Al-Mumti’u (6/381)]
Basi ikiwa ni hivi, sindano zote hazitengui Swawm hata kama ni za kulishia. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
11- Kupiga mswaki
Kupiga mswaki ni jambo lililosuniwa kisharia –kama ilivyotangulia- na hakuna naswi yoyote inayomzuia mfungaji, bali kuna Hadiyth zilizopokelewa ambazo baadhi yake zinathibitisha uhalali wa kupiga mswaki kwa mfungaji, na nyingine zinamhimiza kufanya hivyo wakati wa Swiyaam, lakini ni Dhwa’iyf hazina mashiko. Na asli ni kuwa mswaki unaruhusiwa, na kama ungekuwa unaharibu Swawm, basi Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) angetueleza hilo na Swahaba wangelinukulu kutokana na ugumu wa kuepukana nao kwa watu wote.
Fuqahaa wote wamekubaliana kuwa inajuzu mfungaji apige mswaki, ijapokuwa ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy na Kihanbali wamependelea kuacha kupiga kwa mfungaji baada ya jua kupinduka ili kuibakisha harufu mbaya ya kinywa ambayo inanukia vizuri zaidi kwa Allaah kuliko harufu ya miski.
Ninasema: “Lililo wazi zaidi ni kuwa hakuna ubaya kupiga mswaki nyakati zote. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.
Je, inajuzu kutumia dawa ya meno (tooth paste) kwa mfungaji?
Kwa mujibu wa yaliyotangulia, inajuzu kutumia mswaki wa brashi na dawa kwa mfungaji kama atahakikisha haipenyi kufika kooni. Ni bora kuitumia usiku na kuacha mchana. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
12- Kumeza kohozi النخامة
"النخامة" Ni kile kinachotoka kupitia tundu mbili za pua wakati wa kujikohoza (kamasi), au kohozi linalopanda toka kifuani. Kohozi haliharibu Swawm kwa mujibu wa Madhehebu ya Hanafiy, Maalik na riwaya toka kwa Ahmad, kwa kuwa umezaji wake ni wa ndani ya kinywa usiohusiana na kinachotoka nje, hivyo ni sawa na mate. [Raddu Al-Muhtaar (2/101), Al-Mughniy (2/43) na Jawaahir Al-Ikliyl (1/149)]
Ama Ash-Shaafi’iy na Hanbal, wao wanasema inafaa kuyameza kama hayakufika kinywani (toka kifuani au kooni), na kama yatafika kinywani mwake akayameza, basi atakuwa amefungua. [Rawdhwat At-Twaalibiyn (2/360) na Kash-Shaaf Al-Qinaa (2/329)]
Ninasema: “Lililo dhahiri zaidi ni kuwa hakuna ubaya kuyameza hata kama yako ndani ya kinywa chake madhali si kwa niya mbaya, au akakusudia kuyala au kuyanywa”.
13- Kuyameza yasiyowezekana kujikinga nayo kama:
(a) Mabaki ya chakula yaliyoganda kwenye meno kama ni kidogo kwa kuwa haiwezekani kuzuia yasichanganyike na mate. Ni sharti asikusudie kuyameza, au akashindwa kuyaengua apate kuyatema. [Radd Al-Muhtaar (2/98), Ar-Rawdhwat (2/359) na Kash-Shaaf Al-Qinaa (2/329)]
(b) Damu kidogo toka kwenye fizi na meno. Lau fizi zake zitatoa damu, na mate yake yakaingia kooni mwake yakiwa yamechanganyika na damu bila kufika tumboni, basi Swawm yake haibatiliki kwa mujibu wa kauli ya Mahanafiy, kwa kuwa hilo haliepukiki isipokuwa damu ikiyazidi mate, hapo itabatilika.
Ama Mashaafi’iy, wao wanasema kuwa Swawm yake itabatilika kwa kumeza mate yaliyochanganyika na damu. Wao wanaizingatia damu kuwa najisi na haifai kuimeza. [Raddu Al-Muhtaar (2/98), Ar-Rawdhwat (2/359) na Kash-Shaaf Al-Qinaa (2/329).
Ninasema: “Lililo dhahiri ni kuwa haifai kufanya kusudi kumeza damu kwa kuwa imeharamishwa. Na ikiwa kuimeza kutamshinda au ikawa vigumu kwake kujizuia asiweze kuimeza au hakujua, basi Swawm yake haibatiliki”.
(c) Vumbi la njiani, unga, poda na mfano wa hayo katika ambavyo haiwezekani kujikinga navyo.
14, 15, 16- Kula, kunywa na kujimai kwa kusahau
17- Kutapika bila kujitapisha
Nyuma kidogo tumezielezea dalili za kutofisidika Swawm kwa mambo haya.