17-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Laylatul Qadr Na Fadhila Zake
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swiyaam
17-Laylatul-Qadr Na Fadhila Zake
Allaah Ta’aalaa Amesema:
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾
Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatil-Qadr (usiku wa Qadar).
وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ ﴿٢﴾
Na nini kitakachokujulisha ni nini huo Laylatul-Qadr?
لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾
Laylatul-Qadr ni mbora kuliko miezi elfu.
تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ ﴿٤﴾
Wanateremka humo Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Rabb wao kwa kila jambo.
سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ ﴿٥﴾
Amani mpaka kuchomoza Alfajiri. [Al-Qadr: 1-5]
Suwrat hii Tukufu imepangilia fungu la fadhwaail za Usiku huu kama ifuatavyo: [At Tas-hiyl litaawiyl At-Tanziyl cha Sheikh wetu Mustwafaa Al-‘Adawiy (Juz-u ‘Amma (2/448)]
1- Kwamba Allaah ‘Azza wa Jalla Ameiteremsha Qur-aan katika Usiku huu kama Alivyosema Ta’aalaa:
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ﴿٣﴾
Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika usiku uliobarikiwa, hakika Sisi daima ni Wenye kuonya. [Ad-Dukhaan (44:3)]
2- Kwamba Allaah ‘Azza wa Jalla Ametukuza shani yake kwa kuutaja na kwa Neno Lake:
((وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ))
Na nini kitakachokujulisha ni nini huo Laylatul-Qadr?
3- Kwamba ‘ibaadah ndani ya Usiku huu inashinda ‘ibaadah katika miezi elfu moja isiyo na Laylatul Qadr ndani yake.
4- Kwamba Malaika Huteremka makundi kwa makundi katika Usiku huu. Imesemwa: Wanateremka na rahmah nyingi, baraka nyingi na utulivu. Imesemwa: Wanateremka na kila jambo ambalo Allaah Amelihukumu na Amelikadiria kwa mwaka huo kama Alivyosema:
فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ﴿٤﴾
Katika (usiku) huo hupambanuliwa kila jambo la hikmah.
أَمْرًا مِّنْ عِندِنَا ۚ إِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ﴿٥﴾
Ni amri kutoka Kwetu, hakika Sisi ndio Wenye kutuma (Rusuli). [Ad-Dukhaan (44:4,5]
5- Kwamba amani na utulivu hutanda katika Usiku huu kwa watu wa iymaan, na salamu za Malaika huandamana juu yao ndani ya Usiku huu.
6- Toka kwa Abu Hurayrah toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((من صام رمضان إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه، ومن قام ليلة القدر إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه))
((Mwenye kufunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, hughufiriwa madhambi yake yaliyotangulia. Na mwenye kusimama [kufanya ‘ibaadah katika] Laylatul Qadr kwa iymaan na kutarajia malipo, hughufiriwa madhambi yake yaliyotangulia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2014) na Muslim (759)]
Usiku Huu Ni Upi [Unakuwa Tarehe Ngapi]?
Hakuna shaka yoyote kwamba Laylatul Qadr iko katika Ramadhwaan kwa Neno Lake Ta’aalaa:
((إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ))
((Hakika Sisi Tumeiteremsha [Qur-aan] katika Laylatil-Qadr [usiku wa Qadar])). [Al-Qadr (97:1)]
..pamoja na Kauli Yake Ta’aalaa:
((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ ))
((Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan)). [Al-Baqarah (2:185)]
Ama kuuainisha, Al-Haafidh Ibn Hajar amesema: “’Ulamaa hakika wamekhitalifiana makhitilafiano mengi sana kuhusu Laylatul Qadr, na tumepata katika hilo zaidi ya kauli 40 katika madhehebu zao”. [Kisha akazitaja kauli hizo na dalili walizotoa watu wake]. [Fat-hul Baariy (4/309 - Salafiyyah].
Na wengi wao wamesema unapatikana katika Kumi la Mwisho la Ramadhwaan kwa Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriyy kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘ alayhi wa aalihii wa sallam) amesema):
((....فابتغوها في العشر الأواخر))
((..basi upanieni katika Kumi la Mwisho)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2018) na Muslim (1167) toka kwa Abu Sa’iyd[
Na wengi wao pia wamesema unapatikana katika (hesabu ya) witri katika Kumi la Mwisho kutokana na neno lake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((نحروا ليلة القدر في الوتر من العشر الاواخر))
((Itafuteni Laylatul Qadr katika witr ya Kumi la Mwisho)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2017)]
Na wengi wao kadhalika wamesema ni Usiku wa tarehe 27, na hii ni kauli ya kundi la Swahaba. Ubayya bin Ka’ab ameikata kauli hii kuwa haina shaka na ameiapia kama ilivyo katika Swahiyh Muslim. [Swahiyh Muslim (762) na At-Tirmidhiy (3351)]
Ninasema: “Ninaloliona mimi ni kuwa Laylatul Qadr hupatikana katika Kumi la Mwisho, na katika masiku ya witri inakuwa na uhakika zaidi, nayo huhama ndani ya masiku hayo, na haihusiani tu na Usiku wa tarehe 27, kwani yaliyosimuliwa toka kwa Ubayya kuwa ni Usiku wa tarehe 27, hilo ni katika mwaka mmoja tu na haina maana kuwa kila mwaka itakuwa ni 27. Lidulishalo hili ni kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliisadifu Laylatul Qadr Usiku wa tarehe 21 kama ilivyo katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwakhutubia na kuwaambia:
((إني أريت ليلة القدر ثم أنسيتها، فالتمسوها في العشر الأواخر في الوتر، وإني رأيت أني أسجد في ماء وطين))
((Hakika mimi nilionyeshwa Laylatul Qadr kisha nikasahaulishwa, basi itafuteni katika Kumi la Mwisho katika witr, na hakika mimi nimeona kwamba mimi nasujudu katika maji na udongo))… Abu Sa’iyd amesema: ((Tulipata mvua usiku wa ishirini na moja, na paa la Msikiti likatona maji sehemu anayoswalia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), nikamwangalia na yeye ametoka kwenye Swalaat As-Subh na uso wake umelowa udongo na maji)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2018) na Muslim (1167)]
Na hili ndilo linalodulishwa na jumla ya habari zilizokuja kuhusu hilo. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.
Kufichwa Laylatul Qadr
Bila shaka Laylatul Qadr imefichwa ili waja wajitahidi kufanya ‘ibaadah katika kila usiku wa Ramadhwaan kwa matarajio ya kuwa usiku wowote unaweza kuwa ndio wa Laylatul Qadr. Basi atakayekuwa na habari ya yakini katika usiku wowote, basi ataukeshea kwa ‘ibaadah, na anayetaka kuusadifu na kuupata kiuhakika, basi ni juu yake amshukuru Allaah kwa kujifaraghisha Kwake kwa ‘ibaadah katika Mwezi wote. Na hii ndio siri ya kutotajwa siku maalum ya kupatikana kwake. Na huenda hili linaashiriwa na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((إني خرجت لأخبركم بليلة القدر، فتلاحى فلان وفلان، فرفعت [يعنى: رفع علمها]، وعسى أن يكون خيرا لكم، فالتمسوها...))
((Hakika mimi nilitoka niwahabarisheni [siku maalum ilioainishwa ya] Laylatul Qadr, fulani na fulani wakazozana, basi ikaondoshwa [yaani, kuijua kwake kukaondoshwa], na huenda ikawa kheri kwenu, basi utafuteni…)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2023)]
Vipi Muislamu anajitahidi kuipata Laylatul Qadr?
Mwenye kukoseshwa asiupate Usiku huu wa Baraka, basi amekoseshwa kheri yote, na hakoseshwi kheri yake isipokuwa mkoseshwa. Na kwa ajili hiyo, inatakikana kwa Muislamu mwenye pupa ya kumfanyia twa’a Allaah, aukeshe Usiku huo akiwa na iymaan na tamaa ya kupata malipo yake makubwa, na ajitahidi zaidi katika Kumi la Mwisho kufuata alivyofanya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Toka kwa ‘Aaishah amesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anajitahidi asivyojitahidi katika masiku mengine)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1174)]
Anapaswa akithirishe Swalaah katika Usiku huu, ajitenge na wanawake na awahimize ahli wake kufanya twa’a ndani yake. Toka kwa ‘Aaishah amesema: ((Alikuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) linapoingia Kumi [la Mwisho], hujiandaa na kujitahidi ukomo wa jitihada, hukesha usiku wake, na huwaamsha wakeze)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2024) na Muslim (1174)]
Na haya yote ili awe na uhakika wa kupata yaliyoahidiwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliyesema:
((من صام رمضان إيمانا واحتسابا، غفر له ما تقدم من ذنبه))
((Atakayefunga Ramadhwaan kwa iymaan na kutarajia malipo [toka kwa Allaah], hughufiriwa dhambi zake zilizotangulia)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]
Du’aa katika Laylatul Qadr
Imestahabiwa kuomba du’aa katika Usiku huo na kukithirisha na hususan du’aa iliyokuja katika Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema:
((يا رَسُولَ اللهِ، أرَأيْتَ إنْ عَلِمْتُ أيُّ لَيْلَةٍ لَيْلَةُ الْقَدْرِ، مَا أقُولُ فِيها؟ قَالَ: ((قُولي: اللَّهُمَّ إنَّكَ عَفُوٌّ كَرِيمٌ تُحِبُّ العَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي)).
((Ee Rasuli wa Allaah! Nieleze ikiwa nitajua usiku fulani ndio wa Laylatul Qadr, niseme nini?” Akasema: ((Sema:
اللَّهُمَّ إنَّكَ عَفُوٌّ كَرِيمٌ تُحِبُّ العَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي
Ee Allaah! Hakika wewe ni Mwingi wa kufuta kabisa madhambi, Mwingi wa ukarimu, Unapenda kufuta kabisa madhambi, basi Nifutie kabisa dhambi zangu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (3760) na Ibn Maajah (3850)]
Alama za Laylatul Qadr
Laylatul Qadr ina alama ambazo hujulikana kwazo. Kati ya alama hizo ni zile ambazo hupatikana katika Usiku wenyewe kama:
1- Anga kuwa safi na upepo kutulia. Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: “Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((ليلة القدر ليلة سمحة، طلقة لا حارة ولا باردة، تصبح الشمس صبيحها ضعيفة حمراء))
((Laylatul Qadr ni Usiku mtulivu mwangavu, si wa joto wala baridi, jua asubuhi yake hupambauka dhaifu jekundu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Twayaalsiy (349), Ibn Khuzaymah (3/231) na Al-Bazzaar (1034)]
2- Utulivu na ushwari ambao Malaika huteremka nao. Mwanadamu huhisi utulivu wa moyo, hukikuta kifua chake kikikunjuka, na huhisi ladha ya ‘ibaadah katika Usiku huu ambayo haipati katika masiku mengineyo.
3- Mtu anaweza kuiona usingizini kama ilivyotokea kwa baadhi ya Swahaba.
Kati ya alama ambazo huonekana baada ya Usiku huo kupita ni kama:
4- Jua kuchomoza asubuhi yake likiwa safi bila miale. Toka kwa Ubayya bin Ka’ab kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((صبيحة ليلة القدر تطلع الشمس لا شعاع لها، كأنها طست، حتى ترتفع))
((Asubuhi ya Laylatul Qadr jua huchomoza bila miale [umbo lake] mithili ya kikaangio mpaka linyanyuke)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1174)]
Angalizo
Watu wa kawaida wana visa vingi sana vya uongo vilivyojazwa chumvi kuhusiana na Laylatul Qadr pamoja na itikadi nyingi mbovu. Kati ya itikadi hizo ni kuwa katika Usiku huo miti husujudu, majengo hulala, maji chumvi hugeuka maji tamu, mbwa hawabweki na mengineyo yaliyo bayana ubovu wake na ubatilifu wake.