14-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Marufuku Za Ihraam
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah
14-Marufuku Za Ihraam
Ni mambo ambayo Allaah Amemkataza aliyehirimia kuyafanya, na Akamharamishia madhali yuko kwenye Ihraam. Marufuku hizi ziko vigawanyo viwili.
(a) Marufuku Inayoharibu Hajj
Ni kujimai kabla ya tahalluli ya kwanza (kabla ya kutupia Jamaratul Aqabah kwa mujibu wa kauli yenye nguvu zaidi). Hii ni marufuku yenye madhambi makubwa zaidi na yenye athari mbaya zaidi kwa ‘amali ya Hajj. Allaah Amesema:
((فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ))
((Na atakayekusudia kuhiji (akahirimia), basi asifanye tendo la ndoa wala ufasiki wala mabishano katika Hajj)). [Al-Baqarah (2:197)]
Imepokewa kauli swahiyh toka kwa Ibn ‘Abbaas, Ibn ‘Umar na Qataadah kuwa maana ya الرفث katika Aayah hii ni kujimai. [Angalia athari hizi katika Tafsiyr At-Twabariy (4/125-126) kwa Asaaniyd Swahiyhah]
Wengine wamesema الرفث ni kumzungumzisha mwanamke maneno yasiyolaiki kuhusiana na jimai na mfano wake. Ibn Jariyr amekhitari kuwa neno ni jumuishi na linakusanya maana hizo zote.
Ibn Qudaamah amesema: “Ama kufisidika Hajj kwa kujimai kwenye utupu, hili halina mvutano”. [Al-Mughniy (3/334), na Al-Ijma’a cha Ibn Al-Mundhir (uk. 1444)]
Ibn Al-Mundhir kasema: “ ’Ulamaa wote wamekubaliana kuwa Hajj haifisidiki kwa kufanya jambo lolote baada ya kuhirimia isipokuwa jimai tu”.
Ninasema: “Hapa kuna mambo kadhaa:
La kwanza:
Ama kutolea dalili Aayah hii Tukufu kwa kusema kwamba maana ya الرفث hapo ni jimai, sisi tunaona kuwa shabaha kuu inayolengwa hapo ni kuzuia jimai isifanywe, na sio kwamba jimai inafisidi Hajj. Na kama si hivyo, basi ingelazimu kusema kuwa mabishano pia yanafisidi Hajj, na hakuna aliyesema hilo [isipokuwa Ibn Hazm]. [Ar-Rawdhwat An-Nadiyyah (1/254)]
La pili:
Hakuna katika suala hili Hadiyth yoyote Swahiyh Marfuw’u toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam).
La tatu:
Ijma’a iliyonukuliwa na Ibn Al-Mundhir na wengineo, je inatenguka kwa aliyoyanukuu Ash-Shawkaaniy katika kitabu chake cha Nayl Al-Awtwaar toka kwa Daawuwd Adh-Dhwaahiriy? Kwa msingi kwamba Ijma’a hii haijajikita kwa nguvu moja kwenye jambo lenyewe mbali na khitilafu ambazo zinaweza kupatikana katika mchanganuo wake.
Ibn ‘Abbaas na Abu Haniyfah wamesema: “Hajj haitenguki kwa kujimai baada ya [Kusimama] ‘Arafah”.
Na Maalik amesema: “Akijimai Yawm An-Nahr (tarehe kumi) kabla ya kutupia Jamarah, Hajj yake itabatilika, na kama atajimai Yawm An-Nahr baada ya kutupia Jamarah, basi Hajj yake haibatiliki. Na kama atajimai baada ya Yawm An-Nahr kabla ya kutupia Jamarah, basi Hajj yake haibatiliki?”
Ash-Shaafi’iy kasema: “Akijimai katika kipindi cha baina ya Kuhirimia na Kutupia Jamaratul Aqabah, basi Hajj yake itaharibika. Na kama atajimai baada ya Kutupia, basi Hajj yake ni kamili”.
Kisha wamekhitalifiana makhitalifiano mengi kuhusiana na linalompasa kufanya mtu aliyejimai kama itakavyokuja mbeleni. [Angalia Al-Muhallaa (7/189)]
La nne: Ni ipi adhabu ya mwenye kujimai? Nini afanye?
Mtu akimwingilia mkewe kabla ya tahalluli ya kwanza, atapata madhambi na Hajj yake itabatilika kwa mujibu wa kauli ya ‘Ulamaa wengi. Atapaswa kuikamilisha Hajj yake –pamoja na kuharibika kwake- kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:
وَأَتِمُّوا الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلَّـهِ
((Na timizeni Hajj na ‘Umrah kwa ajili ya Allaah)).
Na wote wawili (mke na mume) ni lazima wahiji mwaka ujao pamoja na kuchinja (ngamia).
Hivi ndivyo walivyofutu Ibn ‘Umar, Ibn ‘Amri na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhum). Toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake amesema: ((Mtu mmoja alimwendea Ibn ‘Umar akamuuliza kuhusu mtu aliyehirimia akamwingilia mkewe. [Ibn ‘Umar] akamwelekeza aende kwa ‘Abdillaah bin ‘Amri, naye akamwambia kuwa Hajj yake imebatilika. Akauliza: Je, akae asihiji tena? Akasema hapana, bali atoke pamoja na watu na afanye kama wanavyofanya. Na kama mwaka ujao utamkuta, basi ahiji na achinje. Wakarudi wote wawili kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar wakamweleza. Tukatuma mtu kwenda kwa Ibn ‘Abbaas amuulize. Naye akamwambia yale yale aliyoyasema Ibn ‘Umar. Akarudi kwake akamweleza, na mtu yule akamuuliza: Na wewe unasemaje? Akasema: Kama walivyosema)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (1/4/142) na Al-Bayhaqiy (5/167)]
Lakini Adh-Dhwaahiriyyah wanaona kuwa jimai huharibu ‘amali za Hajj na huzibatilisha, na mfanyaji ataondoka na hatoendelea na Hajj yake, kwa kuwa ‘amali yenyewe ishaharibika. Wamesema: “Imepokelewa Hadiyth Swahiyh toka kwa Rasuli wa Allaah (Swallah Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuwa Hajj ni mara moja tu. Hivyo basi, mwenye kumlazimisha aendelee na Hajj hiyo mbovu, kisha amlazimishe tena afanye Hajj nyingine (mwakani), basi anakuwa amemlazimisha Hajj mbili, na hii ni kinyume na agizo la Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)”. [Al-Muhallaa (7/189) na zinazofuatia)]
Baadhi ya Taabi’iyna wamesema kuwa atafanya tahalluli kwa kufanya ‘Umrah na atalipa. Wanaifanya kuwa ngazi ya mtu ambaye amepitwa na Kisimamo cha ‘Arafah. Hivyo atatahallal kwa ‘Umrah na kuvua Ihraam.
Ninasema: “Hakuna shaka kuwa lililo na nguvu zaidi ni kauli sahihi waliyosema ‘Ulamaa watatu Swahaba na kutekelezwa na Wanachuoni wengi ya kuwa Hajj ya mwenye kujimai huharibika na anawajibika kuendelea na Hajj yake. [Imehadithiwa pia kuharibika Hajj kutokana na kujimai toka kwa ‘Umar, ‘Aliyy na Abu Hurayrah kwa Asaaniyd Dhwa’iyf].
Na kuwafuata Swahaba katika hili ni bora zaidi kutokana na ukina wa ufahamu wao na usahihi wa rai zao, na hususan pakizingatiwa kuwa hilo ni la akiba zaidi katika dini. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.
Faida kadhaa:
1- Ikiwa mwanamke atalazimishwa kufanya jimai, basi Hajj yake ni sahihi na hakuna fidia juu yake kinyume na mume wake kwa mujibu wa kauli mbili sahihi za ‘Ulamaa. [Angalia Al-Majmuw’u (7/404)]
2- Akijimai baada ya tahalluli ya kwanza na kabla hajatufu na kusai, basi Hajj yake haiharibiki lakini atapata dhambi. Ni lazima atoke kwenye Ihraam na ahirimie tena upya –akiwa amevaa nguo zake za Ihraam (izaar na ridaa)- ili atufu Twawaafu ya Ifaadhwah akiwa amehirimia, kwa kuwa aliharibu sehemu iliyobaki ya Ihraam yake. Hivyo ni lazima aanze upya na atoe fidia. [Ash-Sharh Al-Mumti’u cha Ibn ‘Uthaymiyn (7/184)]
3- Akijimai kabla ya tahalluli ya kwanza kwa kusahau kuwa ameshahirimia [Al-Muhallaa (7/186) na Al-Majmuw’u (7/364)]
Akijimai aliyehirimia kabla ya kutahaluli na ‘Umrah, au kabla ya tahalluli ya kwanza ya Hajj hali ya kuwa amesahau kuwa ameshahirimia, basi kauli sahihi inasema kuwa Hajj yake haiharibiki, na hatotoa kafara yoyote wala kingine chochote. Na hii ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
((وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ))
((Na wala hakuna dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini isipokuwa katika yale yaliyoyakusudia nyoyo zenu)). [Al-Ahzaab (33:5)]
(b) Marufuku Zenye Kufisidi Hajj
1- Mwanaume kuvaa nguo iliyoshonwa
Ni haramu kwa mwanaume kuvaa nguo iliyoshonwa au inayofanana nayo kwa kiasi cha kiungo cha mwili. [Al-Majmuw’u (7/269) na Al-Muhallaa (7/80). Nguo iliyoshonwa haikusudiwi yenye uzi, kwani Sunnah ni kuvaa kipande cha chini na cha juu [izari na ridaa] hata kama vimeshonwa kwa makubaliano ya Maimamu]
Asivae shati, suruali, kilemba, kofia, juba, khufu mbili, soksi mbili, glovu mbili na mfano wake. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba mtu mmoja alisema: Ee Rasuli wa Allaah! Ni nguo zipi anavaa mwenye kuhirimia? Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:
((لا يلبسُ القمص، ولا العَمَائِمَ ، وَلاَ السَّرَاوِيلاَتِ، ولا البَرنس، ولا الخِفَافَ، إلا أحدٌ لا يجِدُ نَعْلَيْنِ، فَلْيَلْبَسْ خُفَّيْنِ، وَلْيَقْطَعْهُمَا أسفلَ من الكعبين، وَلا يَلْبَسْ من الثياب شيئا مَسَّهُ زَعْفَران أوْ وَرْسٌ))
((Asivae nguo yenye mikono [kama kanzu au shati], wala vilemba, wala suruali, wala barnas [vazi linalofunika mwili hadi kichwa], wala khufu isipokuwa mtu ambaye hana viatu, huyo atavaa khufu mbili, na azikate chini ya visigino viwili. Na wala asivae nguo yoyote yenye harufu ya zafarani au wars [aina ya mmea wenye harufu nzuri])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1542) na Muslim (1177)]
Faida
Kivazi hiki kilichoharamishwa kwa mwanaume kinachukulika kwa namna ilivyozoeleka katika kila kivazi. Ikiwa atajizungushia kanzu, au akajitanda juu au akajitanda chini kwa suruali jambo ambalo si la kawaida, basi hakuna tatizo kwa hili, kwa kuwa hapo suruali inakuwa ni kama kipande cha juu na cha chini cha Ihraam (izaar na ridaa). [Al-Majmuw’u (7/270) na Majmuw’u Fataawaa Sheikh Al-Islaam (26/109)]
Asiyepata isipokuwa suruali na khufu mbili
Ambaye hakupata kipande cha juu na cha chini cha Ihraam lakini akapata suruali na khufu mbili –na akazihitajia kutembelea- basi inajuzu kwake kuvaa anachokipata. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: ((Nabiy (Swallah Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitukhutubia ‘Arafaat akisema:
((من لم يجد الإزار فليلبس السراويل، ومن لم يجد النعلين فليلبس الخفين))
((Asiyepata kipande cha chini (izaar), basi avae suruali, na asiyepata viatu basi avae khufu mbili)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1843) na Muslim (1178)]
Hadiyth hii inadulisha kuwa inajuzu kuvaa suruali kama ilivyo –kama hakupata kipande cha chini- na halazimishwi aipasue ili ajitande nayo chini –kama wanavyosema Fuqahaa wa Kihanafiy- na wala hatodaiwa chochote; si fidia wala kingine chochote. Kwa kuwa, lau fidia ingelikuwa wajibu, basi Nabiy angesema hilo. Na haya ni madhehebu ya Jumhuri kinyume na Mahanafiy.
Kama hakupata viatu, atavaa khufu mbili. Lakini je, atazikata –kama ilivyokuja kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Umar? au hatozikata kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas?
Ahmad amesema si lazima azikate, na kauli hii imekhitariwa na Ibn Taymiyah ambaye amesema: “Ni bora ahirimie na viatu viwili ikiwa ni wepesi.. na kama hakupata viatu viwili, basi atavaa khufu mbili, na si lazima azikate chini ya visigino viwili. Kwani Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliamuru kukata mwanzoni, kisha akaruhusu baada ya hapo kuzivaa kama zilivyo huko ‘Arafaat. Kwanza aliruhusu zilizokatwa, kwa kuwa zinakuwa kama viatu kwa kukatwa”.
Wengine wamesema: Kukata khufu mbili ni uharibifu wa mali, nao umekatazwa.
Lakini Jumhuri wamesema ni lazima kukata sehemu iliyo chini ya vifundo viwili vya miguu kwa kuipa nguvu Hadiyth ya Ibn ‘Umar ambayo imegusia kukata chini ya vifundo viwili badala ya Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ambayo haijagusia hilo bali imeacha mlango wazi.
Ninasema: “Na hili ni bora zaidi kuliko la kwanza. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
2- Mwanaume kufunika kichwa chake kwa chenye kushika kichwa
Mwanamume asivae kofia (kibaragashia) wala kilemba na mfano wake. Ni kwa kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika Hadiyth iliyotangulia nyuma kidogo ya Ibn ‘Umar isemayo:
((لا يلبس القمص ولا العمائم))
((Asivae nguo yenye mikono [kama kanzu au shati], wala vilemba)).
Asifunike kichwa chake kwa khimari (ghutrah na mfano wake) kutokana na ujumuishi wa neno lake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuhusiana na Swahaba aliyeangushwa na ngamia wake ‘Arafah akavunjika shingo na kufa:
((ولا تخمروا رأسه))
((Na wala msifunike kichwa chake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1851) na Muslim (1206)]
Na hii ni jumla ya kila kifunikacho. Haisemwi kuwa inahusishwa tu na vilemba pasina vingine vyenye kufunika kichwa, kwani cha jumla hakihusishwi na kimoja katika vipengele vyake isipokuwa katika hali ya kukinzana –kama inavyoelezwa katika taaluma ya Usuwl- na hapa hakuna mkinzano. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
Na kama atakaa kwenye kivuli cha kitu kisichogusana naye kama mwavuli, au gari, au mti na mfano wake, basi hakuna ubaya kwa hilo kama tutakavyokuja kuzungumzia hilo mbeleni.
3- Mwanamke kuvaa niqabu, burqui na glovu mbili
Ni kwa ziada ya yaliyokuja kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Umar iliyotangulia katika kauli yake:
((ولا تنتقب المحرمة، ولا تلبس القفازين))
((Na mwanamke aliyehirimia havai niqabu, wala havai glovu mbili)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1838), Abu Daawuwd (1825), At-Tirmidhiy (833) na An-Nasaaiy (5/133)]
Matamshi haya yana mvutano: Je yamesemwa na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)? Au yapo katika orodha ya semi za Ibn ‘Umar?
Al-Haafidh katika Al Fat-h katilia nguvu la mwisho. [Angalia: Fat-hul Baariy (4/64). Imetiliwa nguvu na Sheikh wetu –Allaah Amhifadhi- katika Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/483)]
‘Ulamaa wamekhitalifiana suala la mwanamke kuvaa niqabu. Jumhuri wamezuia lakini Mahanafiy wamejuzisha. Ni kwa riwaya iliyoko kwa Fuqahaa wa Kishaafi’iy na Kimaalik. [Fat-hul Baariy (4/65)]
Ninasema: “Kwa msingi wa kauli inayokataza mwanamke aliyehirimia kuvaa niqabu, inajuzu kwake kuuteremsha ushungi wake toka kichwani hadi usoni wanapopita wanaume wasio maharimu wake sawasawa ukigusa uso wake au usiguse, kwa kuwa mwanamke kakatazwa niqabu, na kushusha ushungi hakuzingatiwi kama niqabu. Dalili ya hili zitakuja mbeleni, si mbali”.
4- Mwanaume au mwanamke aliyehirimia kutumia manukato mwilini au kwenye nguo
Ni kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar:
((ولا تلبسوا من الثياب شيئا مسّه زعفران أو ورس))
((Na wala msivae nguo yoyote yenye harufu ya zafarani au wars [aina ya mmea wenye harufu nzuri])). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]
Na kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa mhirimiaji aliyevunjwa shingo na ngamia wake:
((لا تحنّطوه، ولا تخمروا رأسه، فإنه يبعث يوم القيامة ملبيا))
((Msimtie manukato, na wala msifunike kichwa chake, kwani hakika yeye atafufuliwa Siku ya Qiyaamah huku akileta Talbiyah)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]
5- Kunyoa nywele za kichwa
Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
((وَلَا تَحْلِقُوا رُءُوسَكُمْ حَتَّىٰ يَبْلُغَ الْهَدْيُ مَحِلَّهُ))
((Na wala msinyoe vichwa vyenu mpaka mnyama afikie machinjoni pake)). [Al-Baqarah (2:196)]
‘Ulamaa wote wanasema ni haramu kunyoa kichwa sawasawa mwanaume au mwanamke, na kama atanyoa, basi atalipa fidia. [Al-Majmuw’u cha An-Nawawiy (7/262)]
Lakini kama nywele zitamsababishia adha, itajuzu kuzinyoa lakini atatoa fidia. Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
((فمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ بِهِ أَذًى مِّن رَّأْسِهِ فَفِدْيَةٌ مِّن صِيَامٍ أَوْ صَدَقَةٍ أَوْ نُسُكٍ))
((Na atakayekuwa miongoni mwenu mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake (ikambidi anyoe); basi atoe fidia kwa kufunga Swiyaam au kutoa swadaqah au kuchinja mnyama)). [Al-Baqarah: (2:196)]
Aayah hii ilishuka kwa sababu ya Ka-’ab bin ‘Ajarah wakati Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipompitia –akiwa amehirimia- huku chawa wakipukutika usoni kwake. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamuuliza: ((Je, vijidudu hivi vinakusumbua?)). Akasema: Na’am. Akamwambia:
((احلق رأسك، وصم ثلاثة أيام، أو أطعم ستة مساكين، أو أنسك بشاة))
((Nyoa kichwa chako, na funga siku tatu, au lisha masikini sita, au chinja mbuzi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1814), Muslim (1201) na wengineo.
Je, inakatazwa kukata nywele tu au kunyoa sehemu nyingine isiyo kichwa?
An-Nawawiy amesema: [Al-Majmuw’u (7/262)]: “Maswahibu zetu wamesema: Haramisho halihusiani na kunyoa kichwa tu, bali huharamishwa kuondosha nywele kabla ya wakati wa tahallul. Na kwa kuziondosha, ni lazima kutoa fidia ni sawa nywele za kichwa, ndevu, sharubu, kwapa, kinena na sehemu nyingine za mwili. Na ni sawa akiziondosha kwa kunyoa, au kupunguza, au kuzinyofoa, au kuzichoma na mfano wa hivyo. Na hakuna khilafu katika haya yote kwetu sisi”.
Ninasema: “Hakuna shaka kuwa dalili ni mahsusi zaidi kuliko hukmu. Hivyo haiswihi hukmu kutolewa dalili isipokuwa kama itasemwa: “Dalili hapa ni Qiyaas”. Kwa hiyo tunasema: Asli na tanzu ni lazima ziwe sawa katika sababu. Mwenye kuifanya sababu ya katazo la kunyoa kichwa kuwa ni kuzuia burudiko la mwili (nao ni usemi wa walio wengi), basi huyo atazuia kunyoa nywele nyingine za mwili. Na mwenye kuifanya sababu kuwa Muhrim akinyoa kichwa chake, basi anapomosha kwa kunyoa huko nusuk halali ambayo ni kunyoa au kupunguza, basi huyo hatozuia isipokuwa kunyoa kichwa tu. Wameliunga hili mkono kwa kusema kuwa asili ni halali katika kinachoondoshwa katika nywele, na hilo halizuiliwi isipokuwa kwa dalili”. [Amelieleza hili Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah) katika Al-Mumti’u (7/131-133)]
Ninasema tena: “Pamoja na yote hayo, la akiba zaidi ni kuifuata kauli ya Jumhuri katika suala hili inayokataza kunyoa nywele za kichwa chake, sharubu zake, kwapa zake na kinena chake. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.”
Faida
Hakuna ubaya kwa Muhrim kukuna kichwa chake hata kama zitadondoka nywele bila kukusudia kuzidondosha.
6- Kukata kucha
Ibn Al-Mundhir amenukuu Ijma’a isemayo ni haramu kwa Muhrim kukata kucha. Ibn Qudaamah amesema: “ ‘Ulamaa wamekubaliana wote kuwa ni marufuku kwa Muhrim kukata kucha zake. Wengi wao akiwemo Hammaad, Maalik, Ash-
Shaafi’iy, Abu Thawr na Asw-haab Ar-Ra-ay wanasema ni lazima alipe fidia akizikata”.
Na ‘Atwaa amesema: “Si lazima atoe fidia, kwa kuwa sharia haikugusia hilo”. [Al-Ijma’a cha Ibn Al-Mundhir (57) na Al-Mughniy (5/388)]
Ninasema: “Ikiwa mwono wa Ijma’a ni sahihi, basi utakuwa ni hujja wajibishi. Na kama si sahihi, basi utafiti ufanyike kujua undani kama ilivyo katika suala lililopita la kunyoa nywele za sehemu nyingine za mwili”.
Lakini Daawuwd Adh-Dhwaahiriy amelikhalifu hili kwa kujuzisha kukata kucha zote na bila fidia yoyote. [Al-Majmuw’u (7/263)]
An-Nawawiy kasema: “Ibn Al-Mundhir na wengineo wamenukuu Ijma’a ya Waislamu ya kuharamisha kukata kucha katika Ihraam, na huenda wao hawakumzingatia Daawuwd, na kumzingatia ndani ya Ijma’a ni kutegua uwiano..”.
Ninasema: “Ibn Hazm vile vile amelikhalifu hili kwenye Kitabu chake cha Al-Muhallaa (7/246). Amejuzisha kukata kucha”.
Faida
Ash-Shanqiytwiy (Rahimahu-Allaah) katika Kitabu chake cha Adhwaaul Bayaan (5/404) ametoa dalili ya kuharamisha kukata kucha kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُم
kwa mujibu wa Tafsiyr ya baadhi ya Swahaba na Taabi’iyna waliosema kuwa قضاء النفث maana yake ni kunyoa kichwa, kukata kucha, na kunyofoa nywele za kikwapa. Akasema (Rahimahu-Allaah) “Na kwa msingi wa tafsiyr tajwa, Aayah inadulisha kuwa kucha ni kama nywele kwa aliyehirimia, na hususan kuchinja mnyama kukiwa “kumeatwifiwa”na ثُمَّ. Hivyo imedulisha kuwa kunyoa, kukata kucha na mengineyo, yanatakikana yafanywe baada ya kuchinja”.
Faida
Kucha yake ikivunjika, basi aikate, na hapana kitu juu yake.
7- Vishawishi vya jimai
An-Nawawiy kasema: “Ni haramu kujikabilisha na yenye kusisimua matamanio ya kimwili kama kumweka mke mapajani, kumpiga kisi na kumgusa kwa mkono kwa matamanio kabla ya tahalluli mbili. Ikiwa ameshaingia kwenye Ihraam halafu akafanya kusudi kujikabilisha na matamanio hayo, basi ni lazima fidia, nayo ni mbuzi au badali yake ya kulisha masikini au kufunga. Halazimiwi fidia ya ngamia ni sawa akimwaga au asimwage manii, bali fidia ya ngamia itamlazimu kama atajimai, na hakuna makhitalifiano kati ya Fuqahaa kuhusu hili. Kujikabilisha kwa matamanio hakuharibu ‘amali yake ya Hajj ni sawa akimwaga au asimwage. Na haya yote kama atafanya hivyo huku anajua yuko kwenye Ihraam, lakini kama amesahau, basi hana fidia, na hakuna makhitalifiano kuhusu hili”.
Ninasema: “Dalili ya kuharamisha hilo inaingia ndani ya ujumuishi wa Kauli Yake Ta’aalaa فلا رفث kama ilivyoelezwa nyuma.
Lakini mimi sijaipata dalili yoyote kutoka kwenye Qur-aan au Sunnah inayowajibisha kuchinja mnyama kwa aliyejikabilisha kwa matamanio bila kujimai. Labda tu niichukue toka kwenye qaaidah ya Fuqahaa isemayo: “Kufanya lililoharamishwa ndani ya Ihraam kunawajibisha kafara”, lakini pamoja na hivyo, qaaidah hii haina muamana.
Maalik naye anasema kuwa ikiwa atamzongazonga mkewe, au akampiga kisi, au akamgusa na akamwaga manii, basi Hajj yake itaharibika, na atawajibika kuhiji tena mwaka ujao. Na kama atapiga busu, au akamvaa, au akajisugua sugua kwa raha bila kumwaga wala kuingiza dhakari, basi ni lazima atoe kafara. [Al-Mudawwanah (1/327)]
Ama Ibn Hazm, yeye amehalalisha yote yaliyo chini ya jimai kwa msingi kwamba الرفث maana yake ni jimai tu na si vinginevyo”.
8, 9- Kuposa na kufunga ndoa
Ni kwa Hadiyth ya ‘Uthmaan bin ‘Affaan aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((لَا يَنْكِحُ اَلْمُحْرِمُ, وَلَا يُنْكِحُ, وَلَا يَخْطُبُ))
((Muhrim haoi, wala haozeshi, wala haposi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na
Muslim (1409), At-Tirmidhiy (840), Abu Daawuwd (1841) An-Nasaaiy (5/292) na Ibn Maajah (1966)]
An-Nawawiy kasema: “Agizo la Hadiyth hii linafuatwa na baadhi ya Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam”.
Pia ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Is-haaq. Wanaona Muhrim hafai kufunga ndoa, na akifunga basi ndoa yake ni baatwil.
Hadiyth hii ya ‘Uthmaan imepingwa na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) aliyesema: ((Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwoa Maymuwnah akiwa Muhrim)). [Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1837) na Muslim (1410)]
Abu Haniyfah na Ath-Thawriy wamesema hivi hivi, wakajuzisha Muhrim kuoa.
Lakini hili la kujuzisha Muhrim kuoa limejibiwa na Jumhuri kwa majibu kadhaa yaliyopita kwenye mkondo wa nguvu. [Angalia Al-Muhallaa (7/200), Al-Mughniy (3/158), Fat-hul Baariy (4/62), Zaadul Ma’aadiy (3/372) na Sharhul ‘Umdah cha Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah (2/194)]
Kati ya majibu hayo ni:
1- Ni kuwa kauli hii ya Ibn ‘Abbaas imeshtukiwa na kuchukuliwa kama ni mazigazi na mawazo yake tu. Sa’iyd Ibn Al-Musayyib amesema: “Ni mazigazi ya Ibn ‘Abbaas –hata kama ni khalati yake-, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakumwoa ila baada ya kufanya tahalluli”.
Ahmad kasema: “Hadiyth hii ni makosa”.
2- Ibn ‘Abbaas wakati huo alikuwa mtoto wa miaka kumi. Mtoto kama huyu anaweza asijue mambo mengi yaliyojiri katika zama zake.
3- Maymuwnah mwenyewe pamoja na Abu Raafi’i ambaye alikuwa mshenga wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika ndoa hiyo, wamethibitisha kuwa Rasuli alimwoa baada ya tahalluli.
Toka kwa Yaziyd bin Al-Aswamm amesema: ((Maymuwnah bint Al-Haarith amenihadithia akisema: Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwoa akiwa ameshavua Ihraam)). Amesema: ((Alikuwa ni khalati yangu na khalati ya Ibn ‘Abbaas)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1411), Abu Daawuwd (1843), At-Tirmidhiy (845), Ibn Maajah (1963) na wengineo]
Na toka kwa Abu Raafi’u amesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwoa Maymuwnah akiwa amevua Ihraam, akamtengenezea kichumba cha kulala naye, na mimi nilikuwa mshenga kati yao)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (841) kwa Sanad Dhwa’iyf, lakini inatiwa nguvu na Hadiyth iliyoitangulia. At-Tirmidhiy ameitia ila kwa Irsaal. Na mimi sioni Irsaal kuwa ni tatizo kwa kuwa Yaziyd ameichukua moja kwa moja toka kwa Maymuwnah]
4- Ni kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwoa katika ‘Umrat Al-Qadhwaa "عمرة القضاء" na Makkah wakati huo ni eneo la vita. Rasuli akapatana nao kusimamisha vita kwa muda ili aweze kuingia na kufanya ‘Umrah kwa muda wa siku tatu tu kisha atoke. Akaja kutoka Madiynah akiwa amehirimia ‘Umrah. Na hakuna shaka kuwa alimwoa baada ya kutimiza ‘Umrah yake, kisha akarudi pamoja naye toka Makkah. Naye alikuwa anahirimia toka Dhul-Hulayfah, na hivyo hali inabainisha kuwa alimwoa akiwa Muhrim. Ama aliyehadithia kuwa alimwoa akiwa amevua Ihraam, basi atakuwa ameuona ukweli wa mambo na akauelezea.
5- Tukichukulia kwamba Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ni Swahiyh, tutaona kuwa kitendo kimepishana na kauli –katika Hadiyth ya ‘Uthmaan-, hivyo ni lazima kutanguliza kauli, kwa kuwa kitendo kinaendana na uhalali asili, nao ni kuwa ndoa ni halali katika hali zote, wakati kauli inanukuu toka kwenye asili. Hivyo basi, kwa hali hii, Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas inakuwa imenasikhiwa. Na hapa haijuzu kutanguliza kitendo kwa kuwa kutalazimu kubadili hukmu mara mbili, na hii ni kinyume na qaaidah ya ahkaam. [Al-Haafidh ameashiria katika Al-Fat-h (9/166) kuwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ni Swahiyh toka kwa Abu Hurayrah na ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)].
Ninasema: “Bali kuna maneno kwa wote wawili. Na huenda kutokana na hilo, Ibn ‘Abdul Barri amesema katika At-Tamhiyd (3/153): Simjui Swahaba yeyote aliyesimulia toka kwake kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwoa Maymuwnah akiwa Muhrim isipokuwa Ibn ‘Abbaas”.
Ninasema: “Haya ni majibu ya nguvu kwa kuwa yanaendana na Usuwl. Yanatiliwa nguvu vile vile na kuthibiti Makhalifa Waongofu kuharamisha ndoa ya Muhrim kwa Makhalifa Waongofu. Toka kwa Ghatwafaan toka kwa baba yake: ((Kwamba ‘Umar alifarikisha baina yao, yaani mwanaume aliyeoa naye ni Muhrim)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik katika Al-Muwattwaa (869), na toka kwake Al-Bayhaqiy (5/66). Angalia Al-Irwaa (1038)]
‘Aliyy amesema: ((Muhrim haoi, akioa ndoa yake hurejeshwa)). [Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy]
Kuna baadhi ya ‘Ulamaa waliolichukulia jambo hili kama linamhusu Rasuli tu na hususan suala hili la kuoa ambalo yeye ana umahususi wake pekee unaojulikana. Lakini nguvu ya majibu yaliyotangulia iko juu kwa kuwa umahususi unaodaiwa hapa umekosa dalili. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
10,11- Kufanya maasia, kuzozana na kulumbana
Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
((فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ))
((Na atakayekusudia kuhiji (akahirimia) katika miezi hiyo, basi asifanye tendo la ndoa wala ufasiki wala mabishano katika Hajj)). [Al-Baqarah (2:197)]
12- Kuwinda wanyama wa nchi kavu
Ni sawa kwa kuua, au kuchinja, au kuashiria, au kuonyesha. Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:
((وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُمًا))
((Na mmeharamishiwa mawindo ya nchi kavu madamu mtakuwa katika Ihraam)). [Al-Maaidah (5:96)]
Na Neno Lake Subhaanah:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْتُلُوا الصَّيْدَ وَأَنتُمْ حُرُمٌ))
((Enyi walioamini! Msiue mawindo na hali mko katika Ihraam)). [Al-Maaidah (5:95)]
Na kwa Hadiyth ya Ibn Qataadah ambayo sehemu yake inasema: ((Walipoondoka, wote walihirimia isipokuwa Abu Qataadah, yeye hakuhirimia. Na walipokuwa wanakwenda, ghafla wakaona punda milia. Abu Qataadah akawashambulia na akamuua jike kati yao. Wakashuka wakala nyama yake. Wakasema: Hivi tunakula nyama ya mnyama aliyewindwa na sisi tuko katika Ihraam? Tukabeba nyama iliyobakia ya punda jike. Walipofika kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) walisema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika sisi tulikuwa tumehirimia, na Abu Qataadah hakuwa amehirimia. Tukaona punda milia, Abu Qataadah akawashambulia na akaua punda jike. Tukashuka tukala nyama yake. Kisha tukasema: Hivi tunakula nyama ya kiwindwa na sisi tuko kwenye Ihraam? Tukabeba nyama iliyobakia. Akasema (Rasuli): ((Je kuna yeyote kati yenu aliyemwamuru kuwashambulia au kumwashiria?)). Wakasema hapana. Akasema: ((Basi kuleni nyama yake iliyobakia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1824) na Muslim (1196).
Adhabu ya mwenye kuua mnyama
Allaah Ta’aalaa Amesema:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْتُلُوا الصَّيْدَ وَأَنتُمْ حُرُمٌ ۚ وَمَن قَتَلَهُ مِنكُم مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاءٌ مِّثْلُ مَا قَتَلَ مِنَ النَّعَمِ يَحْكُمُ بِهِ ذَوَا عَدْلٍ مِّنكُمْ هَدْيًا بَالِغَ الْكَعْبَةِ أَوْ كَفَّارَةٌ طَعَامُ مَسَاكِينَ أَوْ عَدْلُ ذَٰلِكَ صِيَامًا لِّيَذُوقَ وَبَالَ أَمْرِهِ ۗ عَفَا اللَّـهُ عَمَّا سَلَفَ ۚ وَمَنْ عَادَ فَيَنتَقِمُ اللَّـهُ مِنْهُ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ ذُو انتِقَامٍ))
((Enyi walioamini! Msiue mawindo na hali mko katika Ihraam. Na atakayemuua (mnyama) miongoni mwenu kwa kusudi, basi malipo yake itakuwa ni kilicho sawa na alichokiua katika wanyama wa mifugo. Kama wanavyohukumu wawili wenye uadilifu miongoni mwenu. Mnyama huyo afikishwe Ka’bah, au kafara ya kulisha maskini, au badala ya hayo, kufunga swiyaam ili aonje matokeo maovu ya jambo lake. Allaah Ameshasamehe yaliyopita; na yeyote atakayerudia tena, basi Allaah Atamlipiza (kumuadhibu). Na Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye kulipiza)). [Al-Maaidah (5:95)]
Aayah hii Tukufu inadulisha kuwa muuaji mnyama anachaguzishwa adhabu moja kati ya tatu. Ataitolea kafara yoyote aitakayo, ni sawa awe anajiweza kimali au hajiwezi. Adhabu hizo ni:
Ya kwanza: Achinje mfano wa mnyama aliyemuua kama atapata mfano wake katika wanyama wa kufugwa. Atagawa swadaqah nyama yake kwa masikini wa Al-Haram. Anaweza kumchinja wakati wowote anaotaka, na si lazima achinje siku maalum za kuchinja.
Muradi wa mfano ni yule anayefanana naye kwa sura na umbo na si kwa thamani. Atamchinja aliyefanana zaidi kwa sura na umbo na mnyama aliyemwinda. Akiwinda fisi atachinja kondoo, akiwinda paa atachinja mbuzi, na akiwinda mbuni atachinja ngamia jike na mfano wa hivi.
Toka kwa Jaabir amesema: ((Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuhusu fisi. Akasema:
((هو صيد، ويجعل فيه كبش، إذا صاده المحرم))
((Ni mnyama wa kuwindwa, na hulipiwa fidia kondoo Muhrim akimwinda)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3801) na wengineo. Imeelezwa kuwa Swahiyh katika Al-Irwaa (1050)]
Toka kwa Jaabir: ((Kwamba ‘Umar bin Al-Khattwaab alilipa kondoo kwa fisi, na mbuzi kwa paa, na kichanga cha mbuzi kwa sungura, na mbuzi wa miezi minne kwa jerboa [mnyama kama panya])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik (947), na toka kwake Ash-Shaafi’iy (987), na toka kwake Al-Bayhaqiy (2/183). Angalia Al-Irwaa (1051)].
Salaf katika Swahaba na Taabi’iyna walilipa ngamia jike kwa kuwinda mbuni. [Ibn Qudaamah amenukuu katika Al-Mughniy (5/204,404), na Sheikh wa Uislamu katika Sharhul ‘Umdah (2/283), Ijma’a ya Swahaba juu ya hilo na kwa yaliyotangulia toka kwa ‘Umar. Angalia Muswannaf wa ‘Abdul Razzaaq (8213) na Al-Muhallaa (7226)].
Na hii ni kauli ya Maalik na Ash-Shaafi’iy. Ibn Hazm amesema hakuna katika ngamia jike anayefanana na mbuni kwa upande wa urefu wa shingo, wala umbo wala sura.
Ama akiwinda punda milia, ngamia na nyati, basi atatoa ng’ombe.
‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu) alihukumu atolewe mbuzi kwa kuwindwa njiwa. [Al-Haafidh kasema ni Hasan. Imekharijiwa na Ash-Shaafi’iy katika Al-Umm (2/214) na Al-Bayhaqiy (5/502). Ibn Hajar katika At-Talkhiysw (2/285) amesema kuwa Isnaad yake ni Hasan]
Pia, Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) alihukumu hivyo hivyo. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (5/205). Angalia Al-Irwaa (1056)]
Ama kiwindwa ambacho Swahaba hawakukitolea hukmu -katika vilivyotangulia na vinginevyo- katika hali hiyo, itabidi tuwalete mahakimu wawili waadilifu na wajuzi wa kutoa hukmu ya ufananisho. Na kama hawakupata mshabaha wa mnyama wa kufugwa, basi ni lazima kutoa thamani yake, na haijuzu kutoa fedha taslimu, bali thamani ya fedha hiyo itanunuliwa chakula, kisha atachaguzwa kati ya mambo mengine mawili kati ya matatu.
Ya pili: Amtie thamani mnyama mfananishwa kwa dirham. Thamani hiyo atanunulia chakula kisha atakigawa swadaqah kwa masikini, kila masikini kibaba. Haitotosheleza kutoa fedha. [Angalia Al-Majmuw’u (7/423)]
Ya tatu: Afunge badala ya kuchinja mnyama mfananishwa na kulisha kibaba kimoja kila siku kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri.
Kulisha na kufunga hufanywa sehemu yoyote aitakayo mtu, kwa kuwa Allaah Mtukufu Hakuyawekea mpaka mambo hayo mawili. [Al-Muhallaa (7/235)]
Ikiwa kundi la watu litashiriki pamoja kuua mnyama
Watu hawa hawatakuwa isipokuwa na adhabu moja tu. Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
((فَجَزَاءٌ مِّثْلُ مَا قَتَلَ مِنَ النَّعَمِ))
((basi malipo yake itakuwa ni kilicho sawa na alichokiua katika wanyama wa mifugo)). [Al-Maaidah (5:95)]
Hakuna katika kiwindwa isipokuwa mfano wake na si mifano yake. Toka kwa ‘Imaad bin Abiy ‘Ammaar: ((Kwamba waachwa huru wa Ibn Az-Zubayr walimuua fisi wakiwa kwenye Ihraam, wakamuuliza Ibn ‘Umar (kuhusu kitendo hicho). Akasema: Chinjeni kondoo. Wakauliza: Kwa kila mmoja wetu? Akasema: Bali kondoo mmoja kwenu nyote)). [Isnaad yake ni Hasan. Imekharijiwa na Ad-Daaraqutwniy (2/250) na Ibn Hazm (7/237)]
Hakuna Swahaba yeyote aliyejulikana kwenda kinyume na Ibn ‘Umar. Haya pia ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na kundi la Salaf.
Hivyo, wauaji watashirikiana katika adhabu moja na kulisha kumoja. Lakini wakichagua kufunga, basi kila mmoja ni lazima afunge siku zote, kwa kuwa Swiyaam haishirikiwi na hilo haliwezekaniki kinyume na fedha.
Mwenye kuua mnyama kisha akaua mwingine
Ni lazima atoe fidia kwa kila mnyama. Na Kauli Yake Ta’aalaa:
وَمَنْ عَادَ فَيَنتَقِمُ اللَّـهُ مِنْهُ
si yenye kumwondoshea adhabu, kwani Allaah Hakusema kwamba hakuna malipo juu yake, bali Amewajibisha malipo kwa mwenye kumuua mnyama kwa kukusudia. Hivyo malipo ni kwa kila mwenye kuua pamoja na adhabu (ya mnyama mwingine) kwa mwenye kurudia kuua. [Al-Muhallaa (7/238) na Al-Majmuw’u (7/437)]
Mwenye kuua kwa kusahau
Jumhuri ya ‘Ulamaa; Abu Haniyfah, Maalik na Ash-Shaafi’iy wanaona kwamba mwenye kukusudia na mwenye kusahau, wote wawili ni lazima watoe malipo. Dalili zao ni:
1- Wamesema: “Allaah Amewajibisha kafara kwa mtu aliyemuua Muumini kwa makosa, hivyo tumelichukulia hilo Qiyaas kwa aliyeua mnyama kwa makosa.
2- Wamesema: “Ilivyokuwa kwamba mwenye kuharibu mali za watu kwa kukusudia au kwa makosa ni lazima azilipe, na mnyama ni Mali ya Allaah, basi ni lazima alipe kwa kuua kwa kukusudia au kwa bahati mbaya”.
3- Baadhi wengine wamesema: “Mwenye kukusudia ametajwa ili ijulikane kuwa hukmu ya mwenye kukosea pia ni hiyo hiyo”.
Lakini Ibn Hazm anasema kuwa mwenye kusahau kuwa yuko kwenye Ihraam na bila kukusudia, hana malipo na hana madhambi kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:
((وَمَن قَتَلَهُ مِنكُم مُّتَعَمِّدًا))
((Na atakayemuua (mnyama) miongoni mwenu kwa kusudi)).
Amesema kwa kuwa Allaah kuonjesha adhabu kutokana na matokeo mabaya ya kosa hilo, na makamio makali ya kumlipizia, Waislamu wawili hawatofautiani kuwa hayo yote hayamhusu kabisa aliyekosea wala asiyekusudia maasia au kuyanuilia. Allaah Anasema:
((وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ))
((Na wala hakuna dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini isipokuwa katika yale yaliyokusudiwa na nyoyo zenu)). [Al-Ahzaab (33:5)]
Madhehebu haya yamenukuliwa toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab, ‘Abdur Rahmaan bin ‘Awf, Ibn ‘Abbaas, Sa’iyd bin Jubayr, Ibn Al-Musayyib, Twaawuws, Al-Qaasim bin Muhammad Saalim bin ‘Abdullaah, ‘Atwaa na Mujaahid.
Kisha Ibn Hazm amezijibu hoja za Jumhuri kwa maneno murua na mantiki ya upeo wa juu. Ukipenda waweza kuzirejea. Allaah Ndiye Mwezeshaji wa mambo yote.
Wanyama ambao si haramu kuwaua au kuwawinda kwa Muhrim
1- Wanyama ambao kiasili ni wa kufugwa
Tumetangulia kusema kuwa ni haramu kuua au kuwinda wanyama wa nchi kavu. Ama wanyama wa kufugwa kama ngamia, ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku, hao hawaharamishwi kama hawakugeuka na kuwa wanyama wakali. Ikiwa ngamia atamtoroka mmiliki wake Muhrim kisha akampata na akamuua kwa kumlenga (kwa mshale, risasi n.k), basi ni halali hata kama ngamia huyu akigeuka na kuwa mkali wa kudhuru, kwa kuwa asili yake ni wa kufugwa.
2- Kiwindwa cha baharini
Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:
((أُحِلَّ لَكُمْ صَيْدُ الْبَحْرِ وَطَعَامُهُ مَتَاعًا لَّكُمْ وَلِلسَّيَّارَةِ ۖ وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُمًا ۗ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ))
((Mmehalalishiwa mawindo ya bahari na chakula chake ni manufaa kwenu na kwa wasafiri. Na mmeharamishiwa mawindo ya nchi kavu madamu mtakuwa katika Ihraam. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mtakusanywa)). [Al-Maaidah (5:96)]
[Ash-Sharhul Mumti’u ‘Alaa Zaadil Mustanqa’i (7/167) kwa mabadilisho kidogo].
3- Mnyama ambaye ni haramu kuliwa
Ni kama wanyama wakali na wenye meno na kucha, kwa kuwa hawana thamani na wala si wa kuwindwa. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na kauli ya Mahanbali kinyume na Jumhuri ambao wamewajibisha fidia kwa kumuua mnyama mkali. [Al-Muhallaa (7238). Angalia Tafsiyr Ibn Kathiyr (2/98)]
4- Wanyama tulioamuriwa tuwaue na wenye madhara
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amewataja watano ambao huuawa watu wakiwa kwenye Ihraam na wakiwa kwenye tahallul.
Toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((خمس من الدواب كلهن فواسق، يُقتلن في الحل والحرم: الغراب، والحدأة، والعقرب، والفأرة والكلب العقور))
((Watano katika wanyama, wote ni wadhurifu, huuawa katika tahallul na katika Ihraam: Kunguru, mwewe (kite), nge, panya na mbwa anayeng’ata watu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1829) na Muslim (1198)]
Sheikh wa Uislamu amesema: “Na vyote vyenye kuwadhuru watu au kuharibu mali zao, basi inaruhusiwa kuviua, ni sawa madhara yake yawe ya uhakika kama mnyama mkali anayeweza kumshambulia Muhrim, au mnyama ambaye madhara yake hayana mwamana kama nyoka, nge, panya na mbwa anayeng’ata watu. Wanyama hawa na mfano wao, huingia kinyemela kwa watu bila kuhisiwa na madhara yao yanakuwa makubwa yasiyotabirika”. [Sharhul ‘Umdah (1/136)]
Maswahibu wetu wamesema: “Kuwaua kumesuniwa”.
Pia hapana ubaya kuua mbu, nzi, viroboto na chawa kama wanasababisha kero, na Muhrim hadaiwi chochote. [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/118) na Al-Muhallaa (7/245)]
5- Kumuua mwanadamu mshambuliaji
Mtu anahitajika kujiepushia madhara yoyote yatokanayo na wanadamu wenzake au wanyama hata kama mtu atamshambulia na haikuwezekana kumwondosha isipokuwa kwa kupigana naye, basi apambane naye. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((من قتل دون ماله فهو شهيد))
((Anayeuawa akipigania mali yake basi huyo ni shahidi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2480) na Muslim (141)]
13- Kula kilichowindwa kwa ajili yake, au kwa ishara yake au kwa msaada wake
Ni kwa yaliyotangulia katika Hadiyth ya Abu Qataadah Rasuli aliposema:
((أمنكم أحد أمره أن يحمل عليها، أو أشار إليها؟ قالوا: لا، قال: فكلوا))
((Je kuna yeyote kati yenu aliyemwamuru kuwashambulia au kuwaonyeshea?)). Wakasema hapana. Akasema: ((Basi kuleni)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]
Aliyevua Ihraam akiwinda mnyama kisha akamlisha Muhrim, basi inajuzu ale nyama lakini kama hajawindwa kwa ajili yake. Toka kwa ‘Abdur Rahmaan bin ‘Uthmaan At-Tamiymiy amesema: ((Tulitoka pamoja na Twalha bin ‘Ubaydillaah –tukiwa tumehirimia- na yeye akapewa zawadi ndege. Twalha akiwa amelala, baadhi yetu walimla, na wengine walisita kula. Twalha alipoamka, aliwaunga waliokula na kusema: Tulimla pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1197) na wengineo]
Hadiyth hii inachukulika kuwa ndege huyo hakuwa amewindwa kwa ajili yake.
Na kama amemwinda kwa ajili ya kumlisha Muhrim, basi haitojuzu kumla. Na hili linafahamika kutokana na Hadiyth ya Asw-Swa’ab bin Jath-thaamah kwamba alimpa zawadi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) punda mlia na Rasuli akamrudishia. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipoona huzni katika uso wake alimwambia:
((إنَّا لم نرُدَّه عليك إلَّا أنَّا حُرُمٌ))
((Sisi hatukukurudishia isipokuwa sisi hakika tuko kwenye Ihraam)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1825) na Muslim (1193)
Hivyo inachukulika kuwa alimwinda kwa ajili ya kumpa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akiwa Muhrim, na yeye hakukubali.
Na haya ni madhehebu ya Jumhuri ya ‘Ulamaa, na Ibn Al-Qayyim ameyatilia nguvu akisema kuwa athari zote za Swahaba kuhusiana na hili zinaonyesha ufafanuzi huu. [Angalia Zaadul Ma’aad (1/164), Tahdhiyb As-Sunan (5/215)].