14-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Swiyaam za Sunnah
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swiyaam
14-Swiyaam za Sunnah
[Nimefaidika katika mlango huu kutokana na aliyoyakusanya ndugu yangu mfadhili Usaamah ‘Abdul ‘Aziyz –Allaah Amlipe jaza yake- katika Kitabu chake cha Swiyaamu At-Tatwawwu’i Fadhwaiilu wa Ahkaam]
Sharia imewapa watu utashi na kuwaraghibisha kufunga masiku yasiyo Ramadhwaan ambayo ni:
1- Siku Sita za Shawwaal
Imesuniwa Ramadhwaan ifuatishwe kwa Siku Sita za Shawwaal –si lazima kufuatanisha- kwa kuwa kufunga masiku haya ni sawa na Swiyaam ya mwaka. Toka kwa Abu Ayyuwb Al-Answaariy kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((من صام رمضان، ثم أتبعه ستا من شوال، كان كصيام الدهر))
((Aliyefunga Ramadhwaan, kisha akaifuatishia [siku] Sita za Shawwaal, inakuwa kama Swawm ya mwaka)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1164), Abu Daawuwd (2433), At-Tirmidhiy (759), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (2862) na Ibn Maajah (1716)]
Na bila shaka limekuwa hilo kama Swawm ya mwaka kwa kuwa jema moja hulipwa kwa kumi mfano wake. Na Ramadhwaan ni kwa miezi kumi (siku 300), na sita (za Shawwaal) ni kwa miezi miwili (siku 60). Ni kama inavyoeleza Hadiyth ya Thawbaan toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam):
((من صام رمضان، فشهر بعشرة أشهر وصيام ستة أيام بعد الفطر، فذلك تمام صيام السنة))
((Mwenye kufunga Ramadhwaan, basi mwezi ni kwa miezi kumi, na kufunga siku sita baada ya kufungua, basi huko ni kutimia Swiyaam ya mwaka)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ahmad (5/280), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (2860) na Ibn Maajah (1715)]
‘Ulamaa wengi wakiwemo Ash-Shaafi’iy na Ahmad wamestahabisha kuifunga Sunnah hii. Lakini Abu Haniyfah, Abu Yuwsuf na Maalik, wao wanaona ni karaha kuifunga ili watu wasije kuamini kwamba ni waajib kuandamishia na Ramadhwaan. Ukaraha huu hauna mashiko kwa kuwa unakinzana na Hadiyth Swahiyh bayana. Kisha kuandamiza, bila shaka kumehofiwa mwanzoni mwa mwezi, ama mwishoni mwake, kunakuwa kumetenganishwa kati yake na siku nyingine na siku ya ‘Iyd ambayo haijuzu kufunga. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/238), Sharh Al-‘Umdah (2/556), Al-Mughniy (4/438), Fat-hul Qadiyr (2/349) na Haashiyat ‘Aabidiyn (3/421).
Anayedaiwa siku za kulipa za Ramadhwaan, je afunge Sita Shawwaal kwanza kabla ya kulipa Ramadhwaan?
Linaloonekana kutokana na Hadiyth iliyotangulia ya Abu Ayyuwb ni kuwa kupata fadhila ya thawabu za Swawm ya mwaka, kumeshurutishiwa kuifunga Ramadhwaan (kwanza) kisha kuifuatilishia siku Sita za Shawwaal. Hivyo Swawm ya Sita Shawwaal haitangulizwi kabla ya kulipa Ramadhwaan. [Amelieleza hili Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahul Laah) kama ilivyo katika Al-Mumti’u (6/448)]
Ninasema: Isipokuwa kama itasemwa kuwa kauli yake (Rasuli):
((ثم أتبعه ستا)) imeendana na mazoea ya watu wengi kufanya hivyo (kufunga mfululizo), na si ilivyofahamika katika Hadiyth. Na kwa msingi huo, inajuzu kufunga Sita Shawwaal kabla ya kulipa Ramadhwaan na hususan kwa yule ambaye amebakiwa na siku chache kabla ya kumalizika Mwezi Shawwaal. Na Hadiyth ya Thawbaan ambayo haikutaja kuandamisha inabeba maana hii. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
2,3 - Swawm ya Muharram, na usisitizo zaidi tarehe tisa na kumi (‘Aashuwraa)
Imestahabiwa kukithirisha kufunga Mwezi wa Muharram kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((أفضل الصيام بعد رمضان شهر الله المحرم، وأفضل الصلاة بعد الفريضة صلاة الليل))
((Swiyaam bora zaidi baada ya Ramadhwaan ni Mwezi wa Allaah Al-Muharram, na Swalaah bora zaidi baada ya za Faradhi ni Swalaah ya Usiku)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1163) An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (605) na Ibn Maajah (1742)]
Stahabisho linasisitizika katika kufunga tarehe kumi ya Muharram (‘Aashuwraa). Toka kwa Abu Qataadah kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((صيام يوم عاشوراء أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله))
((Funga Siku ya ‘Aashuwraa, ninataraji kwa Allaah Asamehe [madhambi ya] mwaka ulio kabla yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1162)]
Ibn ‘Abbaas aliulizwa kuhusu funga ya Siku ya ‘Aashuwraa akasema: ((Sikujua kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amefunga siku yoyote anatafuta fadhla zake kuliko masiku mengine yote isipokuwa Siku hii, wala mwezi wowote isipokuwa Mwezi huu, yaani Ramadhwaan)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2006) na Muslim (1132)]
Imestahabiwa kufunga kabla yake tarehe tisa ya Muharram kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: ((Wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipofunga ‘Aashuwraa na akaamuru ifungwe walisema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika hiyo ni Siku ambayo Mayahudi na Manasara wanaitukuza. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:
((فإن كان العام المقبل –إن شاء الله- صمنا اليوم التاسع))
((Basi ikiwa mwaka ujao –Akipenda Allaah- tutafunga Siku ya Tisa)).
Akasema: Mwaka ujao haukuja mpaka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘ alayhi wa aalihii wa sallam) akafariki)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1134)]
Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad wamestahabisha kukusanya kati ya Funga ya tarehe tisa na tarehe kumi ya Muharram ili kutojishabihisha na Mayahudi katika kuifunga tarehe Kumi pekee. [Sharh Az-Zarqaaniy (2/237) na Al-Majmuw’u (6/383)]
Angalizo
Baadhi ya ‘Ulamaa wamestahabisha kufunga tarehe kumi na moja kuunganisha na tarehe Tisa na Kumi wakitolea dalili kwa yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((صوموا يوم عاشوراء وخالفوا اليهود، صوموا قبله يوما وبعده يوما))
((Fungeni Siku ya ‘Aashuwraa, na fanyeni kinyume na Mayahudi, fungeni kabla yake siku na baada yake siku)), lakini Hadiyth hii ni Dhwa’iyf sana, haina dalili ya kustahabisha kufunga tarehe kumi na moja. Watu walijue hili. Imekharijiwa na Ahmad (2418), Al-Humaydiy (485), Ibn Khuzaymah (2095) na wengineo.
4- Kukithirisha kufunga katika Mwezi wa Sha’abaan
Hakika Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akiufunga Mwezi wote isipokuwa siku chache mno. Toka kwa ‘Aaishah amesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anafunga mpaka tunasema hatofungua, na hufungua mpaka tunasema hatofunga, na sikumwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amekamilisha kufunga mwezi isipokuwa Ramadhwaan, na sikumwona akifunga zaidi kuliko [anavyofunga] katika Sha’abaan)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1969) na Muslim (1156)]
Angalizo mbili
La kwanza: Kuifanya nusu ya Sha’abaan siku maalumu ya kufunga ni bid’a
Mtu ambaye si ada yake kukithirisha kufunga Sha’abaan, au kufunga Masiku Matatu Meupe, kisha akaja kuifanya tarehe kumi na tano ya Sha’abaan kuwa siku maalum ya kufunga akiitakidi kuwa siku hii ina fadhila maalum, basi kitendo chake hicho ni bid’a, kwa kuwa hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh iliyopokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) inayozungumzia fadhila za nusu ya Sha’abaan. Hadiyth zote zilizosimuliwa kuhusu hili ni ima Dhwa’iyf mno au ni za kutengenezwa kama Hadiyth Marfuw’u ya ‘Aliy:
((إذا كانت ليلة النصف من شعبان فقوموا ليلها وصوموا نهارها...))
((Utakapokuwa usiku wa nusu ya Sha’abaan, basi simameni usiku wake na fungeni mchana wake)). [Dhwa’iyf sana. Imekharijiwa na Ibn Maajah (1388)]
La pili: Hakuna katazo lililothibiti kuzuia kufunga baada ya nusu ya Sha’abaan
‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na Swawm ya Sunnah baada ya tarehe kumi na tano ya Sha’abaan. Jumhuri wanasema inajuzu kufunga, lakini ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy wanasema ni makruhu wakitolea dalili Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((إذا انتصف شعبان فلا تصوموا))
((Ikiingia nusu ya Sha’abaan, basi msifunge)). [Munkar. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2337), At-Tirmidhiy (738), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (2911), Ibn Maajah (1651) na Ahmad (2/442). ‘Abdur Rahmaan bin Mahdiy, Ahmad, Yahyaa bin Mu’iyn, Abu Zar-’ah na wengineo wameikataa Hadiyth hii. Na mimi nimeikosoa katika maelezo yangu kuhusu Kitabu cha Sharhu Al-Bayquwniyyah cha Ibn ‘Uthaymiyn (uk. 22-24). Al-‘Allaamah Al-Albaaniy (Rahimahul Laah) kasema ni Hadiyth Swahiyh!!]
Hadiyth hii ni Dhwa’iyf kwa kauli yenye nguvu. Maimamu ambao kauli zao hazina shaka kuhusiana na jambo hili wameikataa. Hivyo basi, hakuna ubaya mtu kufunga baada ya kuingia nusu ya pili ya Sha’abaan, na hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ambazo ni Swahiyh. Ni kama Hadiyth iliyotangulia ya Bi ‘Aaishah kuhusiana na Rasuli (Swalla Allah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kukithirisha sana kufunga Sha’abaan, na Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((لا يتقدمن أحدكم رمضان بصوم يوم أو يومين، إلا أن يكون رجل كان يصوم صومه فلبصم ذلك اليوم))
((Asiitangulie kabisa mmoja wenu Ramadhwaan kwa Swawm ya siku moja au siku mbili, isipokuwa awe mtu alikuwa anafunga Swawm yake, basi na aifunge siku hiyo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1914) na Muslim (1082)]
Katika Hadiyth hii, kuna katazo la kufunga siku moja au siku mbili tu za mwisho za Mwezi wa Sha’abaan kwa ajili ya kuchelea ziada katika mwezi mtu akabeba yasiyohusu isipokuwa kama itakuwa ni Swawm ambayo ni ada yake kuifunga, hapo hakuna ubaya. Toka kwa Ummu Salamah amesema: ((Sikumwona Nabiy wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anafunga miezi miwili mfululizo isipokuwa Sha’abaan na Ramadhwaan)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (726), An-Nasaaiy (4/150), Ibn Maajah (1648) na Ahmad (6/293)]
5- Kufunga Siku ya ‘Arafah kwa wasiohiji
Imestahabiwa kwa asiyehiji afunge Siku ya ‘Arafah. Ni kwa Hadiyth ya Abu Qataadah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((صيام يوم عرفة أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله، والسنة التي بعده))
((Swawm ya Siku ya ‘Arafah ninataraji kwa Allaah Asamehe [madhambi ya] mwaka wa kabla yake, na mwaka wa baada yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1162)]
Makusudio ya kusamehewa madhambi ya miaka miwili ni ima Allaah Ta’alaa Anamghufiria madhambi ya miaka miwili [kwa sharti ya kuepuka madhambi makubwa], au Allaah Anamlinda katika miaka hii miwili asifanye ma’asia. [Al-Majmuw’u cha An-Nawawiy (6/381)]
Haistahabiwi kwa Hujaji kufunga ‘Arafah. Hakika ulikuwa ni mwongozo mwema wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na Makhalifa wake Waongofu kutofunga Siku ya ‘Arafah huko ‘Arafah. Toka kwa Maymuwnah (Radhwiya Allaah ‘anhaa): ((Kwamba watu walifanya shaka kama Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amefunga Siku ya ‘Arafah. Nikampelekea gilasi ya maziwa –naye amesimama katika kisimamo- akanywa na watu wanaangalia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1989) na Muslim (1124)]
Ibn ‘Umar aliulizwa kuhusu kufunga Siku ya ‘Arafah huko ‘Arafah akasema: ((Nilihiji pamoja na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) naye hakuifunga, pamoja na Abu Bakri naye hakuifunga, pamoja na ‘Umar naye hakuifunga, pamoja na ‘Uthmaan naye hakuifunga, na mimi siifungi, na siamuru kuifunga, na wala sikatazi kuifunga)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (751), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (2826) na Ahmad (2/47)]
Ni bora zaidi kwa Hujaji asifunge Siku ya ‘Arafah kwa kufuata alivyofanya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) pamoja na Makhalifa Wake. Kutofunga kutampa nguvu ya kuomba du’aa na kuleta adhkaar katika kisimamo hiki. Na haya ndiyo madhehebu ya Jumhuri ya ‘Ulamaa. [Al-Majmuw’u (6/380), At-Tamhiyd (21/158), na Sharh Al-‘Umdah cha Sheikh wa Uislamu (2/47)]
6- Swawm ya Jumatatu na Alkhamisi
Toka kwa ‘Aaishah amesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akijitahidi sana asikose Swawm ya Jumatatu na Alkhamisi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (745), An-Nasaaiy (2186) na Ibn Maajah (1739)]
Na Usaamah bin Zayd alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuhusu funga ya Jumatatu na Alkhamisi, na Rasuli akasema:
((ذانك يومان تعرض فيهما الأعمال على رب العالمين ، وأحب أن يعرض عملي وأنا صائم))
((Hizo ni siku mbili ambazo huonyeshwa ‘amali kwa Mola wa walimwengu, nami napenda ‘amali yangu ionyeshwe nikiwa nimefunga)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (2357), Ahmad (5/201) na Al-Bayhaqiy katika Ash-Shu’ab (3821]
7- Swawm ya Siku Tatu za Kila Mwezi
Toka kwa Abu Hurayrah amesema: ((Ameniusia Rafiki yangu kipenzi (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) [mambo] matatu: Kufunga Siku Tatu za kila Mwezi, rakaa mbili za Adh-Dhuhaa, na niswali Witr kabla ya kulala)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1981) na Muslim (721)]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia ‘Abdullaah bin ‘Amr:
((وصم من الشهر ثلاثة أيام، فإن الحسنة بعشر أمثالها، وذلك مثل صيام الدهر..))
((Na funga katika mwezi siku tatu, kwani hakika jema ni kwa kumi mfano wake, na hiyo ni kama Swiyaam ya mwaka..)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1976) na Muslim (1159)]
Na inastahabiwa yawe masiku Matatu Meupe, nayo ni tarehe 13, 14 na 15 ya kila mwezi kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((صيام ثلاثة أيام من كل شهر، صبام الدهر، أيام البيض صبيحة ثلاث عشرة وأربع عشرة وخمس عشرة))
((Swiyaam ya Siku Tatu za kila Mwezi ni Swiyaam ya mwaka. Masiku meupe asubuhi ya kumi na tatu, kumi na nne na kumi na tano)). [Hadiyth Swahiyh Lishawaahidih. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (2419), Abu Ya’alaa (7504) na At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (2/2499) toka kwa Jariyj. Ina Hadiyth wenza toka kwa Abu Dharri na Qataadah bin Milhaan]
8- Kufunga siku moja na kula siku moja (Swawm ya Daawuwd ‘Alayhis Salaam)
Hii ndio Swawm bora zaidi, ya kiuwiano zaidi, na inayopendwa zaidi kwa Allaah ‘Azza wa Jalla. Toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam amesema:
((أحب الصلاة إلى الله صلاة داود عليه السلام، وأحب الصوم إلى الله صيام داودـ، وكان ينام نصف الليل، ويقوم ثلثه، وينام سدسه، ويصوم يوما ويفطر يوما)) وفي رواية ((وهو أعدل الصيام))
((Swalaah inayopendwa zaidi kwa Allaah ni Swalaah ya Daawuwd ‘Alayhis Salaam, na Swawm inayopendwa zaidi kwa Allaah ni Swiyaam ya Daawuwd, na alikuwa analala nusu ya usiku, na anasimama theluthi yake na analala sudusi yake, na anafunga siku moja na anakula siku nyingine)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1131) na Muslim (1159)]
Na katika riwaya: ((Nayo ndiyo Swawm ya uwiano zaidi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1976) na Muslim (1159)]
Lakini hili limeshurutishwa kwa ambaye hatopoteza Aliyomwajibishia Allaah kwa sababu ya kufunga, na kama atapoteza faradhi, au ikamshughulisha asiweze kukidhi mahitaji ya mkewe na watoto, basi itakuwa marufuku kwake. [Yamedondolewa haya toka Ash-Sharh Al-Mumti’u cha Ibn ‘Uthaymiyn -Rahimahul Laah- (6/474)]
Faida
Imestahabiwa mtu asiache mwezi kupita bila kufunga Swawm yoyote. Toka kwa ‘Abdullaah bin Shuqayq amesema: “Nilimuuliza ‘Aaishah: Je, Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anafunga mwezi maalum mbali ya Ramadhwaan? Akasema: ((Wal Laah, hakufunga mwezi maalum isipokuwa Ramadhwaan mpaka umalizike, na hakula [mwezi wowote] mpaka afunge sehemu yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1156)]
Hivyo ni mustahabu mtu asiuache mwezi ukapita bila kufunga Swawm yoyote, kwani Swawm za Sunnah hazihusishwi na wakati maalumu, bali mwaka wote unafaa kwa Swawm isipokuwa siku ambazo ni haramu kufunga, ijapokuwa lililo bora zaidi ni kufunga masiku ambayo yamekokotezewa na sharia. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.