19-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Sunan Za Twawaaf
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah
19-Sunan Za Twawaaf
1- Kutawadha kabla ya Kutufu
Ni kwa Hadiyth ya Mama ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa): ((Jambo la kwanza aliloanza nalo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) wakati alipokuja ni kuwa alitawadha, kisha akatufu Nyumba)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1615) na Muslim (1235)]
Na hiki ni kitendo tu kinachodulisha kuwa kufanya hivyo ni jambo mustahabu na halifikii kiwango cha uwajibu. Na wudhuu hauingii ndani ya wigo wa ujumuishi wa ‘amali za Hajj mpaka usemwe kuwa ni bainisho la kauli yake Rasuli:
((خذوا عني مناسككم))
((Jifunzeni kutoka kwangu matendo yenu ya Hajj)).
Kisha, inayumkinika alitawadha kwa ajili ya Swalaah baada ya kumaliza Twawaaf.
Kiujumla, Twawaaf ni dhikri, hivyo ni vizuri mtu kuwa twahara wakati anapoifanya kutokana na Hadiyth ya mtu ambaye alimsalimia Nabiy: ((Naye hakumjibu mpaka akaelekea [ukuta, akatayammamu], akapukusa uso wake na mikono yake miwili, halafu akamjibu salaam)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1875) na wengineo]
2- Kupitisha chini ya kikwapa kipande cha juu cha nguo ya Ihraam
Hii ni kwa wanaume tu. Atapitisha sehemu ya kati ya izari yake chini ya kwapa lake la kulia na atazitupia ncha zake mbili juu ya bega lake la kushoto, na bega lake la kulia litabaki wazi. Ni kwa Hadiyth ya Ya-‘alaa bin Umayyah: ((Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitufu bega lake la kulia likiwa wazi)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1883), At-Tirmidhiy (859) na Ibn Maajah (2954). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]
Kuacha bega la kulia wazi ni Sunnah kwa mujibu wa Jumhuri ya ‘Ulamaa kwa wanaume tu pasina wanawake katika mizunguko yote. Limesuniwa hili kwa kila Twawaaf inayofuatiliwa na Kusai kama Twawaaf Al-Quduwm kwa anayetaka Kusai baada yake, Twawaaf ya ‘Umrah na Twawaaf ya Ziara kwa aliyechelewesha Kusai. Ama Fuqahaa wa Kihanafiy, Kishaafi’iy na Kihanbali, wao wanasema haachi bega wazi isipokuwa katika Twawaaf Al-Quduwm tu. [Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (29/134)]
Angalizo
Kuacha bega wazi kunafanyika wakati wa Twawaaf tu na si kwa ‘amali nyingine za Hajj kama wanavyofanya watu wengi tokea anapohirimia na kuendelea na hali hiyo mpaka anapotahalluli. Huku ni kujingikiwa na Sunnah, na hata utamwona anaswali bega likiwa wazi. Jambo hili limekatazwa kama tulivyoeleza katika mambo yaliyo makruhu katika Swalaah.
Hivyo basi, baada ya kumaliza Twawaaf yake, anatakikana aiweke sawa nguo yake ya juu na alifunike bega lake la kulia, kwa kuwa mahala pa kufunuliwa bega ni wakati wa Kutufu tu.
3- Kwenda mwendo kasi kidogo katika mizunguko mitatu ya kwanza (kwa wanaume tu)
Nako ni kuharakisha mwendo kwa hatua za mkaribiano na kuyatingisha mabega mawili bila kuruka, na hili linafanyika katika mizunguko mitatu tu ya kwanza, minne iliyobakia atatembea mwendo wa kawaida.
Mwendo kasi ni Sunnah katika kila Twawaaf baada ya Kusai. Toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) amesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuja na Swahaba Zake Makkah huku homa ya Yathrib ikiwa imewadhoofisha. Washirikina wakasema: Kesho watakujieni watu ambao homa imewakondesha, na imewapiga vibaya. Wakakaa karibu na nusu mduara ya ukuta wa Al-Ka’abah [ili kuwaangalia na kuwacheza shere]. Na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akawaamuru [Swahaba] waende mwendo kasi katika mizunguko mitatu ya kwanza, na watembee mwendo wa kawaida kati ya Nguzo Mbili ili washirikina wauone uimara na ukakamavu wao. Washirikina wakasema: Hivi ni hawa mliodai kuwa homa imedhoofisha? Hawa ni wakakamavu kuliko kadha na kadha)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1602) na Muslim (1266)]
Nguzo Mbili zilizokusudiwa katika Hadiyth hii ni Jiwe Jeusi na Nguzo ya Yamaaniy. Walipokuwa kati ya sehemu hizi mbili, washirikina walikuwa hawawezi kuwaona, hivyo walipata nafasi ya kupumzika ili wabakie na nguvu zao.
Hii ilikuwa katika ‘Umrat Al-Qadhwaa mwaka wa saba. Lakini mwendo kasi umebakia ni Sunnah katika mizunguko mitatu kamili ya kwanza. Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliifanya katika Hajj yake –na ilikuwa baada ya kuikomboa Makkah na watu kuingia katika Dini ya Allaah makundi kwa makundi- kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Jaabir: ((…akaenda kasi mara tatu, na akatembea kawaida mara nne)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma mara nyingi]
Na katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikwenda haraka mizunguko mitatu, na akatembea kawaida minne katika Hajj na ‘Umrah [toka nusu duara ukuta hadi Jiwe Jeusi])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1604), Muslim (1261) na wengineo bila nyongeza, na ziada iko kwa Ibn Maajah (2950)]
Kwenda mwendo kasi katika mizunguko mitatu ya awali ni Sunnah iliyobakia ingawa sababu yake haipo tena ya kuwatia hasira washirikina. Linalotilia nguvu kubakia kwake ni kuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaah ‘anhu) alikuwa amekusudia kuiacha akisema: ((Unatuhusu nini tena mwendo kasi? Hakika tulikuwa tumewaonyesha kwao washirikina, na Allaah Ashawaangamiza”. Kisha akasema: “Jambo ambalo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amelifanya, basi sisi hatupendi kuliacha)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1605) na Muslim (1270)]
Haifai kisharia kulipia mwendo kasi
Kama hakuweza kwenda mwendo kasi katika mizunguko mitatu ya kwanza kutokana na msongamano na mfano wake, basi hatoilipia kwa minne iliyosalia, kwa kuwa umbile la mizunguko hii minne ni utulivu (kwenda taratibu), hivyo haibadilishwi. [Fat-hul Baariy (3/551)]
Wanawake hawaruhusiwi mwendo kasi
[Al-Ummu (2/150), Al-Mughniy (3/394), Fat-hul Baariy (3/551) na Sharhu Muslim (3/397)]
Wengi katika ‘UIamaa wamelisema hili hata baadhi yao wamenukuu Ijma’a.
‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) amesema: ((Enyi kundi la akina mama! Hampaswi mwendo kasi katika Nyumba. Nyinyi kwetu ni kiigizo)). [Hasan Lighayrih. Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (5/84) na Ibn Abiy Shaybah (1/4/121)]
Mfano wa maneno haya yamenukuliwa toka kwa Ibn ‘Umar kwa njia sahihi. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (5/84) na Ibn Abiy Shaybah (1/4/121)]
Na pia imesimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Masalaf wengine. [Isnaad yake ni Layyin. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (1/4/122). Katika Sanad yake yuko Muhammad bin ‘Abdur Rahmaan bin Abiy Laylaa]
4,5- Kuligusa Jiwe Jeusi kwa mkono na kulibusu katika kila mzunguko ikiwezekana
Ni Sunnah kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: ((Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipowasili Makkah akiligusa Jiwe Jeusi anapoanza Kutufu, anakwenda kasi mizunguko mitatu kati ya saba)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1603) na Musim (1261)]
Toka kwa Naafi’u amesema: ((Nilimwona Ibn ‘Umar akiligusa Jiwe kwa mkono wake, kisha akabusu mkono wake, na akasema: Sikuliacha hili toka nilipomwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalhii wa sallam) akilifanya)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1267)]
‘Umar bin Al-Khattwwaab alilibusu Jiwe na kusema: ((Lau si mimi kumwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akikubusu, basi nisingelikubusu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1605) na Muslim (1270)]
Kama hakuweza kulibusu au kuligusa
Imestahabiwa aliguse Jiwe kwa mkono wake na alibusu kama ataweza. Kama ataligusa na ikawa uzito kulibusu, basi ataubusu mkono wake. Ikishindikana kuligusa kwa mkono, anaweza kuligusa kwa fimbo na mfano wake kisha ataibusu. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitufu katika Hajj ya Kuaga akiwa juu ya ngamia akaligusa Jiwe kwa bakora yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1607)]
Kama hakuweza kabisa kuligusa, basi ataliashiria kwa mkono wake na atapiga Takbiyr. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitufu Nyumba juu ya ngamia. Kila alipoijia Nguzo [Jiwe], aliiashiria kwa kitu alichokuwa nacho na akapiga Takbiyr)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1613)]
Na imepokewa kiusahihi toka kwa Ibn ‘Umar: ((Kwamba alikuwa anapoigusa Nguzo husema Bismil Laah Allaahu Akbar)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdur Razzaaq (8894) na Al-Bayhaqiy (5/79). Al-Haafidh kasema ni Swahiyh katika At-Talkhiysw (2/247)]
6- Kusujudu juu ya Jiwe Jeusi
Toka kwa Ibn ‘Umar amesema: ((Nilimwona ‘Umar bin Al-Khattwwaab akilibusu Jiwe na akisujudu juu yake, kisha akarudi akalibusu na akasujudu juu yake, halafu akasema: Hivi ndivyo nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh kama ilivyo katika Al-Irwaa (4/312)]
Na hili limethibiti vile vile toka kwa Ibn ‘Abbaas kutokana na kitendo chake.
Al-Albaaniy (Rahimahul Laah) kasema katika Al-Irwaa (4/312): “Inaonekana kutokana na ujumla wa yaliyotangulia kuwa kusujudu juu ya Jiwe Jeusi kumethibiti kukiwa Marfuw’u na Mawquwf. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.
7- Kuigusa kwa mkono Nguzo ya Al-Yamaaniy
Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: ((Sikumwona Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akigusa [kingine chochote] katika Nyumba isipokuwa Nguzo Mbili za Al-Yamaaniy)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1609) na Muslim (1267)]
Mwanamke asisongane na wanaume
Haitakikani mwanamke apigane vikumbo na wanaume kwa ajili ya kuzigusa Nguzo Mbili au kulibusu Jiwe Jeusi wakati wa Twawaaf. Toka kwa ‘Atwaa amesema: ((‘Aaishah alikuwa anatufu sehemu kando na wanaume, hachanganyikani nao. Mwanamke mmoja akamwambia: Kazana tuguse ee Mama wa Waumini! Akasema: Kazana wewe, mimi niache. Akakataa. [‘Atwaa amesema] Wanatoka usiku wakiwa wamejibadilisha na kutufu pamoja na wanaume, lakini wao walikuwa wanapoingia Al-Ka’abah husimama mpaka wanaume watolewe)).
Ummu Salamah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alipolalamika, Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia:
((طوفي من وراء الناس وأنت راكبة))
((Tufu nyuma ya wanaume ukiwa umepanda [mnyama])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1618) na Abdur Razzaaq (5/67)]
Nguzo Mbili za Kishaam haziguswi
Ni kwa Hadiyth iliyotangulia nyuma kidogo ya Ibn ‘Umar. Kwa kuwa Nguzo ya Kaskazini na Magharibi (mwelekeo wa nusu duara ukuta) haziko ndani ya misingi iliyojengwa na Ibraahiym ‘Alayhis Salaam kama ilivyotangulia.
8- Kuomba du’aa baina ya Nguzo Mbili za Yamaaniy
Toka kwa ‘Abdullaah bin As-Saaib amesema: ((Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akisema baina ya Nguzo na Jiwe:
رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّار
[Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1892), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (3934), Ahmad (3/411) na wengineo. Hilo limethibiti vile vile kwa kufanywa na ‘Umar na mwanawe kwa yaliyoelezewa na ‘Abdur Razzaaq (8966-8964)]
Sheikh wa Uislamu amesema katika Al-Fataawaa (26/122): “Imestahabiwa kwake wakati wa Kutufu amdhukuru Allaah Ta’aalaa na amwombe kwa du’aa za kisharia. Kama atasoma Qur-aan kwa sauti ya chini, basi si vibaya. Na hakuna adhkaar maalum toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), si kwa amri yake, wala kauli yake, wala maelekezo yake, bali mtu ataomba wakati wa Twawaaf du’aa zote zilizothibiti. Na du’aa maalum ambazo baadhi ya watu wanazileta chini ya bomba la mfereji wa maji ya paa la Al-Ka’abah (gutter) na mfano wa hilo, du’aa hizo hazina asili yoyote. Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akitamatisha Twawaaf yake baina ya Nguzo Mbili kwa kusema:
((رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّار))ِ
..kama alivyokuwa anatamatishia du’aa zake nyinginezo.
9- Kumalizia kwenye Maqaamu Ibraahiym –baada ya Twawaaf- na kusoma:
((وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى))
10- Kuswali rakaa mbili nyuma ya Maqaamu Ibraahiym baada ya Twawaaf ikiwezekana.
11- Asome katika rakaa hizi mbili:
((قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ)) na ((قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ))
Sunani hizi tatu za mwisho zimethibiti katika Hadiyth ndefu ya Jaabir inayozungumzia sifa ya Hajj ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Jumhuri ya ‘Ulamaa wanasema rakaa mbili nyuma ya Maqaam baada ya Twawaaf ni Sunnah kinyume na Mahanafiy wanaosema kuwa kwao wao ni waajib. Nayo ni riwaya toka kwa Ahmad, na kauli toka kwa Mashaafi’iy. Fuqahaa wa Kimaalik wamekubaliana nao katika Twawaaf ya Nguzo tu pasina nyinginezo. [Fat-hul Qadiyr (2/154), Haashiyatu Al-‘Adwaa (1/467), Mughnil Muhtaaj (1/492) na Al-Mughniy (3/394)]
Fuqahaa wa Kishaafi’iy na Kimaalik wanaona kuwa akiswali Swalaah ya Faradhi baada ya Kutufu, itamtosheleza na Rakaa mbili za Twawaaf.
Rakaa mbili za Twawaaf huswaliwa wakati wowote bila ya ukaraha ijapokuwa katika nyakati ambazo Swalaah imekatazwa kuswaliwa. Ni kwa Hadiyth ya Jubayr bin Mutw’im kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alisema:
((يا بني عبد مناف، لا تمنعوا أحدا طاف بهذا البيت، وصلى أية ساعة شاء من ليل أو نهار))
((Enyi Baniy ‘Abdi Man aaf. Msimzuie yeyote aliyeitufu Nyumba hii, na akaswali saa yoyote aitakayo usiku au mchana)). Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (869), An-Nasaaiy (5/223) na Ibn Maajah (1254)]
Haijuzu kupita mbele ya anayeswali katika Al-Haram na kwenye sehemu nyingine
Ama tamshi la Sheikh wa Uislamu (Rahimahul Laah): “Lau mwenye kuswali ataswali ndani ya Msikiti (Al-Masjid Al-Haraam) na watu wanatufu mbele yake, haitokuwa makruhu, ni sawa akipita mbele yake mwanaume au mwanamke. Na hili ni katika mambo mahsusi ya Makkah”. [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/122)]
Mimi siijui dalili yoyote kuhusiana na umahususi huu, Na asili ni kutokujuzu kupita mbele ya mwenye kuswali kama ilivyotangulia katika mlango wa Swalaah. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
12- Kunywa Maji ya Zamzam na kuyamimina kichwani baada ya Kutufu na kuswali rakaa mbili
Hadiyth ya Jaabir inasema: ((Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikwenda mwendo kasi kidogo mizunguko mitatu [ya kwanza] toka kwenye kikuta cha kiduara hadi kwenye Jiwe, akaswali rakaa mbili, kisha akarudi kwenye Jiwe. Halafu akaenda kwenye Zamzam na akanywa toka humo, akajimwagia kichwani mwake, kisha akarejea, na akaigusa Nguzo…..)). [Imekharijiwa na Ahmad (3/394). Katika Muslim (1218) kumetajwa kunywa tu]
13- Je, mtu ataambatisha kifua chake na shavu lake la kulia na ukuta wa Al-Ka’abah kati ya Jiwe Jeusi na Mlango [wa Al-Multazam]?
Imesimuliwa kuwa Nabiy (Swallah Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alilifanya hilo Siku alipoikomboa Makkah. Toka kwa ‘Abdur Rahmaan bin Abiy Swafwaan amesema: ((Rasuli wa Allaah alipoikomboa Makkah, nilichomoka haraka, nikamwona Rasuli wa Allaah ametoka toka kwenye Al-Ka’abah yeye pamoja na Swahaba Zake, wakiwa wameigusa Nyumba tokea mlangoni hadi kwenye Al-Khatwiym (Kikuta cha nusu duara), na wakaweka mashavu yao juu ya Nyumba, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) yuko kati yao)). [Isnaad yake ni Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1898)]
Na imesimuliwa toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake amesema: ((Nilitufu pamoja na ‘Abdullaah bin ‘Amri, na alipoelekea sambamba nyuma ya Al-Ka’abah nilisema: Hivi huleti isti’aadhah? Akasema: Tunajilinda kwa Allaah na moto. Kisha akaenda mpaka akaligusa Jiwe, akasimama kati ya Nguzo na Mlango, akakiweka kifua chake, uso wake na mikono yake miwili hivi –akaikunjua mpaka mwisho- na akasema: Hivi ndivyo nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akifanya)). [Isnaad yake ni Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1899), Ibn Maajah (2962), Al-Bayh aqiy katika As-Sunan (5/93), na katika Ash-shu’ab (4058) kwa Sanad Dhwa’iyf]
Ninasema: “Hadiyth zote mbili ni Dhwa’iyf. Lakini je, moja yao inapata mwega kwa nyingine? Hili ni la kulitafiti. Kisha hili la kujiambatisha kifua na mashavu linayumkinika liwe wakati wa kuaga, na liwe katika jingine. Lakini Jumhuri wamesema: Imesuniwa asimame kwenye Al-Multazam (kati ya Jiwe Jeusi na Mlango wa Al-Ka’abah) baada ya Twawaaf ya Kuaga na aombe du’aa, kwa kuwa hapo ni katika mwahala ambapo du’aa hujibiwa kama ilivyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”. [Zaadul Ma’aadiy (2/298), Sharhu Ibn ‘Aabidiyna (1/170-187), Rawdhwat At-Twaalibiyna (3/118), na Kash-shaaful Qinaa (2/513)]
Mazungumzo, kuelimisha na kujibu swali katika Twawaaf
Inajuzu kuzungumza wakati wa Twawaaf. Twawaaf haibatiliki wala haibebi umakruhu, lakini ni bora kuacha isipokuwa kama maneno ni ya kheri kama kuamrisha mema, au kukataza munkari, au kumwelekeza asiye jua, au kujibu fatwa na kadhalika.
Toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) –alipokuwa anatufu Al-Ka’abah- alimpitia mtu ambaye alikuwa amefunga mkono wake kwa mtu mwingine kwa kamba au uzi au kitu kingine kisicho hivyo, Nabiy akaikata kwa mkono wake kisha akamwambia: ((Mwongoze kwa [kumkamata] mkono wake)). [Al-Majmuw’u cha An-Nawawiy (8/62-63)]
Kutufu juu ya kipando
Inajuzu Kutufu juu ya kipando –hata kama mtu anaweza kutembea- kutokana na dharura. ((Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitufu juu ya ngamia na kuigusa Nguzo kwa bakora yake)) ili watu wapate kumuona. Ni kwa Hadiyth ya Jaabir aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitufu Nyumba katika Hajj ya Kuaga juu ya mnyama wake, na [alisai] kati ya Swafaa na Marwah [juu ya mnyama pia] ili watu wamwone, ili achomoze, na ili wamuulize, kwani watu walimzonga)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1215)]
Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, na riwaya toka kwa Ahmad. Wanasema hakuna tatizo lolote kwa aliyepanda hata bila ya udhuru. Lakini Mahanafiy na Mahanbali wanasema ni lazima atembee kwa hali yoyote. Na akina Maalik wanasema ni lazima atembee lakini katika Twawaaf ya Wajibu tu. Na kama atatufu kwa kupanda naye anaweza kutembea, basi ni lazima achinje mnyama. [Al-Badaai’u (2/128), Haashiyatul ‘Adhwaa (1/468), Al-Mughniy (3/397) na Nihaayatul Muhtaaj (3/275)]
Lenye mashiko ni kuwa hawajibikiwi na chochote. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.