16-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Masiku Ambayo Imekatazwa Kufunga
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swiyaam
16-Masiku Ambayo Imekatazwa Kufunga
1,2- Siku Mbili Za ‘Iyd Mbili
‘Ulamaa wote bila makhitalifiano wameharamisha kufunga Siku ya ‘Iyd El-Fitwr na Siku ya ‘Iyd El-Adhwhaa kwa hali zote, sawasawa akifunga mtu kwa nadhiri, au Sunnah, au kafara au jinginelo. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/207), Al-Mughniy (4/424) na Fat-hul Baariy (4/281)]
Ni kwa Hadiyth ya Abu ‘Ubayd mwachwa huru wa Ibn Azhar aliyesema: ((Nilishuhudia ‘Iyd pamoja na ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaah ‘anhu) akasema: Siku hizi mbili, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amekataza kuzifunga: Siku ya kufungua kwenu kutokana na Swiyaam yenu, na Siku nyingine mnakula ndani yake kutokana na nusuki zenu [Hijja])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1990) na Muslim (1137)]
Na toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhwiya Allaah ‘anhu): ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amekataza kufunga siku mbili: Siku ya Al-Fitwr na Siku ya Kuchinja)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1991) na Muslim (1138)]
3- Masiku ya Tashriyq
[Ni masiku matatu baada ya Siku ya Kuchinja (Siku ya ‘Iyd Al-Adhwhaa), nayo ni Siku ya pili, ya tatu na ya nne ya ‘Iyd Al-Adhwhaa]
Haijuzu kuyafunga masiku haya Swawm ya Sunnah kwa kauli ya ‘Ulamaa wengi. Ni kwa Hadiyth ya Nubayshah Al-Hadhliy aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam amesema):
((أيام التشريق أيام أكل وشرب))
((Masiku ya Tashriyq ni masiku ya kula na kunywa)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1141)]
Na toka kwa Abu Murrah mwachwa huru wa Ummu Haaniy: ((Ni kuwa yeye aliingia pamoja na ‘Abdullaah bin ‘Amri kwa baba yake ‘Amri bin Al-‘Aaswiy, akawasogezea chakula akisema: Karibu. Akasema mimi nimefunga. ‘Amri akasema: Kula, kwani haya ndio masiku ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anatuamuru tuyalie vyakula, na anatukataza kuyafunga)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2418) na Ahmad (4/197)]
Lakini, Hujaji ambaye hakupata mnyama wa kuchinja anaruhusiwa kufunga katika Masiku haya kama tutakavyoeleza mbeleni. Toka kwa ‘Aaishah na Ibn ‘Umar wamesema: ((Haikuruhusiwa katika Masiku ya Tashriyq kuyafunga ila kwa ambaye hakupata mnyama wa kuchinja)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1997-1998)]
4- Kufunga Siku ya Ijumaa pweke
Haijuzu kufunga Siku ya Ijumaa ila kwa mtu aliyefunga siku moja kabla yake, au siku baada yake, au alikuwa anafunga siku na anakula siku nyingine na Swawm yake ikasadifiana na Ijumaa, basi hakuna ubaya.
Toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((لا يصم أحدكم يوم الجمعة إلا أن يصوم قبله أو يصوم بعده))
((Asifunge mmoja wenu Siku ya Ijumaa isipokuwa akifunga kabla yake au akifunga baada yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1985) na Muslim (1144)]
Na toka kwa Juwayriyah bint Al-Haarith (Radhwiya Allaah ‘anhaa): ((Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliingia kwake Siku ya Ijumaa na yeye [Juwayriyah] amefunga akamuuliza: Je ulifunga jana? Akasema: Hapana. Akasema: Unataka kufunga kesho? Akasema: Hapana. Akasema: Basi fungua)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1984) na Muslim (1143)]
Na haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Abu Haniyfah na Maalik wamekhalifu hili wakisema kuwa hakuna ukaraha. [Haashiyat Ibn ‘Aabidiyna (3/336), Al-Muwattwa (1/330), Sharhu Muslim (3/210) na Al-Mughniy (4/427)]
Mahanafii wametoa dalili kwa Hadiyth ya Ibn Mas’uwd: ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anafunga siku tatu za mwanzo wa kila mwezi, na ni mara chache mno anafungua Siku ya Ijumaa)). [Isnaad yake ni laini. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2450), At-Tirmidhiy (742), An-Nasaaiy (2367), Ibn Maajah (1725) kupitia kwa ‘Aaswim toka kwa Zarr bin Hubaysh toka kwa Ibn Mas’uwd. Riwaya ya ‘Aaswim toka kwa Zarr ina maneno]
Dai hili linajibiwa na majibu mbalimbali. Kati ya majibu hayo ni kuwa linaloonekana zaidi ni kwamba Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, na hata tukijalia kuwa ni Swahiyh, itachukulika kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anafunga siku moja kabla yake au baada yake pamoja nayo, na dalili haitimii kwa kuwepo uwezekaniko bali uhakika. [At-Talkhiysw (2/216) na Subulus Salaam (2/347)]
Isitoshe, hiki ni kitendo na ile ni kauli, na kauli inatangulizwa kabla ya kitendo kama kuna mgongano na kutowezekana kuoanishwa.
Ama Maalik, -Rahimahul Laah- yeye katazo halijamfikia, na aliyejua hujjah hutangulizwa kabla ya ambaye hakujua.
Faida
Siku ya Ijumaa ikisadiafiana na Siku ya ‘Arafah, basi hakuna ubaya kuipwekesha kwa Swawm, kwani katazo linahusiana na kuikusudia Siku yenyewe ya Ijumaa kwa Swawm. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi. [Sharhu Al-‘Umdah (2/6532) na Az Zaad (2/86)]
5- Kufunga Siku ya Shaka
Haijuzu kupokelewa Ramadhwaan kwa kufunga siku moja au mbili kwa nia ya akiba kwa Ramadhwaan, lakini hii ni kwa yule ambaye hakusadifu ada yake, au akawa ameunganisha na siku za kabla yake. Kama hakuunganisha wala hakusadifu ada yake, basi ni haramu. [Ni kama kuwa ada yake kufunga siku moja na kula nyingine, au kufunga siku za jumatatu na alkhamisi na kadhalika]
Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliyesema:
((لا يتقدمن أحدكم رمضان بصوم يوم ولا يومين، إلا أن يكون رجل كان يصوم صومه، فليصم ذلك اليوم))
((Asiitangulie kamwe mmoja wenu Ramadhwaan kwa kufunga siku moja au siku mbili, isipokuwa awe mtu alikuwa anafunga Swawm yake, basi na aifunge siku hiyo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1914) na Muslim (1082)]
Na toka kwa ‘Ammaar bin Yaasir amesema: ((Aliyefunga siku ambayo ameifanyia shaka, basi amemwasi Abul Qaasim)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2334), At-Tirmidhiy (681), An-Nasaaiy (4/153) na Ibn Maajah (1645)]
6- Swawm ya Mwaka Mzima
Toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipopata habari kuwa yeye anaandamisha Swawm bila kukatiza akamwambia:
((لا صام من ص
ام الأبد، لا صام من صام الأبد، لا صام من صام الأبد))
((Hakufunga aliyefunga siku zote, hakufunga aliyefunga siku zote, hakufunga aliyefunga siku zote)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1977) na Muslim (1159)]
Na katika Hadiyth ya Abu Qataadah: ‘Umar alisema: Ee Rasuli wa Allaah! Vipi kuhusu anayefunga mwaka mzima?: Akasema:
((لا صام ولا أفطر))
((Hakufunga wala hakula)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1162)]
Ni makruhu mtu kufunga mwaka mzima, hata kama hatohisi uzito au udhoofu, na hata kama hakufunga masiku yaliyokatazwa kuyafunga. Akiyafunga basi ni haramu pia. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
Je kuna uhalali wa kufunga Rajab?
Hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) wala kwa Swahaba Wake inayozungumzia kuhusu fadhla ya kufunga Rajab. Hadiyth zote zinazozungumzia fadhla hizo ni Dhwa’iyf, bali ni za kutunga na za uongo. [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/290), Latwaaiful Ma’aarif (uk. 228), na Subulul Jarraar (2/143)]
Hivyo, haijuzu kuweka azima maalum ya kufunga Rajab au kuufanya mwanzo wake spesheli kwa Swawm. ‘Umar alikuwa anawapiga watu wanaoifunga. Toka kwa Kharshah bin Al-Hurr amesema: ((Nilimwona ‘Umar anapiga viganja vya watu katika Rajab mpaka wanaviweka kwenye madeste, na anawaambia: Kuleni, hakika huu ni mwezi ambao watu wa ujahili walikuwa wanautukuza)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (3/102) na Ibn Kathiyr katika Musnad Al-Faaruwk (1/285).
Na toka kwa Muhammad bin Zayd amesema: ((Ibn ‘Umar alikuwa anapowaona watu na wanayoyaandaa kwa ajili ya Rajab, basi anachukia hilo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (3/102)]
Na toka kwa ‘Atwaa amesema: ((Ibn ‘Abbaas alikuwa anakataza kufunga Rajab yote ili isifanywe ‘Iyd)). [Hadiyth Swahiyh. Imekhatijiwa na ‘Abdul Razzaaq (7854)]
Na baadhi ya Wanachuoni wamestahabisha kufunga Rajab kwa kuwa ni katika Miezi Mitukufu. [Al-Majmuw’u (6/386), Muqaddimaat Ibn Rushd (1/242) na Nayl Al-Awtwaar (4/293)]
Ninasema: “Allaah Ta’alaa Ameitaja Miezi Mitukufu kimahususi na Amekataza kufanya dhulma ndani yake kutokana na utukufu wake ingawa dhulma imekatazwa nyakati zote. Allaah Ta’aalaa Anasema:
((إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللَّـهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّـهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ۚذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ ۚ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ ۚ وَقَاتِلُوا الْمُشْرِكِينَ كَافَّةً كَمَا يُقَاتِلُونَكُمْ كَافَّةً ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ))
((Hakika idadi ya miezi mbele ya Allaah ni kumi na mbili katika hukmu ya makadirio ya Allaah, (tangu) siku Aliyoumba mbingu na ardhi. Kati ya hiyo iko minne mitukufu. Hivyo ndiyo Dini iliyo nyoofu. Basi msijidhulumu humo nafsi zenu, na piganeni vita na washirikina wote kama wao wanavyokupigeni vita nyote. Na jueni kwamba Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa)). [At-Tawbah (9:36]
Basi hapa imekatazwa kufanya madhambi katika miezi hii kutokana na utukufu wake kwa Allaah Ta’aalaa, na kwamba adhabu inaweza kuwa maradufu kwa madhambi, kama ambavyo malipo huongezwa kwa ‘amali njema. Lakini je, hii ina maana kwamba Miezi hii tu ihusishwe kwa Swawm kati ya miezi mingine iliyobaki, na hasa tukizingatia kuwa hakuna kuhusiana na hili Hadiyth yoyote Swahiyh toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), bali Hadiyth moja tu Dhwa’iyf isemayo kwamba Rasuli alimwambia mtu toka kabila la Baahil:
((صم من الحرم واترك))
((Funga katika Miezi Mitukufu na wacha))? [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2428), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (2743) na Ahmad (5/28)]
Isitoshe, tafsiyr ya Aayah ina picha nyingine, nayo ni kuwa muradi wa Kauli Yake Ta’aalaa:
فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ
Basi msijidhulumu humo nafsi zenu,
Msiyageuze ya haramu ya miezi hii kuwa halali, wala ya halali kuwa haramu. [Tafsiyr At-Twabariy (6/366)]
Hivyo tunasema, lililothibiti ni kufunga Mwezi wa Muharram kama tulivyobainisha nyuma. Ama Swiyaam ya Rajab na kuufanya mwezi huu kuwa mahsusi kwa funga –na hasahasa pamoja na kuitakidi ubora wake- basi haijuzu.
Lakini kama atafunga baadhi ya masiku ya mwezi huu bila kuwa mwenye kufanya matukuzo ya kijahiliya, na bila kulifanya kuwa hilo ni jambo la lazima, au akatenga mahususi baadhi ya siku zake akafululiza kuzifunga, au nyusiku zake akafululiza kusimama kuswali akiwa na uhakika kuwa hayo ni Sunnah, basi hakuna ubaya. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi. [Angalia Tabyiynul ‘Ajiyb bimaa warada fiy fadhwli Rajab cha Al-Haafidhw Ibn Hajar (uk 70)]
Hukmu ya kuipwekesha Jumamosi kwa Swawm tu
Toka kwa ‘Abdullaah bin Busri toka kwa dada yake kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((لا تصوموا يوم السبت إلا فيما افترض عليكم، وإن لم يجد أحدكم إلا لحاءـ عنبة أو عود شجرة فليمضغه))
((Msifunge Siku ya Jumamosi isipokuwa lile mlilofaradhishiwa, na kama mmoja wenu hakupata isipokuwa gome la mzabibu au kijiti cha mti, basi alitafune)). [Maimamu wamesema ina kasoro. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2421), At-Tirmidhiy (744), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (2762), Ibn Maajah (1726) na Ahmad (6/368). Maalik amesema ni Hadiyth ya uongo. Abu Daawuwd amesema ni Mansuwkh. Al-Haafidh kasema ni Mkorogeko (Mudhwtwarib) [Iliyoelezwa kwa riwaya mbili zinazogongana]. At-Twahaawiy kasema ni Shaadh [iliyoelezewa na mmoja mwenye kuaminika tofauti na wengi wenye kuaminika], na pia Sheikh wa Uislamu na wengineo. Nimeihakiki katika maelezo yangu kuhusu Sharhu Al-Mandhwuwmat Al-Bayquwniyyah cha Ibn ‘Uthaymiyn (uk 24)]
‘Ulamaa wametofautiana kuhusiana na fiqhi ya Hadiyth hii katika kauli mbili:
Ya kwanza:
Inajuzu kufunga Swawm ya Sunnah Siku ya Jumamosi hata kwa kuipwekesha. Ni madhehebu ya Maalik. Na inafahamiwa kutokana na maneno ya Ahmad, na imekhitariwa na Ibn Taymiyyah na Ibn Al-Qayyim. [Al-Inswaaf 3/347), Iqtidhwaau As-Swiraatw Al-Mustaqiym (2/575) na Mukhtaswar As-Sunan (3/298)].
Na hawa wamesema Hadiyth ni Dhwa’iyf na wakaleta badala yake Hadiyth Swahiyh zinazohimizia kufunga ‘Arafah, Sita Shawwaal, ‘Aashuwraa, Siku Tatu Nyeupe, na kufunga siku moja na kula siku nyingine. Hivyo ni lazima siku moja kati ya masiku haya isadifiane na Jumamosi!!
Vile vile Hadiyth ya kufunga siku moja kabla ya Ijumaa au siku moja baada yake, na kauli ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa Juwayriyyah alipofunga Siku ya Ijumaa:
((أتريدين أن تصومي غدا؟))
((Je wataka kufunga kesho?))… na yote haya tushayaeleza.
Ya pili:
Ni makruhu kuipwekesha Jumamosi kwa Swawm. Ni madhehebu ya Jumhuri; Hanafiy, Shaafi’iy na Hanbal. [Al-Majmuw’u (6/440), Al-Badaai’u (2/79) na Al-Mughniy (4/428)]
Wameichukulia Hadiyth hii kuwa inakataza kuipwekesha Jumamosi kwa Swawm kwa kuwa kufanya hivyo ni kujishabihisha na Mayahudi. Wamelitilia nguvu hili kutokana na yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas ya kwamba Ummu Salamah alisema: ((Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akikithirisha zaidi kufunga kati ya masiku siku ya Jumamosi na siku ya Jumapili)). Alikuwa anasema:
((إنهما عيدان للمشركين وأنا أريد أن أخالفهم))
((Hakika siku hizi mbili ni sikukuu kwa Mapagani, na mimi nataka kwenda kinyume nao)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (2776), Ahmad (6/323) na wengineo kwa Sanad Dhwa’iyf]
Ninasema: “Ama Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Busr, tumeona Maimamu wengi wameikosoa. Na juu ya msingi huo, hakuna ubaya kuifunga Jumamosi na hususan ikisadifiana na siku ambayo imesuniwa kisharia kuifunga. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
Ni makruhu kufunga mfululizo bila kupumzika
Ni makruhu kuandamisha Swawm na kufululisha masiku bila kula au kula daku. Ni kutokana na neno lake Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((إياكم والوصال)) -قالها ثلاث- قالوا: إنك تواصل يا رسول الله؟ قال: ((إنكم لستم في ذلك مثلي، إني أبيت يطعمني ربي ويسقيني، فاكلفوا من الأعمال ما تطيقون))
((Hadharini na kufunga bila kufungua)) –alilisema mara tatu- Wakasema: Hakika wewe unafunga bila kufungua ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Hakika nyinyi hamko kama mimi katika hilo. Hakika mimi ninalala na Mola wangu Ananilisha na Ananinywesha, basi bebeni katika ‘amali mnazoziweza)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1966) na Muslim (1103) toka kwa Abu Hurayrah]
Lakini, ikiwa hakuna tabu au uzito, basi hakuna ubaya kuendelea na Swawm mpaka wakati wa daku tu. Ni kwa neno lake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((لا تواصلوا، فأيكم أراد أن يواصل فليواصل إلى السحر))
((Msiendelee na Swawm bila kufungua, na yeyote akipenda kuendelea na Swawm bila kufungua, basi aendelee hadi daku)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1967) na Abu Daawuwd (2344)]