54-Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi: الشَّاكِرُ - الشَّكُورُ
Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi
(Maelezo Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Swiffah Zake)
الشَّاكِرُ - الشَّكُورُ
الشَّاكِرُ Ash-Shaakir Mwenye Kupokea Shukurani
|
الشَّكُورُ Ash-Shakuwr Mwingi Wa Shukrani, Mwingi Wa Kukubali Kidogo Kwa Thawabu Tele
|
Allaah (سبحانه وتعالى) ni Pekee Anayetambua na kutoa malipo kwa ajili ya amali ndogo na Ndiye Anayesamehe madhambi makubwa. Allaah (عز وجل) Ndiye Pekee Anayelipa maradufu waja Wake wanyoofu kwa kuwazidishia zaidi pasi na kipimo. Allaah (عز وجل) Ndiye Pekee Anayewatambua na kuwalipa wanaomshukuru na Anamkumbuka anayemdhukuru Yeye (عز وجل). Yeyote anayetafuta kuwa karibu Naye kwa kufanya amali njema, Allaah (عز وجل) Anasogea karibu yake kwa kiwango kikubwa.
Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ اللَّـهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ ﴿١٥٨﴾
Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika alama za Allaah. Basi yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah basi hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo. Na atakayejitolea kufanya khayr basi hakika Allaah ni Mwenye kupokea shukurani, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah (2): 158]
Na pia Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّـهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ ﴿٢٩﴾
Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Allaah na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa kutokana na yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri wanataraji tijara isiyoteketea.
لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٠﴾
Ili (Allaah) Awalipe ujira wao timilifu, na Awazidishie kutokana na fadhila Zake, hakika Yeye ni Mwingi wa kughufuria, Mwingi wa kupokea shukurani. [Faatwir (35): 29-30]