15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Mambo Ambayo Muhrim Anaruhusiwa Kuyafanya Bila Tatizo
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah
15-Mambo Ambayo Muhrim Anaruhusiwa Kuyafanya Bila Tatizo
Baadhi ya Mahujaji huhisi vibaya kuyafanya mambo haya, nayo hayana ubaya wowote.
1- Kuoga bila kuota, na kubadilisha nguo zake za Ihraam (izari na ridai)
Toka kwa ‘Abdullaah bin Hunayn toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Abbaas na Al-Miswar bin Makhramah kwamba walikhitalifiana hapo Al-Abwaa. Ibn ‘Abbaas akasema: Muhrim huosha kichwa chake, na Al-Miswar akasema Muhrim haoshi kichwa chake. Ibn ‘Abbaas akanituma niende kwa Abu Ayyuwb Al-Answaariy nimuulize kuhusu hilo. Nikamkuta anaoga baina ya nguzo mbili za kisima huku akijistiri na nguo, nami nikamsalimia. Akauliza: Nani huyu? Nikasema: “Mimi ni ‘Abdullaah bin Hunayn. ‘Abdullaah bin ‘Abbaas amenituma kwako nikuulize ni vipi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anaosha kichwa chake akiwa Muhrim? Abu Ayyuwb akaweka mkono wake juu ya nguo akaiteremsha kidogo mpaka nikakiona kichwa chake. Kisha akamwamuru mtu ammwagie maji, akamwagia juu ya kichwa chake, akakisogeza kichwa chake kwa mikono yake miwili, akaipeleka mbele na nyuma, kisha akasema: Hivi ndivyo nilivyomwona Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akifanya. [Al-Miswar akamwambia Ibn ‘Abbaas: Sitolumbana nawe milele]. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1840) na Muslim (1205) na nyongeza ni yake]
Hadiyth hii ni dalili juu ya kujuzu kuoga kwa Muhrim.
Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: Huenda ‘Umar bin Al-Khattwaab aliniambia: ((Njoo nishindane nawe kuzamia ndani ya maji tuone nani ana pumzi ndefu zaidi, na sisi tumehirimia)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy]
2- Kuchana nywele
Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwamuru ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) akimwambia:”
((انقضي رأسك وامتشطي))
((Fumua nywele zako na uzichane)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (316) na Muslim (1211)
Hilo linajuzu kama kuna usalama wa kutoanguka nywele yoyote. Kama hakuna usalama, basi hilo ni mahala pa mvutano na ijtihaad. Na lenye nguvu ni kujuzu hilo, kwa kuwa hakuna dalili ya kulizuia.
3- Kukuna mwili na kichwa
Toka kwa ‘Aaishah kuwa aliulizwa kuhusu Muhrim kukuna mwili wake akasema: ((Na’am, aukune na aivute ngozi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik katika Al-Muwattwa (803)]
Hili linadulishwa na Hadiyth ya Abu Ayyuwb iliyotangulia. Na kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu amesema: “Anaweza kukuna mwili wake ukimwasha, na vile vile akioga na zikaanguka baadhi ya nywele zake, hilo halitomharibia kitu”. [Al-Majmuw’at Al-Kubraa (2/368) mlango wa Hijjah ya Nabiy uk. 27]
An-Nawawiy kasema: “Ama Muhrim kukuna kichwa chake, mimi siujui mvutano wowote kuhusu uhalalisho wake…lakini wamesema kuwa ajikune kwa ulaini ili nywele zisidonoke”. [Al-Majmuw’u (7/263)]
4- Kuumika hata kwa kunyoa nywele sehemu ya kuumika
Ni kwa Hadiyth ya Ibn Buhaynah (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliumikwa katikati ya kichwa chake akiwa Muhrim huko Lihaa Jamal –eneo katika barabara kuelekea Makkah-)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1836) na Muslim (1203)]
Sheikh wa Uislamu amesema: “Anaweza kujikuna mwili wake ukimwasha, na kuumikwa kichwani kwake na sehemu nyingine, na kama atahitajia kunyoa nywele za dhakari yake, basi anaweza kunyoa. Kwani imethibiti katika Swahiyh (kisha akaileta Hadiyth iliyotangulia na kusema): Na hilo haliwezekani isipokuwa pamoja na kunyoa baadhi ya nywele…”.
Jumhuri wanasema kuwa inajuzu kuumika kwa sharti nywele zisikatwe, na kama akikata, basi ni lazima fidia. Ibn Hazm amewajibu katika Al-Muhallaa (7/257) akiwaambia baada ya Hadiyth iliyotangulia: “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakueleza kwamba kuna faini katika hilo wala fidia. Na kama ingekuwa lazima, basi asingeacha kusema. Na yeye Rasuli alikuwa ana nywele nyingi ndefu. Na bila shaka tumekatazwa kunyoa nywele katika Ihraam, na shingo ya nyuma (nape) si kichwa, wala si sehemu ya kichwa”.
Faida
Inaingia katika yaliyotangulia kun’goa gego na kutumbua jipu, hayo hayana ubaya.
5- Kunusa maua yanukiayo uzuri na mafuta marashi kwa haja na si kwa kujiburudisha
Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: ((Muhrim anaingia msalani, anang’oa jino lake, ananusa maua mazuri, na ukucha wake ukikatika anautupa)).
Na amesema tena: ((Jiondosheeni vinavyowasumbueni, kwani Allaah ‘Azza wa Jalla Hafanyi lolote kwa vinavyowasumbueni)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (5/62-63)]
Kunusa manukato kuna hali tatu:
[Angalia Ash-Sharhul Mumti’u (7/158-159)]
1- Mtu kuyanusa bila kukusudia. Hili halina ubaya wowote.
2- Akusudie kuyanusa, si kwa ajili ya kupata mwonjo au kujiburudisha, bali kujua ubora wake na mfano wa hilo. Hili pia halina ubaya.
3- Akusudie kupata mwonjo na kuburudika nayo. Hili linakatazwa kwa mujibu wa kauli mbili za karibu zaidi za ‘Ulamaa. Lakini mtu anaweza kusema: Hilo halina ubaya, kwa kuwa si kuyatumia, na wala kunusa hakuna athari yoyote kwa nguo wala kwa mwili.
6- Kuitupa kucha ikikatika
Dalili ya hili ni athar ya Ibn ‘Abbaas iliyotangulia. Sa’iyd bin Al-Musayyib aliulizwa kuhusu kucha ikikatika na yeye ni Muhrim, akajibu: “Ninaikata”. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik katika Al-Muwattwa (805)]
7- Mwanaume kufunika uso
Hakuna ubaya mwanaume kufunika uso wake kwa kutumia alichojitandia au kwa kinginecho kwa ajili ya kujikinga na jua, au vumbi au mfano wa hilo akiwa Muhrim. Hili limesimuliwa toka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan, Zayd bin Thaabit, Ibn Az-Zubayr, Jaabir, Ibn ‘Abbaas na Jumhuri ya Taabi’iyna. Pia ni madhehebu ya Ath-Thawriy na Ash-Shaafi’iy. [Angalia athar zilizonukuliwa toka kwao katika Al-Muhallaa (7/91), na angalia Al-Majmuw’u (7/280)]
Ni moja pia ya kauli mbili katika madhehebu ya Ahmad. [Al-Mubdi’u]
Lakini Abu Haniyfah, Maswahibu zake na Maalik, wao wanaona kwamba Muhrim hafuniki uso wake. Na hili limesimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar, na hutolea dalili kwalo kwa ziada iliyopo kwenye Hadiyth ya Muhrim ambaye ngamia wake alimvunja shingo akafa, na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:
ولا تخمروا رأسه
((Na wala msifunike uso wake)). Na katika riwaya nyingine:
ولا تغطوا وجهه
((Wala msifumike uso wake))
badala ya
ولا تخمروا رأسه
Na ziada hii imekhitalifiwa kwa upande wa usahihi wake. [Hadiyth hii kama ilivyotangulia nyuma, ni Muttafaqun ‘Alayhi, na ziada iko kwa Muslim. Angalia Al-Fat-h (4/47) na Al-Irwaa (4/200)]
Waliyeiona kuwa ni Dhwa’iyf, watasema hakuna ubaya kufunika uso. Ama wanayoiona kuwa ni Swahiyh, kuna baadhi yao waliozuia mwanaume Muhrim kufunika uso wake, na kuna wengine waliohusisha marufuku kwa maiti ya Muhrim na si kwa aliye hai wakichukulia mwonekano wa tamshi. Na hili ni kwa madhehebu ya Ibn Hazm.
Na kuna wengine waliosema kuwa amekatazwa kufunika uso kwa ajili ya kukilinda kichwa chake na hakukusudiwi kufunua uso wake, kwa kuwa, ikiwa watafunika uso wake, hawatoweza kufunika kichwa. Hivyo ni lazima kufanya taawiyl, kwa kuwa Maalik na Abu Haniyfah wanasema: Hakukatazwi kufunika kichwa cha maiti na uso wake. Na Jumhuri wanasema: Inaruhusiwa kufunika uso bila kichwa. Hivyo ni lazima Hadiyth iawiliwe. Amesema katika Al-Majmuw’u (7/281).
8- Mwanamke kushusha ushungi wake usoni toka kichwani
[Majmuw’u Al-Fataawiy (26/112), Al-Muhallaa (7/91) na Al-Mughniy (3/325)]
Tumeshasema nyuma kuwa haijuzu kwa mwanamke kuvaa niqabu na kinachofanana na niqabu kama burqu na mfano wake, na kwamba inajuzu kwake kuteremsha mtandio wake toka kichwani hadi usoni wakati wanapopita wanaume ajanibu, ni sawa mtandio ukigusa uso wake au usiguse. Na hii ni kauli sahihi zaidi kati ya mbili, kwa kuwa kuteremsha hakuitwi niqabu. Toka kwa Asmaa bint Abiy Bakr amesema: ((Tulikuwa tunafunika nyuso zetu wanaume wasituone, na tulikuwa tunazichana nywele zetu kabla ya hapo katika Ihraam)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Haakim katika Al-Mustadrak (1/454)]
‘Aaishah amesema: ((Wapandaji walikuwa wakipita karibu yetu na sisi tuko pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) tukiwa tumehirimia. Wakituelekea, mmoja wetu huteremsha jilbabu yake usoni mwake toka kichwani kwake, na wanapotupita, tunazifunua)). [Hadiyth Hasan Lighayrih. Imekharijiwa na Ahmad (6/30) na Abu Daawuwd (1833) kwa Sanad Dhwa’iyf. Ina Hadiyth wenza zinazoifanya kuwa Hasan]
9- Mwanamke kuvaa nguo yoyote aipendayo ya rangi yoyote
Toka kwa Al-Qaasim bin Muhammad amesema: ((‘Aaishah alikuwa anavaa nguo ya kinjano na yeye amehirimia)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Al-Haafidh katika Al Fat-h (2/405) ameinasibisha kwa Sa’iyd bin Mansuwr, na Isnaad yake amesema ni Swahiyh]
Na toka kwa Asmaa bint Abiy Bakr: ((Ni kwamba alikuwa anavaa nguo za kinjano iliyokoza na yeye amehirimia, hakuna za zafarani)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik (719) na Ash-Shaafi’iy katika Al-Umm (2/126)]
Na toka kwa Yaziyd Al-Faqiyr amesema: ((Nilisafiri pamoja na Ummu Salamah –mke wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)-, na baadhi ya nguo zake zilikuwa ni za kinjano)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abi Shaybah katika Al-Muswannaf]
Na toka kwa ‘Atwaa –kuhusiana na kisa cha ‘Aaishah kutufu pamoja na wanaume- ((Na nikamwona amejitanda abaya la rangi ya waridi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1618) na ‘Abdur Razzaaq (5/67)]
Kivazi cha mwanamke Muhrimah hakihusishwi na rangi nyeupe tu kama wanavyoamini wanawake wengi –na hususan Wamisri- bali anavaa rangi yoyote aipendayo madhali nguo imekidhi shuruti za vazi la kisharia.
10- Mwanamke kuvaa suruali na khufu mbili
Inajuzu kwa mwanamke kuvaa suruali au kingine chochote akipendacho. Hazuiwi kuvaa nguo iliyoshonwa kama anavyozuiwa mwanaume. Lakini anazuiwa kuvaa niqabu na glovu mbili kama ilivyotangulia. Pia ana haki ya kuvaa khufu mbili, na haikatwi sehemu ya juu ya vifundo viwili. [Angalia Al-Ummu (2/126), Al-Mughniy (3/328), Majmuw’u Al-Fataawaa (26/112), Fat-hul Baariy (3/406) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/490)]
Toka kwa Ibn ‘Umar amesema: ((Hakuna ubaya kwa Muhrimah kuvaa khufu mbili na suruali)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (4/92)]
Na toka kwa Saalim toka kwa baba yake: ((Ni kwamba alikuwa akiwafutu wanawake wanapohirimia kuwa wazikate khufu mbili mpaka Swafiyyah alipomjuvya toka kwa ‘Aaishah kuwa alikuwa akiwafutu wanawake wasikate, na yeye akaacha hilo)). [Isnaad yake Ni Swahiyh Marfuw’u. Imekharijiwa na Ash-Shaafi’iy. Imekuja Marfuw’u kwa Abu Daawuwd (1831), Al-Bayhaqiy (5/52)]
11- Mwanamke kuvaa vipambo akipenda
Toka kwa Swafiyyah bint Shaybah kwamba mwanamke mmoja alimwambia ‘Aaishah: ((Ee Mama wa Waumini! Hakika binti yangu fulani ameapa hatovaa kipambo chake katika msimu (Na katika riwaya: katika Ihraam yake). ‘Aaishah akamwambia: Mweleze kwamba Mama wa Waumini anakulalamikia vikali kama hukuvaa vipambo vyako vyote)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ash-Shaafi’iy, na kupitia kwake Al-Bayhaqiy (5/52) na Ibn Abiy Shaybah (1/4/219)]
Toka kwa Naafi’u kwamba: ((Wake wa ‘Abdallah bin ‘Umar na mabinti zake, walikuwa wakivaa vipambo vyao wakiwa wamehirimia)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (1/4/320)]
Na toka kwa Maalik bin Mighwal amesema: ((Nilimuuliza Ibn Al-Aswad: Je, mwanamke aliyehirimia anavaa vipambo vyake?)). Akajibu: ((Alivyokuwa anavivaa kabla ya kuhirimia)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (1/4/320)]
Imepokelewa kwa njia swahiyh kuwa ‘Atwaa alikuwa anachukia vipambo vya umashuhuri, yaani ambavyo kwavyo mwanamke anaonekana ni yeye tu baina ya wanawake wenzake. [Angalia Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/495) cha Sheikh wetu]
12- Kujipaka mwanamke hina na mfano wake akipenda
Mwanamke anaweza kujipaka hina na kinginecho kwa kuwa hakuna katazo lolote toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), kama ambavyo hina si manukato. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Mahanbali, isipokuwa baadhi yao wamelikirihisha hilo kwa kuwa ni katika mapambo. [Angalia Al-Majmuw’u (7/219) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/497)]
‘Ulamaa wa Kihanafi na Kimaalik wamesema: Haijuzu kwa aliyehirimia kujipaka sawasawa ni mwanaume au mwanamke.
Ninasema: “Linaloonekana wazi ni kuwa hakuna dalili ya kuzuia hilo si kwa mwanaume au kwa mwanamke. Na kwa maneno haya, ikiwa mwanamke atavingirisha kitambaa pamoja na hina kwenye mikono yake miwili, basi hakuna ubaya wala hatolipa fidia kwa mujibu wa kauli ya karibu zaidi ya ‘Ulamaa”.
Lakini je, hili linachafua kauli ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((وطيب النساء ما ظهر لونه وخفي ريحه))
((Manukato ya mwanamke ni yale yenye kuonekana rangi yake na yenye kufichika harufu yake?)). [Hadiyth Hasan. Itakharijiwa katika mahala pake, In Shaa Allaah]
Na je, kwa Hadiyth hii, hina inakuwa ni manukato?
Ninasema: “Linaloonekana wazi ni kuwa haiharibu kuwa hina ni katika manukato. Kwa kuwa chenye kukatazwa ni chenye harufu kama ilivyotangulia. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
13- Kujitia wanja kwa dharura
Hakuna ubaya kwa Muhrim kujitia wanja kama ana maumivu machoni. ‘Ulamaa kama alivyonukuu An-Nawawiy wamekubaliana wote kwamba Muhrim anaweza kujitia wanja usionukia kama atadharurika, na hana fidia kwa hilo. [Sharhu Muslim (3/292). Na haya ni madhehebu ya Maalik kama ilivyo katika Al-Mudawwanah (1/342) na Ash-Shaafi’ iy katika Al-Ummu (2/129)]
Toka kwa Shumaysah amesema: “Nilisumbuliwa na jicho langu nikiwa nimehirimia. Nikamuuliza Mama wa Waumini ‘Aaishah kuhusu wanja, akasema: ((Jitie wanja wa aina yoyote isipokuwa wanja manga. Wanja huu si haramu lakini ni pambo, na sisi tunaukirihisha)). Akasema: (Ukipenda, nitakutia wanja wa subiri, nikakataa)). [Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (5/63). Shumaysah huyu hajathibitishwa, isipokuwa ndiye mwenye kisa]
Na toka kwa Ibn ‘Umar amesema: ((Muhrim hujipaka wanja wowote autakao madhali si wa kunukia)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (1/4/424)]