13-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Kulipa Swiyaam Za Ramadhwaan

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swiyaam

 

13-Kulipa Swiyaam Za Ramadhwaan

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1- Mwenye kufungua bila udhuru

 

 

‘Ulamaa wengi wanasema kuwa mwenye kufungua makusudi, ni lazima alipe sawasawa kwa udhuru au bila udhuru. Lakini wamekhitalifiana hawa katika haya:

 

Baadhi yao wamewajibisha kulipa na kutoa kafara kwa aliyekula au    kunywa kwa kuliweka hilo kipimo kimoja na jimai!! [Tumegusia nyuma kidogo kuwa amri ya kulipa kwa mwenye kumjimai mkewe mchana wa Ramadhwaan haikuthibiti toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam).

 

Ni kauli ya Ibn Mubaarak, Ath-Thawriy, Is-Haaq, Abu Haniyfah, na Maalik. Ash-Shaafi’iy na Ahmad ambao wamesema ni lazima alipe bila kutoa kafara.

 

Ama Ibn Hazm, yeye anaona kuwa hakuna dalili ya kisharia ya kulipa akila makusudi bila udhuru, kwa kuwa ‘ibaadah ya muda ina mpaka wa kuanza na kumalizika, na kama itaachwa bila udhuru, basi hakuna sharia inayosema ilipwe ila kwa naswi (dalili) mpya. Hivyo kulazimisha Swiyaam isiyo Ramadhwaan –ambayo amefaradhishiwa kufunga- badala yake, ni wajibisho wa sharia ambayo Allaah Ta’aalaa Hakuiamuru. [Al-Muhallaa (6/180) na Mas-alah (735)]

 

Ninasema (Abu Maalik): “Haya ni madhehebu yenye nguvu zaidi kama ilivyozungumzwa nyuma kuhusiana na kulipa Swalaah zilizompita mtu. Na hapa yanatiliwa nguvu ya kuwa haikuthibiti kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwamuru aliyejimai mchana wa Ramadhwaan alipe pamoja na kuthibiti kafara kama ilivyotangulia nyuma kidogo. Imepokelewa kwa njia swahiyh toka kwa Ibn Mas’uwd kuwa amesema: ((Mwenye kufungua siku moja ya Ramadhwaan bila ya udhuru wala ruksa, haitomfalia Swiyaam ya umri wake wote))”. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (9784)]

 

Hadiyth kama hii imepokewa pia toka kwa Abu Hurayrah.

 

Ninasema: “Lakini katika yaliyotangulia, kujitapisha kwa kusudi kunatolewa nje, kwani mwenye kufanya hivyo atalipa kutokana na naswi inayogusia hilo kama ilivyozungumzwa katika sehemu yake husika. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.  

 

1-     Kulipa Ramadhwaan si lazima kufanyike kwa haraka

 

Kulipa siku zilizompita mtu katika Ramadhwaan kutokana na udhuru wa kisharia si lazima kuwe papo kwa hapo, bali wajibu wake ni wa wigo mpana na wakati mkunjufu. Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) aliyesema: ((Ilikuwa ninakuwa na Swawm ya kulipa ya Ramadhwaan, na siwezi kuilipa isipokuwa katika Sha’abaan)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1950) na Muslim (1146)]

 

Al-Haafidh kasema katika Al Fat-h (4/191): “Katika Hadiyth kuna dalili ya kujuzu kuchelewesha kulipa Ramadhwaan, sawasawa kukawa (kuchelewesha huko) kwa udhuru au bila udhuru”.

 

Lakini pamoja na hivyo, ni vizuri kufanya haraka kulipa kutokana na ujumuishi wa Kauli Yake Ta’aalaa:

((أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ))

((Hao wanakimbilia katika mambo ya khayr; na wao ndio wenye kuyatanguliza)). [Al-Muuminuwn (23:61)]

 

Faida

 

Ikiwa atachelewesha kulipa mpaka ikaingia Ramadhwaan nyingine, basi atafunga Ramadhwaan mpya ilioingia kama alivyoamuriwa. Kisha akila katika Shawwaal, atayalipa masiku anayodaiwa tu na wala hakuna la ziada ya hapo. Si wajibu kwake kulisha wala jingine lolote, kwa kuwa hakuna chochote chenye kuthibitisha hilo kilichorufaishwa kwa Nabiy (Swalla Allaah ’alayhi wa aalihii wa sallam). Haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Ibn Hazm, nayo ndiyo yenye nguvu.

 

Maalik amesema kuwa atalisha katika kuilipa kila siku kibaba kwa kibaba kwa idadi ya masikini ikiwa alifanya kusudi kuacha kulipa. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy pia. [Al-Muhallaa (6/260, 261). Angalia Al-Majmuw’u (6/412)]

 

 

2-     Si lazima kufululiza siku katika kulipa

 

Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa :

فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

 

basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. [Al-Baqarah (2:184)]

 

Ibn ‘Abbaas amesema: ((Hakuna ubaya kama ataachanisha)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Al-Bukhaariy amesema ni Mu’allaq, na ‘Abdul Razzaaq kasema ni Mawsuwl (4/43), na Ad-Daaraqutwniy (2/192) na Al-Bayhaqiy (4/258) kwa Sanad Swahiyh]

 

Abu Hurayrah amesema: ((Azilipe kwa (hisabu) ya witri akipenda)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ad-Daaraqutwniy. Angalia Al-Irwaa (4/95)]

 

Na Anas kasema: ((Ukipenda ilipe Ramadhwaan siku mfululizo, na ukitaka achanisha siku)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (9115) na Al-Bayhaqiy (4/258)]

 

Ama Hadiyth Marfuw’u toka kwa Abu Hurayrah:

((من كان عليه صوم رمضان فليسرده ولا يقطعه))

((Anayedaiwa Swawm ya Ramadhwaan basi aandamishe wala asiikate))..

Hadiyth hii ni Dhwa’iyf haijasemwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). [Imekharijiwa na Ad-Daaraqutwniy (2/191) na Al-Bayhaqiy (4/259). Angalia Al-Irwaa (4/95)]

 

Maimamu wanne wamekhiyarisha kati ya kufululiza au kuachanisha wakati wa kulipa. [Al-Muhallaa (6/261), Masaail Ahmad cha Abu Daawuwd (uk. 95), Al-Majmuw’u (6/412) na Al-Mughny (3/43)]

 

3-     Aliyekufa na anadaiwa Swawm

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu mtu aliyekufa na anadaiwa Swawm. Je msimamizi wake atamfungia? Wana kauli tatu kuhusu hili:

 

Ya kwanza:

 

Hafungiwi, si kwa Swawm ya nadhiri wala qadwaa ya Ramadhwaan. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Maswahibu zake, Maalik, Dhwaahir na madhehebu ya Ash-Shaaf’iy. [Tahdhiyb As Sunan (7/27), Al-Majmuw’u (6/412) na Fat-hul Qadiyr (2/360)].

 

Hoja yao ni:

 

1- Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ))

((Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi)). [An-Najm ( 53:39)]

 

2- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)

 

((إِذَا مَاتَ ابنُ آدم انْقَطَعَ عَنْهُ عَمَلُهُ إِلَّا مِنْ ثَلَاثٍ: صَدَقَةٍ جَارِيَةٍ، أو عِلْمٍ يُنْتَفَعُ بِهِ، أَوْ وَلَدٍ صَالِحٍ يَدْعُو لَهُ))

((Anapokufa mwanadamu ‘amali yake hukatika isipokuwa ya matatu: Swadaqah endelevu, au ‘ilmu inayopatiwa manufaa, au mtoto mwema anayemwombea)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy, Muslim (1631), At-Tirmidhiy (1376), Abu Daawuwd (3880) na An-Nasaaiy (3651)]

 

3- Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Ubaadah bin Nassiy kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

((من مرض في رمضان فلم يزل مريضا حتى مات لم يطعم عنه، وإن صح فلم يقضه حتى الموت أطعم عنه))

((Mwenye kuugua katika Ramadhwaan na akaendelea kuumwa mpaka akafa, basi hatolishiwa chakula, na kama atapona na hakulipa mpaka akafa, basi atalishiwa chakula)). Hadiyth hii haifai kutumika. [Isnaad yake ni Dhwa’iyf. Imekharijiwa na ‘ Abdul Razzaaq]

 

4- Hadiyth ya ‘Amrah: ((Kuwa mama yake alikufa akiwa anadaiwa Swiyaam ya Ramadhwaan, akamwambia ‘Aaishah: Je nimlipie? Akasema: ((Hapana, bali mtolee Swadaqah mahala pa kila siku nusu pishi kwa kila masikini)). [Isnaad yake ni Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Atw-Twahaawiy katika Al-Mushkil (3/142) na Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (4/7)]

 

Na imesimuliwa toka kwake akisema:

((لا تصوموا عن موتاكم وأطعموا عنهم))

((Msiwafungie maiti wenu bali walishieni chakula)). [Isnaad yake ni Dhwa’iyf sana. Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq na Al-Bayhaqiy (4/256)]

 

Wamesema: Naye ndiye aliyesimulia neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam):

((من مات وعليه صوم، صام عنه وليه))

((Mwenye kufa na anadaiwa Swawm, msimamizi wake atamfungia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1952) na Muslim (1147)]

 

Hivyo, Hadiyth inajulisha kuwa lililoamuriwa (na Rasuli) ni kinyume na aliyoyahadithia Bibi ‘Aaishah.

 

 

5- Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: ((Mtu asimswalie mtu, wala mtu asimfungie mtu)). [Isnaad Yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (2918), na kwa Sanad yake Ibn ‘Abdul Barri katika At-Tamhiyd (9/27), na At-Twahaawiy katika Al-Mushkil (6/176)]

 

Na Ibn ‘Abbaas huyu ndiye msimulizi wa Hadiyth ya kumfungia mama itakayokuja mbeleni.

 

6- Wameawilisha Hadiyth ya ((صام عنه وليه)) wakisema muradi wake ni kuwa atamfanyia linalowakilisha Swawm, nako ni kulisha chakula!!

 

An-Nawawiy amesema katika Al-Majmuw’u (6/419) kuwa hii ni taawiyl batilifu ambayo inajibiwa na Hadiyth nyingine.

 

 

7- ‘Ulamaa wa Kimaalik wamesema: Walivyofanya watu wa Madiynah ni kinyume ya hayo!!

 

Ya pili:

 

Hufungiwa nadhiri zake na hulipiwa Swawm zake bila kizuizi chochote. Ni madhehebu ya Abu Thawr na moja ya kauli mbili za Ash-Shaafi’iy –An-Nawawiy ameikhitari-, Ahlul Hadiyth na Ibn Hazm. [Al-Muhallaa (2/7) na kurasa zinazofuatia), Al-Majmuw’u (6/418) na Al-Fat-h (4/226)]

 

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((من مات وعليه صيام صام عنه وليه))

((Mwenye kufa na anadaiwa Swawm, msimamizi wake atamfungia)). [Hadiyht Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]

 

2- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ambaye amesema: ((Mtu mmoja alikwenda kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika mama yangu amekufa naye anadaiwa Swawm ya mwezi, [katika riwaya: Swawm ya nadhiri] je nimlipie? Akasema:

((نعم فدين الله أحق أن يقضى))

((Na’am, deni la Allaah lina haki zaidi kulipwa)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (9153) na Muslim (1148)]

 

3- Hadiyth ya Buraydah amesema: ((Wakati nilipokuwa nimekaa kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), mara akamjia mwanamke mmoja akamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika mimi nilimpa mama yangu Swadaqah ya kijakazi, na yeye amefariki [je nimchukue nimmiliki tena?]. Akasema:

((وجب أجرك، وردها عليك الميراث))

((Ujira wako umethibiti [kwa kumuunga mama yako], na mirathi imemrejesha kwako [kijakazi])). Akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika yeye alikuwa anadaiwa Swawm ya mwezi, je nimfungie? Akasema:

((صومي عنها))

((Mfungie)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1149) na At-Tirmidhiy (667)]

 

4- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: ((Kwamba mwanamke mmoja alisafiri baharini, akaweka nadhiri kuwa ikiwa Allaah Atamfikisha salama safari yake, basi atafunga mwezi mzima. Allaah Ta’aalaa Akamfikisha salama safari yake, naye hakufunga mpaka akafariki. Binti yake au dada yake akaenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), na Rasuli akamwamuru amfungie)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3308) na An-Nasaaiy (3816)]

 

5- Wamejibu dalili za wenye kuzuia (kufungiwa au kulipiwa Swawm maiti) kwa Neno Lake Ta’aalaa:

((وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ))

((Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi)). [An-Najm (53:39)]

 

..wakisema kuwa Aliyeiteremsha Aayah hii Ndiye Aliyeiteremsha Aayah:

((مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ))

((baada ya kutoa wasia aliousia (maiti) au kulipa deni)). [An-Nisaa (4:11)]

 

Na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ameiita Swiyaam deni, hivyo imejulikana kuwa muradi ni kwamba mwanadamu hana isipokuwa kile tu alichokifanyia juhudi mwenyewe, na kwa kile ambacho Allaah na Rasuli Wake Wamekihukumia kuwa anakipata pia kutokana na juhudi alizofanyiwa na mwingine, na Swawm ni katika jumla ya hayo.

 

6- Wameijibu Hadiyth:

((إذا مات ابن آدم انقطع عمله...))

((Anapokufa mwanadamu amali yake hukatika….))..kuwa haihusiana na suala letu hili bali inahusiana na kukatika amali ya maiti, lakini haigusii kukatika amali anayofanyiwa na mtu mwingine wala kukataza hilo.

 

 

7- Wamejibu fatwa ya Ibn ‘Abbaas na ‘Aaishah wakisema kuwa athar zilizopokelewa toka kwao zina mzozo, na kama zingekuwa ziko sawa, basi zingekuwa ni hoja kwa yale waliyoyasimuliwa yakiwa Marfuw’u bila haja ya fatwa zao kama ilivyopitishwa katika taaluma ya Uswuwl.

 

Ya tatu:

 

Hufungiwa nadhiri tu lakini halipiwi Ramadhwaan. Ni madhehebu ya Ahmad, Is-Haaq, Abu ‘Ubayd na Al-Layth. [Tahdhiyb As-Sunan (7/27) na Al Fat-h (4/228)]

 

Dalili zao ni:

 

1- Ni kuwa Hadiyth ya ‘Aaishah ni ya jumla na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ni mahususi, na hii ndiyo inayochukuliwa. Na muradi wake unakuwa Swawm ambayo anaifunga msimamizi wa maiti  ni Swawm ya nadhiri.

 

2- Lililothibiti toka kwa ‘Aaishah kuhusu kukataza kwake kumfungia maiti, ni kuwa katazo hilo linahusiana na Swawm ya faradhi tu na si Swawm ya nadhiri kama ilivyotangulia katika athar ya ‘Amrah toka kwa ‘Aaishah isemayo: ((Kuwa mama yake alikufa akiwa anadaiwa Ramadhwaan…)). Inavyoonyesha hapa ni kuwa yeye hakatazi kumfungia maiti nadhiri kwa kutekeleza aliyoyasimulia kutokana na ujumla.

 

3- Lililothibiti toka kwa Ibn ‘Abbaas –naye ndiye msimulizi wa Hadiyth nyingine kuhusu kumfungia maiti- ni neno lake: ((Mtu akiumwa katika Ramadhwaan kisha akafa bila kufunga, atatolewa chakula na haitokuwa juu yake kulipiwa. Na kama anadaiwa nadhiri, msimamizi wake atamlipia)).  [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2398) na Ibn Hazm (7/7)]

 

 

Na bila shaka yeye ndiye ajuaye zaidi maana ya simulizi yake.

 

4- Fardhi ya Swiyaam inapita mkondo wa Swalaah na kusilimu. Na kama ambavyo mtu hamswalii mtu wala mtu kumsilimia mwingine, ni hivyo hivyo kwa Swiyaam. Na muktadha wa dalili ni kuwa wanachomfanyia maiti baada ya kufa, hakiondoshi dhima yake, hakikubaliwi, na wala hanufaiki kwa kufanyiwa na wengine Fardhi za Allaah zinazompasa.

 

Ama nadhiri, ni kuwa Allaah kimsingi Hakumlazimisha, bali mtu mwenyewe kajilazimishia, hivyo inakuwa ni kama deni alilolikopa ambalo linaingiliwa na uniaba (kufanyiwa).

 

Ninasema (Abu Maalik): “Ambalo mimi naona lina nguvu ni kuwa maiti hufungiwa siku anazodaiwa pamoja na nadhiri bila mpaka wala shuruti, kwa kuwa ujumla (katika Hadiyth ya ‘Aaishah) haukhusishwi na mmoja wa watu wake (katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas) isipokuwa katika hali ya mkinzano –kama ilivyoelezwa katika taaluma ya Uswuwl-, na hapa hakuna ukinzano. Na kwa ajili hiyo, Al-Haafidh amesema katika Al-Fat-h (4/228): Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ni picha inayojitegemea ambayo huulizwa kwayo mtu ambaye imemtokea. Ama Hadiyth ya ‘Aaishah, hiyo ni azimio la kanuni jumla”.

 

Mwisho wa yote haya, tunafahamu kuwa aliyekufa ilhali anadaiwa Swawm, haepukani na moja ya hali tatu:

 

1- Udhuru wake wa kuilipa Swawm uendelee mpaka afe akiwa hawezi kulipa. Huyu hatodaiwa chochote, wala warithi wake, wala katika mali aliyoiacha; hakuna kufungiwa wala kutolewa chakula. [Al-Majmuw’u (6/414)]

 

2- Udhuru wake kuondoka na aweze kulipa Ramadhwaan lakini hakulipa mpaka akafa. Huyu atafungiwa.

 

3- Afe ilhali anadaiwa nadhiri. Huyu atafungiwa na warithi wake.

 

Faida mbili:

 

1- Neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((من مات وعليه صيام، صام عنه وليه))

((Mwenye kufa na anadaiwa Swawm, msimamizi wake atamfungia)), ni habari isiyo kanushi wala amri, lakini ina maana agizi, na taqdiyr yake ni:

((فليصم عنه وليه))

((basi msimamizi wake amfungie)).

 

Na amri hii ni ya Sunnah si ya waajib kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri kinyume na Ahl Adh-Dhwaahir. [Fat-hul Baariy (4/228)]

 

Hili linatiliwa nguvu na riwaya ya Al-Bazzaaz isemayo:

((فليصم عنه وليه إن شاء))

 ((basi msimamizi wake amfungie akipenda)). [Hili lau riwaya hii ni swahiyh,

nayo ni nyongeza isiyopendeza. Angalia Tamaam Al-Minnah (uk. 427)]

 

Na hili ndilo lenye kuendana na qawaaid, kwani asli ya mambo ni mtu kutokuwa na dhima yoyote juu yake, na kwamba mukallaf halazimiki kufanya yanayohusu dhima ya mwingine isipokuwa kwa dalili bayana.

 

2- Aliyekufa ilhali anadaiwa Swawm, na akafungiwa na watu kwa idadi ya siku anazodaiwa, basi hilo litajuzu.

 

 

Ama kulisha chakula, ikiwa msimamizi wake atakusanya masikini kwa idadi ya siku anazodaiwa na akawashibisha, basi hilo pia litajuzu. Hivyo ndivyo alivyofanya Maalik (Radhwiya Allaah ‘anhu).

 

 

Share