02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Hukmu Ya Hajj
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah
02-Hukmu Ya Hajj
Hajj ni Fardhi ‘Ayn kwa kila aliyebaleghe na mwenye uwezo mara moja katika umri wote. Ni nguzo katika nguzo za Kiislamu, na ufaradhi wake umethibiti katika Qur-aan, Sunnah na Ijma’a.
(a) Katika Qur-aan
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
((وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ))
((Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu)). [Aal-‘Imraan (3:97)]
(b) Katika Sunnah
Kuna Hadiyth nyingi sana zilizosimuliwa – zilizofikia mpaka wa Tawaatur - zinazoelezea uyakini na elimu isiyo na shaka yoyote kuhusu kuthibiti Faradhi hii. [Angalia: At-Targhiyb na At-Tarhiyb (2/211)]
Kati ya Hadiyth hizo ni:
1- Ya Ibn ‘Umar kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((بُني الإسلام على خمس: شهادة أن لا إله إلا الله وأن محمدًا رسول الله، وإقام الصلاة، وإيتاء الزكاة، والحج، وصوم رمضان))
((Uislamu umejengwa juu ya (nguzo) tano: Kushahadia kwamba hapana mungu isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah, Hajj na kufunga Ramadhwaan)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (8), Muslim (16) na wengineo]
2- Ya Abu Hurayrah aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitukhutubia akasema:
((يا أيها الناس، قد فرض الله عليكم الحج فحجوا)) ، فقال رجل: أكل عام يا رسول الله؟ فسكت حتى قالها ثلاثا، فقال رسول الله: ((لو قلت نعم لوجبت، ولما استطعتم...))
((Enyi watu! Hakika Allaah Amewafaradhishieni Hajj, basi hijini)). Mtu mmoja akasema: Je, ni kila mwaka ee Rasuli wa Allaah! Akanyamaza mpaka akaliuliza mara tatu. Rasuli wa Allaah akasema: ((Ningelisema na’am basi ingekuwa lazima, na msingeliweza…)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1337)]
(c) Katika Ijma’a
Umma wote umekubaliana kuwa Hajj ni waajib – kwa mwenye kuweza - mara moja tu katika umri wote. [Hii ikiwa hakuweka nadhiri ya kwamba atahiji, na kama ataweka nadhiri hiyo, basi ni waajib vile vile]
Na Hajj ni katika mambo yanayojulikana kwa ulazima katika Diyn, anakufuru mwenye kupinga. [Al-Mughniy (3/217) na Al-Majmuw’u (7/13)]