53-Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi: الْحَلِيمُ
Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi
(Maelezo Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Swiffah Zake)
الْحَلِيمُ
الْحَلِيمُ Al-Haliym Mpole Wa Kuwavumilia Waja
|
Allaah (سبحانه وتعالى) ni Pekee Anayewapa fadhila tele, za namna zote mbili, za nje na za ndani. Anawapa fadhila neema na rahmah viumbe Wake licha ya matendo yao mengi ya uasi na kuruka mipaka. Yeye Allaah (عز وجل) ni Mpole kwa wasiomtii, na Amewabainishia katika Kitabu Chake na Sunnah za Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) tahadharisho na kuwakanya ili huenda wakatubu, na Anawapa muda ili huenda wakawa wenye kurudi kutubia Kwake.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي أَنفُسِكُمْ فَاحْذَرُوهُ ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ حَلِيمٌ ﴿٢٣٥﴾
Na jueni kwamba Allaah Anajua yaliyomo katika nafsi zenu basi jihadharini Naye. Na jueni kwamba hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mvumilivu. [Al-Baqarah (2): 235]
Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):
إِن تُقْرِضُوا اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا يُضَاعِفْهُ لَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ شَكُورٌ حَلِيمٌ﴿١٧﴾
Mkimkopesha Allaah karadhi nzuri, Atakuzidishieni maradufu, na Atakughufurieni. Na Allaah ni Mwenye kupokea shukurani, Mpole, Mvumilivu. [At-Taghaabun (64): 17]