03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Je, Ni Waajib Kuharakia Kuhiji Au Mtu Anaweza Kuchelewesha?

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

03-Je, Ni Waajib Kuharakia Kuhiji Au Mtu Anaweza Kuchelewesha?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Jumhuri ya ‘Ulamaa; Abu Haniyfah – katika riwaya mbili swahiyh zaidi -, Abu Yuwsuf, Maalik na Ahmad wanasema kuwa mwenye kutamalaki masharti ya wajibu wa Hajji – ambayo yatakuja kufafanuliwa - na faradhi ya Hajji ikamtimilia, basi huyo ni lazima ahiji bila kukawia, na kama atachelewesha basi atapata madhambi. [Al-Mughniy 3/241), Al-Majmuw’u (7/85) na Al-Furuw’u (3/242)]

 

Wamelitolea dalili hilo kwa:

 

1-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ))

((Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu)). [Aal-‘Imraan (3:97]

 

2- Kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((أيها الناس إن الله كتب عليكم الحج فحجوا))

((Enyi watu! Hakika Allaah Amewafaradhishieni Hajji, basi hijini)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma]

 

Asili ya jambo lolote ni kulifanya haraka madhali halikutokea la kulizuia. [Kwa sababu ya hili, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikasirika –katika Vita vya Al-Hudaybiyyah - wakati alipowaamuru Swahaba kuvunja Ihraam, nao wakajivuta vuta kama ilivyo elezwa na Al-Bukhaariy (2731)]

 

3- Neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((من أراد الحج فليتعجل))

((Anayekusudia kuhiji, basi afanye haraka)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Ahmad (1737), Ibn Maajah (2883), At-Twabaraaniy (18/287-296), Al-Bayhaqiy (4/340) na wengineo kupitia kwa Abiy Israaiyl Al-Mullaaiy toka kwa Fudhwayl bin ‘Amri toka kwa Ibn Jubayr toka kwa Ibn ‘Abbaas toka kwa Al-Fadhwl. Abu Israaiyl ana udhaifu na ana makosa mengi. Maharaan Abu Swafwaan amemfuatilia -mfuatilio pungufu- toka kwa Ibn ‘Abbaas. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1732), Ibn Abiy Shaybah (3/227), Ahmad (1871), Al-Daaramiy (1984), Al-Bayhaqiy (4/339) na wengineo. Lakini Mahraan hajulikani, ufuatiliaji wake hauna faida. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi]

 

4- Hadiyth Marfuw’u isemayo:

 

((من ملك زادا وراحلة تبلغ إلى بيت الله ولم يحج فلا عليه أن يموت يهوديا أو نصرانيا))

((Mwenye kumiliki masurufu (fedha) na mnyama (kipando) atakayemfikisha kwenye Nyumba ya Allaah, naye asihiji, basi hana budi afe akiwa Myahudi au Mnaswara)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (812)]

 

Lakini kwa upande mwingine, Ash-Shaafi’iy, Muhammad bin Al-Hasan, na baadhi ya Masalaf, wanasema hapati madhambi kwa kuchelewesha Hajji –pamoja na uwezo wa kuhiji- lakini kwa sharti aweke niya ya kweli ya kutekeleza nguzo hiyo siku zijazo.

 

Wametoa dalili wakisema kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliikomboa Makkah mwaka wa nane, na hakuhiji isipokuwa mwaka wa kumi. [Na Hajji ilifaradhishwa katika mwaka wa sita, au wa saba, au wa nane, au wa tisa, au wa kumi wa Hijrah kwa mujibu wa makhitalifiano kati ya ‘Ulamaa. Angalia Al-Majmuw’u (7/87) na Zaad Al-Ma’aad (1/175)]

 

Na kama ingekuwa ni waajib kuharakiziwa, basi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) asingelichelewa kulifanya alilofaradhishiwa na hususan haukuwepo udhuru wowote wa dhahiri kama vita au ugonjwa! [Al-Ummu (2/118) na Al-Majmuw’u (7/87)]

 

Na pia kwa vile, akiiahirisha, kisha akaifanya baada ya hapo, hahesabiwi kama anailipa, na hii inadulisha kuwa inafaa kuichelewesha.

 

Kuhusu Aayah Tukufu, wamejibu wakisema kuwa agizo la kuhiji ndani ya Aayah hii halijawekewa mpaka wala kuainishiwa wakati maalum. Hivyo basi, inaswihi kuifanya wakati wowote ule, na ulazima wa kuifanya haraka hauko, kwa kuwa Aayah itawekewa mpaka bila dalili. Aidha, wamesema Hadiyth zote zenye kuamuru kufanya haraka ni Dhwa’iyf.

 

Ninasema: “Kiini cha mvutano hapa ni je, asili ya amri ni kufanya haraka au kuchelewesha? Muhimu baada ya yote, lililo bora zaidi ni kuharakisha badala ya kuchelewesha –pamoja na uwezo wa kuhiji- kiakiba tu, kwa kuwa mtu hajui kama umri utakuwepo mpaka aje ahiji. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

 

 

 

Share