55-Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi: الْقَرِيبُ - الْمُجِيبُ

Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi

 

(Maelezo Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Swiffah Zake)

 

Alhidaaya.com

 

الْقَرِيبُ - الْمُجِيبُ

 

 

الْقَرِيبُ

Al-Qariyb

Aliye Karibu

 

 

الْمُجِيبُ

Al-Mujiyb

Mwenye Kuitikia

 

 

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Yuko karibu na kila mmoja, na ukaribu huo ni wa aina mbili:

 

 

i) Ukaribu wa kiujumla ambao unamaanisha kuwa Kwake karibu kwa kila mmoja kwa mujibu wa ‘ilmu Yake, utambuzi, kuona, kushuhudia na kuzunguka.

 

 

ii) Ukaribu mahsusi ambao ni maalumu kwa wanaomwabudu, wale wanaomwomba na wanaompenda. Ukweli wa aina hii ya ukaribu hauwezi kufahamika, bali tunachoweza kuona ni athari zake, ukarimu Wake kwa waja Wake, kuwasaidia Kwake na kule kuwafanya wawe imara katika Swiraatw Al-Mustaqiym (Njia iliyonyooka).

 

 

Kutokana na athari za ukaribu huu ni kuwapokelea maombi wale wanaomwomba, na kuwapa uwezo wa kuwa ni wenye kutubu. Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Anayewaitikia, katika ufahamu wa ujumla, wanaomwomba, bila kujali ni akina nani, popote walipo na hali yoyote waliyonayo kama Alivyoahidi. Yeye Allaah (عز وجل) Ndiye Pekee Anawayewaitikia, katika ufahamu mahsusi, wale wanaompenda, wale wanaofuata Shariy‘ah. Pia Yeye Allaah (عز وجل) Ndiye anayeitikia katika haja kubwa na wale waliokata tamaa ya kuitikiwa na viumbe, na kwa hivyo muunganiko wao Kwake umetiwa nguvu kwa namna ya mapenzi, matumaini na khofu.

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah (2): 186]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۚ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ هُوَ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُّجِيبٌ﴿٦١﴾

Na kwa Thamuwd (Tulimpeleka) ndugu yao Swaalih. Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Yeye Ndiye Aliyekuanzisheni katika ardhi, na Akakufanyieni makazi humo; basi mwombeni maghfirah, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu Yuko Karibu kwa ujuzi Wake, Mwenye kuitikia. [Huwd (11): 61]

 

 

Share