19-Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi: التَّوَّابُ
Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi
(Maelezo Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Swiffah Zake)
التَّوَّابُ
التَّوَّابُ At-Tawwaab Mwingi Wa Kupokea Toba Baada Ya Toba
|
Allaah (سبحانه وتعالى), Ambaye Anaendelea kuwageukia kwa maghfirah na msamaha wale wanaogeukia Kwake kwa tawbah, na Anayesamehe makosa ya mwenye kutubu. Wote wanaogeukia kwa Allaah (عز وجل) kwa dhati, Allaah (عز وجل) Anawageukia kwa kuanza kuwapa uwezo wa kutubu na kuelekeza nyoyo zao upande Wake, kisha baada ya hili Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) huwageukia kwa kupokea tawbah zao na kuwasamehe makosa yao.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ﴿١٠٤﴾
Je, hawajui kwamba Allaah Ndiye Anayepokea tawbah ya waja Wake, na Anapokea Swadaqah na kwamba Allaah Ndiye Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [At-Tawbah (9):104]
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾
Enyi walioamini! Jieupusheni sana na dhana kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msifanyiane ujasusi, na wala wasisengenyane baadhi yenu wengineo. Je, anapenda mmoja wenu kwamba ale nyama ya nduguye aliyekufa? Basi mmelichukia hilo! Na mcheni Allaah! Hakika Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al-Hujuraat (49): 12]