52-Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi: الْغَنِيُّ - الْمُغْنِي
Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi
(Maelezo Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Swiffah Zake)
الْغَنِيُّ - الْمُغْنِي
الْغَنِيُّ Al-Ghaniyy Mkwasi Amejitosheleza, Hahitaji Lolote
|
الْمُغْنِي Al-Mughniy Mkwasi, Amejitajirisha
|
Allaah (سبحانه وتعالى) Amejitosheleza kikamilifu pasi na kizuizi. Kushindwa kumeondolewa kwenye ukamilifu Wake na kwa Sifa Zake. Katu hana upungufu wa namna yoyote, haiwezekani kuwa Awe namna yoyote isipokuwa kujitosheleza, kwa sababu hali ya kujitosheleza inatokana na matokeo ya lazima ya Nafsi Yake. Kadhalika, ni muhali Kwake kuwa kitu kingine isipokuwa Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) ni Muumbaji, Mwenye Nguvu Zote, Mpaji na Mwenye kuwakirimu waja wema. Allaah (سبحانه وتعالى) Hana haja ya kitu kwa yeyote. Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) ni Mwenye kujitosheleza Ambaye Mkononi Mwake ndipo kuna hazina za mbingu na ardhi, na hazina za duniani na Aakhirah. Amewatosheleza viumbe Wake wote na ni Mwenye kuwatosheleza Waumini katika viumbe Wake na katika hilo Anawatunikia nyoyoni mwao ‘ilmu ya kumjua Rabb wao na ukweli wa iymaan.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قَوْلٌ مَّعْرُوفٌ وَمَغْفِرَةٌ خَيْرٌ مِّن صَدَقَةٍ يَتْبَعُهَا أَذًى ۗ وَاللَّـهُ غَنِيٌّ حَلِيمٌ ﴿٢٦٣﴾
Kauli njema na msamaha ni bora kuliko swadaqah inayoifuata udhia. Na Allaah ni Mkwasi, Mvumilivu. [Al-Baqarah (2): 263]
Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):
وَرَبُّكَ الْغَنِيُّ ذُو الرَّحْمَةِ ۚ إِن يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَسْتَخْلِفْ مِن بَعْدِكُم مَّا يَشَاءُ كَمَا أَنشَأَكُم مِّن ذُرِّيَّةِ قَوْمٍ آخَرِينَ ﴿١٣٣﴾
Na Rabb wako ni Mkwasi Mwenye rahmah. Akitaka Atakuondosheni na Aweke wengine watakaofuatia baada yenu kwa Atakao, kama vile Alivyokuzalisheni kutokana na vizazi vya watu wengine. [Al-An’aam (6): 133]