12-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Wasiofunga (Swawm) Na Hukmu Zinazowahusu
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swiyaam
12-Wasiofunga (Swawm) Na Hukmu Zinazowahusu
Wasiofunga katika Mwezi wa Ramadhwaan wako katika makundi matatu: [Bidaayatul Mujtahid (1/438)]
(a) Wanaoruhusiwa kufunga au kutofunga
(b) Wasioruhusiwa kufunga (lazima wale)
(c) Ambao ni lazima wafunge
[a] Kundi La Wanaoruhusiwa Kufunga Au Kutofunga Swawm
1- Mgonjwa
Maradhi ni kila lile linalomtoa mtu toka kwenye mpaka wa afya yake kutokana na hitilafu mwilini. [Al-Miswbaah Al-Muniyr, kidahizo (maradhi)]
‘Ulamaa kwa kauli moja wameruhusu mgonjwa kula kisha alipe anapopona. [Al-Mughniy pamoja na sharh (3/16)]
Na asli ya hili, ni Kauli ya Allaah Ta’aalaa:
((وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ))
Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo [Al-Baqarah (2:185)]
Toka kwa Salamah bin Al-Akwa’a (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: “Ilipoteremka Aayah hii
((وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ))
((Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika watoe fidia; kulisha masikini)). [Al-Baqarah (2:184)]
ilikuwa anayetaka kula hula na hutoa fidia mpaka ilipoteremshwa Aayah inayoifuatia”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4507) na Muslim (1145)]
Yaani Neno Lake Ta’aalaa:
((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ))
Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. [Al-Baqarah: 185]
Mgonjwa ana hali tatu: [Al-Mughniy (3/364) na Al-Muhallaa (6/228)]
1- Awe anaumwa ugonjwa hafifu ambao haumuumizi kwa kufunga na wala kufungua hakumletei afueni. Ni kama mafua mepesi, maumivu ya mbali ya kichwa, maumivu ya gego na mfano wa hayo. Huyu haijuzu kufungua.
2- Ni mwenye ugonjwa unaoshitadi au unaokawia kupona, na Swawm inakuwa nzito kwake lakini haimdhuru. Huyu imesuniwa afungue, ni makruhu kufunga.
3- Swawm kuwa nzito kwake na kumsababishia madhara yanayoweza kupelekea kifo. Huyu ni haramu kimsingi kwake kufunga kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
((وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ))
((Wala msijiue)). [An-Nisaa (4:29)]
Mtu mzima wa afya anayehofia ugonjwa kwa kufunga anaruhusiwa kufungua, kwa kuwa ni sawa na mgonjwa anayehofia kuzidi maradhi yake au Swawm kukawiza kupona. Allaah Ta’aalaa Amesema:
((وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ))
((Wala msijiue)). [An-Nisaa (4:29)]
Na Amesema:
((يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ))
((Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu)). [Al-Baqarah (2:185)]
Pia Kasema:
وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ
Na Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika Dini [Al-Hajj: 78]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((إذا أمرتكم بأمر فائتوا منه مااستطعتم))
((Nikiwaamuruni jambo lolote, basi lifanyeni kiasi muwezavyo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (7288) na Muslim (1337)]
2- Msafiri
Sharia inamruhusu msafiri –wa safari ya kupunguza Swalaah- afungue kwa Kauli Yake Ta’alaa:
((وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ))
Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. [Al-Baqarah (2:185)]
Na kama msafiri atafunga, basi Swawm yake itaswihi. Ni madhehebu ya Swahaba wengi, Taabi’iyna na Maimamu wanne wanaosema kuwa kufunga safarini ni swahiyh na kunatosheleza. Lakini imesimuliwa toka kwa Abu Hurayrah, Ibn ‘Abbaas na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhum) –nayo ni madhehebu ya Ibn Hazm- kuwa Swawm si swahiyh na msafiri ni lazima alipe kama atafunga safarini. Kuna kauli nyingine inayosema kuwa ni makruhu kufunga, lakini madhehebu ya Jumhuri yana nguvu zaidi kama tutakavyokuja kubainisha mbeleni.
Lipi bora kwa msafiri, kufunga au kutofunga Swawm?
‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu hili. Suala hili likifanyiwa uhakiki katika pale ambapo nusuus zinakutania, basi tunaweza kusema:
Msafiri ana hali tatu:
1- Swawm kumwelea ugumu au ikamzuia asiweze kufanya jambo la kheri, hapa kufungua itakuwa ni bora kwake. Hili linapatikana katika Hadiyth ya Jaabir aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa safarini akaona msongamano na mtu amewekewa kivuli akauliza: Ana nini huyu? Wakasema: Amefunga. Akasema:
((ليس من البر الصوم في السفر))
((Si katika wema kufunga safarini)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1946) na Muslim (1115)]
Na Hadiyth ya Anas aliyesema: ((Tulikuwa pamoja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) safarini, baadhi yetu wamefunga na wengine hawakufunga. Tukashukia mahala katika siku ya joto, mwenye kivuli zaidi kati yetu ni mwenye guo, na baadhi yetu wanakinga jua kwa mkono. Anasema: Waliofunga wakaanguka na wasiofunga wakasimama, wakafunga mahema na wakawanywesha wasafiri. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:
((ذهب المفطرون اليوم بالأجر))
((Wasiofunga wameondoka na thawabu leo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1119)]
Na katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriy ni kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwaambia Swahaba wake–walikuwa vitani-
((إنكم مصبحو العدو غدا والفطر أقوى لكم))
((Hakika nyinyi mtawapambaukia maadui kesho, na kufungua kutawapeni nguvu zaidi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1120)]
2- Swawm isimwelee uzito na isimzuie kufanya jambo la kheri, hapa kufunga itakuwa ni bora kwake kutokana na ujumuishi wa Neno Lake Ta’aalaa:
((وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُون))
((Na mkifunga Swiyaam ni bora kwenu mkiwa mnajua)). [Al-Baqarah (2:184)]
Toka kwa Abud Dardaai amesema: ((Tulitoka pamoja na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika baadhi ya safari zake katika siku ya joto kufikia mpaka wa mtu kuweka mkono wake kichwani kutokana na joto kali, na hakuna kati yetu aliyefunga isipokuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na Ibn Rawaahah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1945) na Muslim (1122)]
Na toka kwa ‘Aaishah kwamba Hamzah bin ‘Amri Al-Aslamiy alimuuliza Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam): “Je nifunge safarini?”(Alikuwa mwingi wa kufunga). Akamwambia:
((إن شئت فصم، وإن شئت فأفطر))
((Ukitaka funga, na ukitaka kula)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1943) na Muslim (1121)]
Kwa kuwa Swawm –kama haina uzito- inatakasa haraka zaidi dhima na ni nyepesi zaidi kwa mfungaji na hususan anapofunga na watu kuliko kuja kulipa na watu wengine wanakula.
3- Swawm kumletea uzito mkubwa mno usiostahamilika unaoweza kusababisha kifo, na hapa ni lazima ale na ni haramu kufunga. Ni kama ilivyo katika Hadiyth ya Jaabir: ((Kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitoka mwaka wa ukombozi kuelekea Makkah. Akaenda mpaka akafika Kuraa’al Ghamiym, kisha akaitisha gilasi ya maji, akainyanyua mpaka watu wakaiona, kisha akanywa. Baada ya hapo aliambiwa kuwa baadhi ya watu wamefunga, akasema:
((اولئك العصاة، اولئك العصاة))
((Hao ni waasi, hao ni waasi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1114), na mfano wake kwa Al-Bukhaariy (1948) toka kwa Ibn ‘Abbaas]
Wakati wa kujuzu kufungua Swawm kwa msafiri
Kuna hali kadhaa kuhusiana na wakati wa kujuzu kufungua kwa msafiri:
Ya kwanza:
Aanze safari yake kabla ya alfajiri, au alfajiri imkute akiwa njiani safarini, na anuwie kutofunga. Huyu inajuzu kwake kufungua kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa, kwa kuwa yeye ashapata sifa ya kuwa msafiri wakati wa kuwepo sababu ya uwajibu. [Al-Qawaaniyn Al-Fiqhiyyah cha Ibn Jaziy (82)]
Ya pili:
Aanze safari yake baada ya alfajiri (mchana). Jumhuri ya ‘Ulamaa; (Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Ahmad) wanasema hatoruhusiwa kufungua siku hiyo, kwa kuwa Swawm ni ‘ibaadah ambayo inatofautiana kwa ukazi na safari, na viwili hivi vikichanganyika (ukazi na safari), basi hukmu ya ukazi inakuwa juu, mfano wa Swalaah. [Haashiyat Ibn ‘Aabidiyna (2/431), Al-Qawaaniyn Al-Fiqhiyyah (106) na Al-Majmuw’u (6/261)]
Lakini Ahmad, Is-Haaq na Hasan –nalo ni chaguo la Ibn Taymiyah, nayo ndio rai yenye nguvu katika suala hili- wanasema inajuzu kufungua katika siku hiyo. [Al-Inswaaf 3/289) na Majmuw’u Al-Fataawaa (25/212)]
Na hii ni kwa ujumuisho wa Kauli Yake Ta’aalaa:
((وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ))
Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. [Al-Baqarah (2:185)]
Na kwa Hadiyth ya Jaabir tuliyoitaja nyuma kidogo ya kutoka Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwenda Makkah mwaka wa ukombozi ambayo kipande chake kinasema: ((…akaitisha gilasi ya maji baada ya Al-‘Asr, akanywa na watu wanamwangalia)). [Hadiyth Swahiyh. Imeelezwa nyuma kidogo]
Na mfano wake ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ambayo kipande chake kinasema: ((..kisha akaitisha maji, akayanyanyua kwa mkono wake ili watu wayaone, akafungua mpaka akawasili Makkah, na hiyo ni katika Ramadhwaan…)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1948)]
Madhehebu haya yanatiliwa nguvu vile vile na Hadiyth ya Muhammad bin Ka’ab anayesema: ((Nilimwendea Anas bin Maalik –katika Ramadhwaan- na yeye anajiandaa kwa safari, na ngamia wake ameshaandaliwa. Akavaa nguo za safari, akaitisha chakula akala. Nikamwambia: Ni Sunnah? Akasema: Ni Sunnah, kisha akapanda)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (799), Al-Bayhaqiy (4/247), Ad-Daaraqutwniy (2/187), Adh-dhwiyaa Fil Mukhtaara (2602) na wengineo. Al-‘Allaaamah Al-Albaaniy ana tasnifu katika Twaswhiyh yake, ipitie]
Toka kwa ‘Ubayd bin Jubayr amesema: ((Nilipanda jahazi na baba yangu Baswrah Al-Ghaffaariy toka Fustat wakati wa Ramadhwaan. Jahazi likan’goa nanga na kuanza safari, halafu akatengewa chakula chake akaniambia jongea tule. Nikamwambia: Je, si bado unayaona majumba [ya Fustat]? Akasema: Je, umeachana na Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)?)). [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2412), Ahmad (6/398), Ad-Daaramiy (1713) na Al-Bayhaqiy (4/246). Angalia tasnifu iliyodokezewa kabla yake]
Angalizo
Katika Hadiyth hizi mbili za mwisho kuna dalili kuwa msafiri anatakikana ale kabla hajatoka mji aliopo. Ibn Al-‘Arabiy kasema: “Hadiyth ya Anas ni Swahiyh. Inadokeza kujuzu kula safari inapokuwa tayari”. [Naylul Awtwaar (4/271)]
Lakini Jumhuri ya ‘Ulamaa wamekataza msafiri kula kabla hajaondoka mji wake, kwa kuwa kabla hajaondoka hawi safarini, bali anakuwa ni mwenye kukusudia safari.
Ya tatu:
Anuwie kufunga –naye ni msafiri- kisha akaona bora asifunge, huyu inajuzu kula –kama ataona hilo ni bora kwake- kutokana na dalili zilizotangulia katika hali ya pili. Hili limesemwa na Jumhuri kinyume na Maalik na Hanafiy. [Al-Mughniy (3/19), Al-Majmuw’u (6/260), Al-Qawaaniynul Fiqhiyyah (82) na Radd Al-Muhtaar (2/122)]
Kutenguka ruksa ya kufungua kwa msafiri
Ruksa ya kufungua inatenguka kwa msafiri kwa mambo mawili:
La kwanza: Akinuwia kukaa bila kuainisha muda, au muda wa kukaa kisharia [Muda wa kukaa ambao anaruhusiwa kula kwa kauli ya Maalik na Shaafi’iy ni siku nne, kwa Hanbali zaidi ya siku nne, na kwa Hanafiy siku kumi na tano. Maainisho haya ya siku hayana dalili. Angalia Al-Muhallaa (6/244)]
Toka kwa Ibn ‘Abbaas: ((Kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipigana vita vya ukombozi (wa Makkah) katika Ramadhwaan na akafunga, mpaka alipofika Al-Kadiyd –nayo ni maji yaliyopo kati ya Qudayd na ‘Usfaan- [alifungua]. Aliendelea kula mpaka Mwezi ukamalizika)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4275)]
Ni maarufu kwamba ukombozi ulikuwa ni tarehe 20 Ramadhwaan. Hivyo basi, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alifungua akiwa Makkah siku kumi au siku kumi na moja kwa mujibu wa kutofautiana riwaya. Na hakuna shaka kuwa kufungua kwake katika muda huu, hakukanushi kufungua zaidi ya hapo.
Kiufupi ni kuwa aliyenuwia kukaa katika mji ukazi usiojulikana idadi ya siku zake, huyo atafunga na hatokula. Na kama hakunuwia kukaa bali amekaa ili kufuatilia haja yake bila kuwa na niya ya kukaa na hajui lini haja yake ataimaliza, basi huyo anaweza kula. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
La pili: Akirudi mjini kwake
Akirudi anakoishi usiku, na kesho yake ni Ramadhwaan, basi ni lazima afunge bila makhitalifiano. Ama lau kama amewasili mchana, je atajizuia kula hadi Magharibi? Hapa kuna kauli mbili. Yenye nguvu zaidi ni isemayo kuwa halazimiki kujizuia bali ataendelea kula. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Maalik. Imepokewa kwa njia swahiyh toka kwa Ibn Mas’uwd kwamba amesema: ((Mwenye kula mwanzo wa mchana, basi ale mwisho wake)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (9343)]
Abu Haniyfah na Maswahibu zake wanasema: Atajizuia sehemu iliyobaki ya siku kwa kuchukulia Qiyaas cha mtu aliyekula Siku ya shaka akaja kujua kuwa ni Ramadhwaan. Maneno haya yanahitaji kutafitiwa zaidi, kwa kuwa aliyekula Siku ya shaka, amekula kutokana na kutojua, na msafiri huyu amekula kwa sababu halali. [Bidaayatul Mujtahid (1/441-442)]
Kutokana na hili inazalikana faida nayo ni:
Msafiri ambaye hakufunga akiwasili nyumbani mchana wa Ramadhwaan na akamkuta mkewe ametwaharika na hedhi au nifasi, au amepona ugonjwa na hakufunga, anaweza kumwingilia na hana kafara. [Al-Majmuw’u (6/268), nayo ni kauli ya Ash-Shaafi’iy katika Al-Ummu (2/62) na Maalik katika Al-Mudawwanah (1/184)]
Swali: Mtu kazidiwa matamanio ya kimwili na ameshindwa kuvumilia –siku moja- kumjimai mkewe, je anaweza kusafiri naye ili afungue apate kumjimai? Inavyoonekana ni kuwa hakuna ubaya kufanya hivyo. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
3, 4- Mzee kikongwe, bibi kijizere na mgonjwa wa maradhi sugu
‘Ulamaa wote wanakubaliana kuwa mzee kikongwe na bibi kijizere wasioweza kufunga, inajuzu kwao kula bila kulipa. Halafu wakakhitalifiana kuhusu lipi litawalazimu kama watakula. Jumhuri wamesema watalisha maskini kwa kila siku moja, lakini Maalik anasema hawawajibikiwi kulisha masikini ila tu hilo ni zuri wakipenda. [Al-Qawaaniyn Al-Fiqhiyyah (82), Al-Majmuw’u (6/258), Al-Mughniy (3/79), Kash-Shaaf Al-Qinaa (2/309) na Bidaayatul Mujtahid (1/447)]
Kauli ya Jumhuri ina nguvu zaidi.
Na asli ya hili ni Kauli Yake Ta’aalaa:
((وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ))
((Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika watoe fidia; kulisha masikini)). [Al-Baqarah (2:184)]
Toka kwa ‘Atwaa kuwa alimsikia Ibn ‘Abbaas akiisoma Aayah hii, na Ibn ‘Abbaas akasema: ((Si mansuwkhah (haikufutwa), ni kwa mzee kikongwe na bibi kijizere wasioweza kufunga. Walishe mahala pa kila siku masikini mmoja)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4505). Lakini Ibn ‘Abbaas ameisoma:
(وعلى الذين يطوّقونه)
Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika
nacho ni kisomo kisicho cha kawaida. Angalia Tafsiyr At-Twabariy (3/438)]
Na Jumhuri ya Swahaba –akiwemo Ibn ‘Abbaas kwa utafiti unaoendelea kama tutakavyoona mbeleni- wanaona kuwa Aayah hii ni mansuwkhah. Toka kwa Salamah bin Al-Akwa’a amesema: ((Ilipoteremka
وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ
((Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika watoe fidia; kulisha masikini)). [Al-Baqarah (2:184)]
mtu alikuwa (ana khiyari) akitaka anakula na kutoa fidia mpaka ilipoteremka Aayah inayoifuatia, ikafuta hukmu hii)). [Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4507)]
Na tukichukulia kauli inayosema kuwa imefutwa, basi Aayah bado iko pale pale mahala pa kutolewa dalili, kwa kuwa ikiwa imeteremka kuhusiana na mzee mwenye umri mkubwa –kama walivyosema baadhi ya Masalaf- na hata ikiwa imeshuka kukhiyarisha, basi itabaki hivyo hivyo, kwa kuwa mzee anabakia katika haki ya mwenye kuweza kufunga, hivyo mzee huyu anabakia katika hali yake kama alivyokuwa. [Al-‘Inaayat ‘Alal-Hidaayat (2/227- pamoja na Fat-hul Qadiyr]
Kisha mzee kikongwe na bibi kijizere kufutiwa Swawm kunanasibiana na ujumla na ujumuishi wa kuondoshea watu uzito.
Na hukmu ya mgonjwa wa maradhi sugu ni kama ya wazee. [Radd Al-Mukhtaar (2/119), Al-Majmuw’u (6/258), Ar-Rawdh Al-Murabba’a (1/138)]
5,6- Mja mzito na mwenye kunyonyesha
Mwanamke mja mzito akikihofia kijusi chake tumboni, au mwenye kunyonyesha akahofia kichanga chake kutopata maziwa ya kutosha au kutopata kabisa na mfano wa hivyo, basi inajuzu kwao kula bila makhitalifiano yoyote kutokana na kauli yake Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((إن الله عز وجل وضع عن المسافر شطر الصلاة، وعن المسافر والحامل والمرضع الصوم))
((Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla Ameondosha nusu ya Swalaah kwa msafiri, na Swawm kwa msafiri, mja mzito na mwenye kunyonyesha)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ahmad (4/347) na ‘Abdu bin Humayd (Al-Muntakhab) (430). Sheikh wetu amesema ni Hadiyth Hasan]
Lakini ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na linalowalazimu kama wakila kwa kauli tano:
Ya kwanza:
Ni lazima walipe na walishe masikini mmoja kwa kila siku. Ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [At-Tirmidhiy ameinukulu kutoka kwao (3/402 –At-Tuhfah. Angalia rejea zilizotangulia]
Na Wanazuoni wa Kishaafiíy na Kihanbali wanasema ikiwa watakula kwa kujiogopea wenyewe, basi watalipa tu!!
Ya pili:
Watalipa tu. Ni madhehebu ya Al-Awzaa’iy, Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na Maswahibu Zake, Abu Thawr na Abu ‘Ubayd. [Bidaayatul Mujtahid (1/446) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/394)]
Hawa wameichukulia dalili ya kuwekwa kundi moja msafiri, mja mzito na mwenye kunyonyesha katika Hadiyth iliyopita, au wametumia Qiyaas cha mja mzito na mwenye kunyonyesha kwa mgonjwa au msafiri.
Kauli yao hii inajibiwa kwa kusema kuwa msafiri ni lazima alipe kutokana na naswi nje ya Hadiyth, nayo ni Kauli Yake Ta’aalaa:
((وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ))
((Na atakayekuwa mgonjwa au safarini)). [Al-Baqarah (2:185)]
Ama mjamzito na mwenye kunyonyesha, hakuna dalili ya kuwajibisha wao kulipa. Kisha kwa kuiangalia Hadiyth kwa kina, tunakuta kwamba msafiri akipunguza Swalaah safarini, hatakiwi –baada ya kurudi- kutimiza rakaa alizokuwa amepunguza, Basi na isemwe pia kuwa mjamzito na mwenye kunyonyesha hawalazimiki kulipa siku walizokula!! [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/395)]
Ya tatu:
Watalisha tu bila kulipa. Ni kinyume na iliyopita. Ni kauli ya Ibn ‘Abbaas na Ibn ‘Umar. Ni madhehebu ya Is-Haaq, na ni chaguo la Al-‘Allaamah Al-Albaaniy (Rahimahumul Laah).
Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: ((Mzee kikongwe na bibi kijizere waliruhusuwa katika hilo nailhali wanaweza kufunga, wakitaka wanakula na wanalisha kila siku masikini, na hawalipi. Kisha hukmu hiyo ikaondoshwa katika Aayah hii:
فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ
Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi na afunge. [Al-Baqarah: 185]
na ikathibiti kwa mzee kikongwe na bibi kijizere kama hawawezi kufunga, na mjamzito na mwenye kunyonyesha wakihofia [nafsi zao au watoto wao], na walishe kila siku masikini)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Al-Jaaruwd (381), na Al-Bayhaqiy (4/239). Angalia Al-Irwaa (4/18)]
Na katika neno lake “ikathibiti” kuna ujulisho kuwa hukmu hii ilikuwa ni sharia kwa asiyeweza kufunga kama ilivyokuwa sharia kwa mwenye kuweza kufunga, na hii ikafutwa na nyingine ikaendelea. Na bila shaka Ibn ‘Abbaas ameujua usharia wake wote na kuendelea kwake toka kwenye Hadiyth, na si toka kwenye Qur-aan. [Al-Albaaniy (Rahimahul Laah amelielezea hili katika Al-Irwaa (4/24)]
Na hili linatiliwa nguvu na Ibn ‘Abbaas kuithibitisha hukmu hii kwa mjamzito na mwenye kunyonyesha kama wakihofia. Na ni wazi kabisa kuwa wawili hawa si kama mzee kikongwe na bibi kijizere katika kutokuwa na uwezo wa kufunga, bali wao wana uwezo wa kufunga. Na kwa ajili hiyo, alikuwa akimwamuru kijakazi chake mjamzito ale na kumwambia: ((Wewe ni sawa na mzee kikongwe asiyeweza kufunga, basi kula na ulishe kwa kila siku nusu pishi ya ngano)). [Isnaad Yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq (7567) na Ad-Daaraqutwniy (2/206) na amesema ni Swahiyh]
Basi ni kutokea wapi Ibn ‘Abbaas amewapa wawili hawa hukmu hii na kusema kuwa Aayah hii ni mansuwkhah?! Hilo ni kutoka kwenye Sunnah bila shaka.
Toka kwa Naafi’i amesema: ((Binti wa Ibn ‘Umar alikuwa chini ya mwanamume wa Kikureshi, alikuwa mja mzito, kikampata kiu katika Ramadhwaan. Ibn ‘Umar akamwamuru ale na alishe kwa kila siku masikini)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ad-Daaraqutwniy (2/207). Angalia Al-Irwaa (4/20)]
Ya nne:
Mjamzito atalipa, na mwenye kunyonyesha atalipa na atalisha. Ni kauli ya Maalik, na ni kauli ya Wanachuoni wa Kishaafi’iy. [Al-Muhallaa (6/265), Bidaayatul Mujtahid (1/446) na Al-Majmuw’u (6/273)]
Ya tano:
Si lazima juu yao kulipa wala kulisha. Ni madhehebu ya Ibn Hazm [Al-Muhallaa (6/263)]
Amesema: “Swawm ikipomoka, basi kuwajibisha wao kuilipa ni sharia ambayo Allaah Hakuidhinisha, na Allaah Ta’aalaa Hakuwajibisha kulipa isipokuwa kwa mgonjwa, msafiri, mwenye hedhi, mwenye nifasi na mwenye kujitapisha kwa kusudi. Ama kuwakalifisha kulisha, bila shaka haijuzu kwa yeyote kulazimisha faini ambayo haikutajwa na Aayah, wala Sunnah wala Ijma’a”.
Ninasema: “Kauli yenye nguvu zaidi kati ya kauli hizi ni kuwa watakula na watalisha kwa kila siku masikini, na hakuna kulipa juu yao. Ni kauli ya Ibn ‘Abbaas na Ibn ‘Umar, na hakuna Swahaba yeyote aliyekwenda nao kinyume. Kisha Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ina hukmu ya “Raf-’u”, kwa kuwa ni Hadiyth ya Swahaba iliyokuja katika kufasiri yanayohusiana na sababu ya kuteremka Aayah. Na hii ni Hadiyth Musnad kama inavyojulikana katika taaluma ya Mustwalah”. [Angalia Kitabu cha Tadriyb Ar-Raawiy (1/192-193) na ‘Uluwm Al-Hadiyth cha Ibn Swalaah (uk 24)]
[b] Kundi La Ambao Ni Lazima Wale Na Walipe
1,2- Mwenye hedhi na mwenye nifasi
‘Ulamaa wote bila makhitalifiano wanasema haiswihi kufunga kwa mwenye hedhi na mwenye nifasi, na si wajibu kwao, bali pia ni haramu, na baada ya kutwaharika ni lazima walipe. [Al-Mughniy (3/142) na Al-Majmuw’u (6/259)]
Toka kwa Abu Sa’iyd (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: “Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((أليست إذا حاضت لم تصل ولم تصم؟ فذلك نقصان دينها))
((Je, si anapoingia hedhini haswali wala hafungi? Basi hilo ni upungufu wa diyn yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1951)]
Na toka kwa ‘Aaishah amesema: ((Tulikuwa tunapata hedhi wakati wa enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) halafu tunaamuriwa kulipa Swawm na hatuamuriwi kulipa Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (335), Abu Daawuwd (259), At-Tirmidhiy (784) na An-Nasaaiy (4/191)]
Masuala Mbalimbali Kuhusu Swawm Na Mwanamke Mwenye Hedhi
Akitwaharika na hedhi wakati wa mchana
Ataendelea kujiachia atakavyo katika kula na kunywa, na kama mumewe atarudi kutoka safari akiwa hajafunga, anaweza kumjimai. Haitakikani ajizuie siku iliyobakia kwa niya ya kufunga.
Akitwaharika kabla ya Alfajiri
Akitwaharika kabla ya Alfajiri na akanuwia kufunga, Swawm yake itaswihi hata kama atakuja kuoga baada ya Al-Fajiri. Hii ni kauli ya Jumhuri.
Je, mwanamke anaweza kutumia dawa ya kukata hedhi katika Mwezi wa Ramadhwaan?
Hedhi ni jambo ambalo Allaah Amewaumbia nalo wanawake, na wanawake wakati wa enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hawakuwa wakijitaabisha kwa hilo ili waweze kufunga Mwezi kamili, hivyo hilo si jambo linalopendeza.
Lakini ikiwa mwanamke atafanya hilo –na dawa ikawa haina madhara kwake- basi hakuna ubaya. Na akiitumia na damu ikakatika, basi anakuwa na hukmu ya mwanamke aliye twahara, atafunga na wala hatolipa. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
Mwenye damu ya istihaadhwah
Hatojizuia kufunga wala kuswali, bali hayo yote mawili ni lazima ayafanye kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa.
3- Mwenye kuhofia kufa akifunga
Huyu ni lazima ale. [Al-Muhallaa (6/228), Al-Majmuw’u (6/262), Ad-Durru Al-Mukhtaar (2/116) na Al-Qawaaniyn Al-Fiqhiyyah (82)]
[c] Kundi La Ambao Hawaruhusiwi Kula
Ni kila Muislamu aliyebaleghe, mwenye akili, mzima wa afya, mkazi asiye msafiri, na mwanamke aliyetwaharika kutokana na hedhi au nifasi.