20-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Nguzo Ya Tatu Ya Hajj: Sa'yi Kati Ya As-Swafaa Na Al-Marwah
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah
20-Nguzo Ya Tatu Ya Hajj: Sa’yi Kati Ya As-Swafaa Na Al-Marwah
Maana ya Sa’yi
Ni kutembea kati ya Swafaa na Marwah kwenda na kurudi kwa niya ya kutaabudia. Ni “ashwaatw” 7 [mwendo wa kwenda na kurudi] kwa kuanzia As-Swafaa na kumalizia Al-Marwah.
Hukmu yake
Kusai kati ya Swafaa na Marwah ni nguzo kati ya nguzo za Hajj kwa mujibu wa kauli sahihi ya ‘Ulamaa. Ni madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad –katika moja ya riwaya mbili-, Is-Haaq, na Abu Thawr. Ni kauli pia ya Ibn ‘Umar, Jaabir na ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa).
Mwenye kusahau Kusai, au akasahau “shawtw” moja, basi ni lazima arudi kuifanya kamili wakati atakapokumbuka hata kama yuko nchini kwake au sehemu nyingine. Asiporudi, basi Hajj yake itabatilika kwa kuiacha, na haiungwi kwa kuchinja wala kwa jingine lolote. [Fat-hul Qadiyr (2/156), Haashiyatul ‘Adwaa (1/470), Al-Majmuw’u (8/71) na Al-Mughniy (3/385)]
Dalili ya hilo ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
((إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا))
((Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika Alama za Allaah. Basi yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah basi hakuna lawama kwake Kutufu (vilima) viwili hivyo.)). [Al-Baqarah (2: 158)]
‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) amebainisha maana ya kuteremka Aayah hii na dhana yake. Ameweka wazi kwa ufasaha na usahihi hilo katika Hadiyth ifuatayo..
2- ‘Urwah amesema: ((Nilimuuliza ‘Aaishah nikamwambia: Unasemaje kuhusu
Kauli ya Allaah Ta’aalaa:
((إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا))
..Basi Wa-Allaah, hakuna lawama kwa yeyote kama hakutufu As-Swafaa na Al-Marwah? Akasema: Maneno mabaya kabisa hayo umesema ee mtoto wa dada yangu! Hakika hili lau lingelikuwa kama ulivyoliawilisha, ingekuwa hakuna ubaya kwa mtu kama asingetufu vilima viwili. Lakini Aayah hii iliteremshwa kwa ajili ya Maanswaar. Walikuwa kabla hawajaingia katika Uislamu wakilinyanyulia sauti [sanamu la] Manaat At-Twaaghiyah ambalo walikuwa wanaliabudu eneo la Al-Mushallal. Akawa anayehiji anahisi ukakasi Kutufu As-Swafaa na Al-Marwah. Waliposilimu, walimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuhusu hilo. Wakasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika sisi tulikuwa tunahisi ukakasi kutufu baina ya As-Swafaa na Al-Marwah [enzi ya ujahili]. Hapo Allaah Ta’aalaa Akateremsha:
إنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ
‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) akasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akaweka sharia ya Kutufu baina ya vilima viwili, na yeyote hawezi kuacha Kutufu baina yao)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1562)]
3- Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((اسمعوا، فإن الله كتب عليكم السعي))
((Sikieni! Hakika Allaah Amewafaradhishieni Kusai)). [Swahiyh Bituruqihii. Imekharijiwa na Ahmad (6/421) na Al-Haakim (4/70). Angalia Al-Irwaa (1072)]
4- ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) amesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitufu na Waislamu walitufu –anakusudia baina ya As-Swafaa na Al-Marwah- ikawa ni Sunnah [ya Uislamu]. Na kwa uhai wangu, Allaah Haitimizi Hajj ya ambaye hakutufu baina ya As-Swafaa na Al-Marwah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1277) na Ibn Maajah (2986)]
5- Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia ‘Aaishah:
((طوافك بالبيت وبين الصفا والمروة يجزيك أو يكفيك لحجك وعمرتك))
((Kutufu kwako Nyumba, na [Kusai] kati ya As-Swafaa na Al-Marwah, kunakutosheleza au kunakutimizia Hajj yako na ‘Umrah yako)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1897), Al-Bayhaqiy (5/106) na Al-Baghawiy (7/84). Kwa Muslim (1211) ina tamshi la ((Inakuenea Twawaaf yako kwa Hajj yako na ‘Umrah yako)).
Na kama isingelikuwa ni waajib, asingesema inakutosheleza. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
6- Toka kwa ‘Amri bin Diynaar amesema: ((Tulimuuliza Ibn ‘Umar kuhusu mtu ambaye ametufu Nyumba katika ‘Umrah na hakutufu kati ya As-Swafaa na Al-Marwah, je anaweza kumwingilia mkewe? Akasema: Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuja akatufu Nyumba mara saba, akaswali nyuma ya Maqaam rakaa mbili, akatufu kati ya As-Swafaa na Al-Marwah mara saba.
Na tukamuuliza Jaabir bin ‘Abdullaah akasema: Asimkurubie kabisa mpaka atufu kati ya As-Swafaa na Al-Marwah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1646). Na Muslim amekhariji (1234) athar ya Ibn ‘Umar]
‘Ulamaa wana kauli mbili nyingine kuhusu hukmu ya Kusai:
Ya kwanza: Abu Haniyfah, Ath-Thawriy na Al-Hasan Al-Baswriy wanaona kwamba Kusai ni waajib na si nguzo. Atakayeacha, basi ni lazima achinje mnyama, na Hajj yake ni sahihi.
Ya pili: Anas bin Maalik, ‘Abdullaah bin Az-Zubayr na Muhammad bin Siyriyna wanaona kuwa Kusai ni Sunnah na si wajibu, na hakuna lolote analodaiwa mtu kama ataacha. Na hili limesimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas, na linafanana kuwa sawa na madhehebu ya Ubayya bin Ka-‘ab na Ibn Mas’uwd ambao katika maelezo ya pembeni ya Misahafu yao wameandika:
"فلا جناح عليه أن لا يطوف بهما"
((Hakuna ubaya kwake asipotufu vilima viwili)).
Ibn ‘Abdil Barri amesema: “Kilichodondoka katika (maelezo ya kando) Musw-haf wa jamaa hakichukuliwi kuwa hoja, kwa kuwa hakipitishwi kuwa kinatoka kwa Allaah ‘Azza wa Jalla, na wala hakihukumiwi kuwa ni Qur-aan ila tu kile kilichonukuliwa na jamaa kati ya vibao viwili (ndani ya Musw-haf). Na taawiyl bora kabisa iliyosimuliwa kwa Aayah hii ni yale aliyoyaeleza ‘Aaishah”. [At-Tamhiyd cha Ibn ‘Abdul Barri (2/98)]
Kutufu (Al-Ka’abah) na Kusai (kati ya As-Swafaa na Al-Marwah) kwa mwenye kufanya Qiraan na mwenye kufanya Tamattu’i
‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu hili katika madhehebu matatu: [Az-Zaad (2/271), Tahdhiyb As-Sunan (5/243) na Majmuw’u Al-Fataawaa (26/104)]
La kwanza: Kila mmoja kati ya wawili atafanya Twawaaf mbili (Al-Ka’abah) na Kusai mbili (As-Swafaa na Al-Marwah).
Hili limesimuliwa toka kwa ‘Aliyy na Ibn Mas’uwd. Pia ni kauli ya Sufyaan Ath-Thawriy, Abu Haniyfah, watu wa Kuwfah, Al-Awzaa’iy na riwaya toka kwa Ahmad.
La pili: Kila mmoja kati ya wawili atafanya Twawaaf moja (Al-Ka’abah) na Kusai moja (As-Swafaa na Al-Marwah)
Haya yameelezwa na Al-Imaam Ahmad katika riwaya ya mwanaye ‘Abdullaah. Sheikh wa Uislamu na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim wamelikhitari hili.
La tatu: Mwenye kufanya Tamattu’i atafanya Twawaaf mbili na Kusai mbili, na mwenye kufanya Qiraan atasai mara moja.
Ni kauli ya ‘Atwaa, Twaawuws na Al-Hasan. Ni madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad.
Kauli ya madhehebu ya kwanza ni dhaifu kwa kuwa haikuthibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) linalohabarisha hilo. Kikubwa wanachoweza kukishikilia wenye kauli hii ni Kauli Yake Ta’aalaa:
وَأَتِمُّوا الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلَّـهِ
((Na timizeni Hajj na ‘Umrah kwa ajili ya Allaah))
na hakuna ndani yake dalili katika hili. Utimilifu wa Hajj unapatikana hata kama –mwenye kufanya Qiraan- hakutufu isipokuwa Twawaaf moja kama inavyoonekana wazi katika dalili za makundi mawili mengine. Ama kauli mbili nyingine, sababu ya tofauti kati yao, ni kukinzana Hadiyth zilizokuja kuhusiana na hilo:
- Toka kwa Jaabir amesema: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakutufu wala Swahaba Zake kati ya As-Swafaa na Al-Marwah isipokuwa Twawaaf moja tu, Twawaaf ya kwanza)). Twawaaf hapa inakusudiwa Kusai. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1215), At-Tirmidhiy (947), Abu Daawuwd (1895), An-Nasaaiy (2986) na Ibn Maajah (2972)]
Toka kwa ‘Aaishah ((Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia:
((طوافك بالبيت وبين الصفا والمروة يكفيك لحجك وعمرتك))
((Ukitufu Nyumba, na [Kusai] kati ya As-Swafaa na Al-Marwah, kunakutosheleza Hajj yako na ‘Umrah yako)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]
Bibi ‘Aaishah hapa alikuwa anafanya Qiraan kwa kauli swahiyh.
- Toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) amesema: ((..Wakatufu Nyumba na [wakasai] baina ya As-Swafaa na Al-Marwah wale waliokuwa wamenuwia ‘Umrah, kisha wakavua Ihraam [wakatahalluli]. Kisha wakatufu Twawaaf nyingine baada ya kurudi kutoka Minaa. Ama wale waliokusanya Hajj na ‘Umrah, hakika walitufu Twawaaf moja)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1556) na Muslim (1211)]
Ibn Al-Qayyim amesema: “Ima isemwe: ‘Aaishah amethibitisha na Jaabir amekanusha, na kilichothibitishwa kinatangulizwa kabla ya kilichokanushwa. Au isemwe: Muradi wa Jaabir ni wale waliofanya Qiraan pamoja na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na wakaswaga wanyama –nao ni wachache- na hao walisai Sai [Kusai] moja tu na hakukusudia Swahaba wote. Au Hadiyth ya ‘Aaishah itolewe sababu ya kuwa neno lake: (akatufu …hadi mwisho) limepachikwa katika Hadiyth yake. Basi hizi ndizo njia tatu za watu katika Hadiyth yake. [Zaadul Ma’aadi kwa mabadilisho kidogo]
Ninasema: “Ama dai la kupachika, inalazimu kwalo kuwatia makosani vigogo wa hifdhw wenye kuaminika kama Az-Zuhriy na wengineo bila dalili bayana. Hadiyth yake imethibiti, hakuna shaka ndani yake, nayo ina Hadiyth nyingine zinazoipa mwega. [Angalia Kitabu cha Hijjah ya Nabiy cha Al-Albaaniy uk. 90]. Nayo ni dalili kuwa mwenye kufanya Tamattu’u ni lazima afanye Twawaaf mbili [Al-Ka’abah] na Sai mbili [As-Swafaa na Al-Marwah]. Na ‘Aaishah amehifadhi ambayo Jaabir hakuhifadhi. Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas inalitolea ushahidi kuwa aliulizwa kuhusiana na Tamattu’u ya Hajj akasema: ((Muhaajiruna na Answaar walihirimia Hajj pamoja na Wake wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika Hijjah ya Kuaga. Tulipowasili Makkah, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alisema:
إجعلوا إهلالكم بالحج عمرة، إلا من قلد الهدي
Ifanyeni niya yenu ya Hajj ‘Umrah, isipokuwa kwa aliyemvisha mnyama wa kuchinjwa kigwe. Tukatufu Nyumba na [Kusai] As-Swafaa na Al-Marwah, tukawaingilia wake na tukavaa nguo. Akasema (Rasuli):
من قلد الهدي فإنه لا يحل حتى يبلغ الهدي محله
Aliyemvisha mnyama wa kuchinjwa kigwe, basi asivue Ihraam [asitahalluli] mpaka mnyama afike machinjoni mwake. Kisha akatuamuru usiku wa At-Tarwiyah tunuwie Hajj. Na tulipomaliza Manaasik, tulikuja tukaizunguka Nyumba, na As-Swafaa na Al-Marwah, na Hajj yetu ikatimia na tukalazimikiwa mnyama wa kuchinja…)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy ikiwa Mu’allaq Majzuwm, na Muslim nje ya Swahiyh yake ikiwa Mawsuwl, na pia Al-Ismaa’iyliy katika Mustakhraji yake, na kutokea kwake Al-Bayhaqiy (5/23), na wapokezi wake ni watu madhubuti]
Na hili limethibiti kihakika kutokana na inavyoonyesha Hadiyth ya ‘Aaishah ya kuwa mwenye kufanya Tamattu’u ni lazima atufu na asai kwa ajili ya ‘Umrah, kisha avue Ihraam (atahalluli). Halafu atatufu na kusai tena baada ya kutoka ‘Arafah. Ama mwenye kufanya Qiraan, huyo ni lazima atufu mara moja na asai mara moja kwa mujibu wa maneno ya Jumhuri.
Je inajuzu kutanguliza Kusai kabla ya Kutufu Nyumba?
Maalik, Ash-Shaafi’iy, Abu Haniyfah na Maswahibu zao wanaona kwamba mwenye Kusai kabla ya Kutufu, hiyo haimtoshelezi na ni lazima arudie tena. Isipokuwa Maalik na Abu Haniyfah wamesema kuwa atatufu na kusai upya kwa yote mawili. Ash-Shaafi’iy amesema: Atasai tu tena ili kuwe baada ya kutufu. [At-Tamhiyd )6/12) na Al-Majmuw’u (8/105)]
Ninasema: Wanatolea dalili Hadiyth ya ‘Aaishah ya kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia –alipoingia hedhini-:
((افعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت حتى تطهري))
((Fanya (yote) ayafanyayo Hujaji isipokuwa tu usitufu Nyumba mpaka utwaharike)). [Hadiyth Swahiyh. Takhriyj yake imetajwa nyuma]
Kipengele cha dalili toka kwenye Hadiyth hii ni kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwamuru kufanya yote anayoyafanya mwenye kuhiji isipokuwa Kutufu Nyumba tu, na yeye (‘Aaishah) hakusai wala hakutufu. Na lau Kusai kusingelikuwa kumesimamia juu ya kutangulia Twawaaf kabla yake, basi asingelikuchelewesha na hususan pakizingatiwa kwamba mwenye hedhi hakatazwi Kusai -kwa mujibu wa kauli sahihi- kama itakavyobainishwa mbeleni kidogo.
Lakini mtu anaweza kusema: Kuchelewesha ‘Aaishah Kusai mpaka atufu kwanza hakumaanishi kwamba kufanya hivi ni lazima kwa wengine, na hasahasa tukizingatia kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakuulizwa kuhusu ‘amali yoyote iliyotangulizwa au iliyocheleweshwa Yawm An-Nahr [Tarehe 10 Dhul Hijjah] ila alisema:
((افعل ولا حرج))
((Fanya na hakuna ubaya))..
kama itakavyobainishwa mbeleni. Na huyu ni ‘Atwaa, Al-Awzaaiy na kundi la Asw-Haabu Al-Hadiyth.
Je inajuzu kwa mwenye hedhi asai baina ya As-Swafaa na Al-Marwah?
Kuna ziada iliyosimuliwa katika Hadiyth iliyotangulia ya ‘Aaishah:
((افعلي كما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت [ولا بين الصفا والمروة] حتى تطهري))
((Fanya (yote) kama anavyofanya Hujaji isipokuwa tu usitufu Nyumba [wala baina ya As-Swafaa na Al-Marwah] mpaka utwaharike)).
Lakini neno lake (wala baina ya As-Swafaa na Al-Marwah) ni ziada isiyo ya kawaida na haifai. [Angalia Fat-hul Baariy (3/589) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/534)]
Na hata tukiijaalia kuwa ziada hii ipo kwenye Hadiyth, lakini pamoja na hivyo, haionyeshi kuwa kunashurutishwa kuwa twahara kwa mwenye Kusai, kwa kuwa Kusai kunasimamia juu ya kufanywa Twawaaf kabla yake –kwa mujibu wa Jumhuri-, hivyo kizuizi cha Kusai kikawa ni kutotufu.
Na hakuna pia dalili yoyote ya kushurutisha twahara kwa ajili ya Kusai, bali imepokewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn ‘Umar kwamba amesema: ((Akitufu Nyumba, kisha akapata hedhi kabla hajasai baina ya As-Swafaa na Al-Marwah, basi asai kati ya As-Swafaa na Al-Marwah)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah katika Al-Muswannaf (1/4/343)]
Mithili ya kauli hii zimepokewa kauli sahihi toka kwa Al-Hasan, ‘Atwaa, Al-Hakam, Hammaad na wengineo katika Masalaf, nayo ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy. [Muswannaf Ibn Abiy Shaybah (1/4/344) kwa Asaaniyd Swahiyh. Angalia Al-Majmuw’u (8/106)]